viernes, 6 de noviembre de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 32 YA MWAKA-B

JUMAPILI YA 32 YA MWAKA-B
8/11/2015
Somo I: 1Fal 17:10-16
Zab: 146:7, 8-9, 9-10
Somo II: Ebr 9:24-28
Injili: Mk 12:38-44
Nukuu:
Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe,” 1Fal 17:12

Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao,” 1Fal 17:13 

Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi,” 1Fal 17:14 

Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya,” 1Fal 17:16

Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu,” Ebr 9:24
kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu,” Ebr 9:28

“Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu; ambao hula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa,” Mk 12:38-40

Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina,” Mk 12:43 

maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia,” Mk 12:44

TAFAKARI: Mwenye jicho la ukarimu atabarikiwa; Maana huwapa maskini chakula chake.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, karibuni katika tafakari yetu hii ya leo, ambapo leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 32 ya mwaka “B” wa Kanisa. Masomo yote matatu, na hasa somo la kwanza na Injili, yanatuelekeza kuyatafakari kwa undani maneno haya, Mwenye jicho la ukarimu atabarikiwa; Maana huwapa maskini chakula chake,” Mit 22:9. Ukarimu wa mtu si tokea la wingi wa vitu alivyokuwa navyo, bali ni ule moyo wa utayari wake katika kutoa na kushirikisha wengine hata kile kidogo alichokuwa nacho. Huu ndio mtazama na sura halisi ya somo letu la kwanza na Injili.

Wapendwa katika Kristo, somo la kwanza tumepewa simulizi la Nabii Eliya na yule Mama Mjane wa Sarepta na mwanaye. Eliya katika sumulizi hili ni muhitaji kwenye njaa sana. Mama huyu wa Serepta ni muhitaji katika maana ya ujane wake na na uchache wa kile alichokuwa nacho ukilinganisha na ukame uliokuwa unawaandana kwa muda mrefu. Eliya anaomba atengenezewe mkate ale. Katika hali hii Mama huyu anaonyesha moyo wa utayari wake katika kutoa na kushirikisha kile kidogo alichokuwa nacho. Mjane huyu angeweza kukataa na kuonyesha choyo.

Pamoja na hali hilo, anamjibu Eliya na kusema,  Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe,” 1Fal 17:12. Eliya Nabii na mtumishi wa Mungu anatazama tendo hili kwa jicho la ukarimu na kumwambia, “Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao,” 1Fal 17:13. Eliya katika tendo hili anatufundisha kuwa na Imani thabiti kwa kile tukifikiricho na kukitamka kutoka midomoni mwetu pasipo kuwa na shaka juu ya Mungu wetu aliye hai.

Eliya Nabii anayatamka maneno hayo na kusimama juu ya neno lile, Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi,” 1Fal 17:14. Matokea ya Imani thabiti ni neema na baraka tuzipatazo kwa kile tulichonuia kwa Imani.  Hivyo, Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya,” 1Fal 17:16. Mungu wetu ni hai na uwapa masikini chakula chake.

Mama huyu Mjane katika ukarimu wake na moyo wa utayari katika kutoa kidogo alicho nacho, anafanana na Mjane aliyetoa sentí mbili na kuhesabiwa haki kwa kutoa zaidi kuliko wote katika sanduku la hazina. Yesu Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina,” Mk 12:43. Leo watu wengi uonekana wanatoa kiasi kikubwa tu cha pesa au mambo mbalimbali ila kwa msukumo usio wa ibada na kweli itokayo ndani mwao. Hata kile wakitoacho wakati mwingine ni yale mabaki na vilivyowazidi. Ukweli huu unajidhihirisha hata nyakati zile za Yesu. Maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia,” Mk 12:44. Je, unachomtolea Mungu kama sadaka ya shukrani yako ni halali kwa Mungu wetu aliye hai?

 Wapendwa tukiwa wafuasi wa Kristo, Yesu anatupa angalizo tusije dongoka katika mtego wa waandishi. Naye Yesu anatuambia, “Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu; ambao hula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa,” Mk 12:38-40. Unafiki huu ni mbaya sana. Angalizo hili linatuelekeza pia kumtazama vizuri Kristo katika maisha yake na sadaka ya maisha yake aliyoitoa bila kujibakiza. Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu,” Ebr 9:24. Ndani na katika Kristo kuna uondoleo la dhambi zetu na ukombozi kwa sadaka yake pale msalabani. Kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu,” Ebr 9:28. Je, unacho chochote cha kujivunia zaidi ya dhambi zako?

Wapendwa katika Kristo, kama yote mazuri ni mali yake Mungu, kilicho chetu ni dhambi zetu wenyewe. Na kama tulivyo navyo ni mali ya Mungu, basi yatupasa kumtolea kile kilicho bora zaidi hata katika umasikini wetu. Maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao,” 2Kor 8:2. Huku ndiko anakokuzungumzia Mtume Paulo kupanda kwa ukaribu na kuvuna kwa ukaribu, na kupanda haba na kuvuna haba. Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu,” 2Kor 9:6. Hatupaswi kuutazama udogo na umasikini wetu katika kutoa kama tendo la ukarimu na la Ibada. Kuangalia udogo ulio nao na umasikini wako katika kutoa ni kujifungia neema na baraka za Mungu. Hakuna Masikini asiyekuwa na kitu cha kumpa Mungu, na hakuna Tajiri asiyekuwa mwitaji. 

Katika nyumba moja ya malezi, waseminari hupewa kila mwezi Tsh 20,000 kwa matumizi yao madogo madogo. Mseminari Yohane ni mmoja nyumba hii na kama ilivyo kawaida alienda mjini na kujifanyia manunuzi yake na kujibakiza Tsh 2000 kama nauli ya kurudi nyumba ya malezi, na shilingi elfu moja anunue vocha.

Akiwa anaeleka kitu cha daladala Yohane alikutana na Mama mmoja akiwa amembeba mtoto mchanga. Mama huyu alimsalimia Yohane huku akimfunua mtoto wake na kusema, “Kaka naomba shilingi 500 nauli nimkimbize mtoto wangu hospitali. Hali yake ni mbaya sana.” Yohane aliingiwa na hurama na kumpa mama yule shilingi 1000 iliyokuwa kwaajili ya vocha ingawa karoho kalimuuma.

Basi Yohane aliingia kwenye daladala na kuelekea nyumbani. Akiwa ndani ya daladala Kondakta alihitaji nauli, na Yohane alitoa elfu moja aliyokuwa nayo huku Kondakta akimwambia chenchi yako nitakupa utakaposhuka. Yohane alishuka kwenye kituo chake na Kondakta alimrudishia chenchi yake. Jambo la kushangaza ni kwamba Yohane alirudishiwa Tsh 9700, badala ya Tsh 700 ikiwa nauli ni shilingi 300. Yohane alipiga kelele ili daladala ile isimame arudishe kile kilichokuwa kimeongezeka bila mafanikio. Kondakta badala yake alimpa ishara ya kuwa hakuna kilicho haribika.
Wapendwa wana wa Mungu, hakuna aliyetoa kwa ukaribu na kuwa masikini.

Tumsifu Yesu Kristo!


Maana utumishi wa huduma hii hauwatimizii watakatifu riziki walizopungukiwa tu, bali huzidi sana kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo Mungu;kwa kuwa mkijaribiwa kwa utumishi huo, wanamtukuza Mungu kwa ajili ya utii wenu katika kuikiri Injili ya Kristo, na kwa ajili ya ukarimu wenu mliowashirikisha wao na watu wote,” 2Kor 9:12-13

No hay comentarios:

Publicar un comentario