JUMANNE
WIKI YA 21 YA MWAKA-C
Somo: 2The 2:1-3a, 14-17
Zab/Kit: 96:10,
11-12a, 12b-13
Injili: Mt 23:23-26
Nukuu
Mtu awaye yote
asiwadanganye kwa njia yo yote; aliyowaitia ninyi kwa injili yetu, ili kuupata
utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo,” 2The 2:3a,4
“Basi,
ndugu, simameni imara, mkayashike mapokeo mliyofundishwa, ama kwa maneno, ama
kwa waraka wetu,” 2The 2.15
“Na
Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe, na Mungu Baba yetu, aliyetupenda akatupa
faraja ya milele na tumaini jema, katika neema, awafariji mioyo yenu, na kuwafanya
imara katika kila neno na tendo jema,” 2The 2:16-17
“Viongozi vipofu,
wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia,” Mt 23:24
“Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa
mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na
kutokuwa na kiasi,” Mt 23:25
“Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe,
ili nje yake nayo ipate kuwa safi,” Mt 23:26
TAFAKARI: “Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia,”
Mt 23:24
Wapendwa wana wa Mungu,
tulitafakari neno hili kwa undani, “Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia,” Mt 23:24. Bwana
wetu Yesu Kristo alikuja ulimwenguni huku siyo tu kumkomboa mwanadamu kiroho,
bali pia kimwili ikiwa ni pamoja na maisha ya mwanadamu huyu katika ujumla
wake. Ndiyo maana Yesu hakuacha kukemea mila na desturi potofu, Yoh 9:1-25, ukadamizaji
kisiasa na kimifumo, Lk 20:21-26, kidini, Yoh 4:4-30, na hata kiuchumi, Mt
17:24-27. Tunapo tafakari maeneo hayo tajwa, na mengine mengi katika Maandiko
Matakatifu tunagundua ‘misioni’ ya Yesu hapa dunia ilikuwa kukuweka wewe na
mimi huru mwili na roho, na katika kweli na haki. Na hivi ndivyo Yesu asemavyo,
“Basi mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli,” Yoh 8:36
Yesu aliyaisha maisha ya kawaida ya watu wa nyakati
zake, alisafiri nao katika shida na raha zao, alionja uchungu wao, na alitokwa
machozi pamoja nao, Yoh 11:1-43. Yesu katika hali na mazingira haya alikuwa
kweli Mwanadamu. Hapa pamoja na kulia na wanadamu, hakubaki katika hali ile ya
kibinadamu tu, bali alionyesha Umungu wake, Yoh 11:44-45. Hakika Yesu anatupa
mfano mzuri wa kiongozi. Kwa vile aliishi kama kiongozi wa kweli, mwenye
uchungu na dhamana kubwa wa wale aliowajia, Yesu hakusita kukemea uovu aliouona
kwa viongozi wa nyakati zake. Naye anasema, “Viongozi
vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia,” Mt 23:24. Viongozi hawa walikosa
sifa zifuatazo, yaani, hawakuwa nuru, hawakuwa wasimamizi na watetezi wa kweli
na haki, na hawakuwa tumaini pale watu walipokoswa tumaini.
Kiongozi ni nuru kwa sababu uwaongoza watu kutoka
kwenye giza, yaani, uovu ili waufikie mwanga
wanaoutamani, yaani kweli, haki, tumaini na upendo. Hivyo ni sikitiko kubwa
sana kwa wanaoongozwa kuona kiongozi wao kuwa sababu ya maumivu yao na mchochea
uovu. Watu ukosa mwelekeo na maisha ukosa maana. Kiongozi ni msimamizi na
mtetezi wa haki katika mizania ya kweli na haki. Hivyo ‘kuchuja mbu na
kumeza ngamia’ kulimaanisha na kunamaanisha kutokuwa na mizania ya kweli na
haki katika kutoa HAKI. Si jambo la kushangaza kuona mwizi wa kuku kufungwa
gerezani, na wakwapuaji wa rasilimali za Taifa kuendelea kula raha mtaani.
Licha ya kwamba wote, yaani, mwizi wa kuku na mkwapuaji wa rasilimali za Taifa
wanamakosa, mizania ya kweli na haki kwa mujibu wa sheria ichukue mkondo wake.
Naye Yesu anasema, “Ole wenu waandishi na
Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini
mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo
imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache,” Mt 23:23. Kama tumejiwekea
utaratibu kwa nini hatuufwati na mara nyingine wengine kwa madaraka yao
wanakuwa juu ya ‘utaratibu?’ Hili Yesu aliliona na hakuacha kulikemea.
Jambo linguine Yesu alilolikea ni tabia ile ya kufanya
mambo ili kuonekana na watu kuwa unafanya jambo fulani kumbe katika uhalisia wa
jambo hilo unachofanya ni ‘maigizo’ matupu. Unafiki ni saratani mbaya
sana hasa pale tunapo dhamiria kwa
dhati kubadilika na kusonga mbele. Yesu analikemea hili na kusema, “Ole wenu
waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano,
na ndani yake vimejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi,” Mt 23:25. Tusifanye
vitu kama zima moto! Kama utumeamua kufanya vita dhidi ya ufisadi iwe vita
kweli na siyo kufanya mlinganisho wa uovu. Jambo la ajabu ni kwamba uovu ule
unaotuhusu na wakati mwingine kushiriki moja kwa moja tunaufumbia macho. Huku
ndiko kusafisha kikombe kwa nje na kuacha uchafu ndani. Yesu anatoa maelekezo ya
namna ya kufanya na kusema, “Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya
kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi,” Mt 23:26.
Kiongozi licha ya kuwa
tumaini kwa watu, kiongozi ni mwonyesha tumaini hasa pale tumaini hilo
linapotoweka. Na katika hali na mazingira haya ya kutoweka kwa tumaini Mtume
Paulo anasema, “msifadhaishwe upesi hata
kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno,” 2The 2:2a. Ndugu yangu, hapa pale tunapoona kusalitiwa kwa
wale tulio waamini tusiiache kweli na haki, na kusimama imara katika kweli na
haki hiyo. Hivyo, “Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote;
aliyowaitia ninyi kwa injili yetu, ili kuupata utukufu wa Bwana wetu Yesu
Kristo,” 2The 2:3a, 4. Matumaini yetu tuyaweke kwa yule atutiaye nguvu, Flp
4:13. Kila mtu kadiri ya imani yake ayashike maadili yaliyo mema na kuupinga
uovu kwa nguvu zake zote. Na hivi ndivyo Mtume Paulo anavyowafunda Wakristo
wenzake na kusema, “Basi, ndugu, simameni
imara, mkayashike mapokeo mliyofundishwa, ama kwa maneno, ama kwa waraka wetu,”
2The 2.15. Na tumaini letu katika nyakati
hizi za sintofahamu ndilo hili; “Bwana
wetu Yesu Kristo mwenyewe, na Mungu Baba yetu, aliyetupenda akatupa faraja ya
milele na tumaini jema, katika neema, awafariji
mioyo yenu, na kuwafanya imara katika kila neno na tendo jema,” 2The 2:16-17.
Hakuna lisilowezekana kwa Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ewe
Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa
safi,” Mt 23:26
Tusali:-Ee
Yesu tuongoze daima katika kweli na haki. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario