sábado, 21 de noviembre de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 34 YA MWAKA-B, Sherehe ya Bwana Wetu Yesu Kristo Mfalme

JUMAPILI WIKI YA 34 YA MWAKA-B
Jumapili ya Mwisho wa Mwaka
Sherehe ya Bwana Wetu Yesu Kristo Mfalme
22/11/2015
Somo I: Dan 7:13-14
Zab: 93:1-2, 5
Somo II: Ufu 1:5-8
Injili: Yoh 18:33-37
Nukuu:
Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14

Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele,” Ufu 1:5-6

Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam. Amina,” Dan 7:7

Yesu akamjibu, Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?” Yoh 18:34 

Yesu akajibu, Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa,” Yoh 18:36 

Basi Pilato akamwambia, Wewe u mfalme basi? Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu,” Yoh 18:37

TAFAKARI: “Kama ni wana wa Mfalme Yesu Kristo, nifanane naye na kusimama katika Haki na Uzima, Utakatifu na Neema, Upendo na Amani.

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya “34” ya Mwaka “B” wa Kanisa. Leo ni Dominika ya mwisho ya mwaka “B” katika mzunguko wake kadiri ya mpango wa kiliturjia. Ni kwenye Dominika hii ya mwisho ya Mwaka, Mama Kanisa anasheherekea Sikukuu ya Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme. Ufalme wa Bwana wetu Yesu Kristo ni tofauti na falme nyingine katika ulimwengu huu. Ufalme wa Kristo ulijidhihirisha kile atakachokuwa kuanzia pale alipomwilishwa na mwisho kuyatoa maisha yake kwa ajili ya dhambi zako na zangu, yaani kifo cha msalaba. Msalaba Mtakatifu kwa sasa ndicho kiti chake cha hukumu ya haki na amani, utakatifu na neema, na mapendo na Amani. Kofia yake ya kifalme ni taji lake la miiba. Hii ya dhihirisha wazi tabia ya Ufalme wa Kristo, yaani, uvumilivu kwa kila aliyeridhia ufalme wake, unyenyekevu katika kuyajali maslahi ya wengine kwanza kabla ya kwako na yangu, huruma katika kuchukulia na kusamehana ikiwa kuwa tayari kusikiliza hisia za maumivu ya wengine hata kama hayana ukweli. Hili ndilo taji la miiba!

Kwa kumwilishwa, yaani neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Yesu alikubali kuchukuwa mwili na hali ya mwanadamu bila kupoteza asili yake ya kimungu ili awe mkombozi wako na wangu. Hakika kwa kazi hii ilipaswa azaliwe kwenye mahekalu ya dhahabu na yaliyopambwa na nakshi za gharama kubwa. Badala yake tunaambiwa kwamba wachungaji walikimbilia Bethlehemu baada ya kuambiwa na malaika. “Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini,” Lk 2:16. Mfalme huyu anazaliwa horini kama alama na uthibitisho wa kutumika na siyo kutumikiwa. Hapa mimi na wewe tunafundishwa unyenyekevu katika maana ya kujitoa zaidi kwa wengine kuliko kujitazama wenyewe. Hapa mimi na wewe tunafundishwa upendo wa kweli unaojidhihirisha katika kujishusha chini kabisa katika hali za watu. Upendo huu unafikia kilele chake pale msalabani ambapo Mfalme huyu Yesu Kristo anautoa uhai wake waajili ya rafiki zake ambao ni wewe na mimi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Huyu ndiye Kristo Mfalme tunayemsheherekea leo. Yesu Kristo katika ukweli huu anadhihirisha kuwa yeye ni shahidi na mwaminifu, mazaliwa wa kwanza wa waliokufa, aliyetayari kutuosha dhambi zetu kwa damu yake, na kutufanya kuwa ufalme na makuhani wa Mungu. Huu ni umependo wa ajabu sana kwetu. Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele,” Ufu 1:5-6. Kwa nini basi nashindwa kupenda kama Kristo alivyonipenda?

Mamlaka ya Kristo ni ya milele na hivyo kumtenga na falme za leo na sasa. Ufalme wake ni ufalme usioangamizwa. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa,” Dan 7:14. Yesu akiwa kizimbani, Pilato anahoji kwa kejeri asili ya mamlaka na ufalme wa Yesu na mwisho kumwita Mfalme. Yesu akamjibu, Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?” Yoh 18:34. Hata hivyo Yesu anaweka wazi alisi, mamlaka, na ufalme wake. Kwanza kabisa ufalme wa Kristo siyo wa duniani hii. Ingekuwa hivyo kilichompata na hali na namna alivyofanyiwa watumishi wake wangempigania na asingetiwa mikono mwa wayahudi. Kwa maneno mengine ufalme wake ni wa milele. “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa,” Yoh 18:36.

