ALHAMISI WIKI
YA 32 YA MWAKA-B
12/11/2015
Somo: Hek
7:22-8:1
Zab: 119:89,
90, 91, 130, 135, 175
Injili: Lk
17:20-25
Nukuu:
“Ufalme wa Mungu
hauji kwa kuuchunguza; wala
hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo
ndani yenu,” Lk 17:20b-21
“Lakini kwanza, hana
budi kupata mateso mengi, na kukataliwa na kizazi hiki,” Lk 17:25
“maana Mungu humpenda yeye tu akaaye na
Hekima,” Hek 7:28
“Marini kuliko jua, Hekima hupita
makundi ya nyote; ikilinganishwa na nuru, huonekana ya kuwa imezidi,” Hek 7:29
“maradi baada ya nuru ya mchana hufuata
usiku, bali juu ya Hekima hakuna ovu liishindalo,” Hek 7:30
“Hekima huenea kwa nguvu nyingi toka
pembe hii hata pembe hii ya dunia, na kuyaratibisha mambo yote kwa jinsi ya
ufaa,” Hek 8:
TAFAKARI: “Ufalme wa
Mungu umo ndani yenu.”
Wapendwa wana wa Mungu, maisha yako na
makusudi ya kuumbwa kwako na Mungu ni kuishi milele. Ufalme wa Mungu upo ndani
yetu tangu kuumbwa kwetu. Mungu kwa kutuumba kwa sura na mfano wake alianzisha
rasmi ufalme wake ndani yetu. Kwa hiyo ni jukumu yako na langu kuupokea kwa
uhuru ufalme huu na kuwa sehemu ya maisha mapya na Mungu au kuukataa. Hivyo
pamoja na kwamba ufalme huu wa Mungu umo ndani yetu tunayohiari ya kuukataa pia
kwa sababu Mungu haingilii uhuru wetu.
Ni kwa maana hii hatuwezi kusema ufalme
wa Mungu waja kutoka upande gani wa maisha yetu, bali yatupasa kujibiidisha
kila siku kuuelewa na kuuishi. Yesu leo anatuambia, “Ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo huku, au,
kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu,” Lk 17:20b-21. Hii ni
sehemu ya kwanza kuhusu ufalme wa Mungu, yaani ni kufanya juu chini kuutambua
na kuuishi kila siku. Sehemu ya pili kuhusu ufalme wa Mungu ni yale Kristo
aliyojitolea kwa ajili yako, yaani mateso na kifo cha msalaba. Hapa ndipo
tulipohesabiwa haki na Mungu kwa kumtoa mwanaye Mpendwa afe kwa ajili ya dhambi
zetu nasi tuwe huru na warithi wa ufalme wake. Je, unayo sadaka ya kutoa?
Wapendwa wana wa Mungu, kama wewe ni mfuasi kweli wa Kristo
elewa jambo hili: ‘hakuna utukufu pasipo msalaba, na hakuna pasaka pasipo
ijumaa kuu.’ Kristo alijitoa kwa ajili yetu sisi na kukubali kuiendea njia ile
ya mateso kwa ajili ya kweli na haki. Naye Yesu anatuambia hayo yote yatatokea,
“Lakini kwanza, hana budi kupata mateso mengi,
na kukataliwa na kizazi hiki,” Lk 17:25. Nasi kama wafuasi wake Kristo
tutaifuata njia itupelekayo kwenye utukufu na ufufuko tunaposimama katika kweli
na haki na hapo tutaonya mauti yake. Kuufahamu ukweli huu twahitaji hekima ya
Mungu kuyachambua yote kwa busara, na kutenda katika kweli na haki. “Maana Mungu
humpenda yeye tu akaaye na Hekima,” Hek 7:28.
Ndugu yangu tuliyesafiri pamoja kwenye
tafakari hii, tunahitaji sana hekima ya Mungu ili tuyaone mahangiko yetu na
mateso yetu kama sehemu muhimu ya wokovu wetu ambao tayari tunao ndani mwetu.
“Hekima huenea kwa nguvu nyingi toka pembe hii hata pembe hii ya dunia, na
kuyaratibisha mambo yote kwa jinsi ya ufaa,” Hek 8: Tuikubali hekima ili hekima
hiyo itufunulie siri za Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au
Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba
yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na
haki yake; na hayo yote mtazidishiwa,” Mt 6:31-33
No hay comentarios:
Publicar un comentario