JUMATANO WIKI YA 31 YA MWAKA-B
4/11/2015
Somo: Rum 13:8-10
Zab: 112:1b-2, 4-5, 9
Injili: Lk 14:25-33
Nukuu:
“Msiwiwe na mtu cho
chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria,”
Rum 13:8
“Pendo halimfanyii
jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria,” Rum 13:10
“Kama mtu akija kwangu
naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake
waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi
wangu,” Lk 14:26
“Mtu ye yote asiyeuchukua
msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu,” Lk 14:27
“Basi, kadhalika kila
mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu,” Lk
14:33
TAFAKARI: “Pendo halimfanyii jirani neno baya; Pendo ndilo utimilifu wa
sheria. Pendo ni Sadaka.”
Wapendwa wana wa Mungu, karibuni nyote tulitafakari neno la
Mungu kwa siku hii ya leo. Neno UPENDO siyo geni masikioni petu, ila ni kati ya
maneno yaliyochakachuliwa sana na kupoteza umaana wake. Maandiko Matakatifu leo
yanakualika wewe na mimi tulifakari pendo kwa kumchukua jirani yako na yangu
kama kioo cha kujitazama na kuona kama kweli kilicho ndani yako na yangu ndiyo
taswira halisi inayoonekana kwenye kioo hiki ambacho ni kiwakilishi cha jirani
yako. Kwa mtazamo huu wa kweli kutoka kwako kamwe hutoweza kufanya baya kwa
jirani yako. Kwa kutambua ukweli huu ndiko kuitimiza sheria. “Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana
ampendaye mwenzake ameitimiza sheria,” Rum 13:8. Ni kwa nini basi ndugu yangu
unajivika joho la chuki na kutembea nalo nyakati zote na majira yote ya mwaka?
Livue joho hilo la mateso na karaha nawe uwe huru.
Mt. Agustino wa Hippo
anatufundisha kwamba ‘ukipenda kweli utafanya yote, na kipimo cha kupenda ni
kupenda bila kipimo.’ Ni katika maana hii pendo linakuwa utimilifu wa sheria. “Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu
wa sheria,” Rum 13:10. Kinyume chake ni kweli, yaani sharti la kusamehe ni kusamehe bila sharti. Na kwa kufanya hivi pendo
linakuwa utimilifu wa sheria.
Pendo ni Sadaka. Unaweza kutoa bila kupenda,
ila huwezi kupenda bila kutoa. “Kwa maana jinsi hii
Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye
asipotee, bali awe na uzima wa milele,” Yoh 3:16. Hili ndilo
“PENDO SADAKA.” Kwa maana hiyo tunaweza kusema, “Pendo
halimfanyii jirani neno baya; Pendo ndilo utimilifu wa sheria. Pendo ni
Sadaka.”
Pendo Sadaka linaelezwa
vizuri na kwa undani katika Injili yetu ya leo. Yesu anatupatia mapaswa ya
ufuasi wetu kwake, na pendo sadaka tutakalo paswa kutoa. “Kama mtu
akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na
ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa
mwanafunzi wangu,” Lk 14:26. Kumbe kuwa mwanafunzi wa Kristo ni kumpenda kwa
dhati Kristo kule kuliko kwa kwanza. Tuelewe Kristo hasemi tusiwapende wazazi
wetu na ndugu zetu. La hasha! bali Yeye Kristo apewa nafasi ya kwanza. Tunampa
Kristo nafasi ya kwanza kwa sababu hii kubwa, naye anasema, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa
Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Wazazi wetu, ndugu, jamaa
na marafiki zetu wanamwitaji Kristo kwa kuwa ndiye njia halisi, kweli kamili,
na uzima wa milele ili kumfikia Baba yetu wa Munguni. Ni nani basi kati yetu asiyehitaji
hurama na upendo wa Mungu?
Pendo hili ni sadaka
kwa sababu linakutaka pia ujiachie katika mikono ya Kristo na kuachana na yale
yote yanayo ipa heri na matumaini nafsi yako. “Basi,
kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi
wangu,” Lk 14:33. Huku ndiko
kujikana nafsi. Moja ya mambo makubwa ya kujikana nafsi ni kuzishika vyema na
kwa ukamilifu na uaminifu amri za Mungu na neno lake. “Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Mtu asiyenipenda, yeye
hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba
aliyenipeleka,” Yoh 14:15, 24. Ndugu yangu unayesafiri nami kati tafakari hii,
kuzishika amri na neno la Mungu kwa kupenda bila shuruti ndiko kuuchukua
msalaba wa Yesu na kumfuata. “Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma
yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu,” Lk 14:27. Na tu wanafunzi wa Yesu kama tunapendana sisi kwa
sisi.
Pendo hili ni utayari wa kujitoa zaidi na zaidi kwa rafiki
hadi tone la mwisho yaani uhai aliokuwa nao kwa ajili ya wengine. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai
wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Wewe kama Mama au Baba katika
familia unatoa pendo sadaka pale ambapo waithamini ndoa yako na familia yako na
upo tayari kujitoa bila kujibakiza ili wewe upungue Watoto waongezeke na Mwenzi wako wa ndoa
aongezeke. Na kwa tendo hilo, Kristo ataonekana kwa watu. Nami kama Mtawa na
Mkleri yanipasa kwa furaha nithamini maisha yangu ya wakfu na niwe tayari
kupungua ninapotoa huduma kwa wengine bila kujibakiza ili Kristo aongezeke na
kuonekana kwa watu.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Lakini mimi, hasha,
nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo,
ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14
No hay comentarios:
Publicar un comentario