viernes, 30 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI-SIKUKUU YA WATAKATIFU WOTE

JUMAPILI, NOVEMBA 1 2015
Sikukuu ya Watakatifu Wote
Somo I: Ufu 7:2-4, 9-14
Zab: 24:1bc-2, 3-4ab, 5-6
Somo II: 1Yoh 3:1-3
Injili: Mt 5:1-12a
Nukuu:
Na malaika wote walikuwa wakisimama pande zote za kile kiti cha enzi, na za hao wazee, na za wale wenye uhai wanne, nao wakaanguka kifulifuli mbele ya kile kiti cha enzi, wakamsujudu Mungu,” Ufu 7:11

“Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo,” Ufu 7:14b

Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye,” 1Yoh 3:1

Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu,” 1Yoh 3:3 

Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni,” Mt 5:11-12

TAFAKARI: “Utakatifu ndiyo Cheo chako.”

Wapendwa katika Kristo, leo Mama Kanisa kwa furaha kubwa anaadhimisha sikukuu ya Watakatifu wote. Kwa namna ya pekee kabisa mimi na wewe leo tunakumbushwa kwamba ‘Utakatifu ndiyo Cheo chetu.’ Malengo ya Mbatizwa yeyote ni kuwa mkamilifu kama Baba yetu wa mbinguni alivyo mkamilifu. Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48. Huu ndio wito wa kila mbatizwa ili kulifikia taji lile la Utakatifu ambalo ndilo cheo chetu. Ni kuwa na matumaini na Mungu na kila siku kujitakasa na kuepuka kuishi katika hatia.Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu,” 1Yoh 3:3 

Ndugu yangu, tungali hapa dunia wengi wetu hupenda kujipambambanua na ubora wa familia zao, koo zao, makabila yao, itikadi zao za kisiasa na kidini na hata utaifa wao. Tukiishi katika ngazi hii tu bado hatujajua hatma ya uwepo wetu hapa duniani. Huko Mbinguni hatutajulikana kwa hayo niliyoyataja, bali tutajulikana kwa  usafi wetu uliotokana na UTAKATIFU wetu tuliouishi hapa duniani ikiwa ni mahali tu pa maandalizi na kupita.

Kila mmoja wetu aweza kuwa Mtakatifu. Utakatifu wako ni matokeo ya kuwa mwaminifu kwa mambo madogo madogo ya kila siku, na kuyafanya hayo kwa ukamilifu wake. Ni kuwa tayari kumpa Kristo nafasi ndani ya moyo wako ili atende kazi nawe kwa yale yanayompendeza Mungu na jirani yako. Utakatifu wako ni tokeo pia la kufungua milango kwa wote wenye uhitaji bila kujali historia zao na mapungufu yao. Ni kujaribu kufanana na Yesu katika kuwaza, kutathmini na kutenda. Tunapokuwa karibu na Kristo ndivyo tunavyofunuliwa siri za Baba yetu wa mbinguni na ufalme wake.

Ukaribu huu niliousema, utufanya kuwa watoto wapendwa wa Mungu katika utii usio shuruti. Tunatii kwa sababu Mungu anatupenda na anatutakia mema katika ukamilifu wake. Ndugu yangu, Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye,” 1Yoh 3:1. Maisha haya ya utakatifu yatatudai kila siku kusimama katika kweli na haki, na wakati mwingine tutapimwa Imani yetu.

Kupimwa huku kwa Imani kwa weza pia kutuondolea uhai wetu. Basi hili litakapotokea yatupasa kuyasema maneno haya pasipo shaka yoyote, “kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida,” Flp 1:21. Ni kuyaona yote yaliyofaida kwako ni hasara kwa ajili ya Kristo, Flp 3:7. Tunapoyaachia maisha yetu katika kiwango hiki, Kristo kamwe hawezi kutuacha katika taabu hizo. Kristo hubaki kuwa faraja kubwa kwetu katika dhiki na taabu hizo. Naye anatuambia nyakati kama hizo tuwe watu wa kufurahi kwa sababu tunamruhusu Mungu kutenda mambo katika hali yetu ya uduni na Mateso. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni,” Mt 5:11-12. Je, wayafurahia mateso yako?

