jueves, 18 de agosto de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 20 YA MWAKA-C

IJUMAA WIKI YA 20 YA MWAKA-C

Somo: Eze 37:1-14
Zab/Kit: 107:2-3, 4-5, 6-7, 8-9
Injili: Mt 22:34-40
Nukuu
Bwana MUNGU aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi,” Eze 37:5 

 “Basi tabiri, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu, enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli,” Eze 37:12

 “Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu; Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu?” Mt 22:35-36

Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza,” Mt 22:37-38

Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii,” Mt 22:39-40 

TAFAKARI: “Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi.”

Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na maendeleo aliyoyafikia mwanadamu leo, ikiwa ni pamoja na kuishi kwa kujiwekea vilinda uhai wake, “life securities,” hata hivyo uhakika huo bila Mungu ni sawa na kutwanga maji katika kinu. “Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana,” Rum 14:7-8. Ndugu yangu, pamoja na mipango yako ya muda mfupi na mrefu uliyojiwekea, kati yetu hakuna ajuaye ni kitu gani kitakachomtokea sekunde chachetu tu zijazo. Je, tusifanye chochote kwa kuwa huu ndio ukweli? Hapana! Tuyafanye na kuyapanga yote katika usahihi wake, na tufanye hivyo kwa kumshirikisha Mungu kwa kila jambo.

Mara nyingi penye mafanikio-‘kibinadamu,’ wengi wetu hitaji na uwepo wa Mungu huwa hitaji la nyongeza. Tunaamini yote huenda sawa bila Yeye (Mungu) kuwepo. Hiki ndicho kiburi kikubwa sana cha mwanadamu asiye na hofu ya Mungu ndani yake. Hali na mazingira haya yanawakuta wana wa Israeli nyakati zile za Nabii Ezekieli. Mungu anawafananisha waasi hawa wa imani kama mifupa isiyokuwa na nyama. Na hivi ndivyo wana hawa wa Israeli walivyofananishwa na Mungu (mifupa isiyo na nyama wala uhai) katika swala zima la imani. “Mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli; tazama, wao husema, Mifupa yetu imekauka, matumaini yetu yametupotea; tumekatiliwa mbali kabisa,” Eze 37:11. Bila mkono wa Mungu tuyafanyayo hata kama yatavuma sana hayatakuwa na mwisho mzuri. Na hivi ndivyo Nabii Ezekieli alivyozamishwa na Mungu katika tafakari nzito na chukuliwa nje katika roho ya Bwana.

Hata katika hali hii ya uasi na kukosa dira katika imani, Mungu hapendi hata mmoja wetu apotee. Yeye ndiye uhai na uzima kwa kila kipumuacho, na Yeye huweza kubadili tabia na mienendo ya vyote alivyoviumba. Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu,” 1Sam 2:6-7. Mungu akiwa ndiye yote na katika yote, kwa upendo na huruma wake, “humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake,” 1Sam 2:8. Tunapomrudia Mungu katika toba na majuto ya kweli, Mungu huyabadili maisha yetu na kutufanya wapya mbele za macho yake. Na hivi ndivyo alivyoitoa ahadi yake kwa wana wa Israeli na kusema, “Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu, enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli,” Eze 37:12. Naye Mungu asema hivi juu ya mifupa ile ikiwa ni pamoja na hali nzima ya udhaifu wako na wangu kwamba, Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi,” Eze 37:5. Hakuna jambo la kumshinda Mungu kwa sababu namna tulivyo, na vyote tulivyonavyo vyaonyesha Furaha ya Mungu, na kuufunua Utukufu wake.

Ni kwa matiki hii Mzaburi anasema, usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi. Maana atakapokufa hatachukua cho chote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata,” Zab 49:16-17. Ukweli ni kwamba hatukatazwi kuwa matajiri, bali utajiri huo usiwe mwisho wa kila kitu katika maisha yako. Utajiri wako ukuweke karibu na Mungu na jirani yako. Na hii ndiyo maana ya amri ya mapendo, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza,” Mt 22:37-38. Ulifanyalo hilo yaani, kumpenda Mungu kwa moyo, roho, na akili zako zote, yakupasa kufaulu mtihani wake, yaani, ukaribu wako na jirani yako, na hasa katika uhitaji wake. Hivyo, Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii,” Mt 22:39-40. Je, utajiri wako ikiwa ni pamoja na uwe wa kushikika au karama na vipaji ulivyopewa na Mungu, vinakuweka karibu naye (Mungu) na jirani yako? Kama hakuna ukaribu huo, ndugu yangu utajiri huo ulio nao ni balaa kwako.

Tumsifu Yesu Kristo!

Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu, na kuwatoa ninyi katika makaburi yenu, enyi watu wangu,” Eze 37:13

Tusali:- Ee Yesu Mwema, tujalie neema ndani yetu ili tuondokane na hali  ya uasi ndani yetu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario