jueves, 5 de noviembre de 2015

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 31 YA MWAKA-B

IJUMAA WIKI YA 31 YA MWAKA-B
6/11/2015
Somo: Rum 15:14-21
Zab: 98:1, 2-3ab, 3cd-4
Injili: Lk 16:1-8
Nukuu:
 ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu,” Rum 15:16

Basi, nina sababu ya kuona fahari katika Kristo Yesu mbele za Mungu,” Rum 15:17
Maana sitathubutu kutaja neno asilolitenda Kristo kwa kazi yangu, Mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa tendo, kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu,” Rum 15:18-19a

Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa wakili tena,” Lk 16:2b

Yule bwana akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru,” Lk 16:8 

TAFAKARI:Ona fahari katika Kristo Yesu na yahesabu mambo yote yaliyofaida kwako kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.”

Wapendwa wana wa Mungu,   ni kweli kwamba huwezi ‘kuila keki na kuihifadhi kwa wakati ule ule.’ Kwa mantiki hiyo, ama unaila kwa wakati ule ule kwa uhuru na kufurahia utamu wake, au unaihifadhi iwe fahari ya macho yako. Ni kwa maani hii wapendwa, upo uhuru  na furaha kupoteza yote ya ulimwengu huu yenye mtazama wa kifaida na kumpata Kristo, kuliko kumpoteza Kristo na kuyapata ya ulimwengu huu ambayo si yakudumu.

Kwa kumpata Kristo utakuwa na uhakika wa uzima wa milele. Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani,” Yoh 5:24. Kwa kuupata ulimwengu huu na faida zake hakuna umilele ndani yake. Ni hasara isiyorekebishika. Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?” Mt 16:26. Hivyo “Ona fahari katika Kristo Yesu na yahesabu mambo yote yaliyofaida kwako kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.”

Mtume Petro kama mimi na wewe, alipata ugumu sana wa kuelewa maana ya maneno hayo ya Yesu. Hivyo alitaka kujua ni nini matokeo ya sadaka yake ya kuyatoa maisha yake kwa ajili Kristo na Injili kama njia ya wokovu wa ulimwengu mzima. Yesu anatujibu wote kwa pamoja na kusema, “Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili,  ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele,” Mk 10:29-30. Yesu Kristo ananitaka mimi na wewe tuwe na mtazamo mpya kuhusu vitu na fahari zake. Yesu anatutaka pia kulinganisha vitu na fahari zake tukiyathaminisha hayo na uzima wa milele.

Mtume Paulo alifaulu kwa kiasi kikubwa katika mtazamo wa vitu na faida zake, na thamani ile tuipatayo tunapoacha kushikamana na vitu hivyo na faida zake. Naye anasema, Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo,” Flp 3:7-8. Mtume Paulo anaona fahari kubwa sana kumpata Kristo na kuishi kwa ajili ya Kristo hasa kuwa mjumbe mzuri wa habari njema kwa wengine. Kwa sababu hiyo, Mtume Paulo anasema, ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu,” Rum 15:16. Mtume Paulo kesha gundua sababu ya furaha yake, na msukumo wa ndani wa maisha yake.

Ndugu yangu tunayesafiri zote katika tafakari hii hatuwezi kuifikia hatua aliyoifikia Mtume Paulo kama hatujampata Kristo na kuwa sababu ya kila kitu katika maisha yetu. Je, yanitosha kuona fahari katika Kristo kwa vile tu nilibatizwa na leo naishi agano kama mlei kwa sakramento ya Ndoa, Mtawa kwa maisha ya Wakfu, na Mtawa na Mkleri kwa maisha ya wakfu na sakramenti ya Daraja Takatifu? Je, vile nilivyo leo yatosha? Ndugu yangu, Kristo anakuwa sababu ya kila kitu katika maisha yako unapooshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu. Kuzaliwa huku wa pili si tokeo la matendo yako ya haki uyatendayo. Ila ni utayari wa kumpokea na kumruhusu Kristo na Roho Mtakatifu kufanya kazi ndani yako. Hivyo, “wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu,” Tit 3:4-5.  Tokeo la utayari huu wa kukubali kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili katika maisha yetu  huwa sababu na kielelezo cha kuhesabiwa haki na kuurithi uzima wa milele, Tit 3:7.

Mara nyingi baadhi yetu hupenda sana kujilinganisha na kujifananisha na yale tuyafanyao na kusahau kwamba kwa kubaki tu kwenye hayo na hali hiyo kwa yanayoonekana na yasiyodumu tunapoteza sababu na malengo ya masisha yetu hapa duniani. Hata kama wayatenda vyema hayo uyafanyayo, kamwe yasichukue nafasi ya Kristo katika maisha yako. Maana sitathubutu kutaja neno asilolitenda Kristo kwa kazi yangu, Mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa tendo, kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu,” Rum 15:18-19a. Ndugu yangu, chochote kisichokuwa na kibali kutoka kwa Mungu hakidumu na hakina umilele. Bali kama vile tulivyopata kibali kwa Mungu tuwekewe amana Injili, ndivyo tunenavyo; si kama wapendezao wanadamu, bali wampendezao Mungu anayetupima mioyo yetu,” 1The 2:4. Je, wajua ipo siku itakupasa kutoa hesabu mbele ya Mungu kwa hiki unachoishi leo? Je, umejiandaa kwa lipi mbele zake Mungu uku ukijua wazi ndani ya dhamiri yako kwamba  unachokifanya na ulicho hakina kibali chake?

Wapendwa katika Kristo, Injili ya leo inatupatia hali halisi kuhusu hesabu yetu siku ya mwisho. Yesu analisema jambo hilo akitolea mfano wa Tajiri mmoja na Wakili wake dhalimu. Bila kujua siku wala saa, Wakili huyu dhalimu anatakiwa na Tajiri yake kutoa hesabu ya uwakile wake, baada ya Tajiri yake kupata habari ya kutapanywa kwa mali zake. Alichokifanya kwa haraka Wakili yule ni kurejesha uhusiano wa haraka na wateja zake ambao ndio hatma ya maisha yake kwa sasa. Katika jambo hili ilimpasa kutoa msamaha wa madeni bila kuhathiri utajiri wa Tajiri yake. Hivyo, Yule bwana akamsifu wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru,” Lk 16:8. Kwa kuyasema haya, Yesu anatuacha na swali la zito la kujibu. Swali hilo ni hili: Mimi na wewe tunasubiri nini kurejesha uhusiano wetu na Mungu kwa muda na nafasi tuliyonayo sasa tukiwa bado kwenye nuru, yaani, kwa ubatizo wetu na agano letu katika maisha, iwapo Wakili huyu na udhalimu wake aliweza kurejesha uhusiano wake na wateja zake? Wokovu ndiyo sasa.

Tumsifu Yesu Kristo!


Bwana asema hivi, Shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa,” Isa 56:1

No hay comentarios:

Publicar un comentario