IJUMAA WIKI YA
32 YA MWAKA-B
13/11/2015
Somo: Hek
13:1-9
Zab: 19:2-3,
4-5ab
Injili: Lk
17:26-37
Nukuu:
“Huenda ilikuwa kwa kupendezwa na uzuri
wake walivyodhania viumbe hivyo kuwa ni miungu, basi na wajue kadiri gani
Bwana, Mfalme wao, avipitavyo; kwa maana Yeye aliye asili ya uzuri ndiye
aliyeviumba,” Hek 13:3
“Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika
siku zake Mwana wa Adamu,” Lk 17:26
“Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo
ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee
nyuma,” Lk 17:31
“Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na
ye yote atakayeiangamiza ataiponya,” Lk 17:33
Akawaambia, Ulipo
mzoga, ndipo watakapokutanika tai,” Lk 17:37b
TAFAKARI: “Je,
nimejiandaa vyema?”
Wapendwa wana wa Mungu, ni kawaida kwa
kila mmoja wetu kujiandaa kwa matukio mbalimbali ya maisha kutoka hatua moja na
kwenda nyingine. Leo napenda tutafakari matukio matatu muhimu kwa kila mmoja
wetu, na tutazame pia ni kwa namna gani tunajiandaa katika matukio hayo.
Matukio hayo ni kuzaliwa, tukio agano, na kifo. Ni jambo la kawaida
kusheherekea au kukumbuka kwa kusheherekea siku ya kuzaliwa. Tunasheherekea
tukio hili kwa kutambua na kumshukuru Mungu kwa zawaidi ya uhai na maisha
aliyotukirimia bila kipimo. Hapa tunajiandaa vyema na wakati mwingine kwa
gharama za juu kabisa.
Tukio la pili katika maisha ni ‘tukio
agano.’ Tukio agano ni pale mtu anapofikia wakati fulani na kuamua namna
atakavyoishi na kufuata mfumo mwingine wa maisha. Kwa walei ni maisha ya ndoa,
na watawa na makleri ni maisha wa wakfu. Wengi tunatumia muda mwingi sana
kujiandaa katika tukio hili. Hapa pia tunatumia gharama nyingi sana na wakati
mwingine tunakufuru.
Tukio la tatu na la mwisho ni kifo.
Tukio hili kadiri ya tathimini lina maandalizi hafifu sana licha ya kwamba ni
tukio muhimu sana, na wakati mwingine ni zito kupita matukio yote. Unaweza
kujiandaa kwa tukio la kwanza bila la pili, ila huweza kujianda kwa tukio la
kwanza na la pili na ukakwepa tukio hili la tatu hata kama hutaki. Si lazima
kuzaliwa na si lazima kufanya ‘tukio agano,’ lakini kama umezaliwa, na hata
kama hutaki kufanya ‘tukio agano,’ lazima utakufa. Si nia yangu kukuogopesha
ila ndio ukweli. Kwa nini basi tunaingiwa na upofu na usahaulifu wa kuweka
umuhimu wa kutosha katika tukio hili la tatu?
Masomo yetu ya leo yanatupa majibu
halisi ya ukweli kuhusu tukio hili la tatu, yaani kifo. Somo la kwanza linatupa
jibu la kwa nini binadamu hupuuza ukweli kuhusu kifo. Ulevi wa starehe na anasa
na kudhani sisi ndio kila kitu utusahaulisha kuhusu tukio hili la tatu, na
hivyo kuyafanya maandalizi yake kuwa hafifu. “Huenda ilikuwa kwa kupendezwa na
uzuri wake walivyodhania viumbe hivyo kuwa ni miungu, basi na wajue kadiri gani
Bwana, Mfalme wao, avipitavyo; kwa maana Yeye aliye asili ya uzuri ndiye
aliyeviumba,” Hek 13:3. Hata kama tunaufurahia ulimwengu huu kwa vyovyote vile
yatupasa kuelewa yupo mmiliki halali wa vitu vyote. Sisi ni wamiliki wa muda
mfupi tu na tutaviacha kama waliotutangulia walivyo viacha. Tulivikuta na
tutaviacha.
