viernes, 6 de noviembre de 2015

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 31 YA MWAKA-B

JUMAMOSI WIKI YA 31 YA MWAKA-B
7/11/2015
Somo: Rum 16:3-9, 16, 22-27
Zab: 145:2-3, 4-5, 10-11
Injili: Lk 16:9-15
Nukuu:
Sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara, sawasawa na injili yangu na kwa kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na ufunuo wa ile siri iliyositirika tangu zamani za milele,” Rum 16:25

Ndiye Mungu mwenye hekima peke yake. Utukufu una yeye kwa Yesu Kristo, milele na milele. Amina,” Rum 16:27

Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia,” Lk 16:10

Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali,” Lk 16:13

Akawaambia, Ninyi ndinyi mnaojidai haki mbele ya wanadamu, lakini Mungu awajua mioyo yenu; kwa kuwa lililotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu,” Lk 16:15

TAFAKARI: “Moyo usio na shukrani ukausha mema yote. Na mshika mawili kwa pamoja, moja humponyoka.”

Wapendwa wana wa Mungu, masomo yetu ya leo yanatuelekeza kuyatafakari haya: “Moyo usio na shukrani ukausha mema yote. Na mshika mawili kwa pamoja, moja humponyoka.” Barua ya Mtume Paulo kwa Warumi ambayo leo tunaisoma sehemu ya mwisho, inatukumbusha umuhimu wa tendo la shukrani. Mtu hutoa shukrani kwa kuthamini kile alichotendewa au kusaidiwa. Mtu atoapo shukrani kwa yeyote yule, tendo hilo hubadilika na kuwa ombi. Moyo huu wa shukrani uboresha na kustawisha mema uliyotenda au tendewa. Tendo la Shukrani linapotolewa kwa Mungu na kwa moyo thabiti, huwa na tokeo la neema na baraka. Moyo thabiti katika kutoa shukrani upimwa na kile umtoleacho Mungu katika ubora wake.

Mfalme Daudi alimtokea Mungu shukrani yake yenye thamani ya juu kuliko vyote. Naye Mfalme Daudi anasema, wala sitamtolea Bwana, Mungu wangu, sadaka za kuteketezwa nisizozigharimia. Hivyo Daudi akakinunua hicho kiwanja cha kupuria na wale ng'ombe kwa shekeli hamsini za fedha,” 2Sam 24:24b. Tokeo la moyo wa shukrani kwa thamani ya kile tumtoleacho Mungu ni neema na baraka. Daudi anazipata neema hizi na baraka kutoka kwa Mungu. “Naye Daudi akamjengea Bwana madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Basi Bwana aliiridhia nchi, na tauni ikazuiliwa katika Israeli,” 2Sam 24:25. Hivyo moyo wa shukrani uboresha na kustawisha mema uliyotenda au tendewa.

Mtume Paulo katika huduma yake ya uinjilishaji anawashukuru wote waliomwezesha na kuwatumia shukrani zake. Paulo Mtume anaona uwepo wa Mungu kwa kila aliyekutana naye. Paulo anathamini mchango wa kila mmoja katika kazi hii ya uinjilishaji. Huku ni kujali michango ya watu wengine hasa pale tunapofanikiwa na kufikia lengo letu katika maisha. Mara nyingi tunapofanikiwa hujiinua na kuona yote yaliwezekana kutokana na juhudi na bidii zetu. Huu ni ubinafsi uliopindukia. Tambua pia michango ya wengine katika mafanikio yako. Unapotambua michango ya wengine nawe ukatoa shukrani kwao, tendo hilo huwa Ibada kwani hubeba neema na baraka za Mungu.

Wapendwa wana wa Mungu, yale yote tuyafanyayo kwa moyo thabiti kama tendo la shukrani utujengea hofu ya Mungu na mwisho wake tendo hilo huwa kielelezo halisi na sahihi cha yule apasaye kutumikiwa na kuabudiwa. Pamoja na shukrani alizozitoa Paulo kwa watu mbalimbali bado anatambua ni nani mwenye mastahili ya kutumikiwa na kuabudiwa. Hivyo Paulo anasema, Sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya imara, sawasawa na injili yangu na kwa kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa na ufunuo wa ile siri iliyositirika tangu zamani za milele,” Rum 16:25. Ni siri ipi hiyo? Ndugu unayesafiri nami katika tafakari hii, siri anayoisema Mtume Paulo ni kuhusu suala zima la historia ya wokovu wetu na hitimisho lake. Ni kweli kwamba vyote vilifanyika kupitia Kristo, Yoh 1:3,  na kwa upendo wa Mungu Baba vyote vikakombolewa kupitia Kristo, 1Tim 2:5-6, na mwisho vyote vitatukuzwa ndani na katika Kristo, Efe 1:19b-23. Huyu ndiye, Ndiye Mungu mwenye hekima peke yake. Utukufu una yeye kwa Yesu Kristo, milele na milele. Amina,” Rum 16:27.

Injili yetu ya leo inatupa sehemu ya pili ya tafakari yetu, yaani, ‘mshika mawili kwa pamoja, moja humponyoka.’ Sehemu hii ya Injili ni mwendelezo wa Injili tuliyosoma jana tulipotafakari neno hili, ‘Ona fahari katika Kristo Yesu na yahesabu mambo yote yaliyofaida kwako kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.’ Ndugu yangu, unapokuwa na malengo thabiti katika maisha yako hukujengea msisitizo na uaminifu wa jambo hilo unalolifanya. Mafanikio ya mtu ni moja ya tokeo la namna alivyojiwekeza katika kitu hicho. Mkusanyiko wa pamoja wa nguvu zako, akili zako, na juhudi zako zisizo jigawagawa hukupatia matokeo mazuri kwa kile ukifanyacho.

Katika jambo hili la kujigawagawa Yesu anatupa angalizo na kusema, Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali,” Lk 16:13. Kama wataka kumtumikia Mungu fanya hivyo kweli pasipo kujibakiza. Faida yake nikubwa sana, yaani hapa duniani na Mbinguni uzima wa milele. Ila ukijitumikisha tu kwa sababu ya mali, utapata faida ya muda mfupi hapa duniani na kukosa faida ya milele Mbingu, yaani maisha ya uzima na umilele wake. Pamoja na hayo yote niliyoyasema,  mafanikio yako husukumwa na uaminifu wako mwenyewe kwa kile unachofanya hata katika udogo wake. Ndiyo maana leo Yesu anatuambia, Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia,” Lk 16:10. Hivyo ndugu yangu ni kukumbushe tu kwamba, “Moyo usio na shukrani ukausha mema yote. Na mshika mawili kwa pamoja, moja humponyoka.”

Tumsifu Yesu Kristo!

Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake. Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake,” Efe 1:5, 7


No hay comentarios:

Publicar un comentario