JUMANNE WIKI YA 1 YA MAJILIO
1/12/2015
Somo: Isa 11:1-10
Zab: 72:1-2, 7-8, 12-13, 17
Injili: Lk 10:21-24
Nukuu:
“Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi
litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda,” Isa 11:1
“Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu,
roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana,” Isa 11:2
“bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya
wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake,
na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya,” Isa 11:4
“Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala
pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto
mdogo atawaongoza,” Isa 11:6
“Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto
aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira,” Isa 11:8
“Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa
ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali
pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu,” Isa 11:10
Saa ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema,
Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha
wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa
ndivyo ilivyokupendeza,” Lk 10:21
“Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu,
wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye
yote ambaye Mwana apenda kumfunulia,” Lk 10:22
TAFAKARI: “Kwake itasimama kweli, haki, Amani, na Upendo.”
Wapendwa wana wa Mungu, kumkomboa mwanadamu kutoka hali
yake ya mateso, mahangaiko na dhambi, Mungu aliye Kweli, Haki, Amani, na Upendo
kwa makusudi makubwa anapenda kuanzisha uhusiano na yule aliyemuumba kwa sura
na mfano wake. Tendo hili la kuujenga uhusiano wa karibu nasi linamshusha Mungu
chini kabisa katika hali ya mwanadamu. Huu ni upendo mkubwa sana kwetu. Kipindi
hiki cha majilio ni kipindi cha kutafakari upendo huu wa ajabu Mungu anaokwenda
kutufanyia. Ikiwa zawadi hii ni kubwa sana kwetu hatuna budi kujiandaa vizuri
mwili na roho ili atakapokuja atukute tupo safi na wenye afya njema hasa roho
zetu.
Kufanikisha mpango huu, Mungu huyu aliye alfa na omega
atachukua hali yetu ya kibinadamu, na hivyo atazaliwa ikiwa ni moja ya
kushiriki hali yetu ya kibinadamu. Jambo hili linatabiriwa na Nabii Isaya. “Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese,
na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda,” Isa 11:1. Je huyu atakayezaliwa ataongozwa na mamlaka
gani? Hakika kwa vile anakuja kuusimika ufalme wa kweli, haki, amani, na
upendo, “roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu,
roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana,” Isa 11:2. Hivi
ndivyo vitendea kazi vyake. Ujio wake kwetu ni hukumu pia ambayo itasimama
katika haki. Hivyo, “kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa
dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya
midomo yake atawaua wabaya,” Isa 11:4
Ujio wa
mfalme huyu ni ujio wa neema na baraka. Anakuja na kusimika mfumo wema na
kuufifisha mfumo wa uovu. Anakuja kuondoa sintofahumu zetu kati yetu wanadamu
na viumbe vingine alivyoviumba. Huyu hakika ni mfalme wa Amani. Hakutakuwa tena
na sintofahumu kati ya wanyama aliowaumba. “Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala
pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto
mdogo atawaongoza,” Isa 11:6. Mwanadamu ataishi kwa amani na hofu haitakuwepo
tena. “Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto
aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira,” Isa 11:8.
Uwepo wa Mfalme huyu wa kweli, haki, amani na upendo utajidhihirisha kwa utukufu wake. Mataifa
yote watamfuata alipo kwa sababu kuna utukufu. “Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa
ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali
pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu,” Isa 11:10. Haya ndiyo atakayoyafanya
na kuujenga tena uhusiano wetu ulioharibiwa na dhambi zetu.
Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na hayo mazuri yote
yaliyotabiriwa na Nabii Isaya kuhusu Mfalme huyu tunayemsubiri kwa hamasa
kubwa, yatawezekana tu kama tutakuwa tayari kutoa ushirikiana naye. Mungu
atukokoti kama Jemedari katili na mwenye silaha za kutisha. Utawala wake ni
utawala wa Upendo. Mungu hakupenda kutuondolea uhuru na utashi wetu wa
kumfuata. Ametuachia haya yote akijua kabisa kwa kuyatumia vizuri ni njia
rahisi ya kumfikia, hata pale tutakapoyatumia vibari itakuwa njia rahisi pia ya
kumrudia tukifanya toba ya kweli na majuto. Kwa hiyo, ‘aliyekuumba wewe pasipo
wewe hawezi kukukomboa wewe pasipo wewe,’ Mt. Agustino wa Hippo.
Siri ya ukweli huu wa kutoa ushirikia na Mungu ili kuwa sehemu salama anausema Yesu
katika Injili ya leo. Siri hii ni kuwa kama watoto wachanga. Mtoto mchanga
huamini yote kuwa salama anapokuwa mikono mwa wazazi wake. Mtoto mchanga kamwe
hawezi kuacha kutabasamu hata kama akiwa mikononi kwa mtu mwovu. Maana yake
mtoto mchanga mara zote anamtazamo chanya. Hii ndiyo hekima ilifichwa ndani ya
watoto wachanga. Yesu anatutaka kuwa na unyenyekevu huu katika kuamini yote
kuwa salama mikononi mwa Mungu. Naye Yesu, “Saa ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema,
Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha
wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa
ndivyo ilivyokupendeza,” Lk 10:21.
Ndugu
yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, leo Yesu anatufunulia jambo la
pekee sana. Kwanza kabisa ni Yeye tu aliyebabidhiwa yote na Mungu. Pili
hatuwezi kumjua Mungu Baba pasipo Yeye mwana, yaani Yesu Kristo. Kwa maana
hiyo, kuwa na Yesu ni kuwa kwenye mikono salama. Naye Yesu, “Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu,
wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye
yote ambaye Mwana apenda kumfunulia,” Lk 10:22. Je, ulipo na ulipojikabidhi
kuna usalama?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa
salama,” Mit 18:10
No hay comentarios:
Publicar un comentario