JUMATANO WIKI YA 1 YA MAJILIO
2/12/2015
Somo: Isa 25:6-10a
Zab: 23:1-3a, 3b-6
Injili: Mt 15:29-37
Nukuu:
“Na katika mlima huu Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote
karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu
ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake,
iliyochujwa sana,” Isa 25:6
“Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi
katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana
Bwana amenena hayo,” Isa 25:8
“Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye Mungu wetu,
Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na tushangilie na
kuufurahia wokovu wake,” Isa 25:9
“Wakamwendea makutano
mengi wakimletea viwete, vipofu, mabubu, vilema, na wengine wengi, wakawaweka
miguuni pake; akawaponya,” Mt 15:30
“Yesu akawaita
wanafunzi wake, akasema, Nawahurumia mkutano, kwa kuwa yapata siku tatu wamekaa
pamoja nami, wala hawana kitu cha kula, tena kuwaaga wakifunga sipendi, wasije
wakazimia njiani,” Mt 15:32
“Wanafunzi wake
wakamwambia, Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani, hata kushibisha mkutano
mkuu namna hii?” Mt 15:33
“Yesu akawaambia,
Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, na visamaki vichache,” Mt 15:34
“akaitwaa ile mikate
saba na vile visamaki, akashukuru akavimega, akawapa wanafunzi wake, nao
wanafunzi wakawapa makutano,” Mt 15:36
“Wakala wote
wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate makanda saba, yamejaa,” Mt
15:37
TAFAKARI: “Mnayo mikate mingapi? Mungu wetu aliye hai habariki utupu.”
Wapendwa wana wa Mungu, kila mmoja wetu hupenda baraka na
hata kubarikiwa na Mungu kwa yale anayoyafanya na yale anayoyatamani kuyapata.
Ila ukweli ni kwamba Mungu wetu huyu aliye hai kamwe habari utupu. Lazima kuwe
na ushirikiano wako na Yeye kwa kila unachokiomba naye atakibariki. Yesu
anasema, “Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu
atanyang'anywa hata alicho nacho,” Lk 19:26. Maneno haya ya Yesu yanatimia
katika Injili ya leo ambapo tunaona Yesu baada ya kuwalisha makutano kiroho kwa
neno la uzima anaona uhitaji wao wa kulishwa kimwili. “Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema, Nawahurumia mkutano, kwa
kuwa yapata siku tatu wamekaa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula, tena
kuwaaga wakifunga sipendi, wasije wakazimia njiani,” Mt 15:32. Huyu ndiye Mungu anayeyajua mahitaji yetu ya
mwili na roho.
Wapendwa katika Kristo,
maneno hayo ya Yesu yanawatia hofu wanafunzi wake. Hivyo “Wanafunzi wake wakamwambia, Tupate wapi mikate mingi hapa
nyikani, hata kushibisha mkutano mkuu namna hii?” Mt 15:33. Je, ni kweli kwamba Wanafunzi wake Yesu
hawakuwa na chochote ili kibarikiwe? Mungu wetu aliye hai habariki utupu! “Yesu akawaambia, ‘Mnayo mikate mingapi?’ Wakasema, Saba, na
visamaki vichache,” Mt 15:34. Je, ndugu yangu umeelewa kwa nini baraka na neema
hazikufikii? Je, umetoa hata hicho kidogo ulichokuwa nacho Mungu akibariki? Je,
umefanya juhudi yoyote katika tatizo au hitaji lako ili Mungu atie mkono wake wa
baraka? Pasipo chochote na utayari wowote kutoka kwako uwezi pata chochote
kutoka kwa Mungu kwa sababu haujua hata kile utakacho au uombacho. Kwa maana
hivyo, kama tunaomba basi tunaomba vibaya! “Hata mwaomba, wala
hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu,” Yak 4:3.
Mungu
hubariki shughuli na juhudi zetu na siyo utupu. Ukweli huu tunauona katika
muujiza wa kwanza wa Yesu kule Kana, Yoh 2:1-11. Katika muujiza huu tunaona
jinsi ambavyo Yesu alivyoyabariki maji na kuwa divai baada ya Mama Bikira Maria
kutoa taarifa kwa Mwanaye akiamini hata mwangusha, na baadaye kuwaamuru wale
watumishi wa ile Harusi wayajaze maji yale mabalasi sita ya mawe. Mkuu wa Meza
alimwita Bwana Harusi na kumwambia, “Kila mtu kwanza
huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo
dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa,” Yoh 2:10. Baraka ya Mungu
haina kikomo tutimiza yale yanayotupasayo kufanya.
