jueves, 1 de septiembre de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 22 YA MWAKA-C

IJUMAA WIKI YA 22 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 4:1-5
Zab/Kit: 37:3-4, 5-6, 27-28, 39-40
Injili: Lk 5:33-39
Nukuu
Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu,” 1Kor 4:1 

Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu,” 1Kor 4:2

 “Nao wakamwambia, Wanafunzi wa Yohana hufunga mara nyingi, na kuomba dua; na kadhalika wanafunzi wa Mafarisayo; lakini wanafunzi wako hula na kunywa!” Lk 5:33 

Lakini Yesu akawaambia, Je! Mwaweza kuwafanya wafunge walioalikwa arusini, akiwapo bwana arusi pamoja nao?” Lk 5:34 

Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi, ndipo watakapofunga siku zile,” Lk 5:35 

 “Lakini divai mpya sharti kutiwa katika viriba vipya,” Lk 5:38

Wala hakuna anywaye divai ya kale akatamani divai mpya; kwa kuwa asema, Ile ya kale ndiyo iliyo njema,” Lk 5:39

TAFAKARI: Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu.”

Wapendwa katika Kristo, Yesu anapotoa mfano wa vazi kuukuu na jipya, na kwa upande mwingine divai ya zamani na kiriba kipya anataka kutufundisha jambo hili; “kwanza kabisa lazima tujue sababu na malengo ya maisha yetu hapa duniani.” Hatupo hapa duniani kwa bahati mbaya hata kidogo. Tupo katika ulimwengu huu kadiri ya mpango wa Mungu ambao ni dhahiri na mathubuti. Hivyo lolote lile lililo jema mbele ya Mungu huwiishwa na kufanya upya. Katika Injili ya leo tunaona watu wakimletea Yesu malalamiko juu ya kufunga na kuomba.

 Kufunga kwetu na kuomba kwetu uifaidia kwanza kabisa roho zetu na wenzetu. Tunawajibu huo kiimani, na yatupasa kuutekeleza pasipo shaka. Ndiyo maana Yesu anawauliza watesi wake swali hili: “Je! Mwaweza kuwafanya wafunge walioalikwa arusini, akiwapo bwana arusi pamoja nao?” Lk 5:34. Maisha yapaswa kusherehekewa kwa sababu ni mali na zawadi ya Mungu.

Hivyo basi, upya wetu kiimani hutoshelezwa na upya tuupokeao kwa Yesu tunaposhiriki Masakramenti yake tukiwa katika hali ya usafi. Hivyo “divai mpya sharti kutiwa katika viriba vipya,” Lk 5:38. Ndani na katika Kristo kiimani hujengeka kwa matendo madogo madogo yanayompendeza Mungu. Wala hakuna anywaye divai ya kale akatamani divai mpya; kwa kuwa asema, Ile ya kale ndiyo iliyo njema,” Lk 5:39. Ndugu yangu ukiona vinaelea ujue vimeundwa. Je, tufanye nini ili enende katika Kristo na ndani ya Kristo?

Kama tunajua kwamba hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake, Rum 14:7, maisha yetu bila Kristo yatakuwa na walakini mkubwa. Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu,” 1Kor 4:1. Kama tu watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za Mungu, maisha yako hapa duniani na kadiri ya wito wako ni dhamana kubwa kwa sababu yeshathaminishwa kwa damu ya Yesu pale Msalabani. “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Je, watambua thamani ya maisha yako kama mfuasi wa Kristo?

Wapendwa wana wa Mungu, thamani ya Ukristo wako itategemea sana na mamna unavyo mwakilisha Kristo kama wakili wake katika kweli na uaminifu. Ukristo wako usibaki katika jina tu, bali imani ya kweli ndani yako, na Kristo akiwa ndiye kielelezo chako katika yote. Na hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu,” 1Kor 4:2. Ni kuwa mwaminifu katika kuifuata njia yake, yaani, kuubeba msalaba wako kwa uaminifu bila kumsaliti Kristo. Ni kuiishi kweli kadiri ya mafundisho yake Kristo, na zaidi amri ile ya upendo.

Ukipenda kama alivyopenda Kristo utafanya yote yampendezaye Mungu. Na mwisho ni kuuishi uzima wa kweli kwa kushiriki Masakramenti katika hali ya usafi wa moyo, na hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Hali hii ya usafi wa moyo ndiyo impelekeayo Mtume Paulo kusema kwamba, Lakini, kwangu mimi, si kitu kabisa nihukumiwe na ninyi, wala kwa hukumu ya kibinadamu, wala sijihukumu hata nafsi yangu,” 1Kor 4:3. Mara zote tuongozwe na dhamiri safi na yenye hofu ya Mungu. Maana sijui sababu ya kujishitaki nafsi yangu, lakini sihesabiwi haki kwa ajili hiyo; ila anihukumuye mimi ni Bwana,” 1Kor 4:4.

Kuujua wajibu wako na kuutimiza kadiri ya takwa lake na kwa upendo ndiko kutakapo kuhesabia haki. Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu,” 1Kor 4:5. Ndugu yangu, usichoke kutimiza wajibu wako kwa upendo. Hakuna aliyefilisika kwa kupenda na kutoa kwa upendo.

Tumsifu Yesu Kristo!

Lakini divai mpya sharti kutiwa katika viriba vipya,” Lk 5:38


Tusali:-Ee Yesu, tujalie neema ya kutimiza wajibu wetu kwa upendo. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario