JUMATATU
WIKI YA 32 YA MWAKA-B
Kutabarukiwa
Basilika la Laterani
9/11/2015
Somo
I: Eze 47:1-2, 8-9, 12
Zab:
46:2-3, 5-6, 8-9
Somo
II: 1Kor 3:9-11, 16-17
Injili:
Yoh 2:13-22
Nukuu:
“Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali
itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu
maji haya yamefika huko maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi po
pote utakapofikilia mto huo,” Eze 47:9
“Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande
huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda
yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake
yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake
yatakuwa ni dawa,” Eze 47:12
“Maana sisi tu wafanya
kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu,” 1Kor 3:9
“Maana msingi mwingine
hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu
Kristo,” 1Kor 3:11
“Kama mtu akiliharibu
hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni
takatifu, ambalo ndilo ninyi,” 1Kor 3:17
“akawaambia wale
waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa
nyumba ya biashara,” Yoh 2:16
“Wanafunzi wake
wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila,” Yoh 2:17
“Yesu akajibu,
akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha,” Yoh
2:19
“Lakini yeye alinena
habari za hekalu la mwili wake,” Yoh 2:21
TAFAKARI:
“Nasi ni shamba la Mungu Jengo la Mungu, Msingi wake ni Yesu Kristo.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa
anasheherekea siku ya Kutabarukiwa Basilika la Laterano. Historia fupi kuhusu
Basilika hii ya Laterano:
Laterano (kwa Kilatini Lateranus)
ni mtaa wa Roma maarufu hasa kwa sababu kulikuwa na Ikulu mojawapo la Kaisari Konstantino Mkuu. Lakini pamoja na ukweli huo, inaonyesha kwamba Plautius
Lateranus ilikuwa familia moja tajiri katika Falme ya Roma. Plautius
alituhumiwa na Mfalme Nero kwa kula njama dhidi ya Mfalme. Matokeo ya tuhuma
hii ilikuwa kunyang’anywa na kugawanywa kwa mali za familia hii. Hivyo, Mfalme
Constantino baada ya yeye kuruhusu Ukristo katika Dola la Roma (Hati ya Milano 313) ikulu liligeuzwa kuwa
Kanisa ambalo liliwekwa
wakfu na Papa Melkiades (314),
na mpaka leo linaheshimiwa na Kanisa Katoliki kama
Kanisa kuu la Jimbo la Roma
na la ulimwengu mzima.
Tofauti na wanavyodhani wengi, Ukulu wa Papa ni katika kanisa hilo, si
katika Basilika la Mt. Petro huko Vatikano. Jina rasmi ni kanisa la
Kristo Mkombozi, lakini watu wanaliita kwa kawaida kanisa la Mt. Yohane
(Mbatizaji) kwa kuwa nyuma yake ipo batizio
kuu tena juu ya ukuta wake wa mbele kandokando ya sanamu ya marumaru ya Yesu, zipo zile za Yohane Mbatizaji na Mtume Yohane.
Ndani, juu ya altare kuu yanatunzwa mafuvu ya
vichwa vya Mtume Petro na Mtume Paulo. Ndani ya kanisa hilo mara
tano ulifanyika mtaguso ambao
kila mmoja unahesabiwa na Kanisa Katoliki kuwa Mtaguso Mkuu. Mpaka uhamisho wa Avignon (karne ya 14) Mapapa
waliishi karibu na kanisa hilo, na mpaka leo seminari kuu ya jimbo (pamoja
nachuo kikuu cha Kipapa cha
Laterano) iko nyuma yake. Eneo lote ni nje ya mamlaka ya nchi ya Italia na linahesabiwa kuwa
sehemu ya nchi huru ya Vatikano.
Wapendwa pamoja na
maelezo hayo mazuri kuhusu historia ya Kutabarukiwa kwa Basilika hii, masomo
yetu leo yote matatu yanatutaka kutafakari na kuona kuwa “Nasi ni shamba la
Mungu Jengo la Mungu, Msingi wake ni Yesu Kristo,” kwa Sakramenti ya Ubatizo.
Msingi wa Kanisa hili ni Kristo wenyewe aliyelisimamisha kwa mateso, kifo na
ufufuko wake. “Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka,
isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo,” 1Kor 3:11. Kwa
mateso, kifo, na ufufuko wake Kristo
miili yetu imehuishwa na kuwa hekalu la Roho Mtakatifu.
