IJUMAA
WIKI YA 21 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 1:17-25
Zab/Kit: 33:1-2, 4-5,
10ab, 11
Injili: Mt 25:1-13
Nukuu
“Kwa sababu neno la
msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya
Mungu,” 1Kor 1:18
“Yu wapi mwenye hekima?
Yu wapi mwandishi? Yu wapi mlete hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya
hekima ya dunia kuwa ni upumbavu?” 1Kor 1:20
“Kwa sababu upumbavu wa
Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya
wanadamu,” 1Kor 1:25
“Ndipo
ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka
kwenda kumlaki bwana arusi,” Mt 25:1
“Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara,” Mt
25:2
“Akajibu
akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi,” Mt 25:12
“Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa,” Mt 25:13
TAFAKARI: “Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi
mlete hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni
upumbavu.”
Wapendwa wana Mungu, pamoja na ukweli kwamba maisha ni jukumu la muda
mfupi, twahitaji hekima ya kutosha kuendana na jukumu hilo la muda Mfupi,
yaani, maisha. Hekima hiyo iniongoze kutambua bila shaka kwamba niliukuta
ulimwengu huu, na nitauacha siku moja ulimwengu huu. Hivyo nielewe ninao wajibu
licha wa muda mfupi kuufanya ulimwengu huu mahali salama pa kuishi, na
paendelee kuwa hivyo hata nitakapo ondoka katika ulimwengu huu. Kwa mantiki
hiyo, mimi na wewe tuwe daima vyombo vya amani, na habari njema. Ingawa tunayo
mengi ya kufanya, hili la kuwa ‘chombo cha amani na habari njema’ liongoze na
kutafsiri yale yote tuyafanyayo. Na tusema daima kama Mtume Paulo, “Maana
Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima
ya maneno, msalaba wa Kristo usije ukabatilika,” 1Kor 1:17. Msalaba wa Kristo
ndiyo kielelezo halisi (mti) ambacho wokovu wetu ulitundikwa juu yake.
Ndugu yangu
tunayesafiri sote katika tafakari hii, niutazamapo Msalaba Mtakatifu na
kuyatafakari matendo makuu ya Mungu na upendo wake kwetu, ni uweke mbali
ubinafsi wangu, kiburi changu, na kujigamba kwangu. Msalaba uwe fahari yangu
daima. Niseme na kuyaishi maneno hayo mazito kama asemavyo Mtume Paulo kwamba, “Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu
cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu
umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14. Lakini jambo la ajabu
leo na kusikitisha ni kwamba, baadhi yetu na hasa waliopewa mamlaka na ummaa
kwa kuutanguliza ubinafsi wao mbele, kiburi chao, kujigamba kwao na kwa kuusaka
umaarufu pasipo sifa na siha, wapo tayari kuliingiza taifa hili katika
machafuko. Hata hivyo wengi tunapigwa mshangao na kujiuliza swali hili kama
afanyavyo Mtume Paulo; “Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu
wapi mlete hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni
upumbavu?” 1Kor 1:20. Je, twataka yatokee ndipo tuanze vikao vya usuluhishi? Ni
kweli kwamba jamii yetu leo haina tena wazee wenye hekima kama waleta hoja wa
zamani, yaani, Baba Yetu wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na wenzake
wa nyakati zake? Hakika tukiliruhusu hili tuwe tayari kuja kuhukumiwa na historia
tunayoitengeneza sasa kwa mbwembwe kubwa.
Wenye hofu ya Mungu na
wenye kuuthamini Msalaba Mtakatifu ambao wokovu wetu ulitundikwa juu yake, kwao
Msalaba ni nguvu ya Mungu, IKor 1:18b. Ila kwa wanao potea kwa sababu ya
kiburi, majigambo, umaarufu pasipo sifa na siha, Msalaba kwao utabaki kuwa ni
upuzi, IKor 1:18a. Na hivi ndivyo asemavyo Mtume Paulo, “Kwa sababu
neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu
ya Mungu,” 1Kor 1:18. Tunahitaji hekima nyakati hizi kuliko zote, kwa sababu
shetani katukalia kooni na macho yetu hayaoni tena uhalisi wa kitu kama
kilivyo, bali twauona uhalisi wa kitu kama tulivyo katika ubinafsi wetu,
majigambo yetu, na umaarufu wetu pasipo sifa na siha. “Kwa kuwa
imeandikwa, Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao wenye akili
nitazikataa,” 1Kor 1:19. Leo wenye hekima na akili, na hata waliokwisha kuwa
wahudumu kwa nafasi mbalimbali katika taifa hili wameipiga kisogo hekima na
akili yao.
Tumebaki kuisikia
miluzi mingi na hata kuipiga miluzi hiyo ilhali hatujui kwamba kwa kufanya
hivyo ndivyo tunavyozidi kumchanganya mbwa awindaye. Hapa ndipo Mungu
anaporuhusu hekima ya dunia kuwa upumbavu, 1Kor 1:20. Je! Mungu hakuifanya
hekima ya dunia kuwa ni upumbavu?” 1Kor 1:20d. Leo tunajiuliza pia kwa kina,
‘Yu wapi Mwandishi wa kweli, kwenye kuiona kweli, na kuandika kweli?’ 1Kor
1:20b. Wengi wao wameyasaliti maadili yao na fani yao, na kuamua kulitumikia
tumbo lisiloridhika hata lingelishwa vizuri kila siku. Hata hivyo tusilipoteze
tumaini la Mungu na la kweli ndani yetu licha ya sintofahamu hizi za leo na
sasa. “Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua
Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa upuzi wa lile neno
linalohubiriwa,” 1Kor 1:21. Tukilipoteza tumaini, maisha hukosa maana. Na
maisha yakikosa maana, binadamu huwa hatari sana, kwani husukumwa kufanya
chochote kibaya. Je, tunataka ishara zaidi kwa haya tunayoyaona leo na sasa
ndiyo tuamini kesho yetu itakuwa mbaya? La hasha!
