miércoles, 4 de noviembre de 2015

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 31 YA MWAKA-B

ALHAMISI WIKI YA 31 YA MWAKA-B
5/11/2015
Somo: Rum 14:7-12
Zab: 27:1abcde, 4, 13-14
Injili: Lk 15:1-10
Nukuu:
Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake,” Rum 14:7 

Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana,” Rum 14:8

Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia,” Rum 14:9 

Lakini wewe je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu,” Rum 14:10

Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu,” Rum 14:12

Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung'unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao,” Lk 15:1-2

Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu,” Lk 15:7 

Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye,” Lk 15:10 

TAFAKARI: “Acha njia zako ovu changua uzima nawe uishi milele.”

Wapendwa wana wa Mungu, uovu wowote ule hauendani na wema na uzuri wa Mungu. Kama sisi wanadamu ni ufukufu na furaha ya Mungu, uovu ndani yetu hutufifisha sisi wenyewe na kutuweka mbali kabisa na utukufu na furaha ya Mungu. Uovu wa mwanadamu ni kujikataa mwenyewe kuliko wazi, na kuukataa utukufu na furaha ya Mungu iliyo ndani yake, yaani ile chapa ya sura na mfano wa Mungu, Mwa 1:26. Uovu huu ni kujihesabia haki pasipo haki. Binadamu bila Mungu ni sawa na samaki bila maji. Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake,” Rum 14:7. Mtu akisha jihalalishia uovu fulani, hali ile umtia kiburi na upofu. Je, muhimili wa maisha yako upo wapi?

Moja ya mizania ya kweli na haki kwa viumbe vyote licha ya hali na nafasi tulizonazo ni kifo. Hata pamoja na ukweli huu, mtu aliyepigwa upofu na kiburi kinachotokana na kuhalalisha uovu, hakosi kujiinua. Basi ni vyema hata kama huamini hakuna Mungu na Mbingu kwa sababu vyote vya ulimwengu huu kwa kiburi chako unavipata, kinyenyekeshe basi kwa kujua kuwa lazima utakufa. Pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya leo, bado kifo hakizuiliki wala hakitabiriki. Kwa hiyo kama umezaliwa kweli na unaishi leo na sasa kifo kipo. Kifo ni kivuli cha mwili wako na hivyo unacho muda wote. Ni wakati tu ukifika nalo litatendeka.

Ndugu yangu, kifo chako na hasa kama u mfuasi wa Kristo, hakitakuwa na maana bila Kristo. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana,” Rum 14:8. Je, bila Kristo kifo chako kina umaana yoyote? Jambo la muhimu kujua ni hili; kufa kwako kuna maana tu kama kuishi kwako kuna maana na kulikuwa na maana na Kristo. Kuishi katika maana ya Kristo ni kuishi kwa kufafana na Kristo. Tunaishi kwa kufafana na Kristo tunapoishi katika ufalme wake wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki, mapendo na amani. Je, maisha yako ya leo na sasa yanatoa taswira katika maana niliyosema?

Licha ya kwamba tunajua ipo siku kutakufa, ila kifo hicho kitakuwa na maana tu tukiishi au tukifa tu mali ya Bwana. Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia,” Rum 14:9. Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, kesho yetu katika maisha ya umilele na Mungu haitakuwa matokeo ya sifa zetu, madaraka yetu mabaya na ya uonevu kwa wanyonge, akili zetu za ujanja ujanja wa kuzikanyaka haki za watu, wala umaarufu wetu. Kesho yetu katika uzima wa milele ni matokeo ya kuishi leo yetu katika ufalme wa kweli, utakatifu na wa neema, haki, mapendo na amani kwetu sisi na kwa watu wote. Haya ndiyo makusudi ya Mungu kuviweka viumbe vyote chini ya utawala wake Kristo ambaye amemtolea Mungu Mkuu ufalme wa milele na wa ulimwengu wote.

Kama hili nilisemalo lina sema chochote juu ya maisha yako, Lakini wewe je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu,” Rum 14:10. Ndugu yangu, tutawezaje kusimama katika kiti hiki cha hukumu cha Mungu kama ishi yetu leo siyo ishi yetu na Kristo? Tunayo nafasi moja tu kwa sasa. Ili kumrudishia Mungu utukufu wake na furaha yake tuliyoififisha kwa uovu wetu ni kufanya toba ya kweli na majuto. Huu ndio wito wa injili yetu ya leo.

Katika Injili ya leo, Yesu anatoa wito huo kwa kutupatia mifano miwili yenye kuonyesha furaha ya Mungu tunapomrudia baada ya kutambua njia ya uzima aliyotuandalia; Mfano wa kwanza, ni mtu mwenye kondoo mia na kumpoteza mmoja. Naye Yesu anatuambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu,” Lk 15:7. Mfano wa pili ni huu wa mwanamke yule mwenye shilingi kumi akapoteza moja. Naye Yesu anatuambia, “Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye,” Lk 15:10. Shauku hii ya kutafuta kimoja kilichopotea itusukume kujiweka karibu zaidi na Mungu. Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa,” Isa 55:7. Mungu wetu anamaanisha kweli hili alisemalo, yaani kutusamehe kabisa tunapofanya toba ya kweli na majuto. Mzaburi anatuambia ukweli huu kwa kusema, Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe utanijulisha hekima kwa siri, Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji,” Zab 51:6-7. Huyu ndiye Mungu anayependa kuanza upya nawe katika yote  licha ya historia yako mbaya ya huko nyuma. Je, upo tayari kuanza upya na Mungu?

Wapendwa katika Kristo, usipoteze muda wako mwingi kwa kuziangalia dhambi na uovu wa wenzako ilhali nawe upo kwenye mtego huo huo. Yesu kuwa karibu na wadhambi kwa mfano daraja na mpatanishi wetu na Mungu, anaonekana naye mdhambi kadiri ya mitazamo ya Mafarisayo ambao walipenda kujionyesha wasafi nje ila ndani ni ubatili mtupu. Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung'unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao,” Lk 15:1-2. Mimi na wewe hatuna tofauti na watoza ushuru na wenye dhambi. Tunahitaji huruma ya Mungu na msamaha wake.

Tumsifu Yesu Kristo!


Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila. Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana,” 1Pet 3:10-11

No hay comentarios:

Publicar un comentario