martes, 24 de noviembre de 2015

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 34 YA KWAKA-B

JUMATANO WIKI YA 34 YA MWAKA-B
25/11/2015
Somo: Dan 5:1-6, 13-14, 16-17, 23-28
Zab: Dan 3:62, 63, 64, 65, 66, 67
Injili: Lk 21:12-19
Nukuu:
Basi wakavileta vile vyombo vya dhahabu, vilivyotolewa katika hekalu la nyumba ya Mungu lililokuwako Yerusalemu; na mfalme na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wakavinywea,” Dan 5:3

Wakanywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe,” Dan 5:4

Bali umejiinua juu ya Bwana wa mbingu; nawe umeisifu miungu ya fedha na ya dhahabu na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe; wasioona, wala kusikia, wala kujua neno lo lote; na Mungu yule, ambaye pumzi yako i mkononi mwake, na njia zako zote ni zake, hukumtukuza,” Dan 5:23a,d,e

Na maandiko yaliyoandikwa ni haya; MENE, MENE, TEKELI, NA PERESI,” Dan 5:25

Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu,” Lk 21:16-17 

Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu,” Lk 21:18

TAFAKARI: “Ninyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.”

Wapendwa wana wa Mungu, mambo mazuri hayahitaji haraka, na kwenye utaratibu kuna akili. Subira ni moja ya shule yakutupeleka huko kuliko kuzuri na kwenye utaratibu, na hiyo ndiyo akili. Subira kamwe haimpi mtu yeyote nafasi ya  kujiinua kusiko kwake na asili yake. Likitokea jambo hilo kwa makusudi basi huko mbele hapatakuwa pazuri, hapatakuwa na utaratibu, na akili haitakuwepo. Mfalme Belshaza, mtoto wa mfalme Nebukadreza, anakosa subirá, hivyo anavunja utaratibu, na mwisho yote aliyoyafanya yalikosa umakini na mantiki. Kwa yeye kuwa Mfalme hakukumaanisha aweza kufanya yote na atakavyo, hata kuyanajisi madhabahu kwa kuchukua vile vilivyokwisha wekwa wakfu kwa matumizi ya hekalu. Basi wakavileta vile vyombo vya dhahabu, vilivyotolewa katika hekalu la nyumba ya Mungu lililokuwako Yerusalemu; na mfalme na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wakavinywea,” Dan 5:3. Furaha yako ya siku moja isiwe majikwezo yako na kukufanya kuivunja mipaka yako thaminiwa uliyopewa, na mbaya zaidi kwenda kusiko asili yako.

Tendo hilo la Mfalme Belshaza ni tendo la kujiinua kusiko mastahili ambalo ni tokeo la kukosa subira. Madhara yake ni kusifa pasiposifiwa na shukrani kusikostahili. Wakanywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe,” Dan 5:4. Tunapoleta utani, kejeli, na kutokujali kwa vile vilivyovitakatifu katika maana ya kuvinajisi, Mungu hawezi kukaa kimya. Nabii Danieli anamwambia Mfalme Belshaza baada ya ishara mbaya kumtokea unajisi ule alioufanya. Bali umejiinua juu ya Bwana wa mbingu; nawe umeisifu miungu ya fedha na ya dhahabu na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe; wasioona, wala kusikia, wala kujua neno lo lote; na Mungu yule, ambaye pumzi yako i mkononi mwake, na njia zako zote ni zake, hukumtukuza,” Dan 5:23a,d,e. Mwanadamu anapojaribu kukataa ubinadamu wake ndipo anapozidi kuwa mbaya kuliko shetani. Kilichofinyangwa kamwe hakiwezi kuwa kama mfinyanga. Mungu apewe sifa na nafasi yake.

Utawala wa Belshaza unafikia ukomo wake kwa sababu ya kukosa subiri na kujiinua. Tendo hili linampelekea kutokuwa na utaratibu katika kufikiri na kutenda. Hivyo anatoa heshima na shukrani pasipo mastahili hayo. Mwisho yote aliyoyafanya yanakosa mantiki na uhalali. Hapa akili haipo kwa sababu utaratibu haupo. Maandishi yaliyojichora kwenye kuta: MENE, MENE, TEKELI, NA PERESI, yalimaanisha mwisho wa kujiinua kwake. Mene ikimaanisha Mungu ameuhesabu ufalme wake na kuukomesha, Teleki ikimaanisha amepimwa katika mizani naye ameonekana kuwa amepunguka. Na peresi, ikimaanisha ufalme wake umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi. Kumbe mtaka yote kwa pupa ukosa yote.

Katika Injili ya leo Yesu anawaambia wafuasi wake nasi pia maneno haya mazito, ‘subirá yako itaiponya nafsi yako.’ Mwenye subira ufikiri vyema tena kwa undani na upana wake. Mwenye subira huyatazama yote katika jana yake, leo yake, kesho yake, na umilele wake. Kuwa mfuasi hai wa Kristo kuna mapaswa yake. Yesu anatuambia leo mapaswa ya kuwa mfuasi wake hai. Mapaswa yake ni kusalitiwa. Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu,” Lk 21:16-17. Badala yake, katika hali hii Yesu anatuambia tuwe na furaha. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12. Yatupasa kufurahi kwa sababu katika mateso na ugumu huu wa kusimama katika kweli na haki, hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu,” Lk 21:18.

Ndugu yangu tuliyesafiri pamoja katika tafakari hii, elewa kwa hakika kabisa kama kweli huu mfuasi hai wa Kristo, ipo siku ufuasi wako utapimwa. Na hilo kama litatokea jiachie kwake Kristo Yesu. “Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza mtakavyojibu; kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga,” Lk 21:14-15.

Tumsifu Yesu Kristo!


Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?” Zab 27:1

No hay comentarios:

Publicar un comentario