miércoles, 25 de noviembre de 2015

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 34 YA MWAKA-B

ALHAMISI WIKI YA 34 YA MWAKA-B
26/11/2015
Somo: Dan 6:12-28
Zab: Dan 3:68, 69, 70, 71, 72, 73, 74
Injili: Lk 21:20-28
Nukuu:
Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno,” Dan 6:22 

Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danielii katika lile tundu. Ndipo Danielii akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake,” Dan 6:23

Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danielii, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu,” Dan 6:24 

Ndipo mfalme Dario akawaandikia watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, waliokaa juu ya uso wa dunia; Amani na iongezeke kwenu,” Dan 6:25

Mimi naweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya ufalme wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za Mungu wa Danielii; maana yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata mwisho,” Dan 6:26 

Yeye huponya na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya Danielii na nguvu za simba,” Dan 6:27

Basi Danielii huyo akafanikiwa katika enzi ya Dario, na katika enzi ya Koreshi, Mwajemi,” Dan 6:28

watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika,” Lk 21:26 

Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi,” Lk 21:27

Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia,” Lk 21:28 

TAFAKARI: “Kiama kina hofu kwa wale wasio mwamini Mungu aliye Hai.”

Wapendwa wana wa Mungu, habari za mwisho wa nyakati zinawatisha wengi na hasa wale wasio mwamini Mungu aliye hai. Maisha hujawa na hofu kwa sababu ya kuishi kwa kubahatisha bahatisha. Hofu huwa tishio kubwa zaidi pale mtu anapokosa msingi imara wa maisha yake. Watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika,” Lk 21:26. Pamoja na hayo yote tunahitaji kuishinda hofu. Nabii Danieli anaishinda hofu yake kwa sababu anamsingi imara wa Imani yake. Imani yake ipo kwa Mungu aliye hai. Hivyo maagizo ya mfalme Dario kwamba sala zote zielekezwe kwake na siyo kwa Mungu, Danieli anapinga jambo hilo na anazidi kuomba kwa Mungu wake aliye hai. Kosa la kwenda kinyume cha maagizo ya mfalme ilikuwa kutupwa katika tundu la simba na kuliwa hadi kwisha. Hata pamoja na ukatili huo, Danieli Nabii hakuogopa kwa sababu alijua ni nani anayemtumikia, Mungu aliye hai.

Baada ya kutupwa kwenye tundu la simba kwa kukaidi amri ya mfalme, Danieli hakudhurika na simba wale. Danieli anasema, Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno,” Dan 6:22. Mungu hufanya njia pasipo njia hasa kwa wale wanaomtumaini kila wakati. Ni kweli kwamba pamoja na sheria ile mfalme hakutaka kuitekeleza kwa Danieli kwa sababu alimjua Danieli kuwa ni mtu wa Mungu. Mfalme alilazimika kufanya vile kwa shinikizo la watu, na hakuweza kupinga kwa sababu ‘sheria ni msumeno.’ Hata hivyo mfalme hakuacha kuizuia furaha yake alipomwana Danieli mzima licha ya kukaa kwenye tundu la simba kwa usiku mzima. Basi mfalme akafurahi sana, akaamuru wamtoe Danielii katika lile tundu. Ndipo Danielii akatolewa katika lile tundu, wala dhara lo lote halikuonekana mwilini mwake, kwa sababu alikuwa anamtumaini Mungu wake,” Dan 6:23. Tendo hili linaamsha hasira kwa wale walimfitini Danieli kwa mfalme. Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danielii, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu,” Dan 6:24. Ni vyema mara nyingi tukashughulikia maisha na utakatifu wetu, badala ya kuangaika na mambo ya watu wengine. Ona sasa malipo ya wale wafitini wa Danieli. “Mfalme akaamuru, nao wakawaleta wale watu waliomshitaki Danielii, wakawatupa katika tundu la simba, wao, na watoto wao, na wake zao; na wale simba wakawashinda wakaivunja mifupa yao vipande vipande, kabla hawajafika chini ya tundu,” Dan 6:25.  Kati yetu wapo watu kazi yao kubwa kutwa nzima ni kuripoti matukio yasiyo rasmi. Kuripoti matukio yasiyo rasmi na yasiyo na vielelezo hujulikana kama umbea.

Udhihirisho wa Mungu aliye hai kupitia tukio hili la Danieli kutokuliwa na simba, linakuwa wokovu kwa mfalme Dario na ukurasa mpya kwa watu wake. Kwa msimamo imara wa Imani wa Danieli unakuwa ufumbuzi wa tatizo kwa wengi, na wote wanaishi kwa amani na furaha. Mfalme Dario anasema, Mimi naweka amri, ya kwamba katika mamlaka yote ya ufalme wangu watu watetemeke na kuogopa mbele za Mungu wa Danielii; maana yeye ndiye Mungu aliye hai, adumuye milele, na ufalme wake ni ufalme usioharibika, na mamlaka yake itadumu hata mwisho,” Dan 6:26. Kumbe kusimama katika kweli hata kama kweli hiyo imezungukwa na mazingira hatarishi mwisho wake huwa mzuri. Hivyo hakuna mwenye mamlaka ya kuchukuwa maamuzi yako kama waona yapo sawa na yaliyo simama katika kweli na haki. Mungu huyu aliye wa kweli na hai hawezi mtupa mja wake. Yeye huponya na kuokoa, hutenda ishara na maajabu mbinguni na duniani, ndiye aliyemponya Danielii na nguvu za simba,” Dan 6:27. Danieli anatufundisha kusimama katika kweli. Kilicho cheusi na kisemwa kama kilivyo cheusi na kilicho cheupe kisemwe hivyo hivyo kama kilivyo, hata kama mazingira ya kusema hivyo ni hatarishi. Ni kupitia wewe tu Mungu atajidhihirisha kwako na kuwa faida kwako na kwa wengine. Basi Danielii huyo akafanikiwa katika enzi ya Dario, na katika enzi ya Koreshi, Mwajemi,” Dan 6:28. Mafanikio ya Mtu ni tokeo la uthubutu wake kwa yale yanayoonekana magumu na yasiyowezekana.

Mungu huyu aliye hai anaonekana katika uhalisia wake kupitia kazi za Mwanaye Yesu Kristo kama mkombozi. Huyu ndiye aliyetumwa kukomboa kile kilicho anguka kwa sababu ya dhambi. Pamoja na mambo mengi ya kutisha kutokana na mwisho wa nyakati na hasa kuharibiwa kwa hekalu la Yerusalema na watu wake kuteswa na kupelekwa utumwani, Mungu hata acha kamwe kuonyesha nguvu na utukufu wake. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi,” Lk 21:27. Hii ndiyo itakayokuwa ishara ya mwisho kwetu kuhusu mwisho wa nyakati. Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia,” Lk 21:28. Huu ni ule ukombozi wa siku ya mwisho, licha  kweli kwamba kila siku tumepewa ya ukombozi huo.

Basi ndugu yangu tutumie fursa tunazopewa na Mama Kanisa kila siku na hasa kupitia masakramenti yake ili tupata wokovu huo. Kiama kina hofu kwa wale wasio mwamini Mungu aliye hai.

Tumsifu Yesu Kristo!


Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu,” 1Sam 2:6-7

No hay comentarios:

Publicar un comentario