lunes, 23 de noviembre de 2015

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 34 YA MWAKA-B

JUMANNE WIKI YA 34 YA MWAKA-B
24/11/2015
Somo: Dan 2:31-45
Zab: Dan 3:57, 58, 59, 60, 61
Injili: Lk 21:5-11
Nukuu:
            Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele,” Dan 2:44

Haya mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa,” Lk 21:6 

Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao,” Lk 21:8 

Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi,” Lk 21:9 

TAFAKARI: “Fahari na mamlaka za kibinadamu zitapita, utawala wa Mungu utadumu hadi mwisho wa nyakati.”

Wapendwa wana wa Mungu, licha ya kweli kwamba maisha yetu sisi wanadamu katika ulimwengu huu ni ya muda mfupi, maisha hayo kama yalivyo ni fumbo. Mzaburi anasema, Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara,” Zab 90:10. Nafikiri leo Mzaburi huyu angekuwa anaandika haya angesema vingine, miaka 40, na mwenye nguvu miaka 50. Umri wa kuishi has anchi za ulimwengu wa tatu umeshuka sana. Hata hivyo maisha ni fumbo kwa sababu kifo kwa kila mmoja wetu kimefichwa licha ya kwamba ipo siku na kwa wakati wake kila mmoja atafikia kikomo chake hapa duniani. Ndiyo kusema kwamba, “Fahari na mamlaka za kibinadamu zitapita, utawala wa Mungu utadumu hadi mwisho wa nyakati.” Hivyo ni vyema kila mmoja wetu akajishughulisha na mambo yale yatakayojenga uhusiano mzuri na Muumba wake, jirani yake, na mazingira yake. Uzuri wa ulimwengu huu na fahari yake vyote vitapita na kusahaulika. Licha ya kwamba maisha ya mwanadamu hapa duniani kuwa kikomo chake, mwanadamu huyu hawezi sahaulika na Muumba wake kwa sababu kaumwambwa kwa sura na mfano wa Muumba wake, Mwa 1:26. Mungu hawezi kujisahau mwenyewe. Ni kwa maana hiyo na sababu hii, ipo siku kila mmoja ataitajika kutoa hesabu yake mbele za Mungu.

Wakati wa Yesu wapo walio vutwa sana na ulimwengu huu na fahari yake kama ilivyo leo. Wapo waliolitazama Hekalu ya Yerusalemu na kupambwa kwake wakaishia hapo tu wasione zaidi ya Hekalu hilo. Yesu anatutaka tutazame zaidi ya kile tunachokiona. Naye Yesu aliwaambia, Haya mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa,” Lk 21:6. Tunachotakiwa kukitazama ni uwepo wa ufalme wa kweli wa Mungu na siyo fahari na mamlaka za kibinadamu tu.  Nabii Danieli anatoa tafsiri kwa mfalme kuhusu kubomoka kwa sanamu ile iliyojengwa kwa mikono ya wanadamu licha ya uzuri iliyokuwa nayo. Hii ni kutofautisha falme na mamlaka za wanadamu na ufalme ule wa kweli wa Mungu, ufalme ambao wadumu milele na milele. Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele,” Dan 2:44. Kile kibebacho ufahari wa kibinadamu na kisichotoka kwa Mungu hakina umilele.

Kutokana na ukweli huu kuna hatari ya watu kuja na tafsiri zao kuhusu mwisho wa nyakati kwa lengo hasa la kuwaogopesha watu kwa manufaa yao binafsi. Yesu Kristo anatoa angalizo na kusema, “Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao,” Lk 21:8. Hawa ndio wale wajulikanao kama manabii wa uongo kadiri ya Maandiko Matakatifu. Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule,” Mt 24:24. Je, leo si jambo la kawaida mtu kujiita nabii, askofu, mtume, n.k?

Mambo haya, mfano uaskofu, ukasisi, nk, hakuna anayejitwalia, bali hutwaliwa na Mungu peke yake, ikiwa ni hitaji la Kanisa mahalia kama Mwili wa Kristo inapoonekana inafaa na mhusika anastahili kadiri ya mamlaka iliyopewa Kanisa na Kristo mwenyewe. Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi,” Ebr 5:1. Hata Kristo hakujitwalia mwenyewe kuwa kuhani Mkuu.Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa,” Ebr 5:5. Tujihadhari sana na manabii hawa wa uongo. Mwisho wa nyakati hauji upesi kama tusemavyo au kufikirivyo licha ya mwamba kabla ya mwisho huo kutatokea matokeo ya kutisha. Yesu leo anatuambia ukweli wa jambo hili, Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi,” Lk 21:9. Tunapoona mtu anapanga hadi tarehe ya matukio haya ya mwisho wa nyakati yeye kaupata wapi ukweli huo zaidi ya hiki anachotuambia Kristo? Ndugu yangu tuliyesafiri sote katika tafakari hii usisahau maneno haya ya wahenga wetu: “Wajinga ndio waliwao.”

Tumsifu Yesu Kristo!

“Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe,” Mdo 1:7

Nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele na hekima na maarifa; kumcha Bwana ni hazina yake ya akiba,” Isa 33:6

No hay comentarios:

Publicar un comentario