jueves, 19 de noviembre de 2015

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 33 YA MWAKA-B

IJUMAA WIKI YA 33 YA MWAKA-B
20/11/2015
Somo: 1Mak 4:36-37, 52-59
Zab: 1Nya 29:10bcd, 11abc, 11d-12, 12bcd
Injili: Lk 19:45-48
Nukuu:
“sasa adui zetu wamevunjwa nguvu, basi tupande tukapatakase mahali patakatifu na kupatabaruku,” 1Mak 4:36

“Kulikuwa na furaha kubwa kwa watu, na aibu ililetwa na mataifa iliondolewa,” 1Mak 4:58
“Yuda na ndugu zake, na jamii yote ya Israeli, walikata shauri ya kuwa siku  za kuitabaruku madhabahu ziadhimishwe kwa furaha na shangwe kila mwaka kwa wakati wake, muda wa siku nane tangu ishirini na tano ya mwezi Kislevu,” 1Mak 4:59

akiwaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi,” Lk 19:46 

Naye akawa akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza,” Lk 19:47 

TAFAKARI: “Na kilichowekwa wakfu na kibaki kwa ajili hiyo daima.”

Wapendwa wana wa Mungu, wakfu ni hali au namna ya kujitenga kwa ajili maalumu na yenye malengo na uhusiano na Mungu. Ni tendo la kujisalimisha binafsi. Kwa maneno mengine ndiyo kuabudu kwenyewe. Kilichowekwa wakfu huwa kwa ajili ya matumizi yenye uhusiano na Mungu. Kitu hicho huwa ni kwa ajili ya Mungu. Kila kitu kilichowekwa wakfu katika Israeli kitakuwa chako,” Hes 18:14. Hekalu au nyumba ya kuabudia na vilivyomo ndani yake huwekwa wakfu kwa matumizi hayo tu. Na wana wa Israeli, na makuhani na Walawi, na watu wengine katika hao waliohamishwa, wakaiweka wakfu nyumba ya Mungu kwa furaha,” Ezr 6:16. Ni kwa mwono huu  na hitaji hili tunaona katika somo la kwanza Yuda na ndugu zake wanatambua uhumuhi wa sehemu ya kuabudu na kutolea sadaka za kuteketezwa ambayo hawakuwa nayo walipokuwa chini ya maadui zao. “Sasa adui zetu wamevunjwa nguvu, basi tupande tukapatakase mahali patakatifu na kupatabaruku,” 1Mak 4:36. Lazima wapatakase na kupatabaruku kwa sababu walinajisiwa na kutumika visivyo.

Tendo hili la kuurudisha tena uhusiano na Mungu ni tendo la furaha na historia. Hali hiyo inawakuta Yuda na ndugu zake. “Kulikuwa na furaha kubwa kwa watu, na aibu ililetwa na mataifa iliondolewa,” 1Mak 4:58. Unaporudisha uhusiano na Mungu uliopotea ni tendo la kuanza upya na Mungu na kuweka mikakati yenye malengo ya hai na yenye kubeba umilele ndani yake. Hivyo, “Yuda na ndugu zake, na jamii yote ya Israeli, walikata shauri ya kuwa siku  za kuitabaruku madhabahu ziadhimishwe kwa furaha na shangwe kila mwaka kwa wakati wake, muda wa siku nane tangu ishirini na tano ya mwezi Kislevu,” 1Mak 4:59. Kusherehekea matukia yenye uzima wa Imani ndani yake ni kusheherekea uhai.

Umuhimu wa kile kilichowekwa wakfu na kwa ajili ya matumizi rasmi yaliyotengwa na ajili hiyo tunaona kwenye injili ya leo. Yesu anaingia hekaluni na kukuta yatendwayo hayaendani na kile kipasacho kutendwa kwenye hekalu. Naye anawaambia, “Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi,” Lk 19:46. Nyumba ya Mungu pamoja na kutolea sadaka na shukrani zetu ni nyumba ya sala. Yote yale yasiyokuwa na uhusiano wa sala, shukrani, sadaka, na mengine kama hayo, hayapaswi kufanyika mahali hapa. Kabla ya kuteswa, kufa, na kufufuka kwake Bwana Yetu Kristo alijiweka wakfu kwa ajili yetu na kutufanya kuwa viungo vyake akiwa yeye ndiye Mwili, yaani Kanisa. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli,” Yoh 17:19. Kanisa kama mwili wa Kristo, ni kwa namna hiyo ya kutakaswa kupitia sakramenti ya ubatizo nasi tunakuwa viungo vya Kristo. Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake,” 1Kor 12:12, 27. Kwa maana hii, miili yetu imewekwa wakfu ndani na katika Kristo. Hivyo matendo yote machafu katika mwili ni kwenda kinyume na kutengwa huko kuliko wekwa kwa ajili ya Kristo.Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha!” 1Kor 6:15.

Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na miili yetu kuwa ni viungo vya Kristo na kuwekwa wakfu kwa ajili ya Kristo, mwili wa mtu ni hekalu la Roho Mtakatifu.  Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu,” 1Kor 6:19-20. Ndugu yangu, na kilichowekwa wakfu na kibaki kwa ajili hiyo daima.

Tumsifu Yesu Kristo!


Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi,” 1Kor 3:17

No hay comentarios:

Publicar un comentario