Kifo wakati mwingine uonekana kipo
mbali sana hasa pale tunapozama katika anasa na malimwengu. Wakati wa Nuhu na
hata Lutu habari za Mungu na uwepo wake hazikuonekana kama kitu cha pekee kwa
wengi hasa wale walioishi katika mfumo wa “ponda mali.” Ila hata kama hatuna
hisia na Mungu, Yeye hupo hai na anayaona yote tuyafanyayo. Siku ya kuzungumza
na kila mmoja wetu kwa wakati wake inakuja. Hivyo, “Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika
siku zake Mwana wa Adamu,” Lk 17:26. Itakapofika siku hiyo tutapigwa na
mshangao kwa vile hatutakuwa tumejiandaa vya kutosha kwa sababu tu ya kupuuzia
kama walivyompuuzia Nuhu kuitengeneza Safina ilhali hapakuwa na dalili yoyote
ya mvua, mto, ziwa wala baharí, ila Mungu aliinyeeshea duania kutoka chini.
Mshango mwingine ni kwamba tukio hili la kifo litamkuta
kila mtu pale alipo kwa mshangao. Ni mara ngapi tunaondokewa na wapendwa wetu
ilhali hatukuwa kumeagana vizuri au kuongea nao kwa urefu? Mara nyingi
tunabakiwa na ‘ninge..’ zisizo na idadi. “Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo
ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee
nyuma,” Lk 17:31. Hapa ni pale tunaposema, “lo! Nilikuwa naye leo asubuhi na
sana hatunaye tena!” Hata tukio kama hilo halisemi chochote kuhusu maandalizi
yako?
Yesu anatupatia jibu la mkwamo huu, na kutuweka mkono
salama tusijepigwa na mshangao. Naye
anasema, “Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na
ye yote atakayeiangamiza ataiponya,” Lk 17:33. Kuiponya nafsi katika kuingamiza
ni kuiridhia nafsi kwa yale inayoyataka. Ni pale nafsi inapoegemea katika mwili
na kufanya matendo ya mwili. “Basi matendo ya mwili
ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina,
faraka, uzushi, husuda, ulevi,
ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama
nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo
hawataurithi ufalme wa Mungu,” Gal 5:19-21. Huku ni kuiponya nafsi katika
kuiangamiza.
Ndugu
yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, kuiangamiza nafsi katika kuiponya
ni pale nafsi yako inapoegemea roho, na kutenda matendo ya roho yenye tunda la
roho. “Tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili,
uaminifu, upole, kiasi; juu ya
mambo kama hayo hakuna sheria,” Gal 5:22-23. Huku ni kuiangamiza nafsi yako
katika kuiponya. Je,
mzoga wako utakuwa wapi?
Baada
ya mafundisho haya mazito ya Injili ya leo, watu walitaka kujua hayo
yatatendeka wapi? Yesu anatujibu hivi, “Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai,” Lk 17:37b. Kwa
maana nyingine mwisho wako utategemea ishi yako. Hivyo kama nafsi yako katika
ishi yako itaegemea mwili, ndivyo hivyo mwisho yako itakuwa katika matendo ya
mwili. Tunaoambiwa watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa
Mungu. Vile vile kama nafsi yako itaegemea roho yako, basi mwisho wako itakuwa
tunda la roho. Tunaambiwa juu ya mambo kama hayo hakuna sheria, kwani kwa
kuishi hivyo ndiyo sheria yenyewe aipendayo Mungu. Ni maisha ya kweli na haki.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ni faida gani basi
mliyopata siku zile kwa mambo hayo mnayoyatahayarikia sasa? Kwa maana mwisho wa
mambo hayo ni mauti,” Rum 6:21
No hay comentarios:
Publicar un comentario