Tendo hilo la kukubali kudhalilishwa kiasi hicho Bwana wetu Yesu Kristo hakikumwondolea Ufalme wake, mamlaka yake, wala Umungu wake. Ila kwa tendo hilo ni ponya yetu na kuwa huru kwetu. Hapa ndipo pale tuliponunuliwa kwa gharama kubwa sana, yaani kwa damu yake. Wewe na mimi leo tunathamani kubwa sana mbele ya Mungu kwa sababu tumekombolewa kwa gharama ya damu yake Yesu. “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 18-19. Tendo hili pia licha ya kutufanya kuwa na thamani kubwa sana mbele ya Mungu, limetufanya na linatufanya matajiri. Kwa tendo hili la kuutoa uhai wake kwa ajili yetu, Kristo amekubali kuwa masikini ili wewe na mimi tuwe matajiri. Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Ni kwa ajili ya mambo haya makuu Kristo ni Mfalme na alizaliwa kwa ajili hiyo. Kuja kwake ulimwenguni ni kuusimika ufalme huu na kweli yake. Yesu anamjibu Pilato swali lake la kejeli kuhusu kuwa yeye ni Mfalme. “Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu,” Yoh 18:37. Ndugu yangu wasimama katika kweli? Kama sivyo, bali elewa huisikii sauti ya Kristo. 

Wapendwa katika Kristo, Ufalme wa Kristo ni ufalme wa haki na uzima, ufalme wa utakatitifu na Neema, ufalme wa mapendo na amani. Nasi kwa upendeleo mkubwa tu wana wa ufalme huu kwa sakramenti ya ubatizo. Kwa sakramenti hii tu wana na warithi wa ufalme wa Kristo na Mungu wetu hasa pale tunapoishi ahadi zetu za ubatizo. Hivyo mimi kama mwana wa Mfalme Yesu Kristo nifanane naye na kusimama katika Haki na Uzima, Utakatifu na Neema, Upendo na Amani.

Wapendwa wana wa Mungu ikiwa lengo la kwanza la kuumbwa kwetu na kukombolewa kwetu lililengo kujenga mahusiano mazuri na muumba wetu, lengo la pili tuwapo hapa duniani ni kuudhihirisha ufalme wake. Hapa ninaudhihirisha ufalme wake Kristo kwa kuishi na kusimamia ufalme wa haki na uzima kwa kuyafanya mazingira ninayoishi yawe ya haki na kuchanua kwa uzima wa roho na mwili. Niudhihirishe ufalme wa Mungu kwa kuishi maisha ya utakatifu na neema. Maisha hayo yawe chachu kwa wengine wamwone Kristo kupitia kwangu, na kuwa barua ya kusomwa na wengine. Mtume Paulo anawaambia wakristo wa Korintho, Ninyi ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu, inajulikana na kusomwa na watu wote; mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama,” 2Kor 3:2-3. Mwisho, nikiwa hapa duniani yanipasa kuudhihirisha ufalme wa mapendo na Amani. Ili mazingira ninayoishi na ulimwengu ninaoishi na kunizunguka uwe na mapendo na amani yanipasa muda wote nijihangaishe kwa ajili kuwa mpatanishi. Yesu hasemi ‘heri wenye upendo, au heri wanaojua kupenda wataitwa wana wa Mungu,’ bali ‘heri wapatanishi.’ Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu,” Mt 5:9. Hivyo kuudhihirisha ufalme wa mapendo na Amani, yanipasa kuwa mtapatanishi na ndipo nitaiwa mwana wa Mungu na mrithi wa ufalme wake.

Kutafuta amani siyo KUEPUKA MGOGORO, kukimbia mgogoro, kujifanya hakuna tatizo au kuogopa kuliongelea tatizo huo ni woga kwa hakika. Yesu, mfalme wa amani, hakuogopa kamwe migogoro. Mara nyingine aliuchochea ukatokea kwa faida ya wote. Wakati mwingine tunatakiwa kuepuka migogoro, wakati mwingine kuisababisha, na wakati mwingine tunahitaji kuitatua. Lengo liwe kwa faida ya wote. Ndiyo maana tunapaswa kuomba uongozi wa Roho Mtakatifu daima.
Kuleta amani siyo KUTULIZA HASIRA. Mara nyingi unakubaliana, unakuwa kama jamvi, na unawaruhusu wengine wakukanyage sivyo alivyokusudia Yesu. Alikataa kuacha mambo kama yalivyo, na akachukua msimamo mbele ya upinzani wa waovu.

Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii;

Ni heri kwenda Mbinguni ukiwa na suruali iliyotoboka makalio kwa sababu ya kuhangaika kwa ajili ya kuwa mpatanishi, kuliko kwenda jehenamu ukiwa umevalia suti na tai.

Ni kwa maana hiyo, heri kwenda mbinguni na kuufurahia ufalme wa Mungu ukiwa na kandambili zilizo kwisha kisigino, kuliko kwenda kwenye mateso jehenamu ukiwa umevalia mokasini zenye kisigino cha chuma.

Ni heri kwenda mbinguni ukiwa na jina la Lofa kwa sababu ya kupigania haki za wanyonge, uzima na usalama wao, kuliko kwenda jehenamu kwa jina la Luatani.

Ni heri kwenda mbinguni na kuufurahia ufalme wa Mungu ukiwa mikono mitupu na maisha ye neema, kuliko kwenda jehenamu ukiwa milionea.

Ndugu yangu, hakuna dharau yoyote ili kubwa, kukashifiwa kuliko pindukia, matusi ya kila aina ambayo Yesu hakuyapata. Aliyakubali yote kwa kutupenda upeo ili leo mimi na wewe tuwe huru kutoka utumwa wa dhambi. Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo,” Yoh 13:1

Tumsifu Yesu Kristo!


Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote, Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote,” Zab 145:13

No hay comentarios:

Publicar un comentario