JUMANNE WIKI YA 33 YA MWAKA-B
17/11/2015
Somo: 2Mak 6:18-31
Zab: 3:2-3, 4-5, 6-7
Injili: Lk 19:1-10
Nukuu:
“Lakini yeye aliikaza nia yake madhubuti, nia iliyostahili
umri wake na jadi yake, na mvi zake stahivu, na mwendo wake wa adili tangu
utoto wake katika kuzishika amri takatifu zilizotolewa na Mungu,” 2Mak 6:23a
“Na hata nikiepukana na adhabu ya wanadamu sasa, lakini
sitaweza kuepukana na mikono ya Mwenyezi, nikiwa hai au nimekufa,” 2Mak 6:26
“Basi, nikitoa maisha yangu sasa kwa ushujaa, nitajionyesha
kuwa nimeistahili miaka yangu mingi, na kuwaachia vijana mfano wa kufa mauti ya
fahari kwa hiari na kwa uthabiti, kwa ajili ya amri takatifu zenye heshima,”
2Mak 6:27-28
“ingawa ningaliweza kuepukana na mauti, lakini ninavumilia
maumivu makali mwilini mwangu; hata rohoni mwangu ninayavumilia kwa furaha kwa
sababu ya kicho changu kwake,” 2Mak 6:30
“Hivyo alikufa; na kwa kufa kwake aliacha mfano wa unyofu
na ukumbusho wa wema, si kwa vijana tu, ila kwa jamii yote ya taifa lake,” 2Mak
6:31
“Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia,
Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako,” Lk 19:5
“Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema,
Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi,” Lk 19:7
“Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya
mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila
namrudishia mara nne,” Lk 19:8
“Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa
sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu,” Lk 19:9
“Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile
kilichopotea,” Lk 19:10
TAFAKARI: “Afadhali kufa kwa
heshima kuliko kuishi kwa unajisi.”
Wapendwa wana wa Mungu, ingawa leo dunia inashuhudia
uvunjifu mkuwa wa haki za binadamu, na matokea yake tunaona idadi kubwa ya
wakimbizi ndani na nje ya nchi zao, haya hayakuwa makusudi ya Mungu katika
uumbaji wetu na milki aliyotupatia. “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke,
mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani,
na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu,
akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza,” Mwa 1:28; 2:15. Lakini
jambo la ajabu leo ni kwamba wapo baadhi ya binadamu wenzetu wanaojihesabia
haki kuliko wengine na kwenda kinyume kabisa na mpango wa Mungu juu ya uumbaji
na milki ya vile alivyo viumba.
Upofu wa ubinafsi na uchu wa madaraka umekuwa leo viatu vya
kukanyagia haki za watu na hasa wanyonge. Je, katika hali kama hii yatupasa
kukubaliana na udhalimu na kufa na tai shingoni? Somo letu la kwanza
linatuambia hapana kwa ushuhuda wa Eleazari aliyesimama katika kweli. Kweli
hiyo ndiyo inayokuweka huru. “Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka
huru. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli,” Yoh 8:32, 36.
Eleazari anakataa katu katu kula nyamba ya nguruwe kadiri ya makatazo ya
Maandiko Matakatifu kama yanavyoweka wazi jambo hilo. Kuila nyama ya nguruwe
ilikuwa ni najisi kwa sababu “Nguruwe amepasuliwa ukwato lakini hacheui, huyu
ni najisi kwenu msile nyama zao, wala mizoga yao msiiguse,” Kumb 14:8, Law
11:7. Kwa ukweli huu, Eleazari hayupo tayari kwenda kinyume cha Maandiko Matakatifu
na mila na desturi za jamii yake. Hivyo yupo tayari kwa lolote na hakuwa na
woga wa kufa. “Lakini yeye
aliikaza nia yake madhubuti, nia iliyostahili umri wake na jadi yake, na mvi
zake stahivu, na mwendo wake wa adili tangu utoto wake katika kuzishika amri
takatifu zilizotolewa na Mungu,” 2Mak 6:23a
Wapendwa wana wa Mungu, unavyoishi hapa duniani waweza kuwa
moja ya ukweli huu, yaani kuwa Mhenga, au Lihoka. Mhenga ni yule anayeacha
“legacy,” kitu cha kuigwa, na Lihoka, “bad spirit” ni yule asiyeacha kilicho
kizuri cha kuigwa kwenye jamii. Kwa kuacha kitu cha kuigwa Eleazari anasema
mbele ya watesi wake, “Basi, nikitoa maisha yangu sasa kwa ushujaa,
nitajionyesha kuwa nimeistahili miaka yangu mingi, na kuwaachia vijana mfano wa
kufa mauti ya fahari kwa hiari na kwa uthabiti, kwa ajili ya amri takatifu
zenye heshima,” 2Mak 6:27-28. Wapo wengi sana
miongoni mwetu wanafikwa na mauti ya mtindo huu. Ni masikitiko makubwa
leo kwamba kilichokuwa habari njema si habari, bali kile kisicho habari ndicho
habari. Lakini historia inatuambia kwamba hakuna uovu wowote uliodumu katika
umilele wake. Imani pia inatufundisha kwamba kisicho toka kwa Mungu, na kwa
ajili Mungu na watu wake kamwe hakiwezi dumu katika fahari yake hata kama
kikipambwa kwa mbwembwe zote za ulimwengu huu.
