domingo, 31 de julio de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 18 YA MWAKA-C

JUMATATU WIKI  YA 18 YA MWAKA-C
Somo: Yer 28:1-17
Zab: 119:29, 43, 79, 80, 95, 102
Injili: Mt 14:13-21
Nukuu:
 “Ndipo nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, mbele ya makuhani, na mbele ya watu wote waliosimama ndani ya nyumba ya Bwana, naam, nabii Yeremia akasema, Amina, Bwana na atende hivi; Bwana ayatimize maneno yako uliyotabiri, kuvirudisha hapa vyombo vya nyumba ya Bwana na watu wote waliofungwa, toka Babeli, hata mahali hapa,” Yer 28:5-6 

 “Kisha nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, Sikia sasa, Ee Hanania; Bwana hakukutuma; lakini unawatumainisha watu hawa maneno ya uongo,” Yer 28:15 

Basi Bwana asema hivi, Tazama, nakutuma uende zako toka juu ya uso wa nchi; mwaka huu utakufa, kwa sababu umenena maneno ya uasi juu ya Bwana,” Yer 28:16 

Basi nabii Hanania akafa, mwaka uo huo, mwezi wa saba,” Yer 28:17

Naye Yesu aliposikia; hayo, aliondoka huko katika chombo, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao,” Mt 14:13 

Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao,” Mt 14:14

Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula,” Mt 14:16

TAFAKARI:Nabii atabiriye habari za amani, neno la nabii yule litakapotokea, ndipo nabii yule atakapojulikana, kuwa Bwana amemtuma kweli kweli.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, si jambo la ajabu leo kusikia na hata kuona mifumuko ya unabii na hata wengine kujipambanua kama manabii. Kuwa nabii siyo kitu cha kujitwalia wala kujinasibu, bali ni kuhesabiwa haki na Mungu mwenyewe tukijua kile usemacho ni ujumbe wa Mungu na umetumwa na Mungu kusema hivyo na siyo kadiri ya ndoto zako, au tafsiri zako zenye malengo binafsi. Kwa maantiki hiyo, Nabii atabiriye habari za amani, neno la nabii yule litakapotokea, ndipo nabii yule atakapojulikana, kuwa Bwana amemtuma kweli kweli,” Yer 28:9. Ni katika mizania hii tunaona nani ni nabii wa kweli kati ya Yeremia na Hanania. Hanania anatoa utabiri wa uongo kwa lengo tu la kumfurahisha mfalme kwa sababu ndicho mfalme atakacho kusikia, Yer 28:1-4.

Akijua unabii ule si wa kweli, Ndipo nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, mbele ya makuhani, na mbele ya watu wote waliosimama ndani ya nyumba ya Bwana, naam, nabii Yeremia akasema, Amina, Bwana na atende hivi; Bwana ayatimize maneno yako uliyotabiri, kuvirudisha hapa vyombo vya nyumba ya Bwana na watu wote waliofungwa, toka Babeli, hata mahali hapa,” Yer 28:5-6. Kwa kujipambanua na kuwasadikisha watu kwamba asemacho ni kweli kutoka kwa Mungu, nabii Hanania akaitwaa ile nira iliyokuwa juu ya shingo ya Yeremia, akaivunja,” Yer 28:10. Tendo hili la kuivunja nira juu ya shingo la Yeremia lilimaanisha  ndivyo Bwana atakavyoivunja nira ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, kabla haujatimia muda wa miaka miwili mizima, na kuiondoa shingoni mwa mataifa yote,’ Yer 28:11. Ni mbaya sana kujiinua nafsi yako, na hasa pale utakapo kupata sifa kutoka kwa watu na kujipendekeza kwa wakubwa na kusahau ile kweli. 

Hata hivyo Mungu huwa hamfichi mnafiki. Huyu ndiye Mungu asiye kwenda na mawimbi yetu wanadamu wala matakwa yetu binafsi. Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia, baada ya Hanania, nabii, kuivunja ile nira iliyokuwa juu ya shingo ya Yeremia, kusema,  Enenda ukamwambie Hanania, ukisema, Bwana asema hivi, Umezivunja nira za mti; lakini badala yake utafanya nira za chuma,” Yer 28:12-13. Na nira za chuma ilimaanisha kwamba, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nimetia nira ya chuma juu ya shingo ya mataifa haya yote, ili wamtumikie Nebukadreza, mfalme wa Babeli nao watamtumikia; nami nimempa wanyama wa nchi pia,” Yer 28:14. Kitendo hiki kilimaanisha kwamba, ‘wana wa Israeli hawakutaka kulijua kosa lao lililowafanya kuwa katika hali ile ya utumwa.’

Ingawa Huruma na Neema ya Mungu ipo muda wote na wakati wowote, bila kufanya toba ya kweli na majuto kumrudia Mungu, huruma na neema hiyo ya Mungu itapita tu bila kuguswa nayo. Na wale wote wenye kuupindisha ukweli wa Mungu kama ulivyo hawawezi kubaki salama. Kisha nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, Sikia sasa, Ee Hanania; Bwana hakukutuma; lakini unawatumainisha watu hawa maneno ya uongo,” Yer 28:15. Hii siyo maana ya kuwa Nabii wa Mungu kama mjumbe wake mwaminifu. Na hivi ndivyo Yeremia alivyo ufikisha unabii wa kweli kwa Hanania;  Basi Bwana asema hivi, Tazama, nakutuma uende zako toka juu ya uso wa nchi; mwaka huu utakufa, kwa sababu umenena maneno ya uasi juu ya Bwana,” Yer 28:16. Na unabii huu ulitimia kwa nabii Hanania kwani alikufa mwaka uo huo, mwezi wa saba,’ Yer 28:17

Kristo Yesu ndiye ukamilifu wa nyakati na unabii wote uliyo kwisha tangulia kabla yake. Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana,” Gal 4:4-5. Na Injili ya leo tunaona hali hiyo ya kuwa wana kwa ukarimu wa Mungu kwa watu wake. Yesu anawaonea huruma wale waliokuwa wanasikiliza neno lake la uzima. Kibinadamu wanafunzi wa Yesu wanatoa ushauri kwa Yesu kuwa watu waachwe waende zao vijini na kutafuta chakula. Yesu anawakumbusha wajibu wao kuwa yawapasa kuwalisha watu hao chakula. Hivyo Yesu anawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula,” Mt 14:16. Wapendwa katika Kristo, kwa ubatizo wetu tunashiriki ukuhani wa Kristo, unabii, na ufalme wake. Hivyo kila mbatizwa kadiri ya wito wake anajukumu la kuwapa chakula watu wale aliokabidhiwa. Na zaidi chakula hiki siyo tu hiki cha leo na kesho bali neno la uzima wa milele, ili wamjue Kristo, Mwana wa Mungu kuwa ndiye ‘Njia ya kweli, kweli isiyo shaka, na Uzima wetu,’ Yoh 14:6

Tumsifu Yesu Kristo!

Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula,” Mt 14:16


Tusali:-Ee Yesu, tuepushe na unabii na manabii wa uongo, na mara zote tubaki katika kweli yako. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario