JUMANNE WIKI YA 31 YA MWAKA-B
3/11/2015
Somo: Rum 12:5-16ab
Zab: 131:1abcde, 2, 3
Injili: Lk 14:15-24
Nukuu:
“Basi kwa
kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa
unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa
huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake;
mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu,
kwa furaha,” Rum 12:6-8
“Pendo na lisiwe na
unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema,” Rum 12:9
“Wabarikini
wanaowaudhi; barikini, wala msilaani,” Rum 12:14
“Mpatane nia zenu
ninyi kwa ninyi. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo
manyonge,” Rum 12:16
“Bwana akamwambia
mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani,
nyumba yangu ipate kujaa,” Lk 14:23
“Maana nawaambia ya
kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu,”
Lk 14:24
TAFAKARI: “Je, Mungu ana nafasi gani katika maisha yangu?”
Wapendwa wana wa Mungu, kinachochukua muda
mwingi katika maisha yako ndicho hatma ya maisha yako. Jaribu kuyatazama maisha
yako, hasa mzunguko wa kila siku na uchambue ni kitu gani kinachochukua muda
wako wingi na upime kama kitu hicho ni kielelezo cha maisha yako ya umilele.
Kama kitu hicho hakina mwelekeo wa maisha ya umilele na yenye kubeba taswira ya
ufufuko, nakusihi ubadili njia na mpango mzima wa maisha yako ukitafuta yaliyo
juu Kristo aliko. “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu
Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1. Kuyatafuta yaliyo juu
Kristo aliko ni kutambua kwa undani mambo makuu mawili: kwanza, tafakari kwa
undani kitu cha kufanya kwa ajili ya Yesu kama shukrani kwake kwa kukukomboa na
kukuweka huru kutoka utumwa wa dhambi. Na pili, fikiria mtumizi sahihi ya
vipaji alivyokujalia Mungu kwa ajili ya wengine. Bila shaka ukiyafanya haya
Mungu atakuwa na nafasi ya kwanza katika maisha yako.
Kwa
upande wa vipaji na karama Mungu alizokujalia, elewa kwamba karama hizo ni kwa
kufaidiana. Kwa maana nyingine, yakupasa kupungua ili Kristo aongezeka. Na hiyo
ndiyo furaha ya Kristo. “Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi
kupungua,” Yoh 3:30. Kama Kristo aliyopungua ili Mungu
ajulikane kwa watu kupitia yeye, nasi yatupasa kupungua ili Kristo aonekane
katika maisha yetu na wale wote wanaotuzunguka na wenye hofu ya Mungu. Hivyo
karama na vipaji alivyotukirimia Mungu kwa upendo wake tuvitoe kwa wengine bila
ya kujibakiza.
Kama ni unabiii tuutoe
kwa Imani kweli pasipo shaka bila hofu. Ndugu yangu, kama kitu ni cheupe sema
waupe wake, na kama ni cheusi sema weusi wake. Mkristo aliyebatizwa na
kushirikishwa mambo makuu matatu, yaani unabii, ukuhani na ufalme wa Kristo
kisha akakaa kimya bila kusema chochote na kufanya chochote anapoona haki za
watu zinakanyagwa anausaliti unabii wake na ukristo wake. Hatupaswa kuwa
bendera fuata upepo. Tusimame imara katika kweli na haki hata kama kuna upepo
au hakuna upepo. Hivyo “Basi kwa kuwa tuna karama
zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii
kwa kadiri ya imani; ikiwa
huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake;
mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu,
kwa furaha,” Rum 12:6-8. Huku ni kutoa hesabu ya karama na vipaji alivyotupa
Mungu kila siku ya maisha yetu.
Wapendwa
wana wa Mungu, katika maisha yetu ya kila siku yatupasa kupiga vita uovu wa
aina yoyote ile. Kuupiga vita uovu ni kuwa na mahusiano mazuri; kwanza na nafsi yako. Pili, na jirani yako.
Tatu, na mazingira yako. Na nne, na
Mungu wako. Kwa kuujenga uhusiano huu epuka sana unafiki. Unafiki ni sumu
katika mahusiano yetu na hayo niliyoyasema. Kweli tu ndiyo itakayokuweka huru,
na upendo ndiyo staha yako. “Pendo na lisiwe na
unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema,” Rum 12:9. Hakuna
sababu ya kupoteza muda wako kwa mambo ya majungu na yasiyo na tija katika
maisha yako. Kuwa mtu wa baraka na neema hata pale unapotendewa ndivyo sivyo
kwa sababu wema huushinda uovu. “Wabarikini
wanaowaudhi; barikini, wala msilaani,” Rum 12:14. Ni vyema katika jambo kama hili ukatumia muda
wako kwa wahitaji na hasa kujishughulisha na wanyonge na kuwa sauti za wasio na
sauti katika jamii inayokuzunguka. Hivyo, “Mpatane nia zenu
ninyi kwa ninyi. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo
manyonge,” Rum 12:16. Kwa kufanya hivi utakuwa umetumia muda wako vizuri hapa
duniani.
Ulimwengu
huu tunaoishi leo ni mwaliko wa
kushiriki wema na furaha ya Mungu. Ni wito wa karamu ya Mungu. Mungu
anahitaji uwepo wetu ulio hai bila ya kuwa na udhuru wowote. Kwa maana nyingine
tusiyatamani mambo yale yanayowapa furaha watu kwa muda mfupi tu kwa sababu
hata wakifa hawaendi nayo. Mzaburi anatuambia jambo hili na kusema, “Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya
nyumba yake itakapozidi. Maana
atakapokufa hatachukua cho chote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata,” Zab
49:16-17. Yakupasa kujali matumizi mazuri ya muda wako ungali hapa duniani.
Wapo wengi kati yetu wanapoteza muda wao katika ufahari na mali walizonunua, Lk
14:18. Wapo wengine kati yetu shughuli zao huwa ndio muhimili wa maisha yao, Lk
14:19. Na wapo wengine kati yetu sharehe zao ndiyo kila kitu
kwao, Lk 14:20. Ila tuelewe ukweli huu kwamba, nyumbani kwa Mungu wetu kuna
nafasi ya kila mmoja wetu. Alituumba kwa sura na mfano wake akijua kila mmoja
atakuwa na nafasi endepo tutamwelekea na kufuata maagizo yake. Hivyo kila siku Mungu anatoa mwaliko
wa kushiriki naye katika karamu. “Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende
barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate
kujaa,” Lk 14:23. Furaha ya Mungu ni kuijaza nyumba yake na kushiriki naye
katika karamu aliyotuandalia, yaani maisha ya umilele.
Mwisho,
Injili ya leo inatupa angalizo kubwa sana. “Maana nawaambia ya
kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu,”
Lk 14:24. Maneno haya ya wazi ya Bwana wetu Yesu Kristo yanakulenga wewe na
mimi ambao kwa ubatizo wetu ni wazi tumealikwa kuurithi ufalme wa Mbinguni. Ila
tutapigwa butwaa kutokuiona mbingu hiyo kwa sababu hatukuishi ahadi zetu za
ubatizo. Huku ni kualikwa kwenye karamu ya Mwana Kondoo na kukataa wazi wazi
kwa sababu zetu binafsi na zisizo za tija. Katika Injili ya leo tunaona watu
watatu walioalikwa kwenye karamu na mwisho walitoa udhuru. Mtu wa kwanza
alikuwa amenunua shamba hivyo alitaka aende kulitazama. Wa pili alikuwa amenunu
ng’ombe jozi tano hivyo alitaka aende kuwajaribu. Na wa mwisho alikuwa ameo na
hivyo hana muda na Mungu zaidi ya mke wake. Je, ni kitu gani kinachokuzui kuwa
karibu na Mungu?
Tusifu Yesu Kristo!
“Bwana
yu karibu na wote wamwitao, Wote wamwitao kwa uaminifu,” Zab 145:18
No hay comentarios:
Publicar un comentario