jueves, 26 de noviembre de 2015

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 34 YA MWAKA-B

IJUMAA WIKI YA 34 YA MWAKA-B
27/11/2015
Somo: Dan 7:2-14 
Zab: Dan 3:75, 76, 77, 79, 80, 81
Injili: Lk 21:29-33
Nukuu:
Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye,” Dan 7:13 

Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14

 “Wakati iishapo kuchipuka, mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba majira ya mavuno yamekwisha kuwa karibu. Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea, tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu,” Lk 21:30-31 

Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe,” Lk 21:32-33

TAFAKARI: Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe,”

Wapendwa wana wa Mungu, bila shaka neno “WOSIA” siyo geni masikioni mwako. Wosia ni maneno ya hekima na busara ambaya hutolewa mara chache sana na mtu ambaye yupo mwisho wa kitu fulani, kwa faida na maarifa ya wale anaowaacha katika hali fulani. Wosia ni tokeo la mang’amuzi mapana ya maisha ambayo kwayo kwa pamoja ujumuisha na kutoa tathmini ya yale yaliyopita, ya sasa, na yajayo. Wosia utolewa mara chache sana kwa sababu siyo wote katika hali yao ya mwisho, mfano mwisho wa uhai wao, ufunuliwa umauti wao. Wengi hubaatika kutoa Wosia kutokana na kuuugua kwa muda mrefu na kwa mateso makali, na kwa njia hiyo ufunuliwa umauti wao. Hata hivyo wapo wengine kutokana na maisha yao ya utulivu na tafakuri wakichukulia kila jambo na maana yake katika maisha yao, ufunuliwa pia yale yatarajiwayo kutokea. Hawa nao utoa wosia.

Katika Injili ya leo, Yesu Kristo anatupa wosia kwa yale yatakayojiri ikiwa ni hitimisho la nyakati. Yesu anatumia mifano ya kawaida kulingana na mazingira ya watu wake. Katika jambo hili la kusoma alama za nyakati, Yesu anatumia mfano wa mti aina ya Mtini. Naye anasema, Wakati iishapo kuchipuka (Mitini), mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba majira ya mavuno yamekwisha kuwa karibu. Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea, tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu,” Lk 21:30-31. Ufalme huu wa Mungu ni ule aliofunuliwa katika ndoto Nabii Danieli. Ni ufalme ambao utaushinda uovu kwa wema kama tulivyosoma katika simulizi la ndoto ya Danieli kuhusu wale wanyama. Ni ufalme ulioshuka kutoka mbingu, yaani, neno kufanywa mwili, kumwilishwa na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Hivi ndivyo Danieli alivyofunuliwa katika ndoto: Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye,” Dan 7:13.

Ufalme na utawala huu ushasimikwa kuanzia pale ilipoaanza safari nzima ya wokovu wa mwanadamu, neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Huu ni ukweli usiopitwa na wakati. Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe,” Lk 21:32-33. Ukweli huu wa neno kutokupitwa na wakati ulishafunuliwa pia kwa njia ya ndoto aliyooteshwa Nabii Danieli. Hapa Danieli anamzungumzia Kristo Yesu, mmoja aliye mfano wa mwanadamu aliyekuja na mawingu ya mbingu na kusema,  Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14. Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, wewe upo katika ufalme upi?

Wapendwa katika Kristo, kuwa katika  ufalme wa Kristo ni kufanana na Kristo katika kufikiri, kuona, kutenda, na kuishi. Yesu anatuambia sote kwamba, “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate,” Lk 9:23. Zeozi au mtihani huu wa maisha si wa  mara moja tu, bali kila siku ya maisha yetu. Na kuwa kweli mwanafunzi wa Yesu ni kuuchukua msalaba na kumfuata Yesu. Yesu analisema jambo hili wazi kabisa bila kuficha kitu. Naye anasema,Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu,” Lk 14:27. Je, waufahamu msalaba wako? Tazama vilema vyako! Tazama udhaifu wako! Tazama changamoto zako katika maisha agano unayoyaishi leo na sasa!

Tumsifu Yesu Kristo!


Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina,” Rum 11:36

No hay comentarios:

Publicar un comentario