Mtawa mmoja wa kiume katika Monasteri fulani alijijengea ukaribu sana na Yesu wa Ekaristi Takatifu. Mtawa huyu alikuwa mpishi wa muda mrefu katika Monasteri hiyo. Aliipenda sana kazi yake na kwake ilikuwa moja ya kumtukuza Mungu kupitia huduma hii kwa wanajumuiya wenzake. Kamwe hakuwahi kunung’unika hata pale ambapo kazi zilikuwa nyingi.

Kila asubuhi Mtawa huyu mara baada ya masifu ya asubuhi na Misa Takatifu, huenda bustanini kuchuma mboga na vitu vingine kama maandalizi ya chakula cha Mchana na jioni. Bustani ile ilikuwa baada ya kulipita Kanisa. Hivyo alijiweka ahadi ya kuongea na Yesu wa Ekaristi Takatifu kila siku kabla ya kufika bustanini.

Siku moja akiwa na kikapu chake na kisu aliingia Kanisani na kuanza kusali na kutafari mbele ya ‘Terbenakulo,’ Sehemu zinapohifadhiwa Hostia Takatifu. Mara alishtushwa na sauti ya kengele ya Malaika wa Bwana, iliyoashiria pia ni muda wa chakula cha mchana. Mtawa huyu aliingiwa na hofu kubwa sana kwani alikuwa bado hata bustanini hakuwa amefika.

Mtawa huyu aliondoka kwa haraka ili awahi kuomba msamaha kwa watawa wenzake kwa kutokuandaa chakula kile cha mchana. Maajabu ni kwamba alipofika tu eneo la jikoni alikaribishwa na harufu nzuri sana ya chakula na kusikia watawa wenzake wakimsifu kwa chakula kitamu alichoandaa. Kila mmoja alitaka kuongea naye na kumpa asante kwa kazi nzuri aliyofanya.

Akiwa ameshika kikapu chake na kisu ndani yake, alionekana akitokwa na machozi ya furaha huku akisema “asante Yesu kwa kuniona na kuniondolea aibu hii.” Watawa wote walibaki midomo wazi! Ndugu huyu alisimulia yote yaliyotokea. Jumuiya yote ilijawa na furaha na kumtukuza Mungu.
Wapendwa wana wa Mungu, tunapokuwa karibu na Mungu, kamwe hawezi kutuacha. Mungu atatupigania hadi mwisho. Hivyo tuwe waaminifu na kufanya yote kwa ukamilifu tukimtanguliza Mungu kwa kila kitu. Mtume Yakobo anatuambia siri hii kwa kusema, Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili,” Yak 4:8. Haya ndiyo maandalizi ya cheo chako, yaani, Utakatifu wako.

Tumsifu Yesu Kristo!


“Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo,” Ufu 7:14b

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 30 YA MWAKA-B

JUMAMOSI WIKI YA 30 YA MWAKA-B
31/10/2015
Somo: Rum 11:1-2a, 11-12, 25-29
Zab: 94:12-13a, 14-15, 17-18
Injili: Lk 14:7-11
Nukuu:          
Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali,” Rum 11:2

Lakini kwa kosa lao wokovu umewafikilia Mataifa, ili wao wenyewe watiwe wivu,” Rum 11:11b

Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili,” Rum 11:25 

Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao.” Rum 11:27 

Kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake,” Rum 11:29

Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe,” Lk 14:8

akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma,” Lk 14:9 

Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi pamoja nawe,” Lk 14:10

Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa,” Lk 14:11 

TAFAKARI: “Pungua ili Mungu awe na nafsi juu ya maisha yako.”

Wapendwa wana wa Mungu, ulimwengu na vyote vilivyomo vyaufunua Utukufu na Furaha ya Mungu. Hivyo uwepo wako kama binadamu ni Utukufu wa Mungu na Furaha yake. Kwa namna nyingine kujikweza kwetu na kutokuenenda kama binadamu ni chukizo kwa Mungu aliyetuumba. Huku ni kuasi na kujitenga na Mungu. Kuukubali ubinadamu wako ni sawa na kupungua ili Mungu awe na nafasi juu ya maisha yako. Mwenye hofu ya Mungu hukiri kwamba, “kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia, Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu,” Zab 90:2. Kuumbwa kwetu kama tulivyo ni mpango wa Mungu na ndiyo maana, Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali,” Rum 11:2.

Lakini jambo la ajabu na kushangaza ni kwamba, binadamu huyu hujisaha sana na kufanya atakayo na kusahau kuwa Mungu ndiye kila kitu kwake. Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye kuizuia?” Isa 43:13. Ulevi wa sifa na madaraka umekuwa moja ya vyanzo vya uasi wa mwanadamu juu ya Ukuu wa Mungu. Ulevi huu wa sifa na madaraka uharibu yote mazuri aliyoyafanya Mungu juu ya mwanadamu na mwisho wa siku yote hujeuka na kuwa ubatili.  Binadamu huenda tu huko na huko kama kivuli; Hufanya ghasia tu kwa ajili ya ubatili; Huweka akiba wala hajui ni nani atakayeichukua,” Zab 39:6. Huku ndiko kujiamini kwa kipumbavu ilhali hatujui hata hatma ya maisha yetu kwa sekunde moja ijayo.

Ndugu yangu, kumcha Bwana ni kuishi katika umilele alioukusudia ndani ya maisha yako. Hizo ndizo fadhili za Bwana kwa kila anayemcha. Ndugu yangu, fadhili za Bwana zina wamchao tangu milele hata milele, Na haki yake ina wana wa wana,” Zab 103:17. Ni kwa upendeleo wake Mungu aliamua kuanzisha uhusiano wake na mtu na mwisho kama Taifa, yaaani, Israeli, ili kukamilisha kile alichokusudia kwa wanadamu wote yaani kutupatia uzima wa milele. Ila kwa kujikweza na kuasi kwa watu hawa mara kwa mara Mungu alijiweka pembeni ili wajifunze na kumrudia kwa unyenyekevu. Hivyo kwa kosa lao wokovu umewafikilia Mataifa, ili wao wenyewe watiwe wivu,” Rum 11:11b. Waisraeli walipewa upendeleo lakini walijisahau bila kujua ukweli huu kwamba, karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake,” Rum 11:29. Majanga yote utupata tunaposhindwa kufahamu mipaka yetu na ubinadamu wetu.

Leo katika somo la Injili Yesu anatupa angalizo hasa tunapoalikwa kwenye tafrija mbalimbali. Tukizama ndani zaidi tunaona kwamba uhai tulionao na maisha tunayoyaishi ni sawa na kualikwa kwenye furaha ya Mungu na utukufu wake. Basi ni vyema mimi na wewe kutambua duniani hapa tunapita tu, na tupo kwa maandalizi ya maisha ya umilele. Yesu anatuwasa hivi kuhusu ukweli huu; Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe, akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma,” Lk 14:8-9. Kama sote tumealikwa harusini ni wazi tumepewa mastahili yaliyo sawa na yule aliyetualika. Basi yatupasa kujua kuwa sote ni waalikwa na siyo ‘mgeni rasmi.’ Kwa utaratibu wa kawaida mbele palipoandaliwa si mastahili yangu. Kumbe ni vyema na busara kutafuta nafasi nyingine. Ili kuwa sehemu salama zaidi, Yesu anatuasa hivi; Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi pamoja nawe,” Lk 14:10. Huku ndiko kwa maneno mengine kupungua ili Mungu awe na nafasi juu ya maisha yako.

Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii utakubaliana nami kwamba kati yetu kwa nafasi tulizokuwa nazo na madaraka tuliyonayo yaliyopitiliza hututia upofu na kutufanya kuwa ndiyo fimbo ya kuchapia wengine. Jeuri hii ndugu yangu tunaipata wapi wakati Maandiko Matakatifu yanatuambia, Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara,” Zab 90:10. Jinyenyekeshe basi na kuwa kile Mungu alichokusudia katika maisha yako.

Tusifu Yesu Kristo!


Bwana huwategemeza wenye upole, Huwaangusha chini wenye jeuri,” Zab 147:6

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 30 YA MWAKA.B

IJUMAA WIKI YA 30 YA MWAKA-B
30/10/2015
Somo: Rum 9:1-5
Zab: 147:12-13, 14-15, 19-20
Injili: Lk 14:1-6
Nukuu:
Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu,” Rum 9:1-2

Yesu akajibu, akawaambia wana-sheria na Mafarisayo, Je! Ni halali kuponya siku ya sabato, ama sivyo?” Lk 14:3

Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa ng'ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya sabato?” Lk 14:5

TAFAKARI: “Binadamu na uhai wake una thamani kubwa sana mbele ya Mungu.”

Wapendwa wana Mungu, tunapotafakari uumbaji wa ulimwengu huu na historia ya wokovu wetu hatuwezi kukwepa ukweli huu; kwanza, Sababu ya kuumbwa kwa ulimwengu huu kulimpa nafasi ya kwanza na ya juu mwanadamu. Mungu alichagua kwa utukufu wake na furaha yake kumuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake, Mwa 1:26-27. Jambo la pili, Uhai wa mwanadamu una thamani kubwa sana mbele ya Mungu. Uhai huu ni mali ya Mungu na zawadi ya Mungu kwetu. Ni jukumu la mtu binafsi na jamii inayomzunguka kuulinda uhai huu kwa gharama zote. Katika jitihada hizi Mungu hatotuacha “Kwa sababu Bwana atawatetea; Naye atawateka uhai wao waliowateka,” Mit 22:23. Je, tunayosababu ya kuhuzunika pale tunapokandamizwa haki zetu na kunyanyaswa kwa uhai wetu? Lazima kuhuzunika kwa sababu siyo mpango wa Mungu bali ni mpango wa mwanadamu anayechukuwa nafasi ya Mungu. Ni hali yetu ya kibinadamu kama asemavyo Mtume Paulo, Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu,” Rum 9:1-2. Pamoja na hali hii bado tunayo matumaini makubwa sana kwa sababu Mungu wetu yu hai na huyaona mateso yote. Ni wakati tu utakapotimia atasimama katika kweli na haki.

Kipindi cha Yesu, Wayahudi kwa kuishika sabato yao, walikubali kuona mtu anatesaka hata kufa kuliko kuivunja sabato. Yesu anazihoji dhamiri zao, akawaambia wana-sheria na Mafarisayo, Je! Ni halali kuponya siku ya sabato, ama sivyo?” Lk 14:3. Maandiko Matakatifu yanatuambia kwamba wao wote walinyamaza. Yesu akalitenda lile lililo jema na lenye kumpendeza Mungu. Ukimya wa watu hawa unadhihirisha ni kwa namna gani haki za watu zinavyokanyagwa ili tu kulinda maslahi binafsi kwa wachache kupitia mgongo wa sheria ambazo ni kandamizi.

Kwa mara nyingine tena, Yesu anahoji dhamiri zao na matendo yao kwa kwenda ndani kabisa kwa yale wanayoyafanya kinyume na sheria zile kandamizi wanazoziamini na kuzishika. Yesu Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa ng'ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya sabato?” Lk 14:5. Jambo hili walilifanya licha ya kuwa vinara wa kushika sabato kwa nguvu zote. Yesu anawathibitishia tena upofu wao juu ya sheria na amri za Mungu. Yesu anawathibitishia pia ukatili wao na uovu wao juu ya mapendo kwa jirani. Je, leo tunafanya tofauti tunapolitazama Taifa letu. Ni mara ngapi wenye haki hushutumiwa na mwisho kuhukumiwa wauaji, na wauaji kuwa huru? Ni mara ngapi tunashuhudia uovu uliokithiri na hakuna hatua yoyote inayochukuliwa na watawala wenye dhamana ya mali na haki za raia zake?

Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, na kama mmoja wa jamii ya watu wa Mungu na Taifa kwa ujumla wake, bado tunayo safari ndefu kuelekea mwanga kamili wa kweli na haki. Safari hii itakuwa fupi tu tukifanya mambo makubwa yafuatayo; Kwanza kabisa tumwogope Mungu na kuwa na hofu ya Mungu, na kwamwe tusichukue nafasi ya Mungu kwani hatutafanikiwa. Pili, kutoka moyoni mwetu tuikatae hali hii ya ukandamizaji kwa mawazo, maneno, na vitendo. Tatu, kila mmoja wetu atimize wajibu wake kwa haki na kweli. Na nne, tujali umoja wetu na uzalendo wetu kama Taifa.

Tumsifu Yesu Kristo!


Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure,” Zab 127:1

miércoles, 28 de octubre de 2015

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 30 YA MWAKA-B

ALHAMISI WIKI YA 30 YA MWAKA-B
29/10/2015
Somo: Rum 8:31b-39
Zab: 109:21-22, 26-27, 30-31
Injili: Lk 13:31-35
Nukuu:
“Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?” Rum 8:31b 

Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki,” Rum 8:33

Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea,” Rum 8:34

Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda,” Rum 8:37 

Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu,” Rum 8:38-39

Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika,” Lk 13:32 

Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, wala hamkutaka,” Lk 13:34 

Angalieni, mmeachiwa nyumba yenu! Nami nawaambia, Hamtaniona tena kamwe, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana,” Lk 13:35

TAFAKARI:Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?”

Wapendwa wana wa Mungu, Mwana falsafa Spinoza aliwahi kusema “kifo hakiwezi kuepukika. Ni lazima tutakukufa. Kinachotusumbua ni hofu kuhusu kifo. Hivyo yatupasa kuishinda hofu. Na hivyo ni vizuri kufikiri kuhusu uhai.” Mpendwa, je wamwamini Kristo Yesu? Kama unamwamini Kristo Yesu hakuna sababu ya kuwa na hofu kuhusu kifo. Kristo Yesu kwa maisha yake, mateso, kifo, na ufufuko wake ni jibu kuhusu aina zote za uovu na kifo. Kristo Yesu ndiye kielelezo chetu kama wafuasi wake. Kristo Yesu ametupatia mfano na jibu kwamba hakuna uovu wowote unaoweza kudumu katika umilele wake. Yesu haogopi vitisho wala kifo.

Yesu anapoambiwa aondoke kwa kuwa Herode anataka kumuua aliwajibu, “Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika,” Lk 13:32. Mnyama huyu Mbweha alitafsiriwa kama mtu asiye na msimamo, kigeugeu na mwongo. Kristo hawezi kutishiwa na mtu wa hali hii na kuacha kutoa huduma kwa watu ikiwa ndiyo sababu na mpango kazi wake kwa watu wote. Ni kwa kupitia Kristo vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema,” Mt 11:5. Kristo pia anaufunua utukufu wake mara baada ya kuushinda uovu anaposema, ‘siku ya tatu nakamilika.’

Mateso tunayoyapata leo au tuliyokwisha yapata kupia wazazi wetu, siyo kwamba historia hiyo ya uovu Mungu haioni. Wakati utimiapo vyote vitafanywa upya. Yesu anapoutazama mji wa Yerusalemu anayakumbuka na kuyaona mateso na uovu wa manabii wake walifanyiwa na kusema, Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, wala hamkutaka,” Lk 13:34. Huu kwetu ni wito wa kuongoka na kuacha njia zetu mbaya na kujisalimisha kwa Kristo. Tusisubiri hadi siku ya Mwisho kwani hatutakuwa na muda tena wa kujisalimisha kwake. Utakuwa muda wa kupokea ukumu yetu kila mmoja kadiri alivyotenda. Yesu anasema, Angalieni, mmeachiwa nyumba yenu! Nami nawaambia, Hamtaniona tena kamwe, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana,” Lk 13:35. Je, kuna sababu ya kusubiri hadi siku ya mwisho? Ndugu yangu natuanze kuishi maisha ya ufufuko kabla ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.

Maisha baada ya ufufuko ni maisha yaliyokamili. Tunayaishi maisha haya ya ufufuko kwa kuhesabiwa haki na kwa kuzaliwa mara ya pili kwa Roho Mtakatifu. Hivyo si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu,” Tit 3:5-7. Je, una sababu yoyote ya kuwa na hofu juu ya maisha yako ukiwa na Kristo?

Tukiwa ndani na katika Kristo tu wateule wa Mungu na hakuna wa kutushitaki kwa sababu Mungu kwa kupitia mwanaye Mpenzi ndiye anayetuhesabia haki. Basi Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki,” Rum 8:33. Katika hali hii hakuwa wa kutuhukumia adhabu kwa sababu tumeshayasalimisha maisha yetu kwa Kristo mwenyewe aliyekubali kufa kwa ajili yetu. Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake,” Rum 6:5. Hapa adhabu ya kifo na hofuzimebatilishwa kwa kifo chake Kristo. Hivyo Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea,” Rum 8:34.

 Ndugu yangu, Kristo akupende vipe tena uamini anakupenda? Huku ndipo Kristo alipotupenda upeo na wakati ulipofika aliyatoa maisha yake kwa sababu yako na yangu. “Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo,” Yoh 13.1. Upendo huu hadi leo Kristo anauthibitisha kwetu tunapoutazama msalaba akiwa ameifungua mikono yake na kusema, ‘tazama ninavyokupenda nimekubali kufa kwa sababu yako.’

Tunapo jisalimisha kwa Kristo hakika nguvu za giza na uovu wa aina yoyote ile hauwezi ukashinda kwa sababu Kristo anatupenda.  Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda,” Rum 8:37. Kutokuwa na Imani pamoja na kutengemea vitu vingine mfano pesa na mamlaka fulani ni moja ya vizuizi vinavyotufanya kushindwa kujisalimisha kwa Jemedari wetu Yesu Kristo.

Wapendwa wana wa Mungu, tunapojisalimisha kwa Kristo hakuna kitu wala kiumbe chochote kinachoweza kututenganisha na upendo wake. Paulo anasema, kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu,” Rum 8:38-39. Ndugu yangu tunayesafiri wote kwenye tafakari hii, bado tu hujakata shauri la kujisalimisha kwa Kristo? Kama bado anza sasa taratibu. Wengine inawachukua muda mrefu na wengine ni rahisi tu. Moja ya njia ya kujisalimisha kwa Kristo ni kuwa tayari kufanya atakayo na apendayo Kristo hata pale tusipotaka kufanya hivyo.

Tumsifu Yesu Kristo!


 Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu,” Rum 8:1

martes, 27 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 30 MWAKA-B

JUMATANO WIKI YA 30 YA MWAKA-B
Sikukuu ya Simoni na Yuda, Mitume
28/10/2015
Somo: Efe 2:19-22
Zab: 19:2-3, 4-5
Injili: Lk 6:12-16
Nukuu:
Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni,” Efe 2:20 

Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana,” Efe 2:21

Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho,” Efe 2:22

akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume; Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote,  na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti,” Lk 6:13b-16 

TAFAKARI: “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, Kristo ni jiwe la pembeni.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Mitume Simoni na Yuda. Mitume kwa ujumla wao, yaani wale kumi na mbili, kwa maisha yao na ushuhuda wao wa Imani ndiyo msingi Imara wa Kanisa letu kama tunavyoliona hii leo. Akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume; Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartolomayo, na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote,  na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti,” Lk 6:13b-16. Sadaka yao kwa maisha yao ya Imani juu ya Kristo Yesu, Kanisa linaendelea kutimiza wajibu wake kama sakramenti ya wokovu wetu. Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la pembeni.

Ukristo wetu na Imani yetu imejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, na Kristo Yesu akiwa jiwe kuu la pembeni. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni,” Efe 2:20. Ni fahari ya kila aliyebatizwa kuishi ahadi zake za ubatizo na kuendeleza msingi huu imara wa Imani. Hivyo kila mmoja wetu kwa njia ya Kristo na kwa sadaka ya maisha yake na wito wake, ameunganishwa hekalu la Mungu. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana,” Efe 2:21. Mitume tunaowasheherekea leo ni mfano wa kuingwa kwetu. Mitume hawa walikuwa mashahidi na manabii katika kipindi chao. Maisha hayakuwa rahisi tunapolitazama Kanisa la Mwanzo. Wengi wao walikufa kwa kuuwawa kikatili, ila hakuna aliyemsaliti Kristo zaidi ya Yuda Eskariote. Leo miongoni mwetu akina Yuda wapo wengi sana. Ni ni changamoto ya Kanisa na maisha yetu ya kijamii.

Wapendwa wana wa Mungu, leo Kanisa linachangamoto nyingi sana. Ili kuzikabili changamoto hizi, yampasa kila mbatizwa kuishi ahadi zake za ubatizo. Pili, kila mmoja wetu kadiri ya wito wake ajitahidi kila siku kufanana na Kristo ambaye ndiye jiwe kuu la pembeni ambapo maisha yetu na sadaka yake upewa maana. Huu ni ushuhuda tosha wa ukimya hata pale ambapo Kristo hakubaliki kutokana na mitazamo tofauti ya Kiimani. Matendo yetu mema humwakilisha vizuri Kristo popote kuliko kile tukiaminicho kwa nadharia tu. Mtume Yakobo anatupatia changamoto hii kwa kusema, Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu,” Yak 2:18.

Wapendwa wana wa Mungu, tuwe waaminifu kwa wito wetu kila mmoja kadiri ya namna yake,  na upendo uliobeba matendo yetu mema kwa watu wote.

Tumsifu Yesu Kristo!


Watakatifu Simoni, na Yuda Mitume, Mtuombee.

lunes, 26 de octubre de 2015

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 30 MWAKA-B

JUMANNE WIKI YA 30 YA MWAKA-B
27/10/2015
Somo: Rum 8:18-25
Zab: 126:1b-2abc, 2cd-3, 4-5, 6
Injili: Lk 13:18-21
Nukuu:
Kwa maana nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu,” Rum 8:18 

Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu,” Rum 8:19 

Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu,” Rum 8:23

Bali tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingojea kwa saburi,” Rum 8:25 

Umefanana na punje ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake,” Lk 13:19 

Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote pia,” Lk 13:21

TAFAKARI: “Tukilinganisha na umilele, maisha ya hapa duniani ni mafupi sana. Imani thabiti ndiyo kielelezo cha kuufikia umilele huo, Ufalme wa Mungu.”

Wapendwa wana wa Mungu, ili kutimiza vizuri maisha yako hupaswi kusahau ukweli wa aina mbili: Kwanza, yakilinganishwa na umilele, maisha ni mafupi sana. Pili, dunia ni makazi ya muda tu. Hatuwezi kukaa hapa kwa muda mrefu, hivyo usijishikamanishe sana nayo. Mfalme Daudi aliomba, "Bwana, nijulishe mwisho wangu, na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani; nijue jinsi nilivyo dhaifu," Zab 39:4

Mpendwa katika Kristo, usisahau kuwa maisha ya hapa duniani ni sawa na kuwa ugenini. Haya si makazi yako ya kudumu, au hatma yako ya mwisho. Unapita tu! Unatembea tu duniani. Mfalme Daudi anatukumbusha, "Mimi ni mgeni katika nchi, usinifiche maagizo yako," Zab 119:19, na Mtume Petro anasema,  "na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni." 1Pet 1:17. Waamini wa kweli wanafahamu wazi kwamba kuna mambo mengi ya maisha kuliko hii miaka michache tunayoishi hapa duniani.

Ni katika mtazamo huu somo la kwanza na Injili yanatutafakarisha kuyaona maisha ya hapa nduniani ni mafupi na hivyo ni muhimu kuyachuchumilia yake ya milele, yaani, ufalme wa mbinguni. Katika hali hii IMANI thabiti ndani na katika Kristo kicho kielelezo chetu leo na sasa ili kuufikia uhalisia huo. Imani hiyo inatupa nguvu ya kuyakabili mateso na mahangaiko yetu ya kila siku za uhai wetu hapa duniani tunapomtazama Jemedari wetu Yesu Kristo aliyeyashinda mateso. Ni kwa Imani  hiyo Mtume Paulo anasema, nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu,” Rum 8:18. Kila kiumbe chenye uhai kina shauku hiyo ndani mwake kwa sababu uwepo wake si wa bahati mbaya. Vyote vilivyoumbwa vinaufunua Utukufu wa Mungu na furaha ya Mungu. Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu,” Rum 8:19. Kufunuliwa huku ndiko kujionyesha wazi kwa Utukufu wa Mungu na furaha yake. 

Utukufu wa Mungu na furaha yake ufikia kilele chake pale ambapo binadamu anapoishi kama binadamu katika utimilifu, ukamilifu, na makusudi ya kuumbwa kwake. Ukweli huu ni kwa viumbe vyote kama vilivyo. Sisimizi uufunua Utukufu wa Mungu na furaha yake anapoishi kweli kama sisimizi katika utimilifu, ukamilifu, na kusudi la kuumbwa kama sisimizi. Kufikia lengo hili kote kwa viumbe vyote na hasa mwanadamu kwa hitaji sadaka kubwa. Wala si hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu,” Rum 8:23. Kwa upande wa mwanadamu moja ya sadaka hiyo ni kuyakubali mateso na mahangaiko kama sehemu ya kutakaswa kwake. Mateso haya katika Imani thabiti ndani na katika Kristo huwa tarajio lisilokuwa na shaka na lenye msingi imara. Ni kweli kwamba, tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingojea kwa saburi,” Rum 8:25. Je, Imani hiyo itupelekeayo kwenye Ufalme wa Mungu ina mfanano gani?

Jibu la swali hili limetolewa katika injili ya leo. Yesu anauliza aufananishe na nini na ufalme wa mbingu? Kwanza Yesu anasema ufalme huu, Umefanana na punje ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake,” Lk 13:19. Maana yake nini? Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, Imani ni kuamini na kusadiki pasipo shaka yale mambo madogo madogo yanayoonekana na yasiyooneka na yenye kuufunua utukufu wa Mungu. Punje ya haradali ni ndogo sana. Lakini katika udogo huu mwisho wake huwa mti mkubwa na ndege wa angani wakakaa katika matawi yake. Imani si jambo la siku moja, bali Imani ukua hatua kwa hatua kadiri tunavyoishi na kuona vitu na mazingira yake kwa mwono wa Kimungu, (Kila kitu kuwa na sababu yake)

Pili, Yesu anasema ufalme wa Mungu umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote pia,” Lk 13:21. Imani ya kweli na thabiti ni nguvu ya ndani ya ajabu kwa mtu ambayo hubadili kabisa mwonekano wa vitu kwa mtu, utendaji, na hata namna ya kuyachukulia mambo. Chachu katika uchache wake hubadili kabisa mwono na umbo wa kile kilichochachushwa. Imani hii ndiyo inayotupa nguvu na dira mpya ya kuyaona maisha kwa namna ya pekee licha ya ufupi wake na sababu ya kuishi kwetu hapa duniani, katika maana ya makazi ya muda mfupi. Makazi haya ni sehemu ya maandalizi ya maisha ya umilele ambayo ndiyo ufalme wenyewe wa Mungu.

Hivyo ndugu yangu tunapoishi hapa duniani mambo haya yatupasa kuyazingatia. Moja,  msingi wa wa maisha wetu lazima ujengwe katika haki. Kwani, yaliyo haki kabisa ndiyo utakayoyafuata, ili upate kuishi na kuirithi nchi upewayo na Bwana, Mungu wako,” Kumb 16:20. Pili, tusienende katika tamaa za wanadamu. Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani,” 1Pet 4:2. Na tatu na mwisho, kuishi kwetu kuwe ndani na katika Kristo. Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida!” Flp 1:21. Kristo ndiye mtetezi wetu na mwokozi wetu. Amina

Tumsifu Yesu Kristo!


Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu, Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee,” Zab 51:10-11