JUMATANO WIKI
YA 32 YA MWAKA-B
11/11/2015
Somo: Hek
6:1-11
Zab: 82:3-4,
6-7
Injili: Lk
17:11-19
Nukuu:
“Hekima ndiyo bora kupita nguvu, na
mwenye busara kuliko shujaa,” Hek 6:1
“Kwa kuwa Bwana, Mfalme wa wote,
hatajizuia kwa ajili ya mtu yeyote, wala hajali ukuu, kwa sababu ndiye Yeye
aliyewafanya wadogo na wakuu pia,” Hek 6:7
“Maana wale waliotunza kwa utakatifu
mambo yale yaliyo matakatifu watahesabiwa kuwa watatifu wenyewe; nao wale
waliofundishwa hayo wataona neno la kujitetea,” Hek 6:10
“wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!” Lk 17:13
“Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani.
Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika,” Lk 17:14
“akaanguka kifudifudi
miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria,” Lk 17:16
“Yesu akajibu,
akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi?,” Lk 17:17
TAFAKARI: “Je, kweli
sina chochote cha kushukuru?”
Wapendwa wana wa Mungu, kukua kiroho
huendana pia na kustaarabika kwa mtu, yaani maisha yanayoongozwa na busara na
hekima. Busara ni tunda la hekima, na busara ya mtu huikuza hekima yake.
“Hekima ndiyo bora kupita nguvu, na mwenye busara kuliko shujaa,” Hek 6:1.
Mwenye hekima hawezi hata mara moja kuyachukulia mambo kimzahamzaha tu. Hekima
ya mtu humsukuma kuyatazama yote anayokutana nayo kwa busara katika
kuyatathimini (mchanganua makini na mahiri), na mwisho kutenda kusiko na shaka.
Utaratibu huu wa kuona kwa busara,
kutathimini, na mwisho kutenda kusiko shaka ni kwa kila mmoja wetu. Ndivyo
Mungu anavyotutaka tuenende katika maisha kwa sababu uwezo huo amemkirimia kila
moja wetu. “Kwa kuwa Bwana, Mfalme wa wote, hatajizuia kwa ajili ya mtu yeyote,
wala hajali ukuu, kwa sababu ndiye Yeye aliyewafanya wadogo na wakuu pia,” Hek
6:7. Pamoja na utofauti wetu ambao ni tokeo la ubinadamu na ubinafsi wetu wa
kujikweza kusiko na sababu katika jamii, Mungu hakuwa na kusudi hilo katika
uumbaji wetu.
Kuanza kukua kiroho kuliko sambamba na
busara na hekima kutakupasa kila siku kuitazama hii dhambi ya kijamii, yaani,
kujenga matabaka yasiyo na maana yoyote. Mbele yake Mungu hakuna aliyezaidi ya
mwingine. Mbele ya Mungu sote tunacheo kimoja tu, yaani Utakatifu wako. “Maana
wale waliotunza kwa utakatifu mambo yale yaliyo matakatifu watahesabiwa kuwa
watatifu wenyewe; nao wale waliofundishwa hayo wataona neno la kujitetea,” Hek
6:10. Kati ya mambo ya kutunza kwa utakatifu ni tendo la SHUKRANI katika maisha
yako. Kumbe inanipasa kila nivutapo pumzi nitoe shukrani kwa Mungu.
Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na shida
na mahangaiko yako ya kila siku bado Mungu anakujalia uhai. Ujumbe wa Mungu
katika hali hiyo yako ya mateso anasema nakupenda na nipo nawe, ila fanya
zaidi. Kwa wale ambao hawajui shida ni kitu gani, Mungu pia anasema nakupenda
na nipo nawe, ila fanya zaidi. Fanya zaidi ya mwenye mateso na mahangaiko ndiyo
njia ya kuondokana na mkwamo huo na ponya yako. Fanya zaidi ya tajiri ndiyo
njia ya ponya yake hasa pale anapokuwa tayari kuyashirikisha aliyonayo na
wengine hasa wahitaji. Ni katika kufanya zaidi ndipo tunapotakaswa. Fanya zaidi
hii inakuwa na uponyaji inapounganika na Kristo.
Katika injili ya leo tunaona ‘fanya
zaidi’ ya waleo wakoma kumi walivyounganika na Kristo na “wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!” Lk 17:13. Lazima kufahamu msaada wako unatoka
wapi hasa pale unapoona giza tupu katika maisha yako. Uponyaji wa wakoma hawa
ni tofauti kabisa na ponyaji nyingine alizokwisha kuzifanya Yesu. Yesu
anawataka ‘kufanya zaidi’ na kuwaambia, “Enendeni, mkajionyeshe kwa
makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika,” Lk 17:14. Wakoma hawa wanatakasika wakiwa njiani. Tendo
hili ya baraka na neema lahitaji shukrani. Ni mambo mangapi tunakutana nayo
njiani ya neema na baraka ila hatuoni sababu ya kushukuru?
Ni
mmoja tu kati ya wale kumi aliyekuja kwa Yesu na “akaanguka kifudifudi miguuni pake,
akamshukuru; naye alikuwa Msamaria,” Lk 17:16.
Tendo hili linamshangaza sana Yesu, naye akamjibu, “Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi?,” Lk 17:17. Ona jinsi tunavyomshangaza Mungu
tunavyokoswa moyo wa shukrani kwa yale anayotutendea. Ndugu yangu tuliyesafiri
pamoja katika tafakari hii, bado tu hauna cha kumshukuru Mungu?
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Kwa maana kila
kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa
shukrani; kwa kuwa kimetakaswa
kwa neno la Mungu na kwa kuomba,” 1Tim 4:4-5
No hay comentarios:
Publicar un comentario