domingo, 15 de noviembre de 2015

TAFAKARI: JUMATATU YA WIKI YA 33 YA MWAKA-B

JUMATATU WIKI YA 33 YA MWAKA-B
16/11/2015

Somo: 1Mak 1:10-15, 41-43, 54-57, 62-63
Zab: 119:53, 61, 134, 150, 155, 158
Injili: Lk 18:35-43
Nukuu:
“Hata hivyo wengi katika Israeli walikaza nia zao kwa uthabiti wasile vitu vilivyo najisi. Waliona afadhali kufa kuliko kuitiwa unajisi kwa vyakula au kulivunja agano takatifu. Wakafa,” 1Mak 1:62-63

Akapiga kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu,” Lk 18:38

Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu,” Lk 18:39

Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona,” Lk 18:40-41 

Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya,” Lk 18:42 

TAFAKARI: “Dhamiri yako iliyo hai na safi ndiyo ponya yako.”

Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na miongozo mingi tunayokutana nayo katika jamii tunayoishi, na hata maisha yale tuliyojichagulia kuishi iwe mlei, mtawa, mtawa na mkleri, “dhamiri yako iliyo hai na safi ndiyo ponya yako.” Kutokana na uongozi mbaya wa Mfalme Antioko wa Israeli kipindi kile Makabayo, walikuwepo wayahudi wachache waliosimama katika kweli iliyoongozwa na dhamiri zao hai na safi bila kuterereka. Mfalme huyu akiwa na nia ya kushirikiana na mataifa jirani alijikuta anaingia mikataba ya kipagani na kumwasi Mungu aliye hai na kweli. Hivyo mila na desturi za Kiyahudi zilipuuziwa na Torati kutokufuatwa na mwisho Sabato kunajisiwa.

Maisha ya Kiyahudi yalionekana kutiliwa mkazo kwenye mambo makuu matatu; moja, umuhimu wa Hekalu Takatifu kama sehemu pekee ya kuabudu na kumtokea Mungu shukrani zao na sadaka za kuteketezwa. Pili, Maandiko Matakatifu, yaani Torati. Na mwisho milki ikiwa ni ardhi pamoja na uongozi madhubuti uliowekwa na Mungu mwenyewe. Hivyo baada ya Mfalme Antioko kupotoka na mwenda nje wa yale atakayo Mungu, wapo wayahudi wachache walioapa kutokwenda kinyume na mwongozo wa Mungu. “Hata hivyo wengi katika Israeli walikaza nia zao kwa uthabiti wasile vitu vilivyo najisi. Waliona afadhali kufa kuliko kuitiwa unajisi kwa vyakula au kulivunja agano takatifu. Wakafa,” 1Mak 1:62-63. Hapa ndipo tunapoona nafasi ya dhamiri hai na safi katika lile lililo kweli na haki.

Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, ni vyema ukafahamu kuwa hakuna mtu anayeishi mwenyewe kama kisiwa. Tunahitajiana na kusaidiana katika kukabiliana na mambo mbalimbali katika maisha. Hata hivyo hitaji hili kamwe lisichukue kile ulicho kilicho hai na safi, yaani, dhamiri yako, ambayo ndiyo wewe mwenyewe. Maandiko Matakatifu ambayo ni moja ya msingi na chimbuko la mafundisho yote ya Kanisa Katoliki, yanaongelea ukweli huu kama tusomavyo kutoka barua ya Mtume Paulo kwa Warumi, Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea; katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu,” Rum 2:14-16. Dhamiri hai na safi ndiyo ponya yako hata kwa wale ambao hawana habari kuhusu Kristo.

Wapendwa katika Kristo, Mungu wetu ni Mungu wa wanadamu wote licha ya tofauti zetu za kiimani. Hakuna anayeishi katika ulimwengu huu kwa sababu yake mwenyewe. Kila mmoja wetu anayochapa ya Mungu ndani yake. Ulimwengu huu ukiwemo na vyote vilivyomo ni Mali yake Mungu. “Au je! Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Siye Mungu wa Mataifa pia? Naam, ni Mungu wa Mataifa pia; kama kwa kweli Mungu ni mmoja, atakayewahesabia haki wale waliotahiriwa katika imani, nao wale wasiotahiriwa atawahesabia haki kwa njia ya imani iyo hiyo,” Rum 3:29-30. Ukweli ni kwamba kila anayeongozwa na mwenye dhamiri hai na safi ataokolewa siku ya mwisho.

Mafundisho ya Kanisa hasa tunaposoma Katekisimu ya Kanisa Katoliki, namba 847 inafundisha juu ya dhamiri hai na safi ambapo hata wale wasiomjua Kristo ndiyo ponya yao. Ukweli huu pia umefafanuliwa vizuri katika mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano, Konstitusio ya Kichungaji juu ya Kanisa katika Ulimwengu wa leo, “Gaudium Et Spesteaches,” “Furaha na Matumaini,” inaelezea ukweli huu kama ifuatavyo; “Jambo hilo haliwahusu wakristo tu bali pia wanadamu wote wenye mapenzi mema, ambao neema ya Mungu hufanya kazi mioyoni mwao, kwa namna isiyoonekana. Maana Kristo alikufa kwa ajili ya watu wote na wito halisi wa binadamu ndio mmoja, ule wa kimungu. Kwa hiyo lazima tuwe na wazo kwamba Roho Mtakatifu anawajalia watu wote uwezekano wa kushiriki fumbo la kipasaka, kwa jinsi anayoijua Mungu,” (no. 22)

Miongozo ya kibinadamu na mwonekano wake unaweza kutunyamazisha hapa na pale kwa kuikandamiza dhamiri iliyo hai na safi kuelekea lililo kweli na haki. Kelele hizo kamwe zisiwe kizuio cha kiu na kweli iliyopo ndani ya mioyo yetu. Leo katika Injili tunaona watu wachache wakijaribu kuzuia dhamiri iliyo hai na safi ya mtu mmoja kipofu aliyekuwa ameketi kando ya njia wakati Yesu akipita. Aliposikia habari ya Yesu alipiga kelele na kusema, “Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu,” Lk 18:38. Jitihada za huyu kipofu zinajaribiwa kuzimwa na baadhi ya watu. Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu,” Lk 18:39. Dhamiri iliyo hai na safi ya Kipofu huyu ikiongozwa na imani aliyokuwa nayo, inakuwa sababu ya uponyaji wake. Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona,” Lk 18:40-41. Imani hii iliyodhabiti na yenye kuongozwa na dhamiri hai na iliyosafi juu ya Mwana wa Mungu, Kristo Yesu, inakuwa uponyaji wake. Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya,” Lk 18:42. Dhamiri hai na safi hukuzwa na kuelimishwa hasa pale tunapopenda kutenda mema kwa vile twatambua jambo jema ni jema kama lilivyo na linastahili kutendwa kila mmoja wetu na hasa zaidi mwenye hofu ya Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo!


Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri,” Rum 13:5

No hay comentarios:

Publicar un comentario