JUMAPILI
YA 1 YA MAJILIO YA MWAKA C
29/11/2015
Somo
I: Yer 33:14-16
Zab:
25:4-5, 8-9, 10, 14
Somo
II: 1The 3:12-4:2
Injili:
Lk 21:25-28, 34-36
Nukuu:
“Katika siku zile, na wakati ule, nitamchipushia Daudi
Chipukizi la haki; naye atafanya hukumu na haki katika nchi hii,” Yer 33:15
“Katika siku zile Yuda ataokolewa, na Yerusalemu utakaa
salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu,” Yer 33:16
“Basi, jiangalieni,
mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya;
siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo; kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu
wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima,” Lk 21:34-35
“Basi, kesheni ninyi kila
wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama
mbele za Mwana wa Adamu,” Lk 21:36
“Bwana na awaongeze na
kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi
nasi tulivyo kwenu,” 1The 3:12
“Iliyobaki, ndugu,
tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea
kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda,
vivyo hivyo mpate kuzidi sana,” 1The 4:1
TAFAKARI:
“Bwana ni haki yetu.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, karibuni katika tafakari ya leo ikiwa Mama Kanisa anaadhimisha
Dominika ya kwanza ya majilio ya mwaka C wa Kanisa. Leo pia kwa namna ya pekee
tunaanza mwaka C wa Kanisa. Masomo na tafakari zetu zitalenga katika kipindi
hiki cha Kanisa. Kipindi hiki cha Majilio Kanisa linajifananisha na Taifa la
Mungu la Agano la Kale linapotarajia kwa hamu kubwa ujio wa Mkombozi. Hivyo
kipindi hiki Mama Kanisa anawaandaa wana wake kuwa tayari kumpokea Mkombozi.
Hata hivyo kipindi hiki cha Majilio kina sura nyingine, ambayo inaufunua ujio
wa siku ya mwisho wa Bwana. Ni kwa namna hii Kanisa limegawa kipindi hiki cha
Majilio katika sehemu kuu mbili nazo ni hizi zifuatazo: Sehemu ya kwanza
inaanza leo hadi hapo tarehe 16 ya mwezi Desemba. Mambo makuu katika kipindi
hiki ni kutafakari juu ya ujio wa pili wa Kristo katika utukufu wake. Sehemu ya
Pili, Mama Kanisa atakuwa anatafakari juu ya
matayarisho ya sikukuu ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Msukumo na wazo
kuu katika kipindi hiki ni “Kristo yu karibu,” Yeye ni Mkombozi na hakimu.
Hivyo basi katika
kipindi hiki cha Majilio tunajitayarisha kwa furaha kumpokea Kristo tukisikia
na kuifuata sauti ya mtu yule aliye nyikani: “Itengenezeni njia ya Bwana.”
Matengenezo ya njia hii hubeba thana nzima ya mwili na roho. Kristo atakapokuja
atukute taa zetu zinawaka nasi tupo macho. Masomo yetu yote matatu yanamwelezea
Bwana wetu na Mungu wetu kama mtu kwenye haki. Haki hii haipindishwi kwa lolote
lile, bali ni matokeo ya ule utayari wetu wakujifungamanisha naye kuliko kweli
na haki. Kama Mungu na Bwana wetu anajua yote kuhusu sisi, basi hatuna chochote
cha kumficha wala kujivunua tukijidanganya kuwa ni mali yetu wenyewe. “Yeye hubadili majira na nyakati; huuzulu
wafalme na kuwamilikisha wafalme; huwapa hekima wenye hekima; huwapa wenye
ufahamu maarifa; yeye hufunua
mambo ya fumbo na ya siri; huyajua yaliyo gizani, na nuru hukaa kwake,” Dan
2:21-22. Ndugu yangu, ni nani basi zaidi ya Mungu wetu? Bwana ni haki yetu!
Siku ya hukumu ya mwisho licha ya kwamba hatujui ni lini, hatuwezi
kuipuuzia kwamba haitakuwepo. Kila kitu kitapita ila neno la Bwana litabaki
milele licha ya utofauti wake kati ya kile kisemwacho na tendo lenyewe kutokea.
Kuchelewa kwa tukio lenyewe kusitutie upofu na uziwi wa kutokuishi kadiri ya
mapenzi ya Mungu na atakavyo. “Mbingu na nchi
zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe,” Lk 21:33. Nabii Yeremia
anatuambia kwamba katika mpango huu wa wokovu na hukumu ya mwisho utafanywa na
Mungu chini ya chipukizi la haki na katika haki hiyo kila mtu atapata mastahili
yake. “Katika siku zile, na wakati ule, nitamchipushia
Daudi Chipukizi la haki; naye atafanya hukumu na haki katika nchi hii,” Yer
33:15. Kuokolewa kwetu ni tokeo la kuishi
katika kweli na haki. Ni rahisi kufanya ujanja ujanja katika ulimwengu huu lakini
si kwa Mungu aliye hai na mwona yote katika yote na muda wote. Hivi ndivyo
atakavyofanya; “Katika siku zile Yuda ataokolewa, na Yerusalemu utakaa
salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu,” Yer 33:16.
Wapendwa katika Kristo, kwa vile muda wetu hapa duniani ni
mfupi sana, ni vyema tukawekeza kwa yale yampendezayo Mungu hakimu wetu wa
haki. Lengo la maisha yako na yangu katika ulimwengu huu siyo kuyafurahia
maisha kwa sababu ya kuyafurahia tu, bali kuyatazama maisha katika umilele wake.
Katika Injili ya leo Yesu anatukumbusha maana halisi ya uwepo wetu katika
ulimwengu huu ukiendana na yale yatupasayo kufanya. “Basi, jiangalieni,
mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya;
siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo; kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu
wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima,” Lk 21:34-35. Namna ufikirivyo kuhusu
hali yako ndivyo kwa namna hiyo huyafinyanga maisha yako. Wapo kati yetu maisha
kwao ni kufurahia kila kunapo nafasi ya kufanya hivyo. Ila Mtume Paulo anasema
juu ya jambo hili; “ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na
furaha katika Roho Mtakatifu,” Rum 14:17. Uzima wa mtu ni zaidi ya haya ya leo
na kesho.
Wapo pia
kati yetu wanafikiri maisha ni kuwa na vitu na utajiri. Muda wao wote ni
kuhangaika kuhusu mali na vitu, na mwisho wa siku ni huzuni na kukata tamaa.
Mzaburi anatupa angalizo na kusema, “Usiogope
mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi. Maana atakapokufa hatachukua cho chote;
Utukufu wake hautashuka ukimfuata,” Zab 49:16-17. Maisha ya utakaso ndiyo salama yetu siku hiyo
ya mwisho. Utakaso huu ndiko tunakoalikwa kila siku kufanana na Yesu. Si jambo
rahisi ila yakupasa kwa moyo wote uamue, ujitahidi kuishi maisha hayo, na utumudu
katika maisha hayo hadi mwisho wake. Kudumu katika maisha hayo ndiko Yesu
anaposema kukesha. “Basi, kesheni ninyi
kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na
kusimama mbele za Mwana wa Adamu,” Lk 21:36. Tunamsubiri Mwokozi wetu kwa
kukesha tukiitakatifunza miili yetu na roho zetu.
Kukesha
huku katika kweli na haki hujionyesha kwa kuwa na mahusiano mazuri na wale
tunaoishi nao kila siku. Upendo ni tokeo la maisha ya kweli na haki, na upendo
huo huo usukuma maisha ya kweli na haki. Mtume Paulo anawasihi watu wake waige
kile alichokifanya kwao na wenzake. “Bwana na awaongeze na
kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi
nasi tulivyo kwenu,” 1The 3:12. Hili ni jambo jema la kuiga. Neno la Mungu,
watu, na mazingira humfinyanga na kumkomaza mtu na kukuza tabia yake. Tabia
njema ndiyo itakayotufikisha kwenye uzima wa milele, na siyo utajiri
tunaouangaikia usiku na mchana. Mwisho wa haya yote twapaswa kufanana na Kristo
kwa sababu ni kwa njia yake wokovu wetu uwezekana. Hivyo, “Iliyobaki, ndugu, tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende
katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na
kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana,” 1The
4:1. Kristo Yesu ndiye kielelezo cha maisha yetu, na ufunuo halisi wa Mungu
Baba. Kukesha huku Yesu anakutafsiri kama “kukaa,” katika neno lake. Kukaa huku
katika neno lake ndiko kunatufanya wanafunzi wake wa kweli ambayo kweli hiyo
itatufanya huru. “Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa
katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena
mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru,” Yoh 8:31.32
Mzee
Damas akiwa amelazwa hospitalini katika uzee wake wa miaka 85, chini ya uangalizi
wa mjuu wake Onesmo, alikuwa na mashaka sana na huduma za Kanisa
(Masakramenti), ikiwemo Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa. Onesmo akijua Babu
yake alikuwa Mkristo na katika hali hii ya ugonjwa wake na mabadiliko ya mara
kwa mara ilimlazimu kumwona Paroko wake kwa kupitia jumuiya yake ili Babu yake
apate huduma hii ya wagonjwa.
Hivyo
baada ya mawasiliano kwenda vizuri kati ya Onesmo, Jumuiya yake, na Paroko,
siku ya jumatatu alfajiri ambayo ni siku rasmi ya kuwatembelea wagonjwa, Paroko
alikwenda hospitalini kumwona Mzee Dismas na kumpa huduma hiyo. Jambo la ajabu
na la kushtusha ambalo halikutegemewa na Paroko na wala Onesmo mjukuu wa Mzee
Dismas, ni pale Mzee huyu alipomwona Padre na kujeukia ukutani uku akilivuta
shuka lake kujifunika gubigubi.
Tendo
hili lilimfikirisha haraka Padre na hivyo alimwomba Onesmo atoke nje kidogo ili
aweze kuongea na Mzee Onesmo. Ilichukua muda kidogo hadi Mzee Onesmo kukubali
kuongea na Padre na kusema kwa nini hataki huduma hiyo.
Tatizo
kubwa la Mzee Dismas lilikuwa hili (nitalisema kwa lugha ya picha), ambalo
aliona fika kabisa hawezi kusamehewa na Mungu. “Padre, nilivyokuwa na umri wa
miaka saba hivi nilikwenda njia panda na kubadilisha vibao vile elekezi. Kibao
kilichoonyesha Dar es Salaam kuelekea
Dodoma, nilikigeuza na kilisomeka Dar es Salaam Iringa. Je, ni wangapi
nimewapeleka pasipo tangu nikiwa na miaka 7 hadi leo? Mungu gani anayeweza
kunisamehe dhambi hii? Sipendi kumdanganya Mungu katika hili. Nipo tayari
kupata adhabu yake," Mzee Dismas aliyasema haya akiwa na hofu kubwa.
Padre kwa
kutambua hofu aliyokuwa nayo Mzee Dismas juu ya tatizo lake, alianza na maneno
haya, “ndugu yangu Dismas, huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Bwana
anasema na anakuambia leo maneno haya mazito kwako, ‘Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji;
zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu,’ Isa 1:18. Je, maneno
haya hayana uzima ndani yako? Sote tunahitaji huruma ya Mungu. Yatupasa sote
kukubali udhaifu wetu na kutii maelekezo ya Mungu.” Baada ya maneno haya Mzee
Dismas alivuta pumzi na kupumua kwa nguvu kama vile mtu aliyetua jiwe kubwa
sana kifuani mwake.
Uso wa Mzee Dismas ulionekana wenye furaha na kukubali
kuungana dhambi zake na kuwa tayari kupokea huduma ile ya Ekaristi Takatifu na
Mpako wa Wagonjwa. Ndugu zangu, katika kipindi hiki cha majilio tunavyojiandaa
kiroho yatupasa kuyatafakari maneno haya ya Bwana wetu Yesu Kristo kwa undani
wake. Yesu anatuambia, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na
mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni
nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo;
nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi,” Mt 11:28-30.
Hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Tujiachie kwake bila kujibakiza. Wokovu ndiyo
sasa.
Ndugu
zangu, niwatakieni majilio mema na yenye kumtafuta Bwana wetu na haki yetu kwa
nguvu zote. Tuyarudi maisha yetu kwa kuyatazama madhaifu yetu na kuyapatia tiba
ya kweli tukimtazama tabibu wetu Yesu Kristo.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa
walio hawawezi. Sikuja kuwaita
wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu,” Lk 5:31-32
No hay comentarios:
Publicar un comentario