JUMATATU WIKI YA 1 YA MAJILIO
30/11/2015
Sikukuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume
Somo: Rum 10:9-18
Zab: 19: 8-11
Injili: Mt 4:18-22
Nukuu:
“Kwa sababu, ukimkiri
Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu
alimfufua katika wafu, utaokoka,” Rum 10:9
“Kwa maana kwa moyo
mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu,” Rum
10:10
“Kwa maana hakuna
tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri
kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka,” Rum 10:12-13
Basi
imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo,” Rum 10:17
“Lakini nasema, Je!
Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno
yao hata miisho ya ulimwengu,” Rum 10:18
“Naye alipokuwa akitembea
kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na
Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi,” Mt 4:18
“Akawaambia,
Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu,” Mt 4:19
“Mara wakaziacha nyavu
zao, wakamfuata,” Mt 4:20
TAFAKARI: “Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.”
Wapendwa wana wa Mungu, mtihani mkubwa kwa mtu yeyote yule
siyo hii tunayoifanya mashuleni na hata vyuoni, bali ni mtihani huu wa
“kuamua,” uwe nini katika maisha yako. Si rahisi kufanya maamuzi hayo na
kuchukua njia nyingine mpya kabisa usiyojua kifuatacho huko mbeleni. Mtu huwa
na uhakika kwa kile alichokiishi jana na anachokiishi leo na sasa. Huu ni
mzunguko wa kawaida katika maisha ya kila mmoja wetu. Kuwekeza maisha yako yote
kwa kile usichokijua humjengea mtu hofu. Leo Kanisa linapofanya sikukuu za
watakatifu na kwa maana ya pekee leo sikukuu ya Mt. Andrea Mtume, ni kusadifu
yale waliyoyaamua na kuyaishi na ndiyo ukuaji wa Kanisa na uhai wake. Walifanya
uamuzi wa kuacha yale waliyoyazoea na yaliyokuwa yanawapa usalama na kufuata
kile wasichokijua wakijisalimisha kabisa katika hicho. “Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata,” Mt 4:20.
Mtume
Andrea akiwa na ndugu yake Simoni Petro walikuwa wavuvi. Kazi hii iliwapa
usalama na mahitaji yao ya kila siku. Yesu anawaita wamfuate nao wanaacha pale
pale waliyokuwa wanafanya na kumfuata. Uamuzi huu ni mzito sana. “Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona
ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife
baharini; kwa maana walikuwa wavuvi,” Mt 4:18. Kazi hii ndiyo iliyowapa makate
wao wa kila siku. Embu fikiri leo kwa kazi unayofanya hasa wale wanaopata
kipato kilichonona, aje mtu tu na kukuambia nifuate. Nini kitakuwa kitu cha
kwanza kufanya? Bila shaka utaanza kumpiga maswali mazito na mwisho kumchukulia
kama mwendawazimu hivi. Mitume hawa wanayaacha yote na kumfuata. Yesu “Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu,” Mt
4:19. Kuwa wavuvi wa watu ni mabadiliko mazima ya mfumo na namna ya kutenda na
kuishi. Hapa ndipo tunaposema Mitume hawa walikuwa majitu ya sifa. Mioyo yao
ilikuwa na ushupavu wa hali ya juu. Ni vigumu sana mtu kuubadili mfumo wa
maisha yake aliouzoea.
Yesu Kristo alikuwa kila kitu katika
maisha yao. Walijua pia hakuna wokovu pasipo
Kristo. Iliwezekanaje hivyo haraka? Bila shaka kwa nguvu na neema za Mungu
iliwezekana pale walipoonyesha utayari wao wa kumsikia Yesu na kumfuata. Mtume
Paulo anatuambia, “kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na
kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka,” Rum 10:9.
Jambo hili la kujisalimisha kabisa mikono mwa Yesu halikuwa na mashaka ndani ya
mioyo ya hawa Mitume ingawa halikuwa jambo rahisi kufanya. “Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa
hukiri hata kupata wokovu,” Rum 10:10
Wapendwa
wana wa Mungu, sababu nyingine ya uwepo wetu hapa duniani licha ya kwamba ni
kwa muda mfupi, ni kuwaelezea watu wengine habari njema ya wokovu wetu. Wewe
uliyebahatika kuifahamu siri hii usibaki nayo mwenyewe. Ni furaha kubwa sana
mbele ya Mungu kama watakuwepo baadhi ya watu waliofika mbinguni kwa sababu
ulitumia muda wako kuwaelezea habari njema ya wokovu wetu. Mitume waliona na
kuupokea wajibu huu mkubwa. “Maana sisi hatuwezi
kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia,” Mdo 4:20. Neno hili sasa si
kwa Wayahudi tu, ila lapaswa kusikika duniani kote. Kwa kupitia Kristo sote
tumeunganishwa na kuwa familia moja yenye mastahili sawa mbele ya Mungu, na
warithi wa ufalme wake. “Kwa maana hakuna
tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri
kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka,” Rum 10:12-13. Mitume
kwa namna ya pekee waliuona wajibu huu mkubwa wa kulihubiri neno la Mungu
pasipo woga.
Msingi wa
haya yote ni Imani ile waliyokuwa nayo Mitume, na kwa namna ya pekee leo Mama
Kanisa anapofanya sikukuu ya Mt Andrea Mtume. Hivyo chanzo cha imani hiyo ni kusikia neno la Kristo. “Basi
imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo,” Rum 10:17.
Je, watu watasikiaje bila kuambiwa? Kumbe leo pia tunakumbushwa mimi na wewe
kwamba kwa sakramenti ya ubatizo wetu inatufanya kuwa wamisionari. Ni wajibu wa
kila mbatizwa kulitangaza neno la uzima na wokovu kwa watu wote. “Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao
imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu,” Rum 10:18. Hivi
ndivyo walivyofanya Mitume, na leo Kanisa limesimama likiwa Kristo ndiye msingi
wake Imara, na Mitume. Mimi na wewe tunadaiwa kuyatoa maisha yetu kama
walivyofanya mitume ili habari njema iwafikie wote ambao bado hawajasikia. Je,
nifanye vipi? Anza hapo hapo ulipo! Kuwa chumvi na mwanga ili uso wa Kristo
uonekana katika maisha yao na yako.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Maana, ijapokuwa
naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu
nisipoihubiri Injili!” 1Kor 9:16
No hay comentarios:
Publicar un comentario