Kwa kuwa
tumehuishwa na kuupokea huo Utakatifu hatupaswi kulibomoa hekalu hili kwa hatia
yoyote ile, na hasa dhambi. Yeyote yule atakayeliharibu hekalu hili, Mungu naye
atamharibu. Leo hekalu hili la Roho Mtakatifu linafanyiwa vituko vya aibu na
vya kusikitisha. Embu fikiri mtu anapomkata vipande vipande mwenzake kwa sababu
ya pesa na utajiri. Embu fikiri ni mimba ngapi zinaharibiwa na kutolewa kwa
kila sekunde. Embu tazama ni wazee wangapi na walemavu wa ngozi wanavyouwawa.
Hakika, “Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo.
Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi,” 1Kor 3:17. Tuone
thamani kuulinda uhai na kuutetea. Uhai ni mali ya Mungu na zawadi ya Mungu
kwetu.
Hekalu
hili, yaani kila Mbatizwa ni Takatifu. Na tunapoongelea Kanisa kwa maana ya
kwanza kabisa siyo Jengo bali ni kila aliyebatizwa. Na tunapoongelea Kanisa hai
maana yake ni kila aliyebatizwa na anayeishi ahadi zake za ubatizo vyema katika
kujali na kuwajibika ipasavyo. Kujali na kuwajibika huku kunachukua pande zote
mbili, yaani, Kanisa kama Wabatizwa, na Kanisa Kama Jengo. Sura na mtazamo huu
wa Kanisa la Mungu ni kama ilivyo shilingi. Mfuasi wa Kristo hawezi kujitenga
na kuchagua kuwa sehemu moja tu na kuacha nyingine. Akifanya hivyo atakuwa bado
hajakamilika.
Injili ya
leo inatupa ufafanuzi mzuri kuhusu mtazamo huu wa Kanisa iliouelezea hapo juu.
Yesu alipoingia hekaluni alikutana na mambo ya ajabu sana. Hekaluni watu
waliokuwa wakiuza ng'ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha. Kwa hali
aliyoikuta na kuiona ilimbidi kuchukua hatua za haraka mara moja. Yesu “akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya;
msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara,” Yoh 2:16. Hili ni Kanisa Takatifu Kama Jengo yapaswa
kufanyika yaliyo matakatifu. Yesu hakuona haya kuvitawanya vyote vilivyokuwa
ndani ya hekalu lile.
Wayahudi walipotaka kupewa
Ishara ili wajue ni kwa mamlaka gani anayafanya hayo, “Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika
siku tatu nitalisimamisha,” Yoh 2:19. Hapa tunaona maana halisi ya Kanisa na
Msingi wake, yaani, Kanisa kama Wabatizwa wote, na Msingi wake ni Kristo
mwenyewe. Kwa maneno hayo ya Yesu kwamba
walivunje hekalu naye katika siku tatu atalisimamisha, “yeye alinena habari za
hekalu la mwili wake,” Yoh 2:21.
Habari
njema ya Kanisa hili ni yale aliyokwisha yatabiri Nabii Ezekieli kama
tulivyosoma na kusikiliza somo la kwanza. Kwanza
kabisa katika habari njema hiyo, Kanisa ni sakramenti ya wokovu wetu. Kwa
kupitia Masakramenti yake tunapata neema na kutujazwa uhai. Nabii Ezekieli
anatumia lugha ya picha, “mito yenye maji yaponyayo,” yaani, kwa tafsiri
tungesema ‘Masakramenti.’ “Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali
itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu
maji haya yamefika huko maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi po
pote utakapofikilia mto huo,” Eze 47:9. Mto huu yaani, Kanisa kwa sasa upo
duniani kote, na Wabatizwa wote wenye kuishi ahadi zao za ubatizo wanazidi
kuponywa na kupata neema za Mungu. “Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande
huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka,
wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa
sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni
chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa,” Eze 47:12. Kwa vile Msingi wa Kanisa
hili katika mfano huu wa mto na maji yake yenye kuponya ni Kristo, kupata neema
na baraka hizi yakupasa kuwa ndani na katika Kristo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Maana hakuna mtu
anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye
anavyolitendea Kanisa,” Efe 5:29
No hay comentarios:
Publicar un comentario