JUMAPILI
WIKI YA 32 YA MWAKA-B
15/11/2015
Somo
I: Dan 12:1-3
Zab:
16:5, 8, 9-10, 11
Somo
II: Ebr 10:11-14, 18
Injili:
Mk 13:24-32
Nukuu:
“Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande
wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo
tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako
wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile,” Dan 12:1
“Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka,
wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele,” Dan 12:2
“Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao
waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele,” Dan 12:3
“Lakini huyu,
alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi
mkono wa kuume wa Mungu; tangu
hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake,” Ebr 10:12-13
“Maana kwa toleo moja
amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa,” Ebr 10:14
“Lakini siku zile,
baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza, na mwezi hatautoa mwanga wake. na nyota za mbinguni zitakuwa
zikianguka, na nguvu zilizo mbinguni zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa
Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu,” Mk 13:24-26
“Amin, nawaambieni,
Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatimie,” Mk 13:30
“Mbingu na nchi
zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe,” Mk 13:31
“Walakini habari ya
siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana,
ila Baba,” Mk 13:32
TAFAKARI:
“Mwisho wako utategemea ishi
yako leo na sasa.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 33 ya Mwaka “B” wa Kanisa.
Masomo yote matatu yanatupa viashirio vya nyakati za mwisho na hukumu yake.
Kama tunavyokaribia kumaliza mwaka “B” wa Kanisa ni vyema pia kutafakari ukweli
kuhusu mwisho wa nyakati, na hukumu ya kila mmoja wetu mbele ya Mungu aliye
Upendo, Haki, Msamaha, Huruma, na Uvumilivu. Sifa zote hizi za Mungu
hazionekani tu mwisho wa nyakati, bali zipo na zinaonekana kila sekunde,
dakika, saa, siku, wiki, mwezi, na mwaka
hadi mwaka unapoivuta pumzi aliyokupa kwa kukupenda, kukuchagua, na kukuumba
uwe kwa sura na mfano wake mwenyewe. Hakika sidhani kama kuna upendo na upendeleo
wa Mungu kwetu kama huu.
Hivyo wapendwa katika
Kristo, jambo la kwanza leo Mama Kanisa anatutaka kwa upendo huo huo wa Mungu,
tuelewe kwamba muda tuliopewa kuishi ni leo na sasa, mwisho wake ni siri ya
Mungu mwenyewe. Na kama mwisho wa muda huo ni siri yake Mungu mwenyewe nasi
hatuna ufahamu juu yake, jambo la pili na la muhimu ni kwamba, mwisho wako
utategemea ishi yako leo na sasa. Mungu wetu ni Upendo na haki, Msamaha, huruma
na Uvumilivu. Kwa mantiki hii, Mungu wetu hawezi kamwe kutuwazia lililo baya. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia
ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini
siku zenu za mwisho,” Yer 29:11. Tunahitaji hekima hii ya Mungu kujua ukweli
huu. Na hekima ya Mungu wetu ni kule kuwa na hofu naye. Hofu hii ya Mungu
itatuongoza katika pendo na haki ya Mungu, Msamaha, Huruma na Uvumilivu wa
Mungu. Wenye kusimama katika kweli hii hadi mwisho ndiyo watakao ng’ara mbele
za Mungu. “Na
walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda
haki watang'aa kama nyota milele na milele,” Dan 12:3. Je, unahitaji kwenda
chuo kikuu kujua ukweli huu? Ni nani basi kati yetu asiyekuwa hata na chembe ya
upendo wa Mungu ndani yake?
Wapendwa wana wa Mungu, habari za nyakati za mwisho zinatisha
sana kwa yule asiyejua matumizi ya muda wake, yaani, leo na sasa, na malengo
mazima ya maisha yake hapa duniani. Nabii Danieli anatuambia hali ya mambo
itakavyokuwa siku hiyo ya mwisho. “Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande
wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo
tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako
wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile,” Dan
12:1. Atakayeokolewa ni yule ambaye jina lake lipo kwenye kitabu cha uzima.
Kitabu hiki cha uzima kipo Mbinguni, ila nakala yake unayo, na unatembea nayo
kila siku. Kitabu hiki cha uzima yanaandikwa yale mazuri tu uyafanyayo kila
upewapo pumzi ya kupumua na aliye kuumba kwa kukupenda na kukuchagua. Na kitabu
hiki ulipewa siku ile ya ubatizo wako kabla ya kupewa mshumaa uwakoa na
kuzibuliwa masikio ili usike neno lake na mdomo ili uungame imani ya Kristo.
Pia kitabu hiki ulipewa mara baada ya kumwagiwa maji ikiwa ni
ishara ya kuvushwa kuelekea nchi ya ahadi (kufa na kufufuka na Kristo), na
baadaye kupakwa mafuta ya Krisma ili uunganike na taifa lake Mungu kuwa kiungo
cha Kristo; kuhani, nabii, na mfalme, hadi upate uzima wa milele mbinguni.
Mbatiza wako alipokupa kitabu hiki aliyatamka maneno haya: “F…(Edgar) umekuwa
sasa kiumbe kipya na kumvaa Kristo. Nguo hii nyeupe iwe ishara ya cheo chako.
Nawe ukisaidiwa kwa maneno na mifano ya jirani zake, ukaifikishe safi katika
uzima wa milele mbinguni,” Misale ya Waamini, toleo la 1996, uk 933.
Nabii Danieli anaendelea kutupa ukweli kuhusu siku ya mwisho
kwa kusema, “Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka,
wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele,” Dan 12:2. Waliolala katika mavumbi ya nchi wataamka, yaani
makaburi yatafunguka na watayaacha makaburi yao na kuingia uzima wa milele.
Mimi na wewe tunayeyapuuzia haya na kuona ni kama hadithi tu za akina Abunuasi,
tutaingia katika aibu ya kudharauliwa milele kwa sababu tu ya kutokuwa makini
kwa yale tuliyoyapokea siku ya ubatizo wetu, yaani kuishi ahadi zetu za
ubatizo.
Jambo
hili alisemalo Nabii Danieli halina tofauti na ukweli anaotuambia Yesu leo
katika Injili, yaani, habari njema ya wokovu wetu. Yesu anatuambia leo, “Lakini siku zile, baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza, na
mwezi hatautoa mwanga wake. na
nyota za mbinguni zitakuwa zikianguka, na nguvu zilizo mbinguni zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa
Adamu akija mawinguni kwa nguvu nyingi na utukufu,” Mk 13:24-26. Je, Mwana wa
Adamu ni nani katika hukumu hii? Ni kwa makusudi makubwa kabisa ‘NENO’
aliyefanyika mwili na kukaa kwetu, yaani Yesu, awe mpatanishi wetu na Mungu. “Kwa kuwa katika yeye
ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi
yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu
vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni,” Kol 1:19-20. Huu ndio uwezo na
mamlaka aliyokuwa nayo Mwana wa Adamu, yaani Kristo Yesu. Je, waweza kukwepa
hukumu hii?
Wapendwa katika Kristo, mara nyingi
tunapoambiwa habari hizi hufikiri hazituhusu na wapo wanaoambiwa na siyo sisi.
Twafanya hivyo kwa sababu tunajihesabia haki pasipo haki. Yesu anaweka bayana
ukweli huu na kusema, “Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote
yatimie,” Mk 13:30. Kwa maana hiyo, “Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe,”
Mk 13:3. Je, ndugu yangu utabadili njia yako mbaya kwa kusikia maneno haya
kutoka mbinguni na kwa malaika? Ukweli wa lini litatokea jambo hili hakuna
anayejua, ila mwisho wa nyakati lazima utafika. “Walakini habari ya
siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana,
ila Baba,” Mk 13:32. Kama jambo hili limefichwa kwetu na ufahamu wetu hauwezi
kujua, tufanye nini sasa ili tuwe njia salama?
Ndugu
zangu, kwanza kabisa ili niwe njia iliyo salama itanipasa kila sekunde
ninayopewa pumzi na Mungu nihesabu nimepewa hiyo tu kwa kujiandaa na umilele.
Jambo la pili, inanipasa kuanzia sasa nitazame upya mahusiano yangu na Mungu,
Wenzengu, hasa jirani zangu, na
Mazingira yanayonizunguka. Swali la kujiuliza katika jambo hili la pili ni
hili; Je, kwa uhusiano huu nilionao kuna mwelekeo wa kuifikia mbingu?
Mtume
Paulo anatupa namna ya kuishi kuielekea mbingu na uzima wake. Naye anasema, “Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la!
Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa
na Kristo Yesu,” Flp 3:12. Kila siku uliyopewa na Mungu ni siku ya kuimarisha
uhusiano wako na Mungu, jirani zako, na mazingira yako. Huku ndiko kukaza
mwendo ukiyachuchumilia yaliyo mbele, yaani, uzima wa milele, kwenye mede ya
thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo. Paulo Mtume anatuambia, “Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba
nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma,
nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo,
niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu,” Flp
3:13-14. Je, una haki au sababu yoyote ya kujihesabia haki mbele ya Mungu kwa
mazingira na hali uliyo nayo sasa? Ni Mungu tu ndiye atuhesabiaye haki kadiri
ya Upendo na Huruma yake kwa sababu ndicho alicho.
Ndugu
zangu katika Kristo Yesu, tunalo kimbilio moja tu katika mkwamo huu wa
sintofahamu kuelekea uzima wa milele. Yesu Kristo ndiye jibu letu. Yesu
ananiambia mimi na wewe kwamba, “Mimi ndimi
njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6.
Kumbe bado haujachelewa kufanya mabadiliko katika maisha yako. Kubadili njia
yako mbaya ni leo na sasa. Mimi na wewe yatupasa kujenga uhusiano mzuri na
Kristo Yesu “Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti
ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake,”
Rum 5:10. Kwa sadaka yake pale msalabani sote tumehesabiwa haki na kuwa warithi
wa ufalme wa Mungu. Kwa sababu, “huyu alipokwisha
kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa
kuume wa Mungu; tangu hapo
akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake,” Ebr 10:12-13. Leo
sadaka hiyo ni adhimisho la Ekaristi Takatifu. Mama Kanisa kama Sakramenti ya
wokovu wetu anaadhimisha Sakramenti hii ya Misa Takatifu kwa wokovu wangu na
wako na wale wote wanaomridhia Mwana wa Mungu. “Maana kwa toleo moja
amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa,” Ebr 10:14. Je, hutaki kutakaswa
kwa adhimisho hili la Ekaristi Takatifu? Je, walichukuliaje adhimisho hili la
Ekaristi Takatifu unapopata nafasi ya kushiriki? Ndugu yangu, uwe mlei, mtawa,
mtawa na mkleri, au mkleri, usifanye jambo hili kwa mazoea. Ni nafasi ya pekee
sana katika maisha yako.
Theresia
Midu alikuwa mhudhuriaji mzuri sana wa Misa Takatifu kila siku na Jumapili.
Adhimisho la Misa kwake lilikuwa na maana tu kwenye kushiriki mwili na damu ya
Yesu. Mara baada ya tendo hili huondoka na kuelekea kwenye biashara yake ya kuuza
genge sokoni. Neno la Mungu, na Baraka ya mwisho wa Misa baada ya Matangazo
haikuwa na maana yoyote kwake kiibada.
Muda
ulipita na mwisho wa maisha yake ulifika. Kwa jinsi alivyoishi hapa duniani na
hasa moyo wake wa kuudhuria Misa kila siku hakuwa na shaka ya kuiona mbingu.
Je, mambo yalikuaje huko mbele ya safari?
Mbele ya
kiti cha hukumu akiwa Mungu na Yesu Mthibitisho wa kila aliyepita kwenye hukumu
hii, na msema neno la mwisho kwa vile alitujua kama tulivyo, na “Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili
yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. Yeye hakutenda dhambi, wala hila
haikuonekana kinywani mwake,” 1Pet 2:21-22
.
Hivyo
ilipofika zamu ya Theresia, Malaika Michaeli alitumwa alilete kalabrasha lake.
Kwa kawaida kwenye kalabrasha hili huandikwa yale mema tu uliyofanikiwa
kuyafanya wakati wa uhai wako. Kwa bahati mbaya kuanzia mwanzo wa ukurasa wa
kwanza hadi wa mwisho hakuna kilichokuwa kimeandikwa zaidi ya nukuu ya
angalizo. Nayo ilikuwa inasema hivi: “alihudhuria sadaka ya Misa Takatifu kama
wajibu na alimpokea Mwana wa Adamu kwa kipindi kile kile alichokuwa Kanisani na
baada ya hapo alimwacha kule kule Kanisani. Hakuondoka naye kwa sababu
hakuisubiri Amani na Baraka ya mwisho ambacho ndicho kielelezo cha upatanisho wa
wanadamu na wewe Mungu Baba kwa kupitia Mwanao Yesu Kristo. Kwa mantiki hii
hana mastahili yoyote kwenye uzima huu wa milele. Zaidi rejea kwenye kitabu cha
uzima kwa taarifa zake zaidi.” mwisho
wa kunukuu. Malaika Michaeli alilifunga kalabrasha lile.
Basi kitabu cha uzima
kililetwa, na Yesu alikifungua. Kwenye kitabu kile walikuwa akina Theresa
wengi, mfano Theresa wa Calcuta, Theresa wa Mtoto Yesu, ila Theresa Midu
hakuwepo kwenye Kitabu hiki cha uzima. Ndipo Mwana wa Adamu, yaani Yesu
akamwambia, “Theresa Midu, tatizo lako hukuishi ahadi zako za ubatizo. Ulipewa
muda wa kutosha kabisa, na kila mara niliingia ndani yako uliposhiriki mwili na
damu yangu, ila hukupenda nibaki nawe. Uliniacha na kuwahi biashara zako na
genge lako. Vyumba vipo vingi kama unavyoona katika ufalme huu. Akina Theresa
wote wamepata vyumba katika ufalme huu ila wewe huna nafasi mahali hapa,” Yesu
alimweleza yote bila kuficha neno. “Je, niende wapi, au wapi nilipoandaliwa?”
Theresa Midu alimuuliza Yesu. Fuata njia hiyo yenye watu wengi na barabara yake
ni pana huko ndipo kwenye kulia na kusaga meno, Mt 13:50. Wapendwa wana wa
Mungu, hii ndiyo adhabu ya kudharauliwa milele.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye
amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho,” Yoh
12:48
No hay comentarios:
Publicar un comentario