JUMATATU WIKI YA 34 YA MWAKA-B
23/11/2015
Somo: Dan 1-6, 8-20
Zab: Dan 3:52, 53, 54, 55, 56
Injili: Lk 21:1-4
Nukuu:
“Naye
mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama
Danielii, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria; kwa hiyo wakasimama mbele ya
mfalme,” Dan 1:19
“Na katika
kila jambo la hekima na ufahamu alilowauliza mfalme, akawaona kuwa walifaa mara
kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake,” Dan 1:20
“Akasema, Hakika
nawaambia, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote; maana, hao wote walitia
sadakani katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote
alivyokuwa navyo,” Lk 21:3-4
TAFAKARI: “Kuwa kile ulicho na jitoe bila kujibakiza, ndivyo
apendavyo Mungu.”
Wapendwa wana wa Mungu, Danielii, Hanania, Mishaeli na
Azaria ni vijana waliowekwa katika majaribia kama kweli wanaweza kutumika
katika ufalme wa Mfalme Nebukadreza. Kama ilivyokawaida, wale waliokuwa
viongozi katika nyumba za kifalme walikuwa matoashi wa kufanywa, yaani waliasiwa
ili walishikwe na ashiki ya kutamani wake wa mfalme. Ndugu hawa, yaani
Danielii, Hanania, Mishaeli na Azaria walikuwa Wayahudi ambao waliishika vyema
torati. Hivyo mapendekezo ya Mfalme kwa wao kula chakula cha kifalme ikiwa ni
pamoja na divai aliyokunywa ilikuwa ni najisi kwao. Hivyo wanaomba kula mtama
tu. Vijana hawa wanaishinda tamaa yao na kuwa kile walicho. Afya yao iliboreka
na kupendeza machoni mwa Mfalme.
Vijana hawa wanakuwa huru juu ya ushawishi si kwa vile
hawapendi kushawishika, ila kwa vile wameamua kusimama katika kweli. Kweli ya
Mungu utufanya kuwa huru. “Tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka
huru,” Yoh 8:32. Kweli hii inawafanya vijana hawa wawe kile walicho na
kumpendezesha mfalme. “Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote
hawakuonekana waliokuwa kama Danielii, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria; kwa
hiyo wakasimama mbele ya mfalme,” Dan 1:19. Hakuna aliyekuwa kama vijana hawa
kwa vile hawakuisaliti kweli.
Wapendwa wana wa Mungu, ukiwa mpenda kweli Mungu atakupigania
hata pale watesi wako watakapoonekana kutokutenda haki juu yako. Mungu uigeuza
midomo lenye kulaani na kuwa midomo ya baraka unaposimama katika kweli. Mfano
mzuri ni maisha ya shujaa wa Afrika ya Kusini, Nelson Mandela. Vinywa vile
vilivyomwona kuwa ni gaidi na muhaini na kumfunga kwa miaka 27, ni vivyo hivyo
hivyo vilivyosadiki kuwa mtu huyu ni shujaa na anastahili kuwa huru. Hivyo, “Na katika kila jambo la hekima na ufahamu alilowauliza
mfalme, akawaona kuwa walifaa mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa
katika ufalme wake,” Dan 1:20. Vijana hawa wanaonekana washindi si kwa uzuri wa
mwono wao, bali kwa vile walisimama katika kweli bila kudondoka. Mungu aliye
hai anakuwa mtetezi wao.
Kusimama katika kweli na kujitoa bila kujibakiza ndiyo mfumo
aupendao Kristo hasa pale tunapoishi katika mazingira ya kubaguana kutoka na
hali na historia zetu. Katika utoaji wa sadaka, mwanamke mjane anahesabiwa haki
kwa tendo la kujitoa bila kujibakiza. Yesu “Akasema, Hakika
nawaambia, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote; maana, hao wote walitia
sadakani katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote
alivyokuwa navyo,” Lk 21:3-4. Je ndugu
yangu umejitoa vilivyo? Ni katika kutoa bila kujibakiza kunakuwa silaha za
haki. Hivyo, “wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa
dhambi; bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo
vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki,” Rum 6:13. Ndugu yangu, “kuwa kile ulicho na jitoe bila kujibakiza, ndivyo
apendavyo Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kama vile Mwana wa
Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya
wengi,” Mt 20:28
No hay comentarios:
Publicar un comentario