JUMATANO WIKI YA 33 YA MWAKA-B
18/11/2015
Somo: 2Mak 7:1, 20-31
Zab: 17:1bcd, 5-6, 8b, 15
Injili: Lk 19:11-28
Nukuu:
“Bali ni yeye Muumba
ulimwengu, yeye aumbaye wanadamu na kukikusudia chanzo cha vitu vyote; naye kwa
rehema zake atakurudishieni roho zenu na uzima wenu, kwa kuwa ninyi sasa
mnajihesabu kuwa si kitu kwa ajili ya amri zake” 2Mak 7:23
“Usiogope mwuaji huyu; jionyeshe umestahilika sawasawa na
ndugu zako. Kubali kufa kwako, ili kwa rehema ya Mungu nikupokee tena pamoja na
ndugu zako,” 2 Mak 7:29
“Mimi siitii amri ya mfalme, bali naitii amri ya sheria
waliyopewa baba zetu kwa Musa,” 2Mak 7:30
“Wewe, uliyebuni kila namna ya uovu juu ya Waebrania,
hutaokoka kabisa katika mikono ya Mungu,” 2Mak 7:31
“Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa
mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi,” Lk 19:17
“Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na
kitu atanyang'anywa hata alicho nacho,” Lk 19:26
TAFAKARI: “Mungu tu ndiye wa kuogopwa.”
Wapendwa wana wa Mungu, mfalme Antioko alikuwa tishio
katika utawala wake hasa pale alipojaribu kupora kwa nguvu dhamiri za watu wake
kwa kuwataka wafanya anayoyataka yeye na kusaliti Imani, mila na desturi zao.
Simulizi la Mama Mkabayo aliyekuwa na watoto saba ndani ya utawala huu dhalimu,
anatoa ushuhuda wa kweli juu ya Imani yake. Kutoa ushuhuda juu ya Imani ni
kuelewa kile unachokiamini. Yakupasa kuelewa unachoamini na kwa imani hiyo
uongeza maarifa juu ya ufahamu wako.
Binadamu na fahari zake na mbwembwe zake zote hupita kama
moshi. Fahari ya mwanadamu ni kwa kipindi kifupi sana. Mama wa familia hii
anaonyesha mwanga mkubwa kwa kile anachokifahamu kuhusu Imani yake. Ukweli huu
unamfanya asiogope kuusema na kuusimamia kweli hata katika hali ya hatari.
Wakuheshimiwa na kuabudiwa ni Mungu kwa sababu, “ni yeye Muumba ulimwengu, yeye
aumbaye wanadamu na kukikusudia chanzo cha vitu vyote; naye kwa rehema zake
atakurudishieni roho zenu na uzima wenu, kwa kuwa ninyi sasa mnajihesabu kuwa
si kitu kwa ajili ya amri zake” 2Mak 7:23. Usia huu anautoa kwa wana wake ambao
walikataa katu katu kula nyamba ya nguruwe ambayo kadiri ya Imani yao ni haramu
na najisi. Nguruwe hakuliwa kwa sababu, “amepasuliwa ukwato lakini hacheui,
huyu ni najisi kwenu msile nyama zao, wala mizoga yao msiiguse,” Kumb 14:8.
Mama huyu anaposhawishiwa na mfalme amshawishi mtoto wake
wa mwisho ili akubali masharti ya mfalme na kumwokoa katika kifo, anamwambia
mtoto wake maneno ya hekima na ujasiri. “Usiogope mwuaji huyu; jionyeshe
umestahilika sawasawa na ndugu zako. Kubali kufa kwako, ili kwa rehema ya Mungu
nikupokee tena pamoja na ndugu zako,” 2 Mak 7:29. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.
Kijana huyu katika udogo wake anawashangaza wengi pale anapoupokea ukweli juu
ya imani yake bila hofu. Naye anawaambia, “Mimi siitii amri ya mfalme, bali
naitii amri ya sheria waliyopewa baba zetu kwa Musa,” 2Mak 7:30. Wangapi leo
tunaujasiri wa kusimama katika imani ya kweli? Hata kama hilo halitoshi,
wangapi leo tu majasiri kuidai haki yako iliyoporwa? Wengi wetu tumekuwa wa
woga hata kushishwa kujua haki zetu, na hata pale tunapozijua haki zetu
tunaingiwa na hofu kuzidai. Woga huu ndio
utumwa wetu.
Wapendwa wana wa Mungu, uovu kamwe huwezi kutawala daima na
kwa muda wote. Wema wa Mungu ndiyo utakao tawala daima. Mara zote katika
historia ya wokovu wa mwanadamu, Mungu aliweza kuwa sauti kwa wale wasio na
sauti. Mungu anauwezo pia kulisimamisha jiwe likaongea badala yake na kufikisha
ujumbe kwa wale wanaohodhi madaraka si kwa kuwasaidia waliowapa dhamana, bali
kwa kujifaidisha wenyewe. Hivyo ujumbe wa mwisho kwa kijana huyu anautoa kwa
watawala wote wanafikiri wanauwezo wa kuchukua nafasi ya Mungu. “Wewe,
uliyebuni kila namna ya uovu juu ya Waebrania, hutaokoka kabisa katika mikono
ya Mungu,” 2Mak 7:31. Hakika adhabu yao ni kubwa!
Tunaposimama katika
Imani ya kweli na hasa pale tunapokuwa na ufahamu wa kile tunachokiamini, ni
Mungu tu wa kuogopwa. Bwana wetu Yesu Kristo anatuambia jambo hili kwa undani.
Naye anasema, “Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili,
kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi. Lakini nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni
yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam,
nawaambia, Mwogopeni huyo,” Lk 12:4-5. Hakuna
kama Mungu wetu aliye hai.
Kila mmoja wetu kapewa
uwezo wa kupambana na mazingira yoyote yale atakayokutana nayo. Uwezo huu siyo
wa kuufungia sehemu fulani na kutokufanya chochote. Injili ya leo inafafanua
jambo hili kwa mifano ya watu watu waliopewa fedha za biashara na mtu mmoja
Kabaila. Aliyepewa kumi alizalisha nyingine kumi, aliyepewa tana alizalisha
nyingine tano, na aliyepewa moja hakufanya chochote zaidi ya kulalamika. Naye
anasema, “Kwa
maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna
usichopanda,” Lk 19:21. Mara nyingi huwa
tunajihukumu wenyewe kwa kutokuviendeleza vipaji alivyotupa Mungu na kubaki
kutamani vipaji vya wengine. Wapo pia wengine kati yetu ambao muda wao wote
maishani ni kuyatafuta yale ambayo yapo nje yao, na mwisho wa siku wanabaki
kuwa vivuli vya wengine na kukosa furaha ya kweli.
Kumbe
leo Kristo anatuambia tuthamini aliyotupatia Mungu, na tuyaendeleze kwa sababu,
“Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye
na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho,” Lk 19:26. Usipo kithamini ulicho
nacho na kukiendeleza kitachukuliwa na kupewa mwingine. Hatua ya kwanza ya
kuthamini kile ulichonacho huanza kwa kuwa mwaminifu kwa yale madogo madogo ya
kila siku na hasa kwa yale tunayopewa dhamana nayo. Watumwa wale waliofanya
vizuri walipewa hakikisho la utendaji wao. “Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile
ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi,”
Lk 19:17. Je, wajua vipaji vyako na uwezo wako?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi ikiwa ninyi,
mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu
aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?” Mt 7:11
No hay comentarios:
Publicar un comentario