JUMAPILI YA 22 YA MWAKA-C
Somo
I: YbS 3:17-20, 28-29
Zab/Kit: 68:4-5, 6-7, 10-11
Somo
II: Ebr 12:18-19, 22-24
Injili:
Lk 14:1, 7-14
Nukuu
“Mwanangu, wakati wa
kufanikiwa uendelee katika unyenyekevu; hivyo utapendwa kuliko mwenye ukarmu,”
YbS 3:17
Kadiri ulivyo mkuu
uzidi kujinyenyekesha, nawe utapata kibali machoni pa Bwana; kwa maana rehema
zake Bwana zi kuu, na siri yake ni kwa wanyenyekevu,” YbS 3:18-20
“Bali ninyi
mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na
majeshi ya malaika elfu nyingi,” Ebr 12:22
“mkutano
mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa
watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika,” Ebr 12:23
“Ukialikwa na mtu
arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye
kustahiwa kuliko wewe, akaja yule
aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa
haya kushika mahali pa nyuma,” Lk 14:8-9
“Bali
ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie,
Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote
walioketi pamoja nawe,” Lk 14:10
TAFAKARI:
“Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye
ajidhiliye atakwezwa,” Lk 14:11
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 22 ya mwaka “C” wa Kanisa. Masomo yetu
yote matatu yamebeba ujumbe wa ‘UNYENYEKEVU.’ Hakika mtu ufanikiwa katika mambo
yake mengi pale anapojinyenyekeza. Unyenyekevu ni msingi wa fadhila zote.
“Mwanangu, wakati wa kufanikiwa uendelee katika unyenyekevu; hivyo utapendwa
kuliko mwenye ukarimu,” YbS 3:17. Kujishusha hakumaanishi ‘UJINGA,’ bali kwa
kufungulia ufahamu wa mengi yanayokuzunguka kadiri ya wito na nafasi yako
katika jamii husika. Ni kwa mantiki hiyo kwamba, “kadiri ulivyo mkuu uzidi
kujinyenyekesha, nawe utapata kibali machoni pa Bwana; kwa maana rehema zake
Bwana zi kuu, na siri yake ni kwa wanyenyekevu,” YbS 3:18-20. Watu wote
walioacha nyuma mazuri na kukumbukwa ni wale waliojinyenyekeza katika yote
waliyokutana nayo kama jaribu.
Kinyume chake ni
kwamba, “Msiba wa mwenye kiburi hauleti kupona, mche wa uovu umepandika ndani yake,”
YbS 3:28. Kushindwa kwa wengi katika maisha na hata kile walicho kadiri ya wito
na nafasi zao utokana na kiburi. Mshahara wa kiburi ni anguko lako mwenyewe.
Kumbe nisichoke kuiomba hekima ya Mungu kila siku ili iniongoze katika busara.
Na “moyo wa busara utatambua mithali, na sikio sikivu ni tama ya mtaalamu,” YbS
3:29. Unyenyekevu utuinua pale tunapojishusha pasipo shuruti. Naye Yesu ndicho
anachotuambia, kwamba, “kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa,”
Lk 14:11
Leo katika somo la
Injili Yesu anatupa angalizo hasa tunapoalikwa kwenye tafrija mbalimbali.
Tukizama ndani zaidi tunaona kwamba uhai tulionao na maisha tunayoyaishi ni
sawa na kualikwa kwenye furaha ya Mungu na utukufu wake. Basi ni vyema mimi na
wewe kutambua duniani hapa tunapita tu, na tupo kwa maandalizi ya maisha ya
umilele. Ukweli huu wa maisha uniweke wazi kwa haya mambo matatu; maisha ni
jukumu la muda mfupi, maisha ni dhamana, na maisha ni jaribu. Na katika Injili
ya leo, Yesu anatuwasa hivi kuhusu ukweli huu wa maisha, na zaidi maisha kama
jaribu. Naye Yesu anatuambi hivi; “Ukialikwa na mtu arusini, usiketi
katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe,
akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza
kwa haya kushika mahali pa nyuma,” Lk 14:8-9.
Kama sote tumealikwa harusini ni wazi tumepewa mastahili yaliyo sawa na yule
aliyetualika. Je, kwa maanisha nini maisha ni JARIBU?
Mwelekeo huu wa maisha, yaani, maisha ni
Jaribu, huonekana katika hadithi ya Biblia yote. Wakati wote Mungu huijaribu
tabia ya watu, imani yao, utii, upendo,
ukamilifu na uaminifu wao. Mungu alimjaribu Ibrahimu kwa kumwambia amtoe
sadaka mwanae Isaka. Mungu alimjaribu Yakobo alipopaswa kufanya kazi miaka ya
ziada ili kumpata Raheli kama mkewe.
Adamu na Hawa walishindwa jaribio katika
bustani ya Edeni, na Daudi alishindwa majaribu yake kutoka kwa Mungu mara
kadhaa. Lakini Maandiko Matakatifu hutupa mifano mingi ya watu walioshinda
majaribu makubwa mfano Yusufu, Ruthu, Esta na Daniel.
Wapendwa wana wa Mungu, ukweli ni kwamba
majaribu hukuza tabia na kuiweka wazi, na maisha yote ni majaribu. Siku zote
unajaribiwa. Mungu siku zote anatazama unavyoenenda kwa watu, matatizo,
mafanikio, migongano, magonjwa, mambo ya kukatisha tamaa, hata hali ya hewa!
Mungu anaangalia hata matendo rahisi
sana kama vile unapofungulia mlango wengine, unapookota kipande cha takataka,
unapoonyesha upole kwa karani au mhudumu, unapomsikiliza mfanyakazi wako wa
nyumbani, nk.
Ndugu yangu, ukweli ni kwamba hatuyajui
majaribu yote ambayo Mungu anatupa lakini tunaweza kutabiri baadhi yake, kwa
kuzingatia Maandiko Matakatifu. Utajaribiwa kwa mabadiliko makubwa,
kucheleweshwa ahadi, matatizo magumu,
sala zisizojibiwa, lawama zisizostahili, na hata mikasa isiyo na sababu. Ndugu,
katika maisha yangu nimetambua kuwa Mungu anajaribu imani yangu kupitia
matatizo, anajaribu tumaini langu kwa njia ya mali, na anajaribu upendo wangu
kwa njia ya watu.
Jaribu la muhimu sana ni jinsi
unavyotenda unapoacha kuhisi uwepo wa Mungu katika maisha yako. Wakati mwingine
Mungu hujiondoa kwa makusudi, na hatuoni uwepo wake. Mfalme Hezekia alipatwa na
jaribu hili. "Walakini kwa Habari ya wajumbe wa wakuu wa Babeli,
waliotumwa kwake kuuliza ajabu iliyofanywa katika nchi, Mungu akamwacha, ili
amjaribu, ili kwamba ayajue yote yaliyokuwemo moyoni mwake." 2Nya 32:31.
Hezekieli akikuwa amefaidi ushirika wa karibu na Mungu, lakini kwa wakati wa muhimu sana Mungu alimwacha
peke yake ili ampime tabia yake, adhihirishe udhaifu wake, na amwandae kwa
MAJUKUMU ZAIDI. Kumbe lengo la majaribu si kutuangamiza, bali tunaandaliwa kwa
mambo makubwa zaidi, na kwa malengo makubwa zaidi ya Mungu.
Wapendwa katika Kristo, ukielewa kuwa
maisha ni jaribu, unatambua kuwa hakuna kitu kidogo katika maisha yako. Hata
tukio dogo sana lina maana kubwa katika kukuza tabia yako. Kila siku ni siku ya
muhimu, na kila dakika ni wasaa wa kukua kitabia, kuonyesha upendo, au
kumtegemea Mungu. Majaribu mengine hata huyatambui. Lakini yote haya yana
matokeo ya milele.
Habari njema ni kwamba Mungu anakutaka
ushinde mtihani huo wa maisha, kwa hiyo haruhusu majaribu unayoyapata kuwa makubwa
kuliko neema anayokupatia katika kukabili majaribu hayo."Jaribu
haliwapati ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu;
ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu
atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili." 1Kor 10:13
Mpendwa katika Kristo, kila unaposhinda
jaribu, Mungu hutambua na kupanga kukupa tuzo la milele. Mtume Yakobo anasema,
"heri mtu astahimikiye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea
taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao." Yak 1:12.
Basi ndugu yangu ninaye safiri nawe
katika tafakari hii, yakupasa kujua kuwa sote ni waalikwa na siyo ‘mgeni
rasmi.’ Kwa utaratibu wa kawaida mbele palipoandaliwa si mastahili yangu. Na
kama nitakuwa mbele nielewe nipo hapo kwa kuhesabiwa haki na yule aliyenialika.
Kama ni kiongozi katika taasisi yoyote ile, nielewe nipo hapa kwa kuhesabiwa
haki hiyo na Mungu kupitia watu wake. Hivyo nifanye yote kadiri ya utaratibu
uliopo wakati huo huo niheshimu mara zote kiapo changu kwa nafasi ile
niliyohesabiwa haki na Mungu kwa kupitia watu wake kwa utaratibu tuliojiwekea.
Hali na mazingira haya yanifanye nizame
ndani zaidi na kuyaona maisha kama jukumu la muda mfupi. Wito huu unikumbushe
mara zote kufanya yale yanayo mpendeza Mungu kuelekea maisha yale ya milele.
Pili, nione ukweli wa maisha na nafasi niliyopewa na watu kuwa ni dhamana.
Ukweli huu unikumbusha mara zote niwapo mbele nipo kwa kuhesabiwa haki kama
kiongozi katika taasisi yoyote ile. Nielewe nimepewa uwakili na siku ya mwisho
itanipasa kutoa hesabu yake. La sivyo na kama hili silifahamu vizuri, ni vyema
na busara kutafuta nafasi nyingine. Na ndivyo Yesu anavyotuambia ili kuwa
sehemu salama zaidi, “Bali
ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie,
Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote
walioketi pamoja nawe,” Lk 14:10. Huku ndiko kwa maneno mengine kupungua ili
Mungu awe na nafasi juu ya maisha yako. Na huu ndiyo unyenyekevu utakao
kupandisha pale unapojishusha.
Ndugu yangu uliyesafiri
nami katika tafakari hii utakubaliana nami kwamba kati yetu kwa nafasi
tulizokuwa nazo na madaraka tuliyonayo yaliyopitiliza hututia upofu na
kutufanya kuwa ndiyo fimbo ya kuchapia wengine. Jeuri hii ndugu yangu tunaipata
wapi wakati Maandiko Matakatifu yanatuambia, “Siku
za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi
chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara,” Zab 90:10.
Jinyenyekeshe basi na kuwa kile Mungu alichokusudia katika maisha yako. Kwa
nini basi wajifananisha na Mungu asiye jaribiwa? Je, wajua idadi ya nywele zako
kichwani? Kama hujui mipaka yako kitazame kifo. Na kama huna hofu ya kifo kwa
kiburi chako, tafakari kwa kina tendo la usingizi/kulala. Hili ni zoezi la
Kifo. Wengi wetu hulala kama kawaida na mara hukosa fursa ya kuamka tena. Je,
hata usingizi siyo jaribu kwako kwamba wewe si lolote wala chochote?
Na
swali la kujiuliza ni hili: Je, mwisho wa hayo yote ni nini? Kama mimi na wewe
sioni maisha ni JARIBU, kujishusha itakuwa vigumu sana. Pasipo unyenyekevu
nitegemee anguko langu binafsi. Na huku ndiko kupoteza lengo la Maisha kuelekea
ule ukamilifu, Mt 5:48-(utakatifu) kama cheo chetu, na mwisho kutokuurithi
ufalme wa mbinguni. Mwenye hofu ya Mungu ataweza kuepuka anguko lake binafsi.
Na huu ndio wa Mungu kwako na kwangu. “Bali
ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa
mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi,” Ebr 12:22. Hili ndilo Kanisa la
wateule yaani, watakatifu. Ni “mkutano mkuu na Kanisa la wazaliwa wa kwanza
walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye
haki waliokamilika,” Ebr 12:23. Ndugu yangu uwapo hapa duniani, “itamfaidia mtu
nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?” Mk 8:36. Tumtazama
Yesu aliye kielelezo chetu. “Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya
kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili,” Ebr 12:24. Huyu ndiye kila
kitu kwako na kwangu. Tujifunze kwake.
Tembo kwa umbo lake
huweza kuyala majani yaliyo juu ya mti na hata yatambaayo chini ardhini. Kwa
uwezo wa mdomo wake, Tembo huyafuruga maji kabla ya kuyanywa. Na sababu kubwa
ya kufanya hivyo ni kuvifukuza mbali vile vyote ‘atarishi’ kwa afya na maisha
yake akiwemo chura.
Lakini pamoja na ukweli
huu juu ya Tembo, ‘SISIMIZI’ kwa umoja wao huweza kumwangusha tembo na kumfanya
kitoweo, na hata jumba la muda tu la kuishi. Kumbe pamoja na ukubwa alio nao
Tembo, uwepo wa SISIMIZI umkumbusha namna ya kutembea vizuri.
Ndugu yangu, kama
ilivyo kwamba hakuna lililo dogo katika maisha, ndivyo hivyo hivyo hakuna aliye
mdogo kama sote tunaishi pamoja katika kweli na haki. Hawa wadogo katika udogo
wao wanaweza kuwa sababu ya wewe kutolifikia lengo lako hata kama nia unayo.
UNYENYEKEVU ndiyo msingi wa fadhila zote.
Na ndivyo Yesu anavyotutaka tufanye katika unyenyekevu na utu wa kweli,
mwamba, “Ufanyapo chakula cha mchana au cha
jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako
wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo,” Lk 14:12. Tuwe tayari hata kuwaalika mahasimu wetu. Huku
ndiko kukomaa kimwili na kiroho.
Na kwa namna nyingine Yesu anatuambi, “Bali ufanyapo karamu
waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri,
kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye
haki,” Lk 14:13-14. Hawa ni wale wote wasio na sauti katika jamii. Nao
wana haki ya kuishi kama wewe unavyoishi kwa kupenda mno starehe, anasa na
tafrija. Kufikia kipimo hiki katika maisha kutakuitaji unyenyekevu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Moyo wa busara utatambua mithali,
na sikio sikivu ni tama ya mtaalamu,” YbS 3:29
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, tujalie fadhila ya Unyenyekevu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario