domingo, 29 de noviembre de 2015

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 1 YA MAJILIO

JUMATATU WIKI YA 1 YA MAJILIO
30/11/2015
Somo: Isa 2:1-5
Zab: 121: 1-2, 3-4a (4b-5, 6-7), 8-9
Injili: Mt 8:5-11
Nukuu:
Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu,” Isa 2:3 

Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe,” Isa 2:4 

Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye,” Mt 8:7

Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli,” Mt 8:10 

TAFAKARI: Ajaye ni Bwana wa Amani.”

Wapendwa wana wa Mungu, Mwokozi tunayemtazamia kwa hamu ni Bwana wa Amani atakayetufundisha njia zake na kueneka katika mapito yake. Sheria yake kuu ni UPENDO. Ni wakati wa kuyajenga upya mahusiano yetu na Bwana huyu wa Amani. Ni Bwana wa Amani wa wataifa yote, na ulimwengu mzima. Nabii Isaya anasema habari za Mkombozi huyu: Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu,” Isa 2:3.

Amani ya Mkombozi huyu inaendana pia na haki. Hivyo ajapo lazima ipite hukumu ya haki, na ndipo atakapousimika utawala wake wa Amani, Haki, na Upendo. Ili mambo haya yatendeke katika utawala wake yatupasa kubadili namna yetu ya kufikiri na kutenda. Ulimwengi wa leo vita na hasa ugaidi vinashamiri kwa nguvu kubwa sana na uhai wa mwanadamu ikiwa ni pamoja na amani vipo reheni. Nabii Isaya anasema, Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe,” Isa 2:4. Tunahitaji sana kwa sasa utawala wa Mkombozi huyu. Lengo la Mungu kuumba ulimwengu pamoja na mambo mengine, aliuumba ili pawe sehemu salama kwa ajili ya uhai wa viumbe vyote alivyoviumba na kwa namna ya pekee Mwanadamu aliyemuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27.

Kujenga mahusiano mapya na Mungu ni pamoja na kuwa na imani dhabiti naye. Leo katika Injili Yesu anakutana na mtu mmoja, Akida, aliyekuwa anauguliwa na mtumishi wake ugonjwa wa kupooza. Akida huyu anamwomba Yesu aende kumponya mgonjwa wake. Yesu anamjibu, Nitakuja, nimponye,” Mt 8:7. Akida huyu akitambua uwezo wake na nafasi aliyokuwa nayo, na ule uwezo wa Yesu, bado anatambua kuwa umbali na uwepo wa Yesu aviweza kumzuia kumponya mtumishi wake. Akida anamtaka Yesu aseme neno tu na mgonjwa wake atapona. Hii ndiyo imani thabiti na isiyokuwa na shaka. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli,” Mt 8:10. Je, waamini kuwa Yesu aweza kutenda maajabu ndani yako? Jenga uhusiano mpya naya kuanzia sasa!

Tumsifu Yesu Kristo!

“Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii,” Lk 17:6


No hay comentarios:

Publicar un comentario