JUMAMOSI WIKI YA 34 YA MWAKA-B
28/11/2015
Somo: Dan 7:15-27
Zab: Dan 3:82-87
Injili: Lk 21:34-36
Nukuu:
“Akanena hivi, Huyo mnyama wa nne atakuwa ni ufalme wa nne juu
ya dunia, utakaokuwa mbali na falme zile zote, nao utakula dunia yote, na
kuikanyaga, na kuivunja vipande vipande,” Dan 7:23
“Naye atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye
atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye ataazimu kubadili majira na
sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu
wakati,” Dan 7:25
“Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu
zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; ufalme wake ni ufalme wa
milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii,” Dan 7:27
“Basi, jiangalieni,
mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya;
siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo,” Lk 21:34
“Basi, kesheni ninyi
kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na
kusimama mbele za Mwana wa Adamu,” Lk 21:36
TAFAKARI: “Tumeumbwa ili tunafanane na Kristo kila siku ya maisha
yetu, na kwa kupitia Yeye tuurithi ufalme wa mbinguni.”
Wapendwa wana wa Mungu, licha ya kwamba Mungu alichagua
kutuumba kwa sura na mfano wake kwa sifa na utukufu wake, na kutupatia heshima
kubwa kuliko viumbe vyote, alipenda pia tuwe na mahusiano naye. Hivyo sababu ya
tatu ya kuumbwa kwetu, Mungu anapenda tufanane na mwanaye Yesu Kristo ili kwa
kupitia Yeye tuurithi uzima wa milele. Ni jukumu la kila mbatizwa kila siku ya
maisha yake kufanana na Kristo kwa sababu, “jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina
la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua
katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile
lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine
awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu
litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 4:10-12. Hivyo maisha yetu hapa duniani
siyo maisha ya anasa na furaha tu kwa sababu hakuna mbingu hapa duniani.
Katika Injili ya leo Yesu anatupa angalizo kuhusa maisha
yetu hapa duniani. Naye anasema, “jiangalieni, mioyo
yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia
ghafula, kama mtego unasavyo,” Lk 21:34. Kwa
vile hatuijui siku ya kiama yetu, yatupasa kuwa macho huku taa zetu zikiwa
zinawaka kama wale wanawali watano wenye busara, Mt 25:4. Katika kile kituo cha
tisa katika simulizi la mateso ya Yesu, njia ya msalaba, tunaambiwa kwamba Yesu
anaanguka mara ya tatu. Moja ya mateso tunayomzidishia Yesu ni dhambi hii kama
sala isemavyo, “mara nyingi mno ninajibovusha kwa kupenda mno starehe, anasa na
tafriji.” Maisha yetu hapa duniani ni mafupi sana ukilinganisha na maisha ya
umilele. Kila mmoja wetu anapaswa kuyapa maisha haya kipaumbele akilenga
maandalizi ya maisha ya umilele. Katika jambo hili Yesu anatuambia, “kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika
haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu,” Lk 21:36.
Kukesha huku ni kufanana na Kristo kila siku kwa kutenda mema na kuishi
utakatifu ule aliouishi ukijipokea kama ulivyo binadamu. Kuishi kama Kristo ni
kuishi katika maisha ya utakaso. Ni kurejesha ile sura na mfano wa Mungu ndani
yetu ilipotezwa na kuchakazwa na dhambi. Huu ndio ufalme aliokuja kuusimika
Yesu Kristo duniani, yaani, kurudisha taswira ile ya Mungu ndani ya mioyo ya
wanadamu.
Kazi hiyo
ya Yesu inafunuliwa katika ndoto ya Nabii Danieli miaka mingi kabla. “Akanena hivi, Huyo mnyama wa nne atakuwa ni
ufalme wa nne juu ya dunia, utakaokuwa mbali na falme zile zote, nao utakula
dunia yote, na kuikanyaga, na kuivunja vipande vipande,” Dan 7:23. Kazi yake ya
kwanza ni kuushinda uovu kwa wema. Nasi kila moja kwa nafasi na wito wake kama
mbatizwa analo jukumu hilo, kuushinda uovu kwa kutenda mema. Hivyo kwa
kushirikishwa kazi hii ya ukombozi kila mmoja kwa nafasi yake, na kuitenda kwa
uaminifu na uadilifu, ndipo utakapokuwa
utakatifu wa kila mmoja wetu. Ni kutoa ushuhuda wa kweli katka maisha ya
kawaida ya kila siku kwa kila mmoja kadiri ya nafasi na wito wake. “Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini
ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; ufalme wake ni
ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii,” Dan 7:27.
Ndugu yangu, kwa nguvu zetu na maarifa yetu hatuwezi kamwe
kuwa kama Yesu pasipo msaada ya Roho Mtakatifu. Twamwitaji Roho Mtakatifu
kutuongoza na kutufunulia yale yaliyojificha katika maisha yetu. Roho huyu
atatuongoza na kufanya njia pale pasipo na njia.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Maana ufalme wa Mungu
si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu,”
Rum 14:17
No hay comentarios:
Publicar un comentario