JUMAMOSI WIKI YA 33 YA MWAKA-B
21/11/2015
Somo: 1Mak 6:1-13
Zab: 9:2-3, 4, 6, 16, 19
Injili: Lk 20:27-40
Nukuu:
“Lakini sasa nayakumbuka mabaya niliyoyafanya Yerusalemu,
jinsi nilivyoichukua vyombo vyote vya fedha na dhahabu vilivyokuwapo, na
kupeleka majeshi kuwaharibu wenyeji wa Yesusalemu bila sababu,” 1Mak 6:12
“Nafahamu ya kuwa kwa sababu hiyo maovu haya yamenipata,
hata, tazama, ninakufa kihoro katika nchi ya kigeni,” 1Mak 6:13
“Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale
wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika
wafu, hawaoi wala hawaolewi,” Lk 20:34-35
“wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na
malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo,” Lk 20:36
“Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote
huishi kwake,” Lk 20:38
TAFAKARI: “Mtafute Bwana ungali hai kwani anapatikana.”
Wapendwa wana wa Mungu, waswahili wanatufundisha hivi;
‘majuto ni mjukuu.’ Wahenga wanaenda mbali zaidi na kusema, ‘ndege mmoja mkoni
ni bora kuliko ndege mia moja porini.’ Naye Mt. Agustino anatuambia ‘hakuna
kesho kama hakuna leo.’ Kumbe leo na sasa ndiyo hatma ya kila kitu katika
maisha yangu. Wengi hatupendi kufanya mabadiliko katika maisha yetu kwa sababu
tunadhani bado tuna muda wa kutosha kufanya hivyo, kwa hiyo hakuna sababu ya
kufanya haraka. Maandiko Matakatifu yanatuambia hivi: “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni,
maadamu yu karibu; Mtu mbaya na
aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye
atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa,” Isa 55:6-7.
Mungu ni Huruma, Upendo, na Msahama. Kamwe hapendi kuona unaangamia katika
dhambi.
Somo letu la kwanza linatufundisha matokea mabaya ya matumizi
mabaya ya madaraka na nafasi tulizopewa kama dhamana katika kutumika kwa ajili
ya wengine. Kweli cheo ni dhamana na uongozi ni kutumika. Somo hilo pia
linatufundisha kujinyenyekesha hasa pale tunapopewa dhamana iwe kubwa au ndogo
kwani mwisho wa siku yatupasa kutoa hesaba yake. Tupewapo dhamana hiyo salama
yetu ipo pale tunapo yafanye yote kwa ukamilifu yanayotupasa kufanya. “Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote
mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa
kufanya,” Lk 17:10. Tatizo letu wengi ni pale tunapopenda
kutumikiwa kuliko kutumika.
Mfalme Antioko anavuna
kile alichokipanda. Utawala wake ulikuwa wa dhuluma sana na wa kutokujali haki
za raia wake. Aliyafanya hayo yote kwa kujua kabisa bila kukumbuka kwamba ipo
siku yote yana mwisho wake. Kwa mamlaka aliyokuwa nayo ilimpasa kuyafanya
utawala wake uwe mahali pazuri pa kuishi. Kinyume chake utawala wake ulikuwa
kilio cha wengi na huzuri kwa wanyonge na wasio na sauti. Wengi walilazimishwa
kuishi kwa kuzisaliti dhamiri zao. Wengi wao pia walikubali kufa kuliko kutenda
dhambi na kwenda kinyume cha imani yao, mila na desturi zao. Mwisho ya hayo
yote mfalme Antioko anakiri na kusema, “Lakini sasa nayakumbuka mabaya niliyoyafanya Yerusalemu, jinsi
nilivyoichukua vyombo vyote vya fedha na dhahabu vilivyokuwapo, na kupeleka
majeshi kuwaharibu wenyeji wa Yesusalemu bila sababu,” 1Mak 6:12. Tamaa ya mali
na madaraka ni janga kubwa sana hasa katika tawala za nchi masikini na zile
zinazoendelea. Ukweli ni kwamba uongozi mbovu na sera mbovu chini ya mfumo
mbovu kikatiba ndiyo sababu ya ugumu wa maisha ya watu licha ya utajiri walio
kuwa nao kama nchi. Wakati ndiyo sasa! Kila mtu amtafute Mungu aliye hai kwani
anapatikana. Sote tumeumbwa si kwa bahati mbaya, bali kwa malengo tena tuishi
milele.