Ndugu yangu, Mtume
Paulo anatuambia hivi, ‘Wayahudi walitaka ishara, na Wayunani
walitafuta hekima; bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa
Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa
Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu,’ 1Kor 1:22-24. Na
tunachohubiri kama wana wa Mungu na warithi wa ufalme wa Mungu si VITA, bali
UPENDO. Na tunapo hubiri huu UPENDO tusisahau kwamba AMANI ni tunda la HAKI.
Pasipo haki amani hutoweka hata kama tutaishikilia kwa makombora. Amani licha
ya kuonekana kuwa ni hali ya utulivu kwa nje, yaani, kimazingira, ni tokeo la
utulivu wa ndani wa kila mmoja wetu; awe mwenye hekima na akili, mjinga,
masikini au tajiri. Hivyo amani siyo kitu cha kubeza hata kidogo kama milango
ya HAKI itafungwa kwa kofuli la CHUMA. “Kwa sababu upumbavu wa Mungu
una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu,”
1Kor 1:25
Wapendwa wana wa Mungu,
Injili ya leo inatutaka tutafakari zaidi kuhusu hekima na busara tuitumiayo
ilhali tukiwa duniani hapa kwa muda huo mfupi. Ni kweli kwamba maandalizi ya
kuishi ufalme huo wa mbinguni yanaanza hapa hapa dunia kama sehemu muhimu ya
kujiandaa. Naye Yesu anatoa mfanano wa ufalme huo wa mbinguni na kusema, “Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali
kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi,” Mt 25:1. Kundi
hili la wanawali kumi ndilo lenye mgawanyiko wa wapumbavu na wenye
busara-hekima. Naam, “Watano wao walikuwa
wapumbavu, na watano wenye busara,” Mt 25:2.
Hapa tunakumbushwa kutumia vyema karama na vipaji vyetu ili siku ya mwisho
tujinyakulie ile taji, yaani UTAKATIFU ambao ndiyo cheo chako kikubwa kuliko
vyote.
Kutotumia vyema
vipaji vyako na badala yake kuishi kwa kuiga vya wengine ni kuwa kundi lile la
wapumbavu waliozima taa zao, na kutokubeba mafuta pamoja nao. Na hii ndiyo
maana ya maneno haya kwamba, “Wale
waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao; bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo
vyao pamoja na taa zao,” Mt 25:3-4. Ndugu yangu, bila cheo hicho, yaani
utakatifu wako, hutoweza kumwona Mungu aliye Mtakatifu. Na kukifikia cheo hiki
huna budi kuvitumia vyema jipaji na karama zako vizuri ungali hapa duniani kama
sehemu pekee ya kujiandaa. Vipaji hivyo ulivyojaliwa na Mungu ni kwa
kufaidiana.
Huo
ndio ufunuo wa Roho ndani yake. Hivyo, “kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa
kufaidiana,” 1Kor 12:7. Ingawa ni vipaji vyako, ila siyo mali yako. Si mali
yako kwa sababu umejaliwa na Mungu kwa ajili ya wengine pia. Na Mungu ndiye
mmiliki nawe upeazimwa kwa muda tu. Usisubiri hadi mwisho wa siku ndio uanze
kuangaika navyo wakati kengele inakaribia kugogwa-mwisho wa maisha yako hapa
duniani. Na hivi ndivyo ilivyokuwa, “Lakini
usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki,”
Mt 25:6. Hapa ndipo wale wapumbavu wanagundua hawakuwa na mafuta katika taa
zao.
“Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni
mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika,” Mt 25:8. Hakuna hofu kwa wale
wanao kutumika na kutumia vipaji vyao vyema, huku wakiuweka ubinafsi wao
pembeni, majigambo yao, na umaarufu wao usio na sifa na siha.
Na
hivi ndivyo ilivyokuwa kwamba, “wale wenye
busara wakawajibu (wapumbavu), wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi;
afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie,” Mt 25:9. Katika hali na
mazingira haya ya kuchelewa, kukurupuka kwako hakutakusaidia sana. Hapa
tunakumbushwa kutumia vyema rasilimali muda, na kuwa macho muda wote kwa yale
tuyafanyayo na tuyatarajiayo. “Na
hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari
wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa,” Mt 25:10. Maisha ya ‘mwendo
kasi’ bila umakini huu wa kutumia vizuri rasilimali muda, na umakini kwa yale
tuyafanyayo na matarajio yake, matokeo yake ni kilio na kusaga meno. Ni wazi
hapatakuwa na nafasi ya kujitetea. Na hivi ndivyo ilivyokuwa kwamba, “wakaja na wale wanawali wengine (wapumbavu),
wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie,” Mt 25:11. Kilio hiki hakitasaidia kwa
sababu tumetumia muda wetu vibaya. Bila shaka tutajibiwa hivi na Mungu, “nawaambia, siwajui ninyi,” Mt 25:12. Kumbe “Basi
kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa,” Mt 25:13. Amina.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Basi
kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa,” Mt 25:13
Tusali:-Ee Yesu, tujalie
utulivu wa ndani. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario