martes, 31 de enero de 2017

TAFAKARI: ALHAMISI; SIKUKUU YA KUTOLEWA BWANA HEKALUNI


SIKUKUU YA KUTOLEWA BWANA HEKALUNI

Siku ya Maisha ya Wakfu-Maisha ya Kitawa

2/2/

Somo I: Mal 3:1-4

Zab: 24:7, 8, 9, 10

Somo II: Ebr 2:14-18

Injili: Lk 2:22-40

Nukuu:

Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi,” Mal 3:1.

Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani,” Mal 3:4.

awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa,” Ebr 2:15.

Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake,” Ebr 2:17.

Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),” Lk 2:22-23.

wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili,” Lk 2:24.

Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako,” Lk 2:29-30.

Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa,” Lk 2:34.

Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake,” Lk 2:40.

TAFAKARI: “Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni. Yesu anatolewa hekaluni kama ilivyo desturi ya Wayahudi kwa kila mzaliwa wa kwanza wa kiume. “Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),” Lk 2:22-23. Hata hivyo, kumkomboa huyu mzaliwa wa kwanza kutoka hekaluni iliwapasa wazazi wake kumtolea Bwana sadaka kama shukrani. “Wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili,” Lk 2:24. Sadaka hii inaonyesha umasikini wa Familia hii Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Ni katika tendo hili pale Hekaluni, Simeoni mtu wa kweli na haki ahadi yake inatimizwa na Mungu. “Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake,” Lk 2:25. Yesu Kristo hapa ndiye nuru halisi na uhuru wa kweli wa wana wa Taifa la Mungu. Kristo ndiye ile nuru aliyokuwa ikisubiriwa, “Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli,” Lk 2:32. Mungu anaifunua nuru ya Yesu ndani ya moyo wa Simeoni naye anayaona makuu ndani ya Yesu: “Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa,” Lk 2:34. Kristo ndiye sababu ya kuanguka na kuinuka wengi, kwa sababu ulimwenguni hapa ni vita dhidi ya mwanga ambaye ndiye Kristo, na giza ambayo ndiye yule mwovu shetani. Watainuliwa wale watakaoambatana na mwanga na wataangushwa wale waambatanao na giza, yaani yule mwovu.

Katika vita hii Mama Bikira Maria hatakuwa salama katika maana ya kufurahia tu uwepo wa mwanaye. Ni katika uchungu na kushiriki mateso ya mwanaye nuru ya kweli na haki itafunuliwa ndani yake. Hivyo ni katika msalaba ambao mwanaye anauendea ndipo utakapokuwepo utukufu wake. “Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi,” Lk 2:35. Kwenye Msalaba Mtakatifu na wenye ushindi wa Bwana Yetu Yesu Kristo ndipo penye utukufu, kufunguliwa kwa mioyo yetu kutoka utumwa wa dhambi, na kuuelekea uzima wa milele. Hivyo kwa Mkristo na Mfuasi wa Kristo, hakuna UTUKUFU pasipo MSALABA.

Kuyafanya mapenzi ya Mungu wakati mwingine hakuhakisi kabisa miono na mitazamo ya kibinadamu. Mitazamo yetu ni kwamba tuwapo karibu sana na Mungu na kufanya mapenzi yake, ndiyo miminiko ya baraka na neema. Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, hatutendi mema wala kuwa waaminifu mbele ya Mungu ili tununue baraka na neema zake, bali tunayafanya hayo yote kwa sababu ndiyo hali na uwepo wa Mungu, na ndivyo impendezavyo sisi kufanya. Uwepo wetu hapa duniani ni moja ya uzuri na utukufu wa Mungu. Mfano wa wale waliyafanya yote vyema ila hayakuendana na miono na mitazamo ya kibinadamu ni Ana binti Fanueli. Tunaambiwa “Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake,” Lk 2:36. Bila shaka Ana kama Mwanamke na Mama, kuwa na familia kamili katika maana ya Yeye, Mumewe na mtoto au watoto ilikuwa moja ya furaha yake kubwa hapa duniani. Pamoja na kukosa hilo, hakuwa na nafasi ya kumlaumu Mungu wala kuasi Imani yake. Aliishi kwa matumaini makubwa ingawa umri wake ulisogea. “Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba,” Lk 2:37. Wangapi kati yetu tunaujasiri huu tunapoona mbele yetu ni giza tupu?

Furaha ya Ana binti Fanueli inakamilika anapokutana na Yesu. Ni kama asemavyo Mt. Agustino kwamba ‘mioyo yetu haitulii mpaka itakapotulia kwako Ee Bwana.’ Ndivyo ilivyokuwa kwa Ana binti Fanueli alipokutana na Yesu. “Huyu (Ana binti Fanueli) alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake,” Lk 2:38. Alichokua akikitazamia amekiona kwa macho yake.

Na “Yule mtoto (Yesu) akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake,” Lk 2:40. Maana yake aliyaishi maisha yetu, furaha zetu, mahangaiko yetu, na kuyashiriki yote bila kutenda dhambi hadi kikomo chake pale Msalabani kwa kutuweka huru. Hivyo “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Je, una chochote chenye thamani  katika ulimwengu huu ambacho waweza kulinganisha na wokovu aliyokupatia Kristo Yesu? Je, tendo hili la Bwana kutolewa hekaluni na yale yote yaliyojiri kule hekaluni yanasema nini katika siku yetu hii ya Watawa duniani?

Wapendwa katika Kristo, Maisha ya Kitawa hayana tofauti na tendo hili la Bwana kutolewa hekalu na kile wafanyacho watawa wanapojiweka wakfu kwa Mungu. Kujiweka Wakfu ni kujitenga kwa kazi MAALUMU kwa ajili ya Kristo, kwa sababu ya Kristo, na Kwa Kristo. Huku ndiko KUJISALIMISHA kwa MTAWA na KUABUDU kuliko na AMANI, FURAHA, na NGUVU. Ndugu yangu, kujitoa kwa Mungu ndiyo kuabudu hasa. Tendo hili la kujisalimisha binafsi huitwa kwa majina mengine; Kujiweka wakfu, Kumfanye Yesu Bwana wako, Kuchukuwa msalaba wako, Kuifisha nafsi, na Kujitoa kwa Roho Mtakatifu. Cha muhimu hapa ni kwamba ulitende, siyo linaitwaje. Mungu anapenda maisha yako yote. Asilimia tisini na tano haitoshi. Ndugu, kuna vizuizi vitatu ambavyo huzuia kujisalimisha kwetu kikamilifu kwa Mungu; Moja, hatuelewi kiasi gani Mungu anatupenda. Pili, tunataka kutawala maisha yetu wenyewe. Na tatu, tunashindwa kuelewa maana ya kujisalimisha.

Je, naweza kumwamini Mungu?

Ndugu yangu, Imani ni jambo muhimu sana katika kujisalimisha. Huwezi kujisalimisha kwa Mungu kama Mtawa au yeyote yule mwenye hofu ya Mungu, mpaka uwe unamwamini, lakini huwezi kumwamini Mungu mpaka umfahamu vyema. Hofu hutuzuia kujisalimisha, lakini upendo huondoa hofu yote. Kadiri unavyotambua jinsi Mungu anavyokupenda, ndivyo kujisalimisha kunavyokuwa rahisi. Jambo hili halitegemei umri wetu wa ukristo wetu, wala kwa maisha ya utawani.

Je, unajuaje Mungu anakupenda?

Ndugu yangu, Mtawa mwenzangu, nawe mwenye hofu ya Mungu, Mungu anakupa ushindi mwingi: Mungu anasema anakupenda, "Bwana ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote." Zab 145:9. Hautoki kwenye uangalizi wake kamwe, "Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, umeelewa na njia zangu zote," Zab 139:3. Yeye anaangalia mambo yote ya maisha yako, "Lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote," Mt 10:30. Alikupa uwezo wa kufurahia aina zote za viburudisho, "bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha," 1Tim 6:17b. Ana mpango mzuri kwa ajili ya imani yako, "Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi; asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zote za mwisho," Yer 29:11. Yeye hukusamehe, "Kwa maana Wewe, Bwana, Umekuwa tayari kusamehe, Na mwingi wa fadhili, kwa watu wote wakuitao," Zab 86:5. Na kwa upendo anakuvumilia, "Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema," Zab 145:8. Ndugu na Mtawa mwenzangu nawe mwenye hofu ya Mungu, Mungu anakupenda kiasi kisichopimika kuliko unavyoweza kufikiri.

Uthibitisho wa ukweli huu ni dhabihu ya Mwana wa Mungu kwa ajili yako. "Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi, " Rum 5:8. Kama unataka kufahamu uthamani wako mbele za Mungu, mwangalie Yesu Kristo na mikono yake ilivyowambwa, akisema, "nakupenda sana! Bora nife kuliko kukukosa."

Ndugu yangu mwenye hofu ya Mungu, na Mtawa mwenzangu, Mungu siyo kiongozi katili wa msafara wa watumwa au mchokozi anayetumia mabavu kutulazimisha kumtii. Hajaribu kuvunja utashi wetu, lakini hutusihi ili tujitoe wenyewe kwake kwa kupenda. Mungu ni mpendwa na mkombozi, na kujisalimisha kwake huleta uhuru, siyo utumwa. Tunapojisalimisha kwa Yesu kikamilifu, tunagundua kwamba yeye si mtawala wa IMLA, lakini RAFIKI ANAYE KUKUBALI MIPAKA YETU. Kikwazo kingine cha kujisalimisha kikamilifu ni majivuno yetu. Hatukubali kwamba sisi ni viumbe tu na kwamba hatuna utawala juu ya kila kitu. Hili ni jaribu kila zamani "mtakuwa kama Mungu, " Mwa 3:8, tamaa hiyo ya kuwa na utawala juu ya kila kitu ni chanzo cha matatizo mengi katika maisha yetu. Maisha ni mapambano, lakini jambo ambalo watu wengi hawaelewi ni kwamba mapambano yetu kama yale ya Yakobo hakika ni mapambano na Mungu! Tunataka kuwa sawa na Mungu, na haitawezekana sisi kushinda pambano hilo.

A. W. Tower alisema, "sababu kwa nini watu wengi bado wanasumbuka, bado wanatafuta, bado wanafanya maendeleo kidogo ni kwa vile bado hawajafikia mwisho wao wenyewe. Bado tunajaribu kuamuru na kuingilia kazi ya Mungu ndani yetu." Ndugu yangu, sisi siyo Mungu na hatuta kuwa kamwe. Sisi ni wanadamu. Ni pale tunapojaribu kuwa Mungu ndipo tunaishia kuwa kama Shetani kabisa, ambaye alitamani jambo hilo hilo.

Tunakubali ubinadamu wetu kiakili lakini siyo kihisia. Tunapokabiliwa na mapungufu yetu, ndipo tunaonyesha uchungu, hasira na chuki. Tunataka kuwa warefu (au wafupi), wenye akili, wenye nguvu, wenye vipawa, warembo, na matajiri. Tunataka kuwa na kila kitu na kufanya kila kitu na tunakata tamaa inaposhindikana. Kisha tunatambua kwamba Mungu aliwapa watu wengine vipawa ambavyo sisi hatuna, na hivyo tunapatwa husuda, wivu, na kujisikitikia.

Nini maana ya kujisalimisha?

Kujisalimisha kwa Mungu si kujiuzulu na kukaa tu kusubiri, au kuamini kuwa yote yameandikwa binadamu hana hiari, au kuwa na udhuru na wivu. Siyo kukubali hali hiyo hiyo uliyo nayo. Inaweza kumaanisha kinyume cha haya; kujitoa sadaka maisha yako au kuteseka ili kubadilisha yanayohitaji kubadilishwa. Mara nyingi Mungu huwaita watu waliojisalimisha kwake kupiga vita kwa jina lake.

Ndugu, kujisalimisha sio kwa uoga au mazulia. Mungu asingependa kupoteza akili alizokupa! Mungu hapendi watu wawe kama mitambo (robots) ili kumtumikia. Kujisalimisha siyo kukomesha utu wako. Badala ya kukomesha utu wako, kujisalimisha huutia nguvu. C. S. Lewis alisema, "kadiri tunavyomruhusu Mungu atutawale ndivyo tunavyozidi kuwa sisi wenyewe-kwa sababu yeye ndiye aliyetuumba. Alibuni namna mbalimbali za watu wote tofauti ambao mimi na wewe tulikusudiwa kuwa...Ni pale ninapomgeukia Kristo, ninapojikabidhi nafsi yangu kwake, ndipo ninapokuwa na ule utu wangu halisi."

Kujisalimisha kunadhihirika vyema katika kutii. Ukisema 'ndiyo, Bwana' kwa chochote anachokueleza. Kusema "Hapana, Bwana" ni kutamka vinyume. Hatuweza kumwita Yesu Bwana na wakati huo huo hatutaki kumtii. Baada ya usiku kucha bila kupata samaki, Simoni Petro alionyesha kujisalimisha pale Yesu alipomwambia kujaribu tena. "Simoni akajibu akamwambia, Bwana Mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu," Lk 5:5. Watu waliojisalimisha hutii neno la Mungu hata kama linaonekana kutokuwa na maana.

Ndugu yangu na Mtawa mwenzangu, nawe mwenye hofu ya Mungu, jambo lingine katika kujisalimisha ni IMANI. Ibrahimu (Mwa 12: 1-4) alifuata maelezo ya Mungu bila kujua alikokuwa akienda. Hana (1Sam 1:1-20) alisubiri wakati wa Mungu bila kujua ni lini. Mama Bikira Maria (Lk 1:26-35) alitarajia muujiza bila kufahamu utatendekaje. Yusufu mume wa Bikira Maria (Mt 2: 19-25) aliamini lengo la mungu bila kujua kwa nini mazingira yalikuwa hivyo. Kila mmoja wa watu hawa alikuwa amejisalimisha kwa Mungu alipomtegemea bila kujibakiza.

Utafahamu umejisalimisha kwa Mungu unapomtegemea Mungu akutengenezee mambo yako badala ya kujaribu kuwafanyia hila wengine, ukapitisha jambo lako, na mwisho ukatawala mazingira hayo. "Ukae kimya mbele za Bwana, Nawe umngojee kwa saburi," Zab 37:7a. Baada ya kujaribu sana, umwamini zaidi. Pia ufahamu kwamba unajisalimisha unapokuwa huchukizwi na lawama na kukimbilia kujitetea. Mioyo iliyojisalimisha huonyesha mahusiano mazuri na wengine. Huwatupilia mbali wengine, hudai haki zako, na hutumikii nafsi yako kama umejisalimisha.

Eneo gumu kwa watu wengi kujisalimisha ni mali na pesa zao. Wengi wamefikiri, "Nataka kuishi kwa ajili ya Mungu lakini pia nataka kupata pesa nyingi ili niishi kwa raha baadaye nipumzike." Kupumzika siyo lengo la maisha ya kujisalimisha, kwa sababu huku ni kushindana na Mungu kwa sababu ya kuweka mkazo kwanza kwa maisha yetu. Yesu anasema, "hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu," Mt 6:24 na kwamba "kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako," Mt 6:21.

Ndugu yangu, kielelezo kikubwa cha kujisalimisha ni Yesu. Usiku ule kabla ya mateso Yesu alijisalimisha kwa mpango wa Mungu. Alisali, "Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe," Mk 14:36. Yesu hakuomba, "Baba, kama unaweza kuniondolea maumivu haya, tafadhali fanya hivyo." Alikuwa tayari amethibitisha kuwa Mungu ana uwezo wa kufanya lolote! Badala yake anaomba, "Mungu kama inapendeza kwako kuniondolea mateso haya, tafadhali fanya hivyo. Lakini kama yanatimiza kusudi lako, ndivyo ninavyotaka pia.

Kujisalimisha halisi husema, "Baba, kama tatizo hili, maumivu haya, ugonjwa huu, au hali yoyote inahitajika kutimiza lengo lako na utukufu kwako katika maisha yangu au ya mwingine, tafadhali usiliondoe." Kiwango hiki cha ukomavu hakiji kwa urahisi. Kwa upande wa Yesu, aliugua sana kuhusu mpango wa Mungu kiasi cha kutoa jasho la damu. Kwa upande wetu, ni vita kali dhidi ya asili yetu ya ubinafsi.

Je, baraka za kujisalimisha ni zipi?

Maandiko Matakatifu yapo wazi kabisa kuhusu unavyoweza kufaidika unapojisalimisha kikamilifu kwa Mungu. Kwanza unapata amani: "mjue sasa Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia," Ayu 22:21. Pili, unapata uhuru: "lakini Mungu na ashukuriwe, kwa maana mlikuwa watumwa wa dhambi, lakini mliitii kwa mioyo yenu ile namna ya elimu ambayo mliwekwa chini yake," Rum 6:17.

Tatu, unapata nguvu za Mungu katika maisha yako. Majaribu makali na matatizo mazito yanaweza kushindwa na Kristo kama atakabidhiwa. Joshua alipoviendea vita vile vikubwa maishani mwake, (Yosh 5:13-15) alikutana na Mungu, akamsujudia, na akasalimisha mipango yake. Kujisalimisha huko kulileta ushindi mkubwa pale Yeriko.

Hiki ni kitendawili: Ushindi huja kwa kujisalimisha, kujisalimisha hakukudhoofishi wewe; kunakutia nguvu. Jisalimishe kwa Mungu, hauhitaji kuogopa au kujisalimisha kwa chochote kile. William Booth, mwanzilishi wa Jeshi la wokovu, alisema, "ukuu wa nguvu za ubinadamu unapimwa kwa kiwango chake cha kujisalimisha."Watu waliojisalimisha ndio Mungu anawatumia. Mungu alimchagua Bikira Maria Mama wa Yesu, siyo kwa sababu alikuwa na kipawa, au utajiri wa uzuri wa umbile, lakini kwa sababu alikuwa amejitoa kikamilifu kwake. Malaika wa Bwana alipomwelezea mpango mgumu wa Mungu, alijibu kwa upole, "Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema," Lk 1:38a. Hakuna kitu kikubwa kama maisha ya kujisalimisha katika mikono ya Mungu. "Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye  atawakimbia," Yak 4:7a.

Je, njia bora ya kujisalimisha ni ipi?

Kila mtu hatimaye hujisalimisha kwa mtu au kitu fulani. Kama sio kwa Mungu, utajisalimisha kwa matarajio au maoni ya watu wengine, au pesa, chuki, hofu, au kwa kiburi chako au tamaa mbaya, au ubinafsi. Uliumbwa kumwabudu Mungu na kama utashindwa kumwabudu, utatengeneza vitu vingine (sanamu) ili uvipe maisha yako.

Ndugu yangu na Mtawa mwenzangu, nawe mwenye hofu ya Mungu, unao uhuru wa kuchagua usalimishe maisha yako, lakini huko huru na matokeo ya uchaguzi huo. E. Stanly Jones alisema, "kama hujajisalimisha kwa Kristo, utajisalimisha kwa machafuko." Kijisalimisha si njia bora ya kuishi; ni njia pekee ya kuishi. Hakuna kitu kingine cha kukufanikisha. Njia nyingine zote hukuongoza kwenye kukutatisha tamaa, na kuziangamiza nafsi. Tafsiri ya King James huita kujisalimisha "huduma yenu yenye maana," Rum 12:1. Tafsiri nyingine inasema, "njia yenye maana zaidi ya kumtumikia." Rum 12:1.

Kusalimisha maisha yako si hisia za kipumbavu kama wengu watuonavyo leo sisi Watawa,  bali ni tendo la akili na busara ambalo unaweza kulifanya kwa ajili ya maisha yako. Ndiyo maana Mtume Paulo anasema, "kwa hiyo tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi kumpendeza yeye," 2Kor 5:9. Nyakati zako za busara zitakuwa zile ambazo unasema ndiyo kwa Mungu.

Wakati mwingine huchukua miaka, lakini hatimaye unagundua kwamba kizuizi kikubwa kwa Baraka za Mungu maishani mwako sio watu wengine, ni wewe mwenyewe-matakwa yako binafsi, kiburi cha hali ya juu, na matarajio yako. Huwezi kutimiza lengo la Mungu kwa maisha yako huku ukikazania malengo yako binafsi.

Kama ataenda kufanya kazi ndani yako, itaanza hivyo. Kwa hiyo mpe yote Mungu: kushindwa kwako hapo nyuma, matatizo yako ya sasa, matarajio yako ya mbele hofu zako, ndoto, udhaifu, tabia, maumivu, na madhara yoyote uliyo nayo. Mtawa mwenzangu, nawe mwenye hofu ya Mungu, mweke Yesu katika kiti cha dereva wa maisha yako na uondoe mikono yako toka kwenye usukani. Usiogope; hakuna chochote katika uongozi wake kinaweza kupoteza dira. Chini ya uongozi wa Kristo unaweza kudumu chochote. Utakuwa na Mtume Paulo, "Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu," Flp 4:13

Wapendwa wana wa Mungu, kujisalimisha kwa Paulo kulitokea katika njia ya Dameski alipoangushwa chini na mwanga mkali uliompofusha. Kwa watu wengine, Mungu anapata mwitikio wetu bila kutumia njia ya ajabu sana. Pamoja na hayo kujisalimisha siyo tukio la wakati mmoja tu. Kuna wakati wa kujisalimisha, na kuna tendo la kujisalimisha, ambalo ni la muda-hadi-muda na maisha yote. Tatizo la sadaka iliyo hai ni kwamba inaweza kutambaa na kutoka madhabahuni, hivyo unaweza kutakiwa kujisalimisha hata mara hamsini kwa siku. Ni lazima ufanye jambo hili kuwa tabia yako ya kila siku. Yesu anasema, "mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate," Lk 9:23

Ngoja nikuonye: unapoamua kuishi maisha ya kujisalimisha kikamilifu, uamuzi huo utapimwa. Wakati mwingine itamaanisha kufanya mambo yasiyostahili, ya gharama, au yanayoonekana hayawezekani. Mara nyingi itamaanisha kufanya kinyume cha unavyojisikia kufanya. Mmoja ya viongozi wakuu wa Kikristo wa karne ya ishirini alikuwa Bill Bright, mwanzilishi wa Campus Crusade for Christ. Kwa kutumia watumishi wa shirika hili duniani pote, kipeperushi cha sheria nne za kiroho, na filamu ya Yesu (iliyoonwa na watu zaidi ya bilioni nne), zaidi ya watu milioni 150 wamekuja kwa Yesu.

Siku moja mtu mmoja alimuuliza Bill, "Kwa nini Mungu anakutumia na kukubariki maisha yako kiasi kikubwa hivyo? Alisema, "Nilipokuwa kijana mdogo, nilifanya mkataba na Mungu. Niliandika na kutia sahihi ya jina langu chini yake. Mkataba huo ulisema. 'Tangu siku hii ya leo na kuendelea, mimi ni mtumwa wa Kristo.'"

Je, umewahi kusaini mkataba kama huo na Mungu?  Au bado unabishana na kupambana na Mungu juu ya haki yake kufanya lolote apendalo kwa maisha yako? Ndugu na Mtawa mwenzangu, sasa ni wakati wako kujisalimisha-kwa neema ya Mungu, upendo na hekima yake. Huyu Yesu si hadithi, mwambie!

Tumsifu Yesu Kristo!

“Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo katika Kristo Yesu,” 2Tim 2:1

Tusali:-Ee Yesu Mwema, kwako ipo furaha ya kweli. Nijalie furaha hiyo katika maisha yangu. Amina

lunes, 30 de enero de 2017

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 4 YA MWAKA-I


JUMATANO WIKI YA 4 YA MWAKA-I

Somo: Ebr 12:4-7, 11-15

Zab: 103:1-2, 13-14, 17-18a.

Injili: Mk 6:1-6

Nukuu:

“Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye?” Ebr 12:7

Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani,” Ebr 12:11

“mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe,” Ebr 12:13

“Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo,” Ebr 12:14-15

Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake,” Mk 6:3.

Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake,” Mk 6:4

TAFAKARI: “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Yesu anatukumbusha wajibu muhimu sana, yaani, tuviheshimu na kuvienzi vilivyo vyetu. Pamoja na hayo yote, hukumu yetu iwe ya kweli na haki. Waswahili wanasema, “masikini mnyongeni, ila haki yake mpeni.” Ni wazi watu wa nyumbani mwake waliyastaajabia yale aliyoyatenda Yesu lakini hawakuutafakari Umungu wake, bali waliutazama zaidi ubinadamu wake tena katika mwono wa historia yake. Nao wanashangaa na kusema, “Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake,” Mk 6:3. Hivyo leo ni wito kwetu kwamba tusimdharau mtu kwa vile tunaifahamu historia yake na asili yake, bali tumtazama katika upya wake.

Ni jambo la kushangaza leo kuona katika jamii yetu Tanzania baadhi yetu kuwaweka watu fulani, au makabila fulani, na hata ukanda fulani wa nchi walipotoka kama watu wasio na maana na kutokuwa na jema lolote. Bila shaka ubaguzi huu unakusudi lake kimkakati. Hata hivyo mikakati yote miovu ni chukizo kwa Mungu. Kuhusu hatari hii, Yesu anasema, “Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake,” Mk 6:4. Kutokuheshimka na kupokeleka kwetu hakutoki nje ya jamii tunayoishi. Mchawi ni sisi wenyewe. Dhambi hii ya kubaguana kunakotokana na familia zetu, koo zetu, makabila yetu, na elimu zetu ni mbaya na yakuogopwa sana. Machafuko mengi ya kijamii na hata kufikia hatua ya mauaji ya kimbari huanza na chokochoko hizi. Hakuna binadamu aliye na thamani zaidi ya binadamu mwingine. Wewe ni nani na una ubora gani zaidi hata umdharau mwenzako kutokana na familia yake, ukoo wake, au kabila lake? Tuelewe kwamba mengine yote hapa duniani ni MBWEMBWE TU!

Tukubali wakati mwingine tunafanya vibaya sana hata kama jambo hilo linatumika kama utani. Utani upo kwa watani, na siyo kwa kila anayejisikia kufanya hivyo. Tuwahesimu watu na utu wao. Tofauti zao ndio uzuri wa Mungu. Hatukuumbwa ili wote tufanane kwa kila kitu. Ikiwa hivyo basi sisi si watu tena bali mitambo-“robots.” Tumuombe Roho Mtakatifu akaye nasi ili tuweze kuyaona matakatifu kwa wale wote tunaoishi nao na wanaotuzunguka.Yote yasiyoongozwa na Roho wa Bwana yanamadhara sana katika maisha yetu. Mungu hatosita kutufundisha kwa njia nyingine ili tumrudie. Na hii ndiyo kazi ya mwalimu yeyote yule au mlezi ye yote yule anayejitambua.

Ndugu yangu, kushindwa kwa mwanafunzi kwa maana nyingine kwa weza dhihirisha kushindwa kwa mwalimu. Kufaulu mtihani wa maisha kwa tegemea sana maisha yanayoongozwa na malengo. Na kufikia lengo lolote lile katika maisha kunaitaji “nidhamu” kama kiungo muhimu sana. Licha ya nidhamu kukuweka katika mstari sahihi kuelekea pale unapopataka, nidhamu hiyo hiyo ukuwajibisha pia pale unaporegea. Na nidhamu hii ndiyo aizungumziayo Yesu na kusema, Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze,” Lk 13:24. Hivyo hakuna yeyote kati yetu asiyependa mafanikio mazuri katika maisha. Hata hivyo kuyapata na kuyafikia mafanikio hayo mazuri kutakuitaji “nidhamu na maadili” kwa kile ukichuchumiliacho. 

Nidhamu na maadili ndicho kiongoza njia cha kufika pale unapopatamani. Nidhamu na maadili mema katika maisha hutustahimilisha hata pale tunapokata tamaa na kukosa mwelekeo kama tokeo la sintofahamu katika maisha. “Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye?” Ebr 12:7. Nidhamu na maadili mema hukupa maana na ufahamu wa maisha unayoyaishi leo kama tokeo la jana, na kesho kama tokeo la leo. Kwa mantiki hii ya nidhamu na maadili katika maisha, “Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani,” Ebr 12:11.

Maisha yenye nidhamu na maadili mema humjenga mtu mwili na roho. Kumbe si vyema sana kujionea huruma na kulalama kwa mambo ambayo yapo chini ya uwezo wako kubadilika na kusonga mbele katika furaha ya kweli. “Kwa hiyo inyosheni mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza, mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe,” Ebr 12:12-13. Ndugu yangu, licha ya kwamba baadhi ya vidonge vya malaria ni vichungu, twawajibika kuvimeza kwa sababu tunataka kupona. Na pona ya ye yote yule mwenye hofu ya Mungu ni hii: Kutafuta “kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo,” Ebr 12:14-15. Ndugu yangu, bila utakatifu hutoweza muona Mungu kwa sababu Yeye ni Mtakatifu.

Tumsifu Yesu Kristo

“Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu; Sujuduni mkiukabili mlima wake mtakatifu; Maana Bwana, Mungu wetu, ndiye Mtakatifu,” Zab 99:9

Tusali:-Ee Bwana Yesu, tujalie amani na watu wote. Amina

domingo, 29 de enero de 2017

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 4 YA MWAKA-I


JUMANNE WIKI YA 4 YA MWAKA-I

Somo: Ebr 12:1-4

Zab: 22:25b-27, 28, 30, 31-32

Injili: Mk 5:21-43

Nukuu:

“tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu,” Ebr 12:2.

“Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu,” Ebr 12:3.

Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule,” Mk 5:25-29

 “Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena,” Mk 5:34.

“Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu?”

Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa sinagogi, Usiogope, amini tu,” Mk 5:35.

TAFAKARI: “Usiogope, amini tu.”

Wapendwa wana wa Mungu, neno “usiogope” lipo mara 366 katika Biblia Takatifu. Hii ina maana Mungu anatuambia kila siku “usiogope”. Unapokuwa na hofu ya kitu chochote, basi kitu hicho ndicho chenye uwezo wa kuamua hatima yako. Kwa watu wa Mungu tunatakiwa tuelekeze hofu yetu kwa Mungu tu na si kwingineko kwani tutakapoielekeza kwa Mungu yeye ni mwaminifu na atatuelekeza kufanya ya Mbinguni.

Maandiko Matakatifu, Biblia, inatuambia haya kuhusu HOFU:- “Bwana wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu,”Isa 8:13. “Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi. Lakini nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo,”Lk 12:4-5. “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili,” Ufu 21:8.

Hofu haileti madhara ya kiroho tu bali hata ya kimwili. Huleta mshituko na penye hofu pana wasiwasi, palipo na haya huleta magonjwa ya “Organic” {sehemu za mwili zifanyazo kazi maalumu} na hitilafu katika shehemu hizi husababisha vidonda vya tumbo {ulcers}, shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya ini, upungufu wa damu mwilini, n.k

Kadiri ya Maandiko Matakatifu haya ni baadhi ya magonjwa yanayosababishwa na hofu: “Kwa sababu hiyo viuno vyangu vimejaa maumivu, utungu umenishika, kama utungu wa mwanamke azaaye; ninaumwa sana, nisiweze kusikia; nimefadhaishwa wa hofu, nisiweze kuona. Moyo wangu unapiga-piga, utisho umenitaabisha, gizagiza la jioni nilipendalo limegeuka likanitetemesha,” Isa 21:3-4

Leo Yesu anakuambia wewe na mimi “usiogope, amini tu.” Yawezekana shida, mahangaiko, na hata ugonjwa ulio nao umekuwa tishio kwako kiasi kwamba umefikia mahali na kukosa mwelekeo. Hata kama kuna hali ya umauti, Yesu anakuambia, “usiogope, amini tu.” Injili ya leo tunaona Yesu anaponya na kurudisha uzima kwa watu wawili kwa nyakati tofauti.  Msingi wa ponyaji zote hizi mbili, yaani mwanamke yule aliyekuwa anatokwa damu kwa muda wa miaka 12, na binti yule wa Yairo mmoja wa wakuu wa sinagogi, ni kukubali uwepo wa Kristo na kuwa na Imani thabiti.

Kama kweli wewe U mfuasi wa Kristo huna sababu ya kuwa na hofu na mashaka juu yake hata kama Dada mauti yu pembeni yako. Usiogope, amini tu. Kuhusu Imani, Yesu anatusihi; “Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu,” Mt 17:20b. Mwanamke yule mwenye kutoka damu kwa muda wa miaka 12 anachukua ujasiri na kuishinda hofu na kulishika vazi la Yesu. Naye anapata uponyaji. “Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia habari za Yesu, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule,” Mk 5:25-29. Hakuna kitu kibaya kama hofu. Wengi hufa bila hata kudhuriwa kwa sababu ya hofu.

Kwa tendo hili Yesu anagundua nguvu kumtoka mwilini mwake, hivyo anawauliza wanafunzi wake ni nani aliyemshika? Kwa upande wa wanafunzi wake Yesu swali hili linaonekana halina maana kwa sababu Yesu alikuwa amesongwa pande zote na watu. Yesu kuuliza kwake huku si kupoteza muda, bali kumpa hakikisho la kweli la huruma ya Mungu mwanamke yule. Hivyo baada ya kuangalia huku na huku, mwanamke yule akiwa na hofu anajisalimisha kwa Mfalme wa Amani, Yesu Kristo. “Na yule mwanamke akaingiwa na hofu na kutetemeka, akijua lililompata, akaja akamwangukia, akamweleza kweli yote,” Mk 5:33. Kujisalimisha huku kunamrudishia Amani, Furaha, na Nguvu. Naye Yesu anamwakikishia hayo na kumwambia, “Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena,” Mk 5:34. Msiba wake wa miaka kumi na mbili umeondolewa leo. Ndugu yangu unayesafiri nami, bila shaka nawe unamsiba wako unaokusumbua. Kristo ndiye njia, kweli, na uzima, Yoh 14:6. Yawezekana kote ulipopita kutafuta njia umezidi kupotea. Yawezekana kote ulipotafuta kweli kuhusu tatizo lako umegonga mwamba. Na yawezekana pia uzima unaoupigania ndio unazidi kudhoofu na kunyauka. Kristo ndiye jibu halisi la hayo matatu: njia ya kweli, kweli halisi, na uzima thabiti.

Baada ya kulitenda jambo hilo kuu, Yesu anaelekea kwa binti yule wa Yeiro. Alipokaribia tu nyumbani kwa Yairo, Yesu anapokelewa na habari ya huzuni. “Hata alipokuwa katika kunena, wakaja watu kutoka kwa yule mkuu wa sinagogi, wakisema, Binti yako amekwisha kufa; kwani kuzidi kumsumbua mwalimu?” Kristo Yesu akiwa ndiye uzima, anamwondolea hofu na mashaka Yairo na kusema, “Usiogope, amini tu,” Mk 5:35. Maneno haya ni mazito sana licha ya uchache wake. Je, unayaamini? Yesu anaenda mbali zaidi pale tunapomwamini angali tukiwa katika sintofahamu zetu. Yesu anaingia ndani na wanafunzi wake wale watatu tu [Petro, na Yakobo, na Yohana] na kusema, “Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu,” Mk 5:39.

Wapendwa wana wa Mungu, unapokutana na Yesu katika mahangaiko yako na kubaki naye katika imani thabiti, tatizo hilo ni sawa na kupita tu. Ni usingizi wa muda mfupi na utaamka katika utu mpya ndani na katika Kristo. Maneno haya ya Yesu yanaonekana kama kejeri kwa wale wasiokuwa na Imani. “Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana,” Mk 5:40.

Ukweli ni kwamba ufahamu wako kuhusu maisha na yote yanayokuzunguka ni mdogo sana ukilinganisha na yale Mungu ayajuaye kuhusu maisha yako na mazingira yanayokuzunguka. Ufahamu wa yote yaliyojificha U na Mungu. “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3. Huyu ndiye Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili akakaa kwetu, Yoh 1:14. Yesu ndiye Uzima wa kweli, na hili analifanya na kudhihirisha nguvu na mamlaka yake. “Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka,” Mk 5:41. Ndugu yangu, ‘usiogope, amini tu.’

Mahangaiko yako hayana umilele. Hilo silo kusudio la kuumbwa wako. Umeumbwa ili uishi milele. Yule Kijana “Mara akasimama, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu,” Mk 5:42. Ndugu yangu, mwanamke yule aliteseka kwa miaka 12, na kijana huyu anarudishiwa uhai wake akiwa na umri wa miaka 12. Wafuasi wa Yesu walikuwa 12 katika huduma yao, na walikusanya makapu 12 ya masalia ya vipande vya mkate na samaki. Na Maandiko Matakatifu yanatuambia pia kulikuwa na makabila 12 ya Wayahudi. Ujumbe tunaopata hapa ni kwamba namba 12 ni UKAMILIFU, ILIYOTOSHA, na YAKUTOSHA. Ukamilifu huu ni pale Mungu anaposema basi inatosha juu ya mahangaiko ya mateso yako na yangu. Tosha yake kwetu ni Amani ya kweli, Furaha ya kweli, na Nguvu. Basi hatuna sababu yoyote ya kufurahia uovu, au kuwa na hofu juu ya kitu chochote kile ila hofu ya Mungu tu.

Wapendwa wana wa Mungu, Waswahili husema ‘ukiona vinaelea ujue vimeundwa.’ Chochote kile kionekanacho na kupendeza machoni petu kina historia yake. Na historia kama mang’amuzi yenye kugusa hisia na maisha ya watu husika, ndiyo msingi wa kile wakiheshimucho na kukitukuza. Ni kwa maana hii hatuwezi kulitazama Kanisa leo katika uimara wake, ueneaji wake,  uinjilishaji wake, na kushamiri kwake, bila kutambua sadaka kubwa aliyoitoa Yesu Kristo pale Msalabani, na wote waliomfuata wakiwemo Mitume wake, na wafiadini Watakatifu waliomwaga damu zao kwa ajili ya imani ya kweli, na katika kweli na haki. Na ndiyo maana, “tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu,” Ebr 12:2. Hili ndilo tumaini letu KUU kama wafuasi wake.

Kutokana na ubinafsi na umimi uliokithiri miongoni mwetu na kutufanya sanamu za kuabudiwa, ulimwengu leo siyo sehemu salama pa kuishi. Kila kukicha imekuwa mchezo wa karata wa kupata na kupoteza. Lakini swali kubwa hapa ni hili; ‘tunapata kwa ajili ya nini na nani, na tunapoteza kwa ajili ya nini na nani? Ni kweli iliyo wazi kwamba, kama mimi na wewe leo tutakuwa tayari kuishi Ukristo wetu na kumfanya Kristo aonekane kwa wengine hasa wanyonge, utawala huo wa kweli na haki utaingia vitani na utawala wa ubinafsi na umimi wenye kuabudiwa na kutukuzwa. Jambo la kusikitisha ni kwamba, utawala huu wa kweli na haki hauna Jeshi wala mahakama kama ulivyo utawala ule wa ubinafsi na umimi. Silaha kubwa ya utawala huu wa haki na kweli ni UPENDO.

Na sababu ya silaha hii ni hizi mbili: Moja, ni juu ya lile lililo kuu, “Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo,” 1Kor 13:13. Na la pili ni kuhusu uzito wa sadaka ambayo mtu aweza kuitoa kwa ajili ya wengine. Kristo ndiye kielelezo chetu katika hili; Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Hakuna tutakachopoteza kwa kufanya tendo hili kwa sababu aliyetuweka huru leo na kupata mastahili ya kuwa wana wa Mungu na warithi wa ufalme wa Mungu, ndiye Kristo aliyeushinda uovu kwa kifo kile cha Msalaba. “Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu,” Ebr 12:3. Na kwa upande wetu katika vita hii dhidi ya uovu, ‘hatujafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi,’ Ebr 12:4. Na kama wafuasi wa Kristo tu askari wa mwanga dhidi ya giza ambalo ndilo uovu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Enenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena,” Mk 5:34.

Tusali:-Ee Yesu Mwema, twakiri ndani ya mioyo yetu kwamba hakuna lisilowezekana kwako na kwa Mungu Baba. Tujalie imani ya kweli katika ukiri huu. Amina

 

sábado, 28 de enero de 2017

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 4 YA MWAKA-I


JUMATATU WIKI YA 4 YA MWAKA-I

Somo: Ebr 11:32.40

Zab: 31:20,21, 22, 23, 24

Injili: Mk 5:1-20

Nukuu:

“Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii; kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga,” Ebr 11:32b-34a

“Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni,” Ebr 11:34b

“wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya,” Ebr 11:36-37

“Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi; kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi,” Ebr 11:39-40.

akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese,” Mk 5:7 

Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini,” Mk 5:13 

TAFAKARI: “Kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu.”               

Wapendwa wana wa Mungu, hakuna kati yetu asiye na jambo lolote la kumshukuru Mungu hata kama tumesongwa na dhiki ya kupindukia. Kushukuru kwa jambo lolote lile ni kuomba tena. Ni mara ngapi sala zetu zimekuwa na muono wa kushukuru? Yawezekana sehemu kubwa ya maisha yako wajiliwa na maumivu makubwa sana pale unaposimama katika kweli na haki. Hata katika mazingira hayo magumu hakuna sababu ya kukata tamaa, wala kumlaumu Mungu zaidi ya kuomba uelewa wa teso hilo kwa mwelekeo huu: “Ee Bwana na Mungu wangu, katika teso hili wataka kunifundisha nini?” Ndugu yangu wewe si wa kwanza katika teso hilo, na wala hautakuwa wa mwisho katika teso hilo.

Ikiwa vyote katika ulimwengu huu vinaelekea katika ukamilifu wake, wewe na mimi tuwe tayari kukabiliana na uovu, na kuushinda kwa kutenda mema. Hatua hii yahitaji imani thabiti katika ufahamu, na umaana wake. ‘Gideoni, Baraka, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samweli na manabii; kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga,” Ebr 11:32b-34a. Kwenye nguvu-ovu, ovu uhalalishwa na kuwa kweli gushiwa, na watu wakaaminishwa hiyo ndiyo kweli.

Hali na mazingira kama haya udhohofisha juhudi za kuitafuta kweli, na giza utanda katika mioyo ya wapigania kweli na haki. Hata hivyo salama yetu ni kutolipoteza tumaini la kweli, na kusimama imara katika imani ya kweli. Neno la Mungu linatuambia kwamba, akina Gidion, Daudi, Samweli na manabii “walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni,” Ebr 11:34b. Je, leo hatuona mfanano wa matendo haya ya kiovu katika jamii yetu?

Ndugu yangu, ukweli ni kwamba, safari ya kuelekea nuru ya kweli ina gharama zake. Aliyeishikilia keki kwa ajili ya wengi, na tena kwa dhuluma, hatokuwa tayari kuiacha ikichukuliwa mikononi kwake kwa ulaini. Kuichukuwa keki hii mikononi kwa dhalimu yakupasa kwanza kujipima nguvu zako, Lk 14:31. Pili, wahitaji kusimama imara bila kulipoteza lengo kwa kuitaka amani na kujiepusha na uovu wa dhalimu wako, Lk 14:32. Na huu ndio mfano wa wale walioteswa bila kupoteza lengo, na waitaka amani bila kujihushisha na uovu, yaani, kulipiza kisasi. “Wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya,” Ebr 11:36-37. Na licha ya sintofahumu zote hizo walizofanyiwa, “watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi; kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi,” Ebr 11:39-40.

Injili ya leo imebeba dhamiri ile ile ila kwa mtindo mwingine wa sintofahamu iletayo teso katika maisha. Hapa tunakutana na uponyaji wa mtu aliyeteswa na kundi kubwa la pepo. Hata walipoulizwa mpo wangapi haikuwa rahisi tutoa jibu la haraka. Badala yake walijibu, ‘Legioni, kwa kuwa walikuwa wengi.’ Uwepo wa Yesu ni vita dhidi ya uovu. Ni vita vya mwanga dhidi ya giza. Jina la Yesu linatisha. Jina hili ni tishio dhidi ya Shetani na mamlaka yake. Ni kwa sababu hiyo, mtu yule alipomwona Yesu, “akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese,” Mk 5:7. Pepo wachafu wanatambua nguvu na mamlaka aliyokuwa nayo Yesu, na wanajua vita dhiki yake hawatashinda. Je, unaliamini jina hili Tukufu na Kuu kuliko Majina Yote?

Na hali ilivyozidi kuwa mbaya, pepo wale waliomba na kujisalimisha chini ya Mamlaka ya jina hili kuu, kwa kuwaingia nguruwe. “Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini,” Mk 5:13. Ukiangalia tendo hili alilofanya Yesu kiuchumi kwa kuwaruhusu wale pepo kuwaingia wale nguruwe waweza kutafsiri kwamba Yesu hakutenda haki kwa mfugaji wa wale nguruwe. Ndugu yangu, viumbe vyote ni mali ya Mungu, na Yeye Mungu anamamlaka yote juu ya viumbe vyake vyote, Zab 24:1. Na maandiko Matakatifu yanatuambia, Neno huyu alifanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14, “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,”Yoh 1:2. Hivyo Yesu alikuwa na mamlaka yote na uamuzi wake ulikuwa sahihi.

Kwa upande mwingine, tendo hili la Yesu linathibitisha upekee na thamani ya mwanadamu kati ya viumbe vyote. Na sababu kubwa ni kwamba Mungu alipenda na kuchagua kumuumba mtu kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Kiumbe huyu, yaani, mwanadamu, imebeba chapa ya Mungu ndani yake. Binadamu anastahili heshima kubwa licha ya tofauti za kibinadamu tunazojiwekea, na zinazotokana na utofauti wa kimaisha, na kwa makusudi kabisa tunaruhusu zitugawe kimatabaka. Pamoja na upekee huu aliokuwa nao Mwanadamu, kamwe Mwanadamu huyu hawezi kumshurutisha Mungu atende kadiri atakavyo yeye. Kwani “Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake,” 1Sam 2:6-8. Kumbe kila alitendalo Bwana lina sababu yake katika umilele wake.

Kama tendo la shukrani, mtu yule aliyewekwa huru na Yesu kutoka mamlaka ya shetani, anaomba kuandamana ya Yesu. “Lakini Yesu hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu,” Mk 5:19. Ndugu yangu, unapotambua mkono wa Mungu katika maisha yako, anza hapo hapo kutoa ushuhuda huo na kulisifu jina la Bwana. Mtakatifu Fransisko wa Assis wakati fulani alisema, ‘hakuna sababu ya kwenda sehemu fulani na kuhubiri, ila tuhubiri kadiri tutembeavyo.’ Kwa upande mwingine, katazo hili ya Yesu kwa mtu huyu asiandamane naye linalenga kukoleza Imani ya kweli sehemu ile Mungu aliyokutendea makuu yake. Hivyo mtu yule “akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu,” Mk 5:20. Ndugu yangu, wewe na mimi tunayo mengi ya kutoa shukrani kwa Mungu. Basi anza hapo ulipo.

Tumsifu Yesu Kristo!

Ee Bwana, Mungu wangu, uangalie, uniitikie; Uyatie nuru macho yangu, Nisije nikalala usingizi wa mauti,” Zab 13:3

Tusali:-Ee Bwana Yesu, usiniache, na wala usijitenge nami. Fanya hima kunisaidia. Amina

 

viernes, 27 de enero de 2017

TAFAKARI: JUMAPILI YA 4 YA MWAKA-A


JUMAPILI YA 4 YA MWAKA-A

Somo I: Sef 2:3; 3:12-13

Zab: 146: 6-7, 8-9, 9-10 Mt 5:3

Somo II: 1Kor 1:26-31

Injili: Mt 5:1-12a

Nukuu

“Mtafuteni Bwana, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi mliozitenda hukumu zake; itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu; huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya Bwana,” Sef 2:3

Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu,” Sef 3:11 

Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la Bwana,” Sef 3:12

“Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya,” Sef 3:13

Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa,” 1Kor 1:26

“Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi,” 1Kor 1:30

Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni,” Mt 5:11-12

TAFAKARI: Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni.”

Wapendwa wana wa Mungu, sehemu kubwa ya maisha ya mwanadamu hapa duniani ni kutafuta maana ya maisha yake, na kuipata ile furaha ya kweli. Binadamu huyu ulifanya jambo hili anapoitazama historia yake kama somo kwa lengo ya kuyarekebisha yale ambayo hayakwenda vyema kwa wakati huu aishipo sasa, ili kule aendapo asipokujua vizuri kuwe na tumaini. Hivyo, somo la Injili ya leo kwa upana wake linaelezea hali halisi katika mahangaiko ya mwanadamu, na ulimwengu huu tunaoishi. Na kwa kulisema hilo, Yesu leo anatutaka tuzitafakari kwa kina heri hizo alizozisema, Mt 5:3-12.

Lakini ili tuifikie furaha ile ya kweli ambayo hiyo ndiyo lengo halisi, hatuna budi kuufahamu ulimwengu huu tunaoishi leo. Bila kuujua ulimwengu huu ambapo ndipo tunapoishi, ni vigumu pia kuiona furaha ile ya kweli inayoendana na malengo ya kuumbwa kwetu. Mimi na wewe tumeumbwa ili tuishi milele. Kwa ufupi na kwa kina, Yesu anatupa siri ya hali halisi ya ulimwengu huu tunaoishi leo. Naye anasema, “Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha,” Yoh 16:20. Pamoja na mazingira kama haya, na tunaposimama kwa lile lililo kweli na haki, Kristo hatotuacha kamwe. Ni kwa sababu hiyo Yesu aliyatoa maisha yake, ili mimi na wewe leo tuwe huru kutoka utumwa wa dhambi na uovu wake wote. “Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22. Hivyo tuitafutapo furaha hiyo ya kweli hatuna budu kujua hali ya ulimwengu wetu tunaoishi kama alivyotufunulia Bwana wetu Yesu Kristo. Je, tunafanye nini sasa?

Jambo la kufanya ni kuziishi heri alizotuambia Bwana wetu Yesu Kristo katika Injili ya leo. Katika tafakari hii sintozipitia heri hizo moja baada ya nyingine, bali niwatake tutafakari heri hizo kwa kuyatazama mambo makuu manne ambayo kwa kiasi fulani yanasema juu ya maisha yetu ya leo. Mambo hayo ni kama yafuatayo: Kwanza, kuwa na nafasi ndani ya moyo wako. Pili, hapo ulipo fanya zaidi na achana na mazoea. Tatu, hapo ulipo kuwa mzalendo kwa kujipokea, kuwapokea wengine, na kuipigania jamii yako-Taifa lako. Na nne, kuwa alama na kielelezo hai cha amani ya kweli hapo ulipo.

Wapendwa wana wa Mungu, tuanze na hili la ‘kuwa na nafasi ndani ya moyo wako.’ Huwezi kuwa na furaha ya kweli kama hakuna nafasi ya Mungu ndani ya maisha yako. Hofu ya Mungu ndani yetu ni mizania ya kujipokea kama tulivyo, na kutufanya tujitahidi kufika pale ambapo tunapatamani. Itakuaje basi kufanya hivyo kama huna nafasi ya Mungu ndani yako? Kuwa na nafasi ndani ya moyo wako, Yesu ameizungumzia katika Injili ya leo kwa mtindo huu, “Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao,” Mt 5:3. Ni umaskini huu wa roho, yaani, kuwa na nafasi ya Mungu ndani yako, kutakao kupeleka katika furaha ile ya kweli, yaani, ufalme ule wa Mbinguni baada ya kuvishinda vita hivi hapa duniani. Haya ndiyo maisha yale ya umilele kama lengo halisi la kuumbwa kwetu, yaani, tumeumbwa tuishi milele.

Pili, ‘fanya zaidi na achana na mazoea.’ Hakuna saratani mbaya katika maisha ya mtindo wowote ule, pale unapofikia hatua ya kuridhika na kila kitu, na kuacha mambo yaende tu kama yalivyo, kwa vigezo kwamba kama juzi na jana ilikuwa hivyo, basi hata leo na kesho itakuwa hivyo hivyo. Mwenendo huu wa maisha ni mwendo wa ‘kufa pole pole’ huku ukiona. Kumbe kuishi maisha yenye malengo ni kufanya zaidi ukijua siyo kwa sababu ya ubinafsi wako, bali kwa ajili ya wengine kwa sasa na hata vizazi vijavyo. Mtume Paulo anatufafanulia vizuri kuhusu kweli hii na kusema, “Mtu asitafute faida yake mwenyewe, bali ya mwenzake,” 1Kor 10:24. Na tutakuwa tunafanya hivyo siyo kwa kuutafuta utukufu binafsi, bali kuifikia tumaini lile ambalo kila mmoja wetu bila kujali historia yake, itikadi zake, familia au kabila, anatamani kuipata. Kwa Mkristo na mfuasi wa Kristo aliye hai hufanya hivyo akijua ukweli huu kwamba, “hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana,” Rum 14:7-8. Hivyo ndugu yangu, kulifikia tumaini hili yakupasa wewe na mimi kuwa na njaa ya tumaini hilo. Ni katika mazingira haya Yesu anasema, “Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa,” Mt 5:6. Je, hali ipo vipi hapo ulipo? Jamii inayokuzunguka inatenda haki nawe ukiwa mmoja wapo? Kama hilo halipo itakuwaje basi uwe na furaha ya kweli? Changamoto hii ni yangu na yako pia. Tuwe na njaa na kiu ya haki. La sivyo hatutaweza kushibishwa, yaani kuwa na furaha ya kweli.

Tatu, hapo ulipo ‘kuwa mzalendo’ kwa kujipokea, kuwapokea wengine, na kuipigania jamii yako-Taifa lako. Ndugu yangu, mizania ya haki na kweli, ipo ndani ya usafi wa moyo wa mtu. Kuna msemo wa kifalsafa usemao kwamba, “mtu hutoa kile alichokuwa nacho.” Hivyo huwezi kutoa kile usichokuwa nacho. Lakini naweza kuifikia mizania hii ya usafi wa moyo kwa kufanya hatua hii muhimu sana katika maisha yangu, yaani, kujipokea kama nilivyo. Hapa simaanishi tu kuyaona mazuri yako na mabaya yako ukaridhika nayo na kutokufanya chochote. Wito wa kila mmoja wetu ni kuwa wakamilifu kama Baba yetu wa Mbinguni alivyo makamilifu, Mt 5:48. Kama hili ndilo lengo msingi la maisha na malengo yangu, sinabudi kuurekebisha udhaifu wangu ili kuufikia usafi ule wa moyo kila siku ya maisha yangu. Hii siyo kazi ya siku moja.

Jambo hili, yaani, ‘kujipokea’ likichukua mkondo wake sawa sawa, mengine hufuata, yaani, kuwapokea wengine, na kuwa tayari kwa maslahi mapana ya jamii inayokuninguka, na Taifa zima. Huu ndio uzalendo tunaouzungumzia hapa, yaani, fanya yote kwa ajili ya wengine kwa kulitazama tumaini lililo mbele yako na kwa wote. Katika kweli hii, jambo hili litawezekana kama Yesu anasemavyo, “Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu,” Mt 5:8. Ni katika moyo ulio safi utofautisha namna ya kufikiri kwetu, kuamua kwetu, na kutenda kwetu. Mlolongo huu ndiyo ule unaotupatia cheo chetu halisi, yaani, utakatifu wako. Hivyo tutamwona Mungu tu tukiwa na cheo hiki, yaani, Utakatifu kwa sababu Mungu wetu ni Mtakatifu.

Na nne, ‘kuwa alama na kielelezo hai cha amani ya kweli hapo ulipo.’ Ni moyo safi huo ambao utuwezesha kuona kitu kama kilivyo, na kusema kama kilivyo, ili kibaki kama kilivyo katika hali yake daima. Tatizo kubwa hapa mara nyingi mimi na wewe huvaa miwani ya ‘tulivyo,’ na kupoteza uhalisi wa jambo au kitu kama tulivyo. Miwani hii ya ‘tulivyo,’ yaweza kuwa itikadi zetu kisiasa na kidini. Miwani hii ya ‘tulivyo inaweza kuwa pia familia zetu, koo zetu, na makabila yetu. Kwa mtindo huo, tutawezaje kuwa wapatanishi wa kweli? Ndugu yangu, tunapoambatana na mambo hayo kwa kushikamanana nayo au kung’ang’ana nayo kama yalivyo, twajisababishia upofu wa kudumu. Ni vyema mimi na wewe tukatoka katika boksi hilo na kupata mwanga halisi wa kuona vizuri ukweli wa kile tukitazamacho. Huku ndiko kuwa ‘wapatanishi’ kama asemavyo Yesu, “Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu,” Mt 5:9. Mungu yu mpatanishi wetu katika maana nzima ya Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Ni upananisho huu ambao kilele chake kilikuwa kifo cha Mwanaye Mpenzi pale msalabani, ambacho kifo hicho kilituhesabia haki kuwa wana na warithi wa ufalme wa Mungu. Hivyo leo mimi na wewe tunapokuwa wapatanishi tunamwakilisha Mungu kama watoto wake. Na huu ndio uwana wa Mungu, yaani, kuwa mpatanishi pale ulipo.

Mambo yote manne tuliyoyaona hapa juu yanahitaji sadaka. Sadaka ya kwanza ni kujikatalia nafsi yako mwenyewe ili uwe na mizania ya kweli na haki katika yale yote utakayokutana nayo kwa kufikia malengo ya mambo hayo manne. Sadaka uitoayo ina maana kwa sababu mbele kuna heri na tumaini. Kielelezo cha heri hiyo na tumaini ni Kristo mwenyewe. Mateso na majaribu lazima tutakutana nayo katika safari hii. Tunapoyaachia maisha yetu katika kiwango hiki, Kristo kamwe hawezi kutuacha katika taabu hizo. Kristo hubaki kuwa faraja kubwa kwetu katika dhiki na taabu hizo. Naye anatuambia nyakati kama hizo tuwe watu wa kufurahi kwa sababu tunamruhusu Mungu kutenda mambo katika hali yetu ya uduni na Mateso. Kwa msisitizo mkubwa Yesu anasema, “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12. Kuna furaha kubwa sana moyoni kuhukumiwa kwa sababu tu umetenda haki na kuishuhudia kweli. Haya ndiyo maisha ya ushuda hasa katika nyakati zetu hizi tunapoona na kushuhudia ubabaishaji kila kona.

Wapendwa wana wa Mungu, leo yako isisubiri kesho ili ujiandae. Kesho hiyo hujaifikia, na jana yako ilishapita bila kufanya chochote. Hivyo, “Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu,” Sef 3:11. Aliyejiandaa ndiye atakaye kuwa mikono salama ya Mungu. Kundi hili ni lile la wenye hofu ya Mungu, Masikini na walioonewa. “Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la Bwana,” Sef 3:12 

Wenye hofu ya Mungu na wanyenyekevu wa moyo, hawana woga wala hofu kwa sababu maisha yao yapo mikononi mwa Mungu. Nabii Sefania anawataja watu hawa kwa kusema, “Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya,” Sef 3:13. Hawa wanajua ni nani wanayemtumikia. Mungu huyu wa kweli na hai hatotuangusha kamwe tunapojitoa kwake bila kujibakiza. Ndugu yangu tuliye safiri wote katika tafakari hii, Hakika hakuna lisilowezekana kwa Mungu! Yote yawezekana kwa IMANI.

Ndugu yangu, kuwa na utajiri iwe wa kiroho na ule wa kushikika na wakati huo huo kubandukana nao, kutakuhitaji unyenyekevu wa hali ya juu. Na waliofanikiwa sana katika maisha ni wale waliojinyenyekeza sana katika maisha hata kama palikuwa na fursa ya wazi kufanya vinginevyo. Na wakati mwingine tunashangazwa na tabia hizi za wachache wetu kuishi maisha ya chini na ya kawaida kabisa licha ya mwamba mazingira na nafasi aliyokuwa nayo katika jamii ni kubwa na ya kuheshimika. Hapa ndipo tunapoona mkono wa Mungu ukifanya kazi pamoja na wale walio mridhia. Wakati mwingine na kwa mshangao mkubwa, Mungu huchagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu,” 1Kor 1:27.

Huyu ndiye Mungu na “tena uvichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko,” 1Kor 1:28. Na watu wa mtindo huu pamoja na mambo yote, hutambua maisha ni dhamana na hakuna cha kujivunia zaidi ya kuwa mawakili wa kweli kwa kile walichokabidiwa kadiri ya wito na nafasi zao katika jamii. Na katika hili Mtume Paulo anasema, “mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu,” 1Kor 1:29. Jambo hili linawezekana tu pale tunapokuwa tayari na kwa moyo thabiti kuishi ndani na katika Kristo Yesu. Kwake ‘yeye tumepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi,’ 1Kor 1:30. Hivyo aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana,” 1Kor 1:31. Fahari hii utuongoza kuyaona maisha yetu kuwa dhamana. Yesu Kristo anasema, "na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi." Lk 16:48. Maisha ni dhamana. Na kadiri Mungu anavyokupa zaidi, ndivyo anakutaka uwajibike zaidi.

Badala yake ni kuishi katika heri hizi nane za shetani:-

  • Heri yao wanajumuiya waliochoka sana, waliobanwa na shughuli na kukosa kukutana na wa wenzao katika shughuli za Jumuiya kila wakati. Kwa maana hao ni wafuasi wangu waaminifu.
  • Heri yao wana-parokia wanaofurahia kutambua tabia za wenzao na mapungufu ya watumishi wa Mungu. Kwa maana hao ndio vitendea kazi vyangu.
  • Heri yao waamini wanaosubiri kuambiwa kufanya kila kitu na kutegemea kupongezwa hata kama hawakufanya chochote. Hakika hao naweza kuwatumia vyema.
  • Heri waamini wanaoguswa na kukwazika kwa vitu vidogovidogo na kuacha kwenda Kanisani na kuacha kusali. Kwa maana hao ni wamisionari wangu.
  • Heri yao hao waamini wanaojitangaza au kudai kuwa wanampenda Mungu na wakati mwingine wanawachukia waamini wenzao na ndugu zao. Hakika hao ni wangu Milele.
  • Heri yao wanajumuiya watenganishi na waletao fujo na chuki. Wataitwa wana wangu.
  • Heri kwa wanafamilia wasiokuwa na muda wa kusali. Maana hao wananiombea mimi.
  • Heri yako wewe unayesoma haya na wewe unayeyasikia haya na kufikiri ni kwaajili ya wengine na siyo wewe mwenyewe. Hakika nimeshakupata tayari.

Tumsifu Yesu Kristo!

Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu,” Mt 5:11

Tusali:-Ee Yesu, furaha ya kweli ni pale ninapokufia katika kweli na haki. Nipe ujasiri ya kukijongea kifo hicho. Amina