ALHAMISI
WIKI YA 20 YA MWAKA-C
Somo: Eze 36:23-28
Zab/Kit: 51:12-13, 14-15, 18-19
Injili: Mt 22:1-14
Nukuu
“Nami
nitalitakasa jina langu kuu, lililotiwa unajisi katika mataifa, mlilolitia
unajisi kati yao; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, asema Bwana
MUNGU, nitakapotakaswa kati yenu mbele ya macho yao,” Eze 36:23
“Maana
nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na
kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe,” Eze 36:24
“Ufalme wa
mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi,” Mt 22:2
“Akawatuma
watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja,” Mt 22:3
“Basi enendeni
hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini,” Mt 22:9
“Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache,”
Mt 22:14
TAFAKARI: Mungu hapendi upotee.
‘Maana
nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na
kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe.’
Wapendwa wana wa
Mungu, ikiwa wewe na mimi leo ni tokeo la upendo wake Mungu, na ndivyo
ilivyompendeza kutuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27, Mungu hapendi upotee.
Naye asema, ‘nitawatwaa
kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha
katika nchi yenu wenyewe.’ Hakika Mungu
aliyaona mateso ya wana wa Israeli na kusema ‘kwa sasa inatosha.’ “Nami nitalitakasa jina langu kuu, lililotiwa
unajisi katika mataifa, mlilolitia unajisi kati yao; nao mataifa watajua ya
kuwa mimi ndimi Bwana, asema Bwana MUNGU, nitakapotakaswa kati yenu mbele ya
macho yao,” Eze 36:23. Mateso ya mwenye haki ni mateso pia ya Mungu kwa sababu
haki ina Yeye. Vita ya haki juu ya mwenye haki, binadamu mvunja haki na mwenye
kuzikanyaga haki za wengine, hatoweza kushinda vita hiyo na hatosalimika katika
mkono wa Mungu.
Wenye haki na walio na
hofu na Mungu husitawi daima katika mikono salama ya Mungu. Maana Mungu asema
hivi juu yao, “nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa
katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe,” Eze 36:24. Kumbe
kiburi cha mwenye jeuri itokanayo na wingi wa nguvu alizonazo siyo zuiyo la
Mungu kuwapigania wana wake waliodhulumiwa katika kweli na haki. Kwa nini basi
twapenda wengine kuishi kama wakiwa katika ulimwengu huu ambao Mungu aliumba
ili ukaliwe na watu bila kujali mila, rangi, na desturi zetu? Wewe ni nani basi
usiyetaka wengine wapumue? Na haki hiyo ya kuwa wewe tu unaipata wapi, na kwa
kibali cha nani? “Maana Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye
aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa,
aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine,” Isa 45:18.
Pamoja na historia zetu mbaya na hata wakati mwingine kumuasi Mungu kwa dhamiri
zetu, bado Mungu anatupenda kama tulivyo.
Na
hata katika udhaifu huu wetu wa kibinadamu Mungu anatuhaidia utakaso na upya
ndani yetu, na kusema, “Nami
nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu
wote, na vinyago vyenu vyote,” Eze 36:25. Hakuna asiye na kinyago chake katika
maana ya ‘dhambi dola’ kwake. Dhambi
dola ni dhambi ile ambayo kila mara ujikuta umedondoka tena na tena. Ni dhambi
ambayo bila shaka kila mara huiungama. Dhambi hiyo ni tawala kwako kama ilivyo
dola ya taifa fulani. Hiki huwa kinyago kwako kwa sababu ndiyo mwonekano wako
wa nje na wenye kuififisha sura ya Mungu ndani mwako. Kumbuka umeumbwa kwa sura
na mfano wake Mungu, Mwa 1:27. Hivyo una chapa ya Mungu ndani yako. Hata katika
hali hii Mungu yupo tayari kukutakasa na kutoka katika kinyago hicho.
Utakaso huu ni nguvu
ile ya Mungu ndani yetu, yaani, “nguvu wezesha, nguvu thubutu.” Nguvu hii ndiyo
anayoisema Mungu kwamba, “Nami
nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo
wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nguvu hii
utuwezesha kuzipokea zile neema atujaliazo Mungu kutimiza yale ya kimungu. Uwezo huu siyo kwa nguvu na bidii zetu
wanadamu, bali ni Mungu mwenyewe kama asemavyo kwamba, “Nami
nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika
hukumu zangu, na kuzitenda,” Eze 36:27. Hizi ndizo neema za Mungu ndani yetu na
zenye kutuwezasha kuyafanya yote ndani na katika Mungu kama wana na warithi
wake. Furaha ya Mungu ni kwa kila mmoja wetu kuwa kile alichoumbwa na mwisho wa
siku kufikia sababu ya kuumbwa kwake, yaani, ‘amjue Mungu, ampende Mungu,
amtumikie Mungu, na mwisho arudi kwake Mbinguni.’ Ni katika maana hii Mungu
anasema, “Nanyi
mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami
nitakuwa Mungu wenu,” Eze 36:28
Upendo huu wa Mungu na
ukarimu wake kwetu wa kushirikisha kila mmoja wetu katika Furaha na Utukufu
wake, Yesu anaufananisha na “mfalme
mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi,” Mt 22:2. Lakini jambo la ajabu ni kwamba
licha ya mfalme huyu kuwaalika watu bure na bila kadi kama ilivyo mazingira
yetu ya leo, hakuna aliyeitikia mwaliko ule kati ya wale walioalikwa kuja
arusini, Mt 22:3. Hata hivyo, kwa kujali
sherehe ile na nafasi ya wale walioalimwa, mfalme hakuacha kusisitiza umuhimu
wa sherehe ile na yale aliyoyaandaa kwa ajili ya wale walioalikwa. Naye Mfalme “Akatuma tena watu kwa wengine,
akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng'ombe
zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini,”
Mt 22:4. Mwaliko huu tunaweza kuufananisha na Sakramenti ya Ubatizo. Kwa
Sakramenti hii ya ubatizo sote tunaalikwa na tunafanywa wana na warithi wa
ufalme wa Mungu. Hata hivyo, bila utayari wetu wa kuziishi ahadi hizo za ubatizo
tutapigwa mshangao kuikosa nafasi hiyo ya kuurithi ufalme wa Mungu.
Ni mara ngapi tunaona
licha ya mtu kupokea Sakramenti hii ya ubatizo anaishi kivyake vyake? Hawa ni
wale wanaozungumziwa katika Injili ya leo kwamba, “Lakini
hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake; nao waliosalia wakawakamata watumwa
wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua,” Mt 22:5-6. Ni mara ngapi tunawaona
Wakristo wenzetu na wabatizwa kutenda matendo yasiyoendana na Ukristo wao? Hii
ni huzuni kubwa kwa Kristo aliyekufia pale Msalabani ili uwe huru kutoka utumwa
wa dhambi, na masikitiko makubwa kwa Mungu tunaposhindwa kuthamini sadaka ya
Mwanaye Mpenzi aliyoitoa pale Msalabani kwa ulimwengu mzima. Na ni kwa “jinsi
hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu
amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele,” Yoh 3:16. Jionee mwenyewe
Mungu asivyopenda upotee!
Hata hivyo kwa ukatili
walioonyesha wale walioalikwa na kwa dhamiri zao kwenda kinyume na ukarimu ule
wa mfalme kwa kuwatenda jeuri watumwa wake na kuwaua, “yule
mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale,
akauteketeza mji wao,” Mt 22:7. Ni wazi kabisa kwamba kila mtu atawajibika kwa
matendo yake kwa sababu ni tokeo la matumizi ya uhuru ulio ndani yako. Je,
Mfalme na kwa mazingira haya anaye mwakilisha Mungu, atasitisha harusi yake kwa
vile walioalikwa hawakwenda? Mt 22:8. La hasha! Ukweli ni kwamba huruma,
upendo, na neema za Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Karamu ya Mungu itafanyika na wengine
wataalikwa hata kama hawakuwa katika mpango mzima wa kile kilichoandaliwa. Na
hivi ndivyo alivyofanya Mfalme na kuwaambia watumwa wake, “Basi enendeni hata njia panda za barabara, na
wote mwaonao waiteni arusini,” Mt 22:9. Bila shaka ndivyo Mungu atakavyofanya
tunapoupuuzia mwaliko wake. Hapa ni pale Mungu anapotukusanya wote bila kujali
mapungufu yetu. Kwa upande wako na mimi ni lazima nione tendo hili kuwa ni
Upendo wa pekee wa Mungu kwangu, na
wakati wa kubadilika na kuthaminisha fursa hiyo ya pekee kama nafasi ya
kubadilika kwa kuwa hayakuwa mastahili yangu.
Na hivi ndivyo ilivyokuwa,
kwamba, “Watumwa wale wakatoka wakaenda
njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni,” Mt
22:10. Kundi hili linamfanano na ‘juya lile lililotupwa
baharini likakusanya samaki wa kila namna, na hata lilipojaa lilivutwa pwani na
ndipo walipotengwa walio wema chomboni na wabaya wakatupwa, Mt 13:47-48.’ Na
hapa ndipo tunapopata maana halisi ya hatua aliyoichukuwa mfalme alipoingia
kwenye ukumbi wa sherehe. Na hali ilikuwa hivi, “lakini
alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja
asiyevaa vazi la arusi,” Mt 22:11. Huyu jamaa aliyegundulika kutokuvaa vazi la
arusi hakutumia vyema nafasi ile aliyokirimiwa bila mastahili yake katika
kuyaondoa mapungufu yake. Huyu ni sawa na muumini aliyepata nafasi ya
kuhudhuria maadhimisho ya Misa Takatifu, mazingira ambayo kabla ya Misa ile
Takatifu kulikuwa na nafasi ya kupokea Sakramenti ya upatanisho, naye asiitumie
nafasi hiyo ilhali anajua hakuwa mkamilifu. Na kinyume chake kutaka kushiriki
meza ya Bwana katika hali hiyo ya dhambi.
Ingawa hatumuoni Kristo
katika hali ya kushikika zaidi ya maumbo yale ya mkate na divai, elewa Kristo
anakuambia kama mfalme huyu alivyomwambia ndugu huyu kwamba, “Rafiki,
uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi?” Mt 22:12. Je, katika hali na
mazingira kama hayo wataka malaika washuke na kukukumbusha wajibu wako huo kama
Mbatizwa? Bila shaka alivyotendewa mtu yule nasi tutatendwa hivyo hivyo kwa
amri ya mfalme na kufungwa ‘mikono na miguu, kutolewa na kutupwa katika giza
la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno,’ Mt 22:13. Na hii ndiyo maana ya
maneno haya kwamba, “waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache,” Mt
22:14. Kwa Sakramenti ya Ubatizo sote tunaitwa kuwa wana na warithi wa Ufalme
wa Mungu. Ila kuteuliwa kwetu na kuingia katika Ufalme huo kutategemea kuishi
vyema ahadi zetu za ubatizo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Rafiki, uliingiaje humu nawe huna
vazi la arusi?” Mt 22:12
Tusali:-Ee
Yesu, nijalie neema ya kuishi vyema ahadi zangu za ubatizo, ili mwisho wa siku
zangu
hapa duniani nisije nikapigwa na mshangao. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario