viernes, 13 de noviembre de 2015

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 32 YA MWAKA-B

JUMAMOSI WIKI YA 32 YA MWAKA-B
14/11/2015
Somo: Hek 18:14-16; 19:6-9
Zab: 105:2-3, 36-37, 42-43
Injili: Lk 18:1-8
Nukuu:
 “Neno lako Mwenyezi alishuka mbinguni kutoka kiti chako cha kifalme, shujaa aliye hodari, katika nchi iliyopasishwa hukumu, mwenye upanga mkali, ndio amri yako isiyopindika,”Hek 18:15

“Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima,” Lk 18:4b-5

Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?” Lk 18:7

Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je!Ataiona imani duniani?” Lk 18:8

TAFAKARI: “Unaweza kutoa bila kupenda, ila uwezi kupenda bila kutoa.”

Wapendwa wana wa Mungu, kuumbwa kwetu wanadamu halikuwa hitaji la Mungu, bali kwa upendo wake alichakugua kutuumba kwa sura na mfano wake. Kwa hiyo lengo la kwanza la uumbaji wetu ni kuishi milele. Kwa tendo hili ni wazi kwamba lengo la pili la uumbaji wetu ni kuwa na mahusiano na Mungu na sisi kwa sisi. Mahusiano haya msingi wake ni upendo. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu,” 1Kor 13:3. Kadhi kama tulivyosoma na kusikia Injili ya leo anampa mama mjane haki yake si kwa kupenda bali kwa kulazimika kutoka na usumbufu. Naye anasema, “Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima,” Lk 18:4b-5. Hivyo unaweza kutoa bila kupenda.

Tunapokuwa na mahusiano mazuri na Mungu kamwe hawezi kutuacha katika mahangaiko yetu. Bwana wetu Yesu Kristo anatupatia uhakikisho huyo. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao?” Lk 18:7. Uvumilivu wa Mungu kwetu ni Imani ile tuliyo nayo juu yake. Kwa imani dhabiti tunauhakika kwa kuyapata yale tumwombayo Mungu wetu aliye huruma na upendo. Yesu anatupa pia uhakika wa jambo hili, ila imani ni moja ya kielelezo kikuu kwa kile tuombacho. Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani?” Lk 18:8. Je, unayoimani kwa hayo uyaombayo?

 Kwa upande mwingine uwezi kupenda bila kutoa. Yesu anasema, “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo,” Yoh 10:11. Yesu kwa kutupenda yupo tayari kutua uhai wake kwa anjili yetu. Upendo ndiyo amri yenyewe. Kristo ndiye kielelezo chetu juu ya upendo na kupenda. Hili ndilo lile neno lililofanyika mwili nalo likakaa kwetu. “Neno lako Mwenyezi alishuka mbinguni kutoka kiti chako cha kifalme, shujaa aliye hodari, katika nchi iliyopasishwa hukumu, mwenye upanga mkali, ndio amri yako isiyopindika,”Hek 18:15. Katika mahusiano haya ayapendayo Mungu, tunaweza kuona pia hata katika amri kuu za Mungu. Amri nne kati ya zile kumi ni uhusiano wa mtu na Mungu. Na zile sita zilizobaki ni uhusiano wa mtu na mtu. Tumpende Mungu na tuwapende watu, na sote tupendane.

Tumsifu Yesu Kristo!


Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo,” 1Yoh 4:8

No hay comentarios:

Publicar un comentario