ALHAMISI WIKI YA 33 YA MWAKA-B
19/11/2015
Somo: 1Mak 2:15-29
Zab: 50:1b-2, 5-6, 14-15
Injili: Lk 19:41-44
Nukuu:
“Wewe u kiongozi, mtu mkuu, maarufu katika mji huu. Una
wana wako na ndugu zako wa kujiweka upande wako. Basi, tangulia wewe, uitimize
amri ya mfalme, kama walivyofanya watu wote wa mataifa,” 1Mak 2:17-18
“Hata mataifa yote katika milki ya mfalme wakimtii,
wakiacha kila mtu dini ya wazee wake na kuchagua kuzifuata amri za mfalme,
lakini mimi sivyo. Mimi na wanangu na ndugu zangu tutaishika njia ya agano la
baba zetu,” 1Mak 2:19-20
“Kila aliye na juhudi kwa ajili ya sheria na kutaka
kulitetea agano, na anifuate!” 1Mak 2:27
“akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii,
yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako,” Lk 19:42
“watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako,
wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako,” Lk 19:44
TAFAKARI: “Ni afadhali kuwa moto au baridi, kuliko kuwa vuguvugu
katika Imani.”
Wapendwa wana wa Mungu, bila shaka mnamfahamu vizuri sana
Chura. Je, waweza niambia chura amesimama au kachuchumaa? Kama tunavyoshindwa
kujua mkao wa chura, ndivyo mtu aliye na imani vuguvugu alivyo. Imani ya mtu ni
ufunuo uliopo kati yake na muumba wake. Mungu ndiye mwanzishaji wa uhusiano huo
wa kiimani, ambaye anajifunua kwa mwanadamu. Mwanadamu aupokeapo mwito huo
ndipo tunapoanza kuzungumzia imani na dini ya mtu. Hivyo muunganiko huu si
tendo la kirafiki kati ya mtu na mtu ambayo lawezwa kubadilishwa kadiri ya
maoni ya mtu na mtazamo wake.
Hali hii inamkuta Matathia na wanawe pale ambapo mfalme
nataka kuchukua nafasi ya Mungu katika fumbo zima la ufunuo huu ambao tokeo
lake ni Imani ya mtu. Matathia anaonyesha uthabiti katika imani, na anaelewa
kile anachokiamini. Waliotumwa na mfalme kumshawishi atolee sadaka kwa miungu
kama walivyokwisha kufanya wengine, wanamwambia, “Wewe u kiongozi, mtu mkuu,
maarufu katika mji huu. Una wana wako na ndugu zako wa kujiweka upande wako.
Basi, tangulia wewe, uitimize amri ya mfalme, kama walivyofanya watu wote wa
mataifa,” 1Mak 2:17-18. Pamoja na kushawishiwa kwa maneno mazuri ya kuvutia
Matathia hakubadili msimamo wake
Matathia anapinga
ushawisho huo na kuonyesha msimamo wake kiimani. “Hata mataifa yote katika
milki ya mfalme wakimtii, wakiacha kila mtu dini ya wazee wake na kuchagua
kuzifuata amri za mfalme, lakini mimi sivyo. Mimi na wanangu na ndugu zangu
tutaishika njia ya agano la baba zetu,” 1Mak 2:19-20. Matathia anaenda mbali
zaidi hasa pale anapoona na kumwua myahudi mwenzake alipojaribu kuisaliti Imani na mapokeo ya
wazee wao. Imani hujanga mfumo mzima wa maisha ya mtu. Ni jambo la kushangaza
kabisa hasa katika jamii yetu tunapoona baadhi yetu licha ya matakatazo ya
imani zao juu ya uovu, wapo mbele kushabikia lililo ovu hata kulitetea.
Bila shaka jamii yetu leo wana ugonjwa wa “UDHAHAMO,”
Upungufu wa Dhamira Hai Moyoni. Iweje leo unaona binadamu mwenzako anauwawa
kikatili nawe waona jambo hili ni sawa na halisema kitu chochote ndani ya nafsi
yako? Inaingiaje akili leo kwa mkono wako unamwua binadamu mwenzako kikatili na
bado unajiona upo sawa? Unajionaje upo sawa pale unapotoa ushauri juu ya
kumdhuru mwenzako na hata kupoteza uhai wake? Wengi husema mtu fulani kauliwa
kinyama. Mnyama hawezi kumwua mnyama mwenzake wa familia ile ile kikatili hivyo.
Huwezi kuona Simba akimwua simba mwenzake kikatili kama anavyofanya binadamu
kwa binadamu mwenzake. Tuyaonayo kwa wanadamu leo ni ugonjwa wa UDHAHAMO.
Binadamu aliyekufa dhamiri ni sawa na Gari jipya lisilokuwa na breki. Hata kama
dereva wake kafuzu vizuri katika fani ya udereva lolote laweza kutokea njiani
na kuwashangaza wengi.
Mshango kama huo unamkuta Yesu anapoutazama mji wa
Yerusalemu na wakazi wake na uzuri wa Hekalu. Kipindi cha Yesu, Wayahudi wengi
hawakuwa wanaishi yale yaliyokuwa yanampendeza Mungu. Torati haikufuatwa kama
ilivyo, bali walifuata tafsiri ya Torati na masimulizi ya wazee, TALMUD, ambao
ulikuwa ukweli wa Mungu ulipotoshwa. Yesu alijua mwisho wa kila kitu kuhusu mji
huu wa Yerusalema na fahari yake. Aliutazama, “akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii,
yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako,” Lk 19:42. Salama ya mji
huu wa Yerusalemu ilikuwa ni kupatanishwa na Mungu kwa kuyaacha matendo yao
mabaya na kumrudia Mungu. Hekalu lenyewe lilikuwa kituo cha biashara. “Akaingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale
waliokuwa wakifanya biashara, akiwaambia,
Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa
pango la wanyang'anyi,” Lk 19:45-46. Michanganyo katika Imani ni hatari sana.
Hata Yesu hakupenda michanganyo hiyo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Walakini mwisho wa agizo
hilo ni upendo utokao katika moyo safi na dhamiri njema, na imani isiyo na
unafiki. Wengine
wakiyakosa hayo wamegeukia maneno ya ubatili,” 1Tim 1:5-6
No hay comentarios:
Publicar un comentario