Jambo ambalo lipo wazi ni hili, hakuna chozi la mtu yeyote
anayemlilia Mungu katika kweli na haki ambalo litapotea bure. Watendao maovu
hasa wale walipewa dhamana na umma wa watu miisho yao kamwe haiwezi kuwa
mizuri. Ukimya wa Mungu katika mateso ya watu wake sio kwamba Mungu huyu haoni
bali huwapa nafasi pia waovu kutubu na kukiri dhambi zao. “Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia
zenu si njia zangu; asema Bwana,” Isa 55:8. Na kwa sababu hiyo Mungu hubaki kuwa Upendo, Huruma, na
Msamaha. Mwisho wa Antioko anaueleza mwenyewe na kusema, “Nafahamu ya kuwa kwa
sababu hiyo maovu haya yamenipata, hata, tazama, ninakufa kihoro katika nchi ya
kigeni,” 1Mak 6:13. Je, Mungu wetu yupo mbali? Mtafute sasa kabla ya kiama.
Tunaposema Mungu ndiye kila kitu tunamaanisha hivyo. Nabii Amosi anatuambia
siri kubwa kuhusu Mungu wetu huyu aliye hai na kusema, “mtafuteni yeye afanyaye Kilimia na Orioni, na
kukigeuza kivuli cha mauti kuwa asubuhi, na kuufanya mchana kuwa giza kwa
usiku; yeye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; Bwana,
ndilo jina lake,” Amo 5:8. Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, jeuri
yako na mbwembwe zako zinatoka wapi juu ya Mungu huyu aliye hai? Jisalimishe!
Wapendwa wana wa Mungu, yeyote yule aliyepewa dhamana
kuuongoza umma wa watu wa Mungu, yampasa kusimama katika haki na kweli. Nabii
Sefania anatuambia kwamba, mwenye kusimama katika unyenyekevu na kutenda haki,
Mungu huificha mtu huyo katika siku ya hasira yake. “Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu
wa dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu;
huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya Bwana,” Sef 2:3. Ni kwa kutafuta haki
katika unyenyekevu na kutenda haki hiyo, hatuna sababu ya kuofia hali ya
ulimwengu ujao.
Yesu katika Injili ya leo anawatoa wasiwasi wale waliomuuliza
juu ya nani hasa atakaye kuwa mume baada ya maisha haya ya duniani ikiwa
mwanamke huyo aliolewa na kurithiwa na ndugu saba wa familia moja. Yesu
anawajibu na kuwaambia, “Wana wa
ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini,
wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka
katika wafu, hawaoi wala hawaolewi,” Lk 20:34-35. Tukiwa hapa duniani ni wakati
wa kuyafanya yote katika wema na haki. Hivyo, kesho yetu ni matokeo ya leo
yetu. Mahitaji yetu tuwapo hapa ulimwenguni ni tofauti na mahitaji yetu tukiwa
mbingu kwenye uzima wa milele. Hivyo walioko huko kwenye uzima wa milele, “wala hawawezi kufa tena; kwa sababu
huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa
ufufuo,” Lk 20:36. Kwa sababu hiyo mahitaji ya kimwili hayana nafasi tena kwani
tutakuwa na miili iliyotukuka. Miili ya ufufuko. Ukweli huu unathibitisha
kwamba Mungu wetu, “si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake,” Lk
20:38. Ndugu yangu, kesho yako katika mikono salama ya Mungu inategemea leo
yako katika mikono ya Mungu iliyo salama. Hivyo mtafute Bwana ungali hai kwani
anapatikana.
Tusifu Yesu Kristo!
“Kutenda haki na hukumu Humpendeza Bwana kuliko kutoa sadaka,”
Mit 21:3
No hay comentarios:
Publicar un comentario