lunes, 9 de noviembre de 2015

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 32 YA MWAKA-B

JUMANNE WIKI YA 32 YA MWAKA-B
10/11/2015
Somo: Hek 2:23-3:9
Zab: 34:2-3, 16-17, 18-19
Injili: Lk 17:7-10
Nukuu:
“Yaani, Mungu alimwumba mwanadamu ili apate kutokuharibika, kwa mfano wake mwenyewe, ila ulimwengu uliingiwa na mauti kwa husuda yake Shetani, nao walio wa upande wake hupata kuionja,” Hek 2:23-24

“Bali roho zao wenye haki wamo mkononi mwa Mungu wala maumivu hayatawagusa,” Hek 3:1

“Machoni pa watu walio wajinga walionekana kwama wamekufa, na kufariki kwao kulidhaniwa kuwa ni hasara yao, na kusafirikwao kutoka kwetu kuwa ni uharibifu wao; bali wao wenyewe wamo katika amani,” Hek 3:2-3

“Wakati wa kujiliwa kwao watang’aa, na kama vimulimuli katika mabua makavu watametameta,” Hek 3:7

“Watahukumu mataifa na kuwatawala kabila za watu, naye Bwana atawamiliki milele na milele,” Hek 3:8

“Wenye kumtumaini watafahamu yaliyo kweli, na waaminifu watakaa naye katika upendo; mradi neema na rehema zina wateule wake,” Hek 3:9

Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10 

TAFAKARI: “Kwa unyenyekevu tenda na ishi lililo haki, simama daima katika kweli.”

Wapendwa wana wa Mungu, matendo mema ya mtu hujionyesha katika unyenyekevu wake. Unyenyekevu wa mtu si katika mwono wa kuyachukulia yote sawa hata pale hali siyo sawa, bali ni unyenyekevu katika haki na kweli. Ninapotambua wajibu wajibu wangu nitajitahiji kuutimiza katika kweli na haki. Je, kulifanya hili ni rahisi? La hasha! Nalifanya hilo kwa sababu ndiyo njia sahihi ya kufanya na haki kwangu na wenzangu, na hili ndilo alipendalo Mungu. Hivyo nipo tayari kuyapokea yote katika kweli na haki bila masikitiko kwa sababu ndani yake kuna uzima wa milele na makusudi ya Mungu katika kuniumba kwangu. Nimeumbwa ili niishi milele.

Ni katika umilele huu ndugu yangu, “Mungu alimwumba mwanadamu ili apate kutokuharibika, kwa mfano wake mwenyewe, ila ulimwengu uliingiwa na mauti kwa husuda yake Shetani, nao walio wa upande wake hupata kuionja,” Hek 2:23-24. Salama yetu katika hili ipo pale tunapoishi katika roho ya kweli na haki. “Bali roho zao wenye haki wamo mkononi mwa Mungu wala maumivu hayatawagusa,” Hek 3:1. Ukweli ni kwamba katika ulimwengu huu wa ushindani hakuna anayekubali kwa urahisi hali yake na kujichukulia kwa unyenyekevu kuanza upya akijitazama nguvu na vipawa vyake. Mara nyingi tunajitazama katika maono ya zaidi ya kile tulicho na mwisho wake tunaangukia pua. Maumivu ya kuangukia pua ni makali sana. Ila wengi wetu tupo moyo  radhi kuyapata maumivu hayo kuliko kuupokea ukweli uliopo ndani yake kwa kujipokea katika madhaifu yetu. Huwezi kamwe kusonga mbele kama huyaoni mapungufu yako. Licha ya kwamba kuna uwezekana wa wewe kuwa mtakatifu, yakupasa kujua kwa sasa wewe si malaika wala mtakatifu. Wewe ni binadamu na kwa kuishinda huo ubinadamu wako Mungu mwenyewe atakufanya kuwa mtakatifu kwa mastahili yake.

Kwa kuupokea unyenyekevu huu wa kuukubali ubinadamu wako, ujiandae kwa dhihaka kutoka kwa wapinzani wako. Ukweli ni kwamba wenye kusimama katika kweli na unyonge wao, “Machoni pa watu walio wajinga walionekana kwama wamekufa, na kufariki kwao kulidhaniwa kuwa ni hasara yao, na kusafirikwao kutoka kwetu kuwa ni uharibifu wao; bali wao wenyewe wamo katika amani,” Hek 3:2-3. Je, lipi lililo jema? Je, ni rafiki yako anayekupigia makofu bila kujua undani wako au Mungu anayekuhesabia haki katika kweli na haki? Kumbe ni vyema kusimama katika kweli na haki kwa sababu hakimu  yetu Mungu hana upendeleo.

Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, elewa jambo hili; mwisho wako wa kusimama katika lililo kweli na haki ndiyo furaha na utukufu wa Mungu wetu wa haki na kweli. Tutakuwa wakamilifu kama Mungu alivyo mkamilifu, Mt 5:48, tukitenda yale yanayofanana na Mungu. Hivyo kwenye kuishi katika kweli na haki, “Wakati wa kujiliwa kwao watang’aa, na kama vimulimuli katika mabua. Hii ndiyo furaha tuipatayo kwa Mungu wetu aliye hai, kweli na haki. Na kwa sababu hiyo, “Wenye kumtumaini watafahamu yaliyo kweli, na waaminifu watakaa naye katika upendo; mradi neema na rehema zina wateule wake,” Hek 3:9. Je, nifanye nini basi ili nikae katika upendo wa Mungu?

Wapendwa wana wa Mungu, lazima nielewe kwamba tendo lolote nilifanyalo lapaswa kuongozwa na unyenyekevu wangu. Nielewe nayafanya haya kwa sababu yanipasa kuyafanya tena kwa umakini mkubwa nikitimiza nafasi yangu kama initakavyo kufanya kwa sifa na utukufu wa Mungu. Ni katika ukweli huu Yesu anatuambia, Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk 17:10. Tutajisikia hali hii pale tu tunaposhinda kujifananisha na kujilinganisha na  yale tuyafanyayo. 

Tumsifu Yesu Kristo!


Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu,” Kol 3:12

No hay comentarios:

Publicar un comentario