Wapendwa
wana wa Mungu, Mungu hukibariki hata kile kidogo tulichonacho tunapokikabidhi
chote kwake. Hili nalo tunaliona kule Sarepta, 1Fal 17:10-16, ambapo Mama yule
mjane akiwa na mtoto wake wakisubiri kula kilichobaki na kufa. Hapa anatokea
Nabii Eliya na kumwamuru mjane yule akitoe kile kilichobaki na kumwandalia “kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa
la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana
atakapoleta mvua juu ya nchi,” IFal 17:14. Mwisho wa baraka na neema za Mungu
ni mwanzo neema na mwendelezo wa baraka za Mungu. Ukweli huu tunauona katika
Injili ya leo kwamba, “wakala wote
wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate makanda saba, yamejaa,” Mt
15:37. Huyu
ndiye Mungu atendaye maajabu kwa wale wote walimridhia pasipo shaka yoyote.
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, tupo kwenye kipindi cha Majilio. Bila shaka kila moja wetu anahitaji
lake na mahangaiko yake ambayo yanaelekea kukuchosha. Basi ni wakati wa pekee
kufanya tafiti moyo ili uweze gundua ni wapi hujatoa ushirikiano wa kutosha na
Mungu. Ujio wa Masiha ni agano la kweli na haki linalotoa fursa ya kuanza upya
na Mungu. Yeye, yaani Masiha, hatatazama historia yako mbaya na ukale wako, ila
atatazama zaidi utayari wako wa kuanza naye katika upya. Nawe utakuwa mpya tu
utakapokuwa tayari kufanya toba ya kweli na majuto. Kutana na Mungu katika
Mlima huo wa Sayuni yako Mpya, yaani utayari wako wa kuanza upya naye. “Na katika mlima huu Bwana wa majeshi
atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya
urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa
juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana,” Isa 25:6. Je, inakugharimu nini ndugu
yangu kufanya toba ya kweli na majuto?
Masiha tunayemsubiri ambaye kwa hakika anakuja kwa nia ya
kutukomboa kutoka hali yetu duni iliyokomazwa na kuzeeshwa kwa sababu ya
dhambi, ndiye atakaye meza mauti yetu na kuyafuta machozi yetu. “Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU
atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika
ulimwengu wote; maana Bwana amenena hayo,” Isa 25:8. Neno la Mungu ni uzima na
halipotei bure unapoliamini mara alitamkapo Mungu. “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na
kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali
amepita kutoka mautini kuingia uzimani,” Yoh 5:24. Ndugu yangu bado una
mashaka?
Ikiwa ujio wa Masiha wetu ni kuujenga uhusiano ulibomolewa
na dhambi zetu, yanipasa kuanza kuujenga uhusiano mwema ndani ya nafsi yangu
mwenyewe, ndugu na majirani zangu, na mazingira yanayonizunguka. Masiha ajale
ni mkombozi mwenye kujenga mahusiano mema na watu wote na mataifa yote. Na “Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye
Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na
tushangilie na kuufurahia wokovu wake,” Isa 25:9. Tutashangilia na kufuraha kwa
sababu kutoka kwake tutapata uzima, kuponywa maradhi yetu, tutatembea kwa
kuponywa ulemavu wetu, tutaona kwa kuponywa upofu wetu, tutaongea kwa kuponywa
ububu wetu, na tutasikia kwa kuponywa uziwi wetu. “Wakamwendea makutano
mengi wakimletea viwete, vipofu, mabubu, vilema, na wengine wengi, wakawaweka
miguuni pake; akawaponya,” Mt 15:30. Je, ndugu yangu uliyesafiri nami katika
tafakari hii hupendi kuongea na masiha kuhusu mkwamo wako kimaisha? Je, hupendi
kutembea naye katika uzima wa milele? Je, hupendi kuona utukufu wake? Je,
hupendi kuongea ukilisifu jina lake? Na, Je! Hupendi kusikia habari njema ya
wokovu anayokuletea? Mimi napenda na
nitakaa naye kwani Yeye ndiye Mzabibu wa kweli nami ni tawi tu. “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani
yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,”
Yoh 15:5
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Nasi tumelifahamu
pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika
pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake,” 1Yoh 4:16
No hay comentarios:
Publicar un comentario