Je, katika hali kama hii ni vyema kuusaliti ukweli na
kukumbatia mitazamo na sheria za wanadamu? Je, ni aheri nikubali ili niwe
salama kumfurahisha mtesi wangu? Jibu ni hapana! Ni kusimama katika kweli na
haki kama alivyo simama Eleazari na kusema, “Na hata nikiepukana na adhabu ya
wanadamu sasa, lakini sitaweza kuepukana na mikono ya Mwenyezi, nikiwa hai au
nimekufa,” 2Mak 6:26. Kuna faida gani kuipata nafuu ya leo na kuishi kwa
kudharaulika na kuikosa mbingu kwa kuisaliti kweli na haki? Afadhali kufa kwa
heshima kuliko kuishi kwa unajisi. Pamoja na kutengwa na washauri marafiki zake
na kubaki mwenyewe, Eleazari hakuisaliti dhamiri yake hai na safi. Kwa kutunza
heshima yake na uzee wake Eleazari hakubadili msimamo wake uliojijenga katika
kweli na haki. Naye anasema kwa ushujaa, “ingawa ningaliweza kuepukana na
mauti, lakini ninavumilia maumivu makali mwilini mwangu; hata rohoni mwangu
ninayavumilia kwa furaha kwa sababu ya kicho changu kwake,” 2Mak 6:30. Pasipo
njia Mungu huifanya njia hata kama kwa sasa lililo ovu litashinda. Ila Mungu wa
haki na kweli atausimamisha utawala wake ulio wa kweli na haki kwa kuridhiwa na
wana wa Taifa lake.
Injili ya leo tunaona simulizi la makutano ya kati ya Yesu
na Zakayo. Zakayo hamwoneyi Yesu aibu pamoja na watu kuyajua madhaifu yake na
ufupi aliokuwa nao. Bado anaona salama yake ipo kwa Kristo tu na siyo mitazama
ya wale walikuwa wanamzunguka. Ili amwone Yesu, Zakayo alipanda juu ya mkuyu. “Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama
juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani
mwako,” Lk 19:5. Tendo hili la Yesu linawashangaza wengi na wengine
wananung’unika. “Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema,
Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi,” Lk 19:7. Kwa utayari wa Yesu kwenda
nyumbani kwa Zakayo, kwa furaha aliyokuwa nayo Zakayo hakuweza kuificha. Hivyo
Zakayo anayaweka yote wazi mbele ya Yesu. “Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama,
Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa
hila namrudishia mara nne,” Lk 19:8. Hii ni toba ya kweli na maungamo ya wazi
mbele ya Yesu aliye sasa njia, kweli na uzima. Maungamo haya ya kweli toka
moyoni mwa Zakayo yanaifunua furaha na upendo wa Mungu kupitia mwanaye Yesu
Kristo na kuonyesha kile hasa Yesu alichokijia ulimwenguni. “Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani
humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu,” Lk 19:9. Wokovu ni kwa kila
mmoja na hasa pale tunapouridhia wokovu huo kwa utashi wetu wenyewe na kwa
dhamiri iliyo hai na safi. Mungu anatutazama utayari wetu katika upya wa
kuyaanza yote naye na siyo historia ya maisha yetu mabaya. “Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na
kuokoa kile kilichopotea,” Lk 19:10. Ndugu yangu, afadhali kufa kwa heshima
kuliko kuishi kwa unajisi. Nafasi ndiyo sasa kusimama katika kweli na haki, na
kuchukia uovu wa aina yoyote ile kwenye maisha yako na jamii inayotuzunguka.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mwenye haki atasitawi kama mtende, Atakuwa kama mwerezi wa
Lebanoni,” Zab 92:12
No hay comentarios:
Publicar un comentario