JUMAPILI YA 21 YA MWAKA-C
Somo
I: Isa 66:18-21
Zab/Kit: 117:1, 2
Somo
II: Ebr 12:5-7, 11-13
Injili:
Lk 13:22-30
Nukuu
“Nami
nayajua matendo yao na mawazo yao; wakati unakuja nitakapokusanya mataifa yote
na lugha zote; nao watakuja, nao watauona utukufu wangu,” Isa 66:18
“Nami
nitaweka ishara kati yao, nami nitawatuma hao waliookoka kwa mataifa, watu
wasioisikia habari yangu, wala kuuona utukufu wangu; nao watahubiri utukufu
wangu katika mataifa,” Isa 66:19
“Ni kwa ajili ya
kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi
asiyerudiwa na babaye?” Ebr 12:7
“Kila
adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini
baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani,” Ebr 12:11
“Mtu mmoja
akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache?” Lk 13:23
“Jitahidini
kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi
watataka kuingia, wasiweze,” Lk 13:24
TAFAKARI:
“Wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa
mwisho.”
Wapendwa
wana wa Taifa la Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya ‘21’ ya mwaka
‘C’ wa Kanisa. Masomo ya leo yanatualika kila mmoja wetu atafakari kwa kina
mwenendo wa maisha na wito wake. Mwenendo huo wa maisha ndiyo sababu na kigezo
cha kuwa wa ‘kwanza au wa mwisho.’ Hata hivyo hatuwezi kusahau kwamba lengo la
kuumbwa kwetu kwa sura na mfano wake Mungu, ni kuishi milele. Kwa hiyo Mungu
anakutakia maisha ya milele. Mungu kama mwalimu lengo lake ni mimi na wewe
tufaulu na kuwa wa kwanza. Ni mwalimu wa pekee na waajabu ambaye hufurahia
kushindwa kwa wanafunzi wake.
Kwa
maneno mengine, kushindwa kwa mwanafunzi kwa maana nyingine kwa weza dhihirisha
pia kushindwa kwa mwalimu. Kufaulu mtihani wa maisha kwa tegemea sana maisha
yanayoongozwa na malengo. Na kufikia lengo lolote lile katika maisha kunaitaji
“nidhamu” kama kiungo muhimu sana. Licha ya nidhamu kukuweka katika mstari
sahihi kuelekea pale unapopataka, nidhamu hiyo hiyo ukuwajibisha pia pale
unaporegea. Na nidhamu hii ndiyo aizungumziayo Yesu na kusema, “Jitahidini kuingia
katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka
kuingia, wasiweze,” Lk 13:24. Hivyo hakuna yeyote kati yetu asiyependa
mafanikio mazuri katika maisha. Hata hivyo kuyapata na kuyafikia mafanikio hayo
mazuri kutakuitaji “nidhamu na maadili” kwa kile ukichuchumiliacho.
Nidhamu na maadili ndicho kiongoza njia
cha kufika pale unapopatamani. Nidhamu na maadili mema katika maisha
hutustahimilisha hata pale tunapokata tamaa na kukosa mwelekeo kama tokeo la
sintofahamu katika maisha. “Ni
kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana
yupi asiyerudiwa na babaye?” Ebr 12:7. Nidhamu na maadili mema hukupa maana na
ufahamu wa maisha unayoyaishi leo kama tokeo la jana, na kesho kama tokeo la
leo. Kwa mantiki hii ya nidhamu na maadili katika maisha, “Kila
adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini
baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani,” Ebr 12:11.
Maisha yenye nidhamu na maadili mema humjenga mtu mwili na roho. Kumbe si vyema
sana kujionea huruma na kulalama kwa mambo ambayo yapo chini ya uwezo wako
kubadilika na kusonga mbele katika furaha ya kweli. “Kwa
hiyo inyosheni mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza, mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka,
ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe,” Ebr 12:12-13.
Ndugu yangu, licha ya kwamba baadhi ya vidonge vya malaria ni vichungu,
twawajibika kuvimeza kwa sababu tunataka kupona.
Hivyo
kwa kulifikia lengo la juu la maisha yako ya Kiroho na Kimwili, na kwa kutumia
lugha ya picha ya Yesu, ni lazima wewe na mimi
kujitahidi kila siku kuingia katika mlango ulio mwembamba. Hii ni
nidhamu na maadili katika maisha yenye kuongozwa na malengo. Bila shaka wembamba
wa mlango huu ni mwaliko wa kuishi kadiri ya yale yanayompendeza Mungu kila
mmoja kadiri ya wito wake. Ni kuishi upendo wa Mungu Baba kweli na kuwa na hofu
ya Mungu kwa kushika na kuziishi vyema amri za Mungu na Kanisa lake kama
familia yake. Utii katika amri za Mungu ni kumpenda Mungu pasipo shaka. “Mkinipenda,
mtazishika amri zangu,” Yoh 14:15. Kuzishika na kuishi katika amri zake ni
pamoja na kutambua ukweli huu kwamba kwa kupitia Mwanaye Mpendwa Yesu Kristo
tutaiona njia ya kuelekea kwake, tunapata uzima wa kweli, na ndani na katika Kristo
mwanaye ndipo penye ukweli wa Mungu Baba na maisha ya umilele.
Utabiri
na ahadi ya Mungu kama tulivyosikia kutoka somo letu leo la kwanza unakamilika
ndani na katika Kristo Yesu. “Nami
nayajua matendo yao na mawazo yao; wakati unakuja nitakapokusanya mataifa yote
na lugha zote; nao watakuja, nao watauona utukufu wangu,” Isa 66:18. Utukufu
huu wa Mungu ni “ISHARA” ambayo Mungu ataiweka kati yetu nyakati zitakapotimia. “Nami
nitaweka ishara kati yao, nami nitawatuma hao waliookoka kwa mataifa, watu wasioisikia
habari yangu, wala kuuona utukufu wangu; nao watahubiri utukufu wangu katika
mataifa,” Isa 66:19. Ishara hii kwa wakati utakapotimia ndiye NENO aliyefanyika
mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Naye Mtume Paulo anaelezea ishara hii kwa
kusema, “Hata
ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na
mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi
awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana,”
Gal 4:4-5. Kupata kupokea hali ya kuwa wana wa Mungu, ni kuwa na uwezekano wa
neema na kweli ndani na katika Kristo Yesu. “Kwa kuwa torati
ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,”
Yoh 1:17
Yesu
anathibitisha ukweli huu kwa kusema, “Mimi ndimi njia, na kweli, na
uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Hivyo, ukweli wa
Kristo na Mungu tunaupata katika Maandiko Matakatifu, uzima wake tunaupata
katika Masakramenti, na njia ya wokovu wetu ni Utukufu tuupatao kupitia njia
aliyoichagua, yaani, Msalaba. Hivyo tunampenda Mungu tunapolishika vyema neno
lake. Yesu anatuambia ukweli huu kwa kusema, “Mtu
asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu,
ila ni lake Baba aliyenipeleka,” Yoh 14:24. Kuishi upendo wa kweli, kuzitii na
kuzishika amri za Mungu na Kanisa, na kuwa na hofu ya Mungu katika yale yote
tunayofikiri, tenda, na kuishi ndiko kuchaguliwa kwetu toka asili. “Na
wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao
akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza,” Rum 8:30.
Hii ndiyo sababu ya
kuchagua kutuumba kwa sura na mfano wake. Mungu
anapenda tuwe wakamilifu kama Yeye alivyo Mkamili. “Basi ninyi
mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48.
Hii ndiyo furaha ya Mungu kwetu. Mungu hupenda kufanya kazi na wale wampendao
pasipo shaka yoyote. Mtume Paulo anathibitisha jambo hili kwa kusema, “Nasi
twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao
katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake,” Rum 8:28. Kila
mwenye hofu ya Mungu ndani yake ameitwa kwa kusudi lake. Ni vyema ukaanza sasa
kuelewa ukweli huu ndani yako na kuishi kadiri Mungu apendavyo.
Katika safari hii ya kuelekea
uzima wa milele tumepewa Roho wa Mungu kutuongoza katika kweli na haki na
kutusaidia katika udhaifu wetu kama wanadamu. “Kadhalika Roho naye
hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho
mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa,” Rum 8:26. Hatuombi jinsi
ipasavyo kwa sababu tunaomba kwa ajili ya tamaa zetu na mara tupatapo kile
tulichokiomba tunatumia vibaya. Ombi la mtindo huu haliwezi jibiwa kwa sababu
hatumruhusu Roho atuongoze. Mtume Yakobo anatupa sababu ya kushindwa kwetu. “Hata
mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu,”
Yak 4:3. Mungu anatupenda kweli na hutupatia yale tuombayo kadiri ya mahitaji yetu. Hivyo hatupaswi kuwa na
mashaka mara tumwendeapo na kuomba yale tunayohitaji.
Mashaka katika maishi
hututia hofu na mwisho wa siku tunatawaliwa na mambo mengi na yasiyo ya msingi
na kukosa dira ya malengo ya maisha yetu hapa duniani. Katika injili tunamwona
mtu mmoja mwenye mashaka anamuuliza Yesu, “Je! Bwana, watu wanaookolewa ni
wachache?” Lk 13:23. Jibu la Yesu linaturudisha kwenye msingi na malengo ya
maisha yetu hapa duniani kama nilivyokwisha elezea hapo mwanzo. Yesu anatujibu
kwa pamoja hasa sisi tulio na mashaka, “Jitahidini kuingia katika
mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia,
wasiweze,” Lk 13:24. Mlango huu mwembamba unatuwajibisha kujua lengo la maisha
yetu hapa duniani, namna ya kuishi ili kufikia lengo hilo, na ni mambo gani ya
msingi yatupasa kuyapa umuhimu katika maisha.
Tusipozingatia jambo
hilo kama nilivyokwisha elezea hapa mwanza, tusishangae siku ya mwisho kuambiwa
maneno haya. Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio
wafanyaji wa udhalimu,” Lk 13:27. Udhalimu wa kwanza kwa mtu utakuwa hali ile
ya kutokutumia muda wake vizuri na neema anazopatiwa bure na Mungu kupitia Mama
Kanisa. Tutashangaa na kupigwa butwaa tutakapoona wale waliotumia vyema muda
wao na neema walizojifunua kwao wakiingia katika maisha ya umilele. Wengi wao
ni wale leo tunaowaona wa mwisho kwa kila kitu kwa sababu tu hawaendani na
mambo ya ulimwengu huu na tamaa zake. “Na tazama, wako walio wa
mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho,” Lk 13:30.
Ndugu yangu tuliyesafiri sote katika tafakari hii, ni wakati sasa wa kuzama
ndani yako na kuhoji nafsi yako kwa hili Yesu alilotuambia leo. Je, lina ukweli
wowote juu ya maisha yako?
Ndugu yangu tuliosafiri
sote katika tafakari hii, ngoja nikuache na kisa hiki. Pamoja na Fisi kupewa
majina mengi na wakati mwingine yenye kuendana na tabia yake, kwa mfano, “Bwana
usafi wa pori,” yapo mambo mengine mazuri tuwezayo kujifunza kutoka kwa fisi.
Je, huamini?
Fisi amwonapo mtu
akitembea huku akiirusha mikono yake mbele na nyuma, tendo hilo humjengea
matumaini kwamba ukono ule upo mbioni kudondoka. Hivyo bila kukata tamaa Fisi
uongozana na mtu huyu kwa kitambo kirefu.
Jambo lingine kama
tabia ya Fisi ni hali ile ya kutokushindwa kwa urahisi hasa kwa yale yaliyo
chini ya uwezo wake. Ukweli huu tunaupata kutoka mazungumzo ya watu
wanapoonyesha hali ya mshangao wa kitu kwa njia ya swali, kuwa “mfupa
ulimshinda fisi mwanadamu atauweza?”
Ni kweli kabisa wewe na
mimi tuna mapungufu yetu kama mwanadamu, yaani, mwenye damu na mifupa. Hata
pamoja na ukweli huo, hatupaswi kuyachukulia mapungufu hayo kama ukuta kwa
kutokuona mbele na mwisho wa yote. Kumbe ni wakati wa kuyatumia yale yaliyo
chini ya uwezo wetu ili kulifikia lile lengo sahihi la maisha yetu-uzima wa
milele. Hapa ndipo tunapoitaji nidhamu na maadili mema. Na hivi ndivyo tupasavyo
kuichagua njia ile nyembamba ili kulifikia lengo.
Ni kutumia kwa
ukamilifu yale machache tuliojaliwa na Mungu licha ya udhaifu tulio nao kama
wanadamu. Huku ni kulenga katika ukamilifu licha ya udhaifu. Nisipojitajidi
katika hili, nijiandae kwa mshangao huu siku ya mwisho kwamba “wako walio wa
mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.”
Tumsifu Yesu Kristo!
“Jitahidini
kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi
watataka kuingia, wasiweze,” Lk 13:24
Tusali:-Ee
Yesu, tujalie ustahimilivu katika maisha yetu kila mmoja kadiri ya wito wake.
Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario