viernes, 30 de diciembre de 2016

TAFAKARI: JANUARI 2, KIPINDI CHA NOELI


KIPINDI CHA NOELI

JANUARI 2

Somo: 1Yoh 2:22-28

Zab: 98:1, 2-3ab, 3cd-4

Injili: Yoh 1:19-28

Nukuu:

Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba na Mwana. Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia,” 1Yoh 2:22-23 

 “Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi, atakapofunuliwa, mwe na ujasiri, wala msiaibike mbele zake katika kuja kwake,” 1Yoh 2:28 

 “Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya,” Yoh 1:23

“Yohana akawajibu akisema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi,” Yoh 1:26

“Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake,” Yoh 1:27

TAFAKARI:Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele.”

Wapendwa wana wa Mungu, tumeumbwa ili tuishi milele. Hili ndilo kusudi kubwa la Mungu kutuumba. Je, mbona tunakufa? Kifo siyo mwisho wa umilele wetu, bali ni mwisho wa mwanzo mpya wa maisha ya umilele tutakapohesabiwa haki na Mungu mwenyewe. Mauti haina nguvu tena kwani ishabatilishwa na Kristo kwa kifo chake pale msalabani. “Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa,” 1Kor 15:21-22. Ni kweli tutakufa ila hatuna sababu ya kuogopa kifo hiki cha mwili. Yatupasa kuishinda hofu ya kufa tukijua kwamba, “Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti,” 1Kor 15:26.

Ni kwa maana hii kwenye misa ya wafu tunasoma utangulizi “Prefacio” ya wafu na hasa ile ya kwanza kwa maneno haya yenye matumaini kwamba, “Sisi tumepata kwake tumaini la ufufuko. Tunasikitika kwa sababu tunajua kwamba lazima tutakufa, lakini tunatulizwa kwa kuwa alituahidia uzima wa milele. Ee Bwana, uzima wa waamini wako hauondolewi ila unageuzwa tu. Nayo makao ya hapa duniani yakisha bomolewa, tunapata makao ya milele mbinguni,” Misale ya Waumini, toleo la nane, 1996, uk. 403. Uzima huu mpya baada ya anguko la wazazi wetu wa kwanza umeletwa na Kristo mwenyewe na hasa sadaka yake pale msalabani. Hivyo yatupasa kumkiri Kristo na kuishi kadiri ya mapenzi yake. Yesu anasema, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6 

Kama alivyo kiri Yohane Mpatizaji juu ya Kristo, lazima nasi tukiri kwamba Yesu ni Kristo. “Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba na Mwana. Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia,” 1Yoh 2:22-23 .Uzushi ni kumchanganya Kristo na mawazo yetu na kile tunachotaka awe. Kufanya hivyo ni kumfanya Kristo awe tokeo la taswira zetu na mfano wetu. Wakati mwingine namna hii ya kufikiri imekuwa ikifanyika katika Kanisa. Tunamfanya Mungu mdoli au sanamu bila kufungua masikio yetu kwa neno lile linalotupeleka katika fumbo lenyewe na uzima wenyewe. Yatupasa kuyasika mafundisho ya kweli toka kwa manabii waliomtangulia Kristo, Yesu Kristo mwenyewe, na mafundisho ya mitume wake walioishi ushuhuda huu wa kweli. “Ninyi basi, hilo mlilolisikia tangu mwanzo na likae ndani yenu. Ikiwa hilo mlilolisikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana, na ndani ya Baba,” 1Yoh 2:24

Hivyo namna ya pekee ya kuwa na umoja na Mungu Baba  na Mwana ni kukubali hili fumbo na kujifungua kwalo. Na kwa namna tulivyo {kuumbwa kwetu}, sisi ni wasikilizaji wa Neno na kwa kulisikiliza ndivyo tunavyobadilishwa na neno hilo. Mwisho wa siku hatutahitajika kutoa hesabu ya ufahamu wetu juu ya neno, bali uaminifu wetu juu ya neno hilo la Mungu. Roho aliye ndani yetu ndiye mwalimu wetu. Ili tuseme NDIYO kwa Kristo yatupasa kusema HAPANA kwa sisi wenyewe ikiwa ni pamoja na madai yetu binafsi ya kimasiya kama alivyosema HAPANA Yohane Mbatizaji.

Katika Injili tunaona mkanganyiko na kuibuka kwa hisia mbalimbali juu ya nani hasa Kristo-Masiha, Yohane Mbatizaji, na Eliya. Ni wazi matendo aliyokuwa anayafanya Yohane Mbatizaji yalivuta hisia labda aweza kuwa Masiha au Eliya mwingine. Hata hivyo Yohana Mbatizaji anakiri na anakanusha jambo hilo kwa kusema, “Mimi siye Kristo,” Yoh 1:20. Je, Yohane ni nani basi kama siye Kristo? “Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya,” Yoh 1:23. Yohane ni mtangulizi na mwaandaji wa yule ajaye na ategemewaye kwa kazi nzima ya ukombozi. Na hata ubatizo alioufanya Yohane Mbatizaji ulikuwa ubatizo wa toba. Ni maandalizi ya ubatizo wenyewe wa Roho Mtakatifu. Hivyo Yohane kwa unyenyekevu wake anasema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi,” Yoh 1:26. Huyo ndiye Kristo wasiyemjua Wayahudi.

Yohane Mbatizaji anajinasua katika hali yote ile ya kujikweza. Yeye siye Eliya na wala siye Masiya. Kuhusu Masiya, ambaye ndiye Kristo, anasema, “Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake,” Yoh 1:26b-27. Hivyo ndugu yangu tuliyesafiri sote katika tafakari hii, lini utajinasua katika hali yako ya kujikweza ili Kristo aongezeke ndani yako? Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua,” Yoh 3:30 

Tumsifu Yesu Kristo!

“Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi, atakapofunuliwa, mwe na ujasiri, wala msiaibike mbele zake katika kuja kwake,” 1Yoh 2:28ç

Tusali: Ee Yesu na Mkombozi wangu, mbele yako sina chochote cha kujikwezwa zaidi ya kukiri udhaifu wangu. Niongoze Katika kweli hiyo. Amina

TAFAKARI: JANUARI 1, SIKUKUU YA BIKIRA MARIA MAMA WA MUNGU


SIKUKUU YA BIKIRA MARIA MAMA WA MUNGU

JANUARI 1

Somo I: Hes 6:22-27

Zab: 67:2-3, 5, 6, 8

Somo II: Gal 4:4-7

Injili: Lk 2:16-21

Nukuu:

“Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia,” Hes 6:27

“Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,” Gal 4:4

“Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu,” Gal 4:7

Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini,” Lk 2:16

“Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake,” Lk 2:19 

Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa,” Lk 2:20 

Hata zilipotumia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba,” Lk 2:21 

TAFAKARI:Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake.”

Wapendwa wana wa Mungu, Leo ni mwaka Mpya. Tulio hai tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa yale yote aliyotujalia na hasa yale tuliyokutana nayo kwa mwaka tuliouaga, tukijua kwamba kila jambo lilikuwa na sababu yake na mapenzi ya Mungu ndani yake. Leo tunapouanza mwaka kwa namna ya pekee Mama Kanisa anaadhimisha siku hii kwa Heshima ya Mama Bikira Maria Mama wa Mungu. Kuuanza mwaka Mpya twahitaji baraka za Mungu, tukisafiri pamoja na Mama Bikira Maria Mama wa Mungu kama mfano hai wa kuiga na kufuata.

Kadiri ya somo letu la kwanza, wana wa Israeli iliwapasa kuliweka jina la Bwana juu ya mambo yote na ndivyo walivyobarikiwa. “Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia,” Hes 6:27. Wana wa Israeli walilishika na kulibeba jina la Mungu kama ilivyo uhusiano kati ya mke na mume. Jina hili la Bwana liliathiri kwa kiasi kikubwa mafanikio yao, wakati mwingine ilikuwa balaa walipoliasi jina hili. Hivyo hatima ya maisha yao ilitegemea namna walivyolichukulia jina hili la Mungu aliye hai. Ndivyo hivyo basi wakati wana wa Israeli walipokuwa uhamishoni na katika unyonge wao, jina la Mungu lilinajisiwa katika mataifa, Eze 36.

Ni kwa namna hiyo hiyo tunaona kwamba wana wa Israeli walipowekwa huru kwa maajabu makubwa ya Mungu, jina la Mungu lilitakatifuzwa, liliinuliwa juu kabisa kutoka unyonge na kudhalilishwa, na kutakatifuzwa, Eze 36. Ni kutoka katika mtazamo huu kulitaja jina la Mungu na watu wake ni chanzo cha baraka na dhana ya ukarimu. Hivyo kuuanza mwaka na kuumaliza yatupasa kuweka vipauwa mbele muhimu na hasa kwa maisha ya kiroho.

Kipauwa mbele namba moja ni kukaa ndani ya jina la Mungu na neno lake. Huko ndiko kwenye uzima wa kweli. Kristo ni Mzabibu nasi ni matawi. “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,” Yoh 15:5. Uzima huu twaupata pia kwa kulishika neno lake; kulisoma, kulipokea, kulitafakari, kulitafiti, na kulikumbuka kusiko kikomo. “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani,” Yoh 5:24.

Kipauwa mbele namba mbili ni kulishwa na kuhuishwa kila mara kwa kupokea Masakramenti katika hali iliyo safi, hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Ndani ya Sakramenti hii ya Ekaristi Takatifu, tunakaa ndani na katika Kristo, na kupata uzima wa milele. Mwili na damu ya Kristo ni chakula na kinywaji cha kweli.  Naye Yesu anasema, “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake,” Yoh 6:54-56.

Pamoja na makuu tuyachotayo kutoka Sakramenti hii, neema na baraka zake, Mtume Paulo anatupa angalizo juu ya Mwili huu na Damu hii ya Kristo. Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana,” 1Kor 11:27. Ndugu yangu, kabla ya kuijongea meza hii ya Bwana jihoji kwanza nafsini mwako. Je, nastahili kwa hali niliyo nayo? Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe,” 1Kor 11:28.  Tusiogope macho ya watu, na wala tusipende kushiriki Sakramenti hii na Karamu hii ya Upendo kwa mazoea. 

Kipauwa mbele namba tatu tusiache kamwe kupatanishwa kwanza na Mungu kwa Sakramamenti ya Upatanisho au Kitubio. Jambo la kusikitisha leo Sakramenti hii ya Upatanishao imekuwa kama ‘kituo cha polisi.’ Walio wengi leo wanataka kuhalalisha dhambi. Sakramenti hii ya Upatanisho imewekwa rasmi na Kristo mwenyewe katika Kanisa, na wahudumu wake ni wale walioteuliwa {kuhesabiwa haki na Mama Kanisa}, kupakwa mafuta,  na kuwekwa wakfu, {Mapandre na Maaskofu} na kwa ajili hiyo huadhimisha Sakramenti hiyo. Hapa tunakutana na Huruma ya Mungu, Msamaha wa Mungu, na Kupatanishwa na Mungu. Naye Yesu anasema, “Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh 20:23. Ndugu yangu tuijongee Huruma ya Mungu, Msamaha wa Mungu, na Kupatanishwa naye {nafsi, jirani, na mazingira}. Mwaka huu tunaouanza unatudai kuishi katika ukweli huu kama kweli twautaka uzima ndani yetu.

Somo letu la pili na Injili linafafanua fumbo zima la kumwilishwa, Neno akafanyika mwili akakaa kwetu, Yoh 1:14. Na hapa ndipo tunapoona nafasi ya Mama Bikira Maria Mama wa Mungu tunaye msherehekea leo katika tendo hili zima. Tendo hili limetokea katika utimilifu wa wakati, baada ya muda mrefu wa kusubiri. “Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,” Gal 4:4. Tendo hili limebeba sehemu kuu mbili kwa wakati mmoja; kwanza linawapa watu uwana wa Mungu kwa kuwafungua kutoka sheria ya Musa. “Wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu,” Gal 4:7. 

Sehemu ya pili, kumwilishwa kwa neno kumefanyika katika hali ya kibinadamu na kwa sheria, yaani, kwa Kristo kuzaliwa na mwanamke chini ya sheria ili kumkomboa huyo mwanadamu aliye katika sheria. Sheria inamweka Kristo katika historia ya wokovu, yaani katika historia ya watu wake. Mwanamke ni kati ya watu, yaani, ndugu zake Kristo aliokuja kuwaweka huru na kuwakomboa kwa kuwafanya kama yeye, yaani, wana wa Baba. Kwa maana hiyo, “Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu,” Rum 8:15-16.

Katika hali hii ya kumwilishwa, tunaona katika Injili yetu ya leo kwamba waamini wa kwanza wa tukio hili ni wachungaji ambao wapo karibu ya Maria Mama yake Yesu  na Mtoto Yesu, walio jiachia wazi kwa Mungu. Hapa Bikira Maria ni Mama kwa utayari na NDIYO yake kwa Neno la Mungu, kwa uamini wake na ukimya ambao unamfanya kupokea fumbo hili: “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:1,14. Mapaswa na ubora wa wana wa Israeli ulikuwa ‘kusikiliza Neno la Mungu.’ Katika tendo hili, Bikira Maria ndiyo kielelezo cha ukamilifu na utimilifu wa Neno hili la kumwilishwa kwa NDIYO yake. “Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema,” Lk 1:38a. Fumbo hili ndilo linalomwinua Bikira Maria katika nafasi hii ya juu kabisa Binadamu kuwekwa. Hivyo katika shina la Daudi limetoka chipukizi ambalo ndilo tumaini na jibu la Mungu kwa watu wake.

Nafasi ya Maria katika tendo hili la utayari wake, yaani Neno kumwilishwa ni uchungu, mateso, na furaha. Yusufu mumewe katika sintofahamu hii anataka kumwacha kwa siri. “Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri,” Mt 1:19. Ndiyo ya Bikira Maria kwa Mungu inakuwa mwanzo wa aibu, ugumu wa kueleweka na mumewe, na maumivu. Hata pamoja na hali hii Bikira Maria hakuwa sababu ya kuzuia mapenzi ya Mungu yasitendeke kwa sifa na Utukufu wa Mungu na watu wake aliowaridhia. Sauti ya Mungu ilimfikia Mama Maria kupitia mwanaye Yesu Kristo aliyemzaa, Simeoni, na wachungaji. Maria aliyaweka yote haya na kuyatafakari  moyoni mwake. U Mama wa Bikira Maria na upana wa kifua chake wa kuyabeba mambo makuu na mazito haukuishia pale horini tu, bali aliendelea kuubeba U Mama huo wa Mungu na hali hiyo hadi Msalabani. Hapa ndipo aliposhuhudia kifo katili dhidi ya mwanaye mpenzi ambaye hakuwa na kosa lolote zaidi ya wema aliyotutendea.

Hakika Mama Bikira Maria aliyastahimili na kuyashiriki kikamilifu mateso ya mwanaye Yesu Kristo. “Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene,” Yoh 19:25. Pamoja na huzuni na uchungu aliokuwa nao Mama Bikira Maria na Yesu ambaye kwa sasa alikuwa tayari kesha wambwa juu msalabani, Yesu analikabidhi Kanisa (kwa mitume) na jumuiya yote ya waamini kwa Mama yake. “Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake,” Yoh 19:26-27. Huyu ndiye Mama Bikira Maria Mama wa Mungu tunaye msheherekea leo. Huyu ndiye tunayetaka kuanza naye mwaka huu mpya tukiwa na imani pasipo shaka kwamba tutamaliza naye mwaka huu salama kama ilivyokuwa NDIYO yake wakati ulipotimia pale horini, na kuendelea na NDIYO yake hadi mwisho pale msalabani ulipotundikwa wakovu  wetu na UTUKUFU wa Kristo na wetu. Hakika yatupasa kumshangilia Mama Yetu Bikira Maria, Mama wa Mungu.

Nilipokuwa likizo nyumbani nilikumbuka tukio la miaka mingi iliyopita mara baada ya kumaliza mwaka wa Malezi huko Mahanje Songea. Nilikuwa na furaha kubwa sana ya kuchaguliwa na kuendelea na masomo ya sekondari katika Seminari ya watawa wa Mt. Fransisco wa Assis huko Maua Seminary-Moshi.

Nikiwa nyumbani Arusha-Njiro najiandaa kwa kuanza masomo hayo ya kidato cha kwanza, niliugua homa ya miguu na kuhisi kupooza na kutoweza kutembea tena. Niliona kama vile ndoto yangu ya kuwa siku moja Mtawa na Padre kuanza kutoweka. Mama yangu Mzazi alinihudumia kwa upendo mkubwa; kuniogesha na kunisaidia hudumu nyingine nilizohitaji kwa hali ile niliyokuwa nayo. Nakumbuka alinibeba mgongoni mwake umbali usiopungua zaidi kilomita 15 hivi kwenda na kurudi, kwani wakati ule hapakuwa na usafiri wa daladala na bodaboda kama ilivyo sasa. Safari hii tulikuwa tunaelekea hospitali ya KCMC-Moshi kwa vipimo zaidi. Hakika Mama yangu alitaabika sana nami. Jambo la ajabu sikuona kukerwa na hali ile niliyokuwa nampatia.

Nilipata vipimo na kurejea nyumbani Arusha-Njiro. Mungu alivyomwema kwa watu wote na nyakati zote, baada ya wiki kama mbili hivi nilianza kupata hauweni. Tarehe za kufungua Seminari zilipowadia nilikuwa tayari kwa masomo na mwenye afya ya kutosha.

Hivyo mwaka huu baada ya miaka kadhaa kupita, Mama yangu Mzazi naye alipatwa na homa ya miguu kama ilivyokuwa kwangu ila kwa tatizo tofauti. Nikiwa likizo ilinipasa kumuhudumia, hasa kumwinua kitandani na kumkominisha kila siku mara baada ya kuadhimisha Misa kigangoni kwetu St. Josephina Bakhita Korona-Njiro. Ilinipasa pia kumpikia kwani karibu ndugu zangu wote wameolewa na kuoa hivyo wanamiji yao. Wajukuu aliokuwa anaishi nao Mama yangu nyumbani asubuhi hadi jioni iliwapasa kuwa shuleni {shule ya upili}. Hivyo muda mwingi nilikuwa naye. Nilimbeba ingawa siyo mgongoni hadi KCMC kwa matibabu. Nilitumia muda mwingi kumfurahisha kwa kumchezea gitaa na kuimba. Kwa kweli nilijaribu kurudisha shukrani zangu japo kwa uchache aliyonitendea miaka hiyo mingi iliyopita.

Leo ninamshukuru Mungu Mama yangu anaendelea vizuri licha kwamba hajapona kabisa. Huu upendo ni sehemu tu ya upendo niliouonja kwa Mama kwa namna alivyotesema na kutaabika nami bila kuchukizwa na karaha nilizompatia. Hakika kama nikiambiwa leo nilipe alichonitendea sintoweza kufanya hivyo hata nikipewa miaka 1000 na Mungu ya kuishi nikiwa nafanya kazi usiku na mchana. Sintoweza kulipa kwa sababu kadiri nitakavyoishi na kuwa hai, ni kwa kipimo hicho hicho deni hili litakavyoongezeka hata kama yeye atakuwa kesha kufa.

Wapendwa wana wa Mungu, kwa sadaka na matojitoleo ya Mama Maria, Mama wa Mungu na hasa kwa NDIYO yake katika fumbo hili la kumwilishwa, mimi na wewe tuna deni kubwa sana la lipa licha ya kwamba Mwanaye Yesu Kristo kesha tulipia deni letu, dhambi zetu kwa sadaka yake pale msalabani. Kwa upande wa kwanza, deni hili ni kuishi upendo wa kweli na haki kwa kila aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni kwa sababu ya upendo huu Kristo alikubali kuyatoa maisha yake kwa ajili yako na yangu. “Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:12-13.  Ni kwa kumkomboa huyu aliyeumbwa kwa sura na mfano wake, Mungu anaruhusu mwanaye ateseke kwa ajili yangu na yako, na Mama Bikira Maria kushiriki mateso haya ya mwanaye. Na sehemu ya pili ya deni hili ni kuwa watakatifu kama Baba yetu wa Mbinguni alivyo Mtakatifu. Utakatifu huu tunaupata kwa kuishi vyema na kuzitumia vyema karama zetu kila mmoja kadiri ya wito wake, kwa kutimiza utume wake vyema.

Tumsifu Yesu Kristo!

Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48

Tusali: Ee Yesu Mwema, niongoze katika kweli na haki. Amina


Herini kwa Mwaka Mpya, 2017


 

miércoles, 28 de diciembre de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI, SIKU YA 7 YA OKTAVA YA NOELI


JUMAMOSI, SIKU YA 7 YA OKTAVA YA NOELI

DECEMBA 31

Somo: 1Yoh 2:18-21

Zab: 96:1-2, 11-12, 13

Injili: Yoh 1:1-18

Nukuu:

Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho,” 1Yoh 2:18 

Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote,” 1Yoh 2:20

“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu,” Yoh 1:1

“Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3

“Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu,” Yoh 1:4

“Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza,” Yoh 1:5

“Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua,” Yoh 1:10

Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea,” Yoh 1:11

“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh 1:12-13

“Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14

“Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema,” Yoh 1:16

“Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,” Yoh 1:17

“Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua,” Yoh 1:18

TAFAKARI:Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu.”

Wapendwa wana wa Mungu, tunaishi katika siku za mwisho. “Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho,” 1Yoh 2:18. Hata hivyo si wakati wa kujawa hofu na wasiwasi. Wanafunzi wa Yesu pia walitaka kujua hasa siku hiyo itakuwa lini. Yesu “Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe,” Mdo 1:7. Kwa muda tulibaki nao kila mmoja wetu atimize vyema utume wake kadiri ya wito na karama alizojaliwa na mwenyezi Mungu.

Matokeo ya utume wako yatadumu milele kuliko matokeo ya kazi zako. Hivyo Yesu anawaambia wafuasi wake, “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi,” Mdo 1:8. Hili ndilo tunalopaswa kufanya sote tulio mpokea Roho huyu Mtakatifu kwa Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara.

Kwa maana nyingine siku ya mwisho ni mpaka pale dunia yote itakapofikiwa na habari njema ya wokovu. Ni pale yote yatakapofikia ukamilisho wake katika umoja ule Yesu aliyotuombe, Yoh 17:18-23. Hivyo kuharakisha siku hii ya mwisho ni sawa na kusema kila mmoja wetu atimize utume wake vyema na habari hiyo ifike kila kona ya dunia. La sivyo ni kupoteza muda bure kubashiri siku ya mwisho. Hakuna ajuaye siku hiyo. Naye Yesu anasema, “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake,” Mt 24:36. Neno, yaani, Yesu kesha fanyika mwili na kesha ushinda ulimwengu, ila tunatembea katika siku zetu za mwisho. Hata hivyo udhihirisho ulio wazi na kamili wa ushindi wa Yesu upo unakuja. Katika safari hii kuelekea udhihirisho huo wazi na kamili kati yetu wapo mbwa mwitu waliovaa ngozi ya kondoo. Katika mtazamo huu, kuishi ni vita. Wapinga Kristo sio wale wazushi tu, bali ni mtindo pia wa kuishi.

Sote tu wapinga Kristo katika maana ya kwamba maisha yetu yasipo akisi ukweli na upendo wa Kristo. Haya ndiyo ayasemayo Mtume Paulo, “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli,” 1Tim 4:1-3. Leo si jambo la ajabu kusikia dini za waabudu mashetani, wajenzi huru-free-masons.

Lakini pamoja na ukweli huo, Kristo ndiye “Nguvu upendo” yenye kuyashukuma na kuyaratibisha yote kuelekea ukamilifu wake, yaani, kusudi la kila kilichoumbwa. Na kusudi la kuumbwa kwetu wanadamu ni kuishi milele. Kuishi ndani na katika Kristo ndiyo sehemu salama na ngome imara. “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote,” Efe 1:17-23.

Kristo kesha shinda ila vita inaendelea dhidi ya wema na uovu. Wale watakaokuwa katika kweli watakuwa katika hatua ya ukomavu na utakaso. Kuzaliwa kuliko kwa kweli kunatoka juu, ambako ndiko kupakwa mafuta kwetu kupitia Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara. “Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote,” 1Yoh 2:20. Hivyo kuishi Ukristo ni vita dhidi ya mpinga Kristo. Utaielewa vizuri vita hii unapofanya tafiti moyo.

Injili ya leo mada kuu ni hii, “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua,” Yoh 1:18. Yesu, Mwana, ni dhihirisho la Baba. Kwa hiyo kwa maneno haya, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu,” Yoh 1:1, kati yetu uwazi wa utufuku wake unawezesha uelewa wetu wa maneno haya, “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14.

Ni kwa mantiki hilo kwamba katika mwili Mungu ni kama Baba, Yoh 1:1-3. Ye yote yule amtazamaye mwana, Yesu Kristo, amwona Baba. “Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?” Yoh 14:9. Ni katika tendo hili la “kuona,” upewa tu yule asikiaye neno, ni yule kwa imani kupitia mwili anaona Utukufu wa Baba. “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh 1:12-13.

Kwa hiyo ujio wa Kristo ni mgogoro katika maana ya mtengano wa wanaoishi katika mwanga na wale waishio katika giza, Kristo akiwa ndiye mwanga wa ulimwengu. Watakao upokea mwanga huu, watapokea kwa imani zawadi zilizo kubwa atakazo kuja nazo. “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh 1:12-13

Wapendwa katika Kristo, pona yetu katika siku hizi za mwisho ni kuishi katika mwanga wa Kristo. Sote tuliobatizwa yatupasa kuziishi ahadi zetu za ubatizo kwa uaminifu. Pia tuwe makini kwa mafundisho ya uongo juu ya kweli na haki ya Kristo, kwani wengi watakuja kwa jina lake.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani,” 1Yoh 4:1

Tusali: Ee Yesu Mwema, nasadiki pasipo shaka yoyote Wewe ndiye Njia, Kweli, na Uzima wa maisha yangu. Amina

 

TAFAKARI: SIKUKUU YA FAMILIA TAKATIFU; YESU, MARIA, NA YOSEFU


SIKUKUU YA FAMILIA TAKATIFU MWAKA-A

Yesu, Maria, na Yosefu

Somo I: YbS 3:3-7; 12-14

Zab: 128: 1-2, 3, 4-5

Somo II: Kol 3:12-21

Injili: Mt 2:13-15, 19-23

Nukuu:

“Amheshimuye baba yake atafanya upatanisho wa dhambi, naye amtukuzaye mama yake huweka akiba iliyo azizi,” YbS 3:3-4

“Amheshimuye babaye atawafurahia watoto wake mwenyewe, na siku ya kuomba dua atasikiwa,” YbS 3:3:5

“Amtukuzaye baba yake ataongezewa siku zake; akimsikiliza Bwana, atamstarehesha mamaye, na kuwatumikia wazazi wake kama mabwana. Mwanangu,” YbS 3:6-7

“Mwanangu, umsaidie baba yako katika  uzee wake, wala usipate kumhuzunisha siku zote za maisha yake,” YbS 3:12

 “Akiwa amepungukiwa na ufahamu umwie kwa upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima sana,” YbS 3:13

Mwenye kumdharau baba yake ni mfidhuli, naye mwenye kumlaani mama yake amekwisha kulaaniwa na Bwana,” YbS 3:16

Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi,” Kol 3:12-13

Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu,” Kol 3:14

 Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana. Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao,” Kol 3:18-19

Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hili lapendeza katika Bwana,” Kol 3:20

Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa,” Kol 3:21

Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize,” Mt 2:13

“Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi,” Mt 2:16

TAFAKARI: Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu,” Kol 3:14

Wapendwa wana wa Mungu, leo tukiwa bado katika kipindi cha kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Kwa namna ya pekee leo, masomo yote matatu yanamulika swala zima la Familia, muundo wake, wajibu wake kwa ujumla na kila mmoja katika familia kadiri ya nafasi yake, Mahangaiko ya familia, na kutengemaa kwa familia yenye kujali na kuwajibika. Bila shaka msingi wa familia ni ule moyo ya upendo wenye kuzaa hali ya kuvumiliana na kutabikiana. Hiki ndicho kifungu cha ukamilifu. Kama asemavyo Mtume Paulo, “Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu,” Kol 3:14. Tukiachia mbali hii Familia Takatifu ya Yesu, Marian na Yosefu, familia zetu si kamili katika maana ya Utakatifu. Familia yetu zina madhaifu mengi sana. Lakini familia hizi ambazo ni dhaifu husimama imara pale wanapotazama, jifunza, na kuishi Utakatifu wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu kama mfano ulio hai wa kuiga.

Ni wazi kwamba familia iliyosimama katika kweli, haki, upendo, huruma, na kusamehana si kazi rahisi na si kazi ya siku moja. Leo tunaposheherekea Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, haikuwa kazi rahisi kwa Maria na wala Yosefu kumlea mtoto Yesu. Tuelewa kwamba Yesu ni Mungu na Mwanadamu. Asili hizi mbili zilileta sintofahamu nyingi kwa Maria na Yosefu katika malezi ya Mtoto Yesu.

Uwepo wa Yesu ulikuwa tishio kubwa sana wa utawala ule wa Herode ambaye mamlaka yalikuwa kila kitu kwake. Hivyo kwa kusikia yaliyosemwa juu ya Mtoto Yesu, Herede anaingiwa na hofu na kuruhusu umwagikaji wa damu zisizo na hatia. Njia aliyochukua Herode haina tofauti na watawala wetu wa leo wanapopatwa na hofu juu tawala zao za mabavu. Wapo wengi wanaouwawa kila dakika ulimwenguni na hasa nchi zetu za kiafrika kwa sababu ya hofu ya madaraka yaliyobebwa na utawala dhalimu.

Hivyo kuhakikisha anamwangamiza Mtoto Yesu, tangazo linatolewa mara moja baada ya kujua wale Mamajusi wamemdanganya kadiri ya maagizo aliyokwisha wapa, yaani, “Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie,” Mt 2:8. Wakijua nia yake mbaya juu ya mtoto Yesu, Mamajusi walishika njia nyingine baada ya kumsujudu mtoto Yesu na kutoa zawadi zao.

Hapa ndipo lilipotolea tangazo la kuwaangamiza watoto wasio na hatia. “Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi,” Mt 2:16. Nguvu ya Mungu na mpango wake kwa wale aliorithia nao ni tofauti na mipango yetu ambayo kwayo haina uzima ndani yake.

Kama Mungu ndiye mweza wa vyote hakuna chochote kitakachozuia mpango huo, kwani nasi kama tulivyo na mamlaka tuliyonayo humtegemea Mungu huyu huyu. “Na hao walipokwisha kwenda zao, (Mamajusi) tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize,” Mt 2:13. Ni nani kama Mungu wetu? Leo tunajionea wenyewe baadhi ya tawala ambazo hazipo tayari kuachia dola kwa AMANI, na hivyo kuleta maafa makubwa ya mauaji ya watu wasio na hatia. Pamoja na ukatili huu, uovu hauwezi kudumu katika umilele wake, kwa sababu uovu hauna umilele. Wale wote wauteteao na kuulinda uovu ujichosha kure. Hivyo, “Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure,” Zab 127:1

Hali na mazingira haya yanaleta hofu kubwa sana katika familia hii Takatifu. Hivyo kama mazingira na hali ya ukimbizi tuionayo leo, hata Yesu ameipitia. Na yanapotokea maafa kama haya wanaotesema ni akina mama na watoto. Mama Marian a Yosefu wanayanusuri maisha ya Mtoto Yesu kwa kukimbilia Misri. Familia hii Takatifu inaishi maisha ya ukimbizi. 

Pamoja na sintofahau hizi, na malezi ya Mtoto Yesu, Bikira Maria alikuwa na muda mwingi wa kutafakari haya asiyoyafahamu. “Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake,” Lk 2:19. Kuyaweka moyoni ni kuyapa nafasi ya tafakari kwa yale tusiyoyajua. Je, wewe kama mzazi mwanao anapofanya ndivyo sivyo, wajiuliza kwa nini amefanya kama alivyo fanya? Kujua chanzo cha tatizo ni bora kuliko kukimbilia kulitatua tatizo. Hivyo tafakari ya Bikira Maria ilimsaidia kufahamu uwezo na kile alicho mwanaye Yesu Kristo.

Muujiza wa kwanza ya Yesu kule Kana unathibitisha ufahamu wa Maria juu ya mtoto wake. Kulipotokea upungufu wa divai, Bikira Maria alienda moja kwa moja na kumwambia Yesu, Mwanaye, kwamba hakuna divai. Bikira Maria hakubaki na jibu la mwanaye, ila alienda moja kwa moja kwa wale wahudumu na kuwaambia,  “Lo lote atakalowaambia, fanyeni,” Yoh 2:5. Kwa tendo hili hakuna shaka kwamba Mama Bikira Maria anaufahamu uwezo wa mtoto wake. Je, leo wazazi wangu muna muda wa kutosha kuwafahamu watoto wenu ikiwa ni pamoja na tabia zao? Basi tujifunze kwa Mama Bikira Maria. Leo tunapoongelea familia na hasa zenye malengo na mwelekeo, tunaongelea familia ndani ya ndoa Takatifu yenye kujali na kuwajibika. Hivyo ni vyema kujua fumbo zima la ndoa na chimbuko la famila kama tunda na matokeo ya ndoa hiyo.

1. Fumbo zima la ndoa na chimbuko la familia

Wapendwa wana wa Mungu, upendo huu wa Mungu kwa watu wake yatupasa kuuona katika mambo yote yenye kutupeleka katika umoja wake, upendo wake, ushirikiano wake na hata katika maagano yetu katika maisha. Ni kwa kupitia umoja huo, upendo huo, na ushirikiano huo wa Mungu na mwanaye mpenzi, Yesu Kristo Mungu hujidhihirisha kwetu kila siku ya maisha yetu hapa duniani. Upendo wa Mungu na mshikamano na mwanaye tunauona katika masakramenti yake, na hasa leo tunavyotafakari kwa ukaribu sakramenti hii ya ndoa. Naye Mtume  Paulo anasema, “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili,” Efe 5:22-23. Hapa upendo wa Mungu kupitia Kristo mwenyewe unaonekana kwa utii huu wanaoishi wana ndoa, na hasa kwa mke kumtiii mumewe. Je, ndoa zetu leo ni salama? Akina mama mnaishi ukweli huu katika agano lenu la ndoa? Leo baadhi ya wanawake wamefikia kuwaita waume zao vyuma chakavu. Je, hayo ndiyo makusudio ya Mungu na muungano wenu huo?

Kwa upande wa wanaume yawapasa kuwapenda wake zao katika kweli na haki. Upendo huu unafananishwa na upendo wa Kristo na Kanisa lake. “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa,” Efe 5:25-27. Wanaume zieshimuni ndoa zetu kwani ndio utakatifu wenu mnapoziishi katika kweli na haki. Wake zenu hawahitaji mambo ya pekee sana zaidi ya kuyasadifu yale wayatendayo kila siku katika familia. Tabia ya kuwaita wake zetu magoli kipa ni chukizo mbele ya Mungu. Muunganiko wenu ni makusudio ya Mungu, na ndivyo alivyoona inafaa.

Utii wa kweli si utumwa kwenu, bali ni ukamilifu wa makusudio ya Mungu katika maisha ya umilele. Wito wenu wa ndoa ni kuufikia umelele wa maisha yenu mlioandaliwa kupitia sakramenti hiyo. Hivyo, “kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo,” Efe 5:24. Ni kuwa na utii katika Kristo kwa sababu yeye anayo maneno la uzima wa milele. Ni kwa kupitia NENO huyu vyote vilifanyika, na kwa kupitia NENO huyu vyote huwa na uzima wa milele, Yoh 1:3. “Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja,” Efe 5:31. Tendo hili la ajabu katika sakramenti hii ya ndoa halimwesabii haki mmoja wa wanandoa kuwa na mambo yake ya pekee na binafsi tena. Hakuna msamiati huu tena wa kusema hiki changu na hiki chako. Kwa kufanya hivyo ni kuujeruhi mwili huu mmoja. Je, jambo hili lina ukweli katika ndoa yako? Je, ni mambo mangapi ya siri unayoyafanya bila kumuhusisha mwenzi wako wa ndoa? Je, hujui kwa kufanya hayo unaijeruhi ndoa yako? Ndugu yangu kama unaishi ukweli huu na kinyume cha sakramenti hiyo ya ndoa, elewa kwamba ndoa hiyo ishakufua katika uhalisia wa mambo na ukweli wa Kimungu. Kilicho baki ni maagizo kuu, na wote mmekuwa wasanii katika sakramenti hii Takatifu.

2. Changamoto kwa watoto na wajibu wao katika familia:

Ni ukweli usiotia shaka kwamba ni wajibu wetu kuwaheshimu wazazi wetu ikiwa ndiyo amri ya nne ya Mungu. Tokeo hilo linatupa heri na miaka mingi katika maisha ya umilele. “Amtukuzaye baba yake ataongezewa siku zake; akimsikiliza Bwana, atamstarehesha mamaye, na kuwatumikia wazazi wake kama mabwana. Mwanangu,” YbS 3:6-7. Tendo la kuwapenda wazazi ni haki na linapendeza machoni mwa Mungu. Ni haki kama asemavyo Mtume Paulo, "enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki," Efe 6:1. Pia tendo hilo lapendeza machoni mwa Mungu, "ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hii lapendeza katka Bwana," Kol 3:20.

Kwa mantiki hiyo, mtume Paulo anaenda mbali na kutupa angalisho kuhusu kuwatii wazazi wetu, na kusema, "maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi," 2 Tim 3:2. Kwa hiyo ndugu yangu jambo hilo ni wajibu, ni shukrani na ni safi kufanya hivyo. “Mwenye kumdharau baba yake ni mfidhuli, naye mwenye kumlaani mama yake amekwisha kulaaniwa na Bwana,” YbS 3:16.  Kwa upande mwingine wazazi ndiyo vielelezo vya Mungu wakiwa kama washiriki wa Mungu katika uumbaji. Kazi hii hata Malaika hakupewa. Ndugu yangu huna Baba zaidi ya Baba uliye naye. Hata kama ni mwendawazimu huyu ndiye Baba yako na unapomweshimu na kutimiza wajibu wako hapo ndipo penye chemchemu ya neema zote. “Amheshimuye baba yake atafanya upatanisho wa dhambi, naye amtukuzaye mama yake huweka akiba iliyo azizi. Amheshimuye babaye atawafurahia watoto wake mwenyewe, na siku ya kuomba dua atasikiwa,” YbS 3:3-5.

Hivyo ni wajibu wa kila mtoto katika familia kuwaheshimu, kuwajali na kuwatunza wazazi katika uzee wao. Tendo hili linakukumbusha kutoa shukrani kwa majitoleo yao katika maisha yako. “Mwanangu, umsaidie baba yako katika  uzee wake, wala usipate kumhuzunisha siku zote za maisha yake. Akiwa amepungukiwa na ufahamu umwie kwa upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima sana,” YbS 3:12-13. Ndugu yangu, namna unavyomjali na kumweshimu mzazi wako ni kwa namna hiyo hiyo utakavyo heshimiwa na kujaliwa na wanao ufikiapo uzee wako. Ni vyema ukawekeza kuanzia sasa katika jambo hili la muhimu katika maisha.

3. Changamoto za wazazi kwa watoto wao, na hasa malezi:

Pamoja na hayo niliyokwisha kuyasema, wazazi yawapasa kuheshi matakwa ya watoto wao ikiwa ni pamoja ya  ndoa za watoto wao wakijua wajibu wao wa kimalezi na kuwaacha watoto wao kuwa huru kuchagua mwenzi wake wa maisha. Pia wapo wazazi wengi wanaowageuza watoto wao kama miradi yao. Kikomo cha famili na kugawanyika ni pale watoto ndani ya familia wanapofikia kuwa na familia. Hili mzazi lazima ulijue na ujiandae vizuri hasa kisaikolojia. Hata kama unampenda vipi mtoto wako huwezi kuzuia asiumwe, asipate matatizo, na wala asife. Cha kushangaza, unakuta binti kaolewa na mara kwa mara mama mzazi yupo beneti naye kwenye shughuli zake, biashara zake, bila taarifa ya Mume wa binti yake. Ndoa ni ya watu wawili. Muwaache. Wewe mama kila mnada unapenda kwenda na binti yako kwa nini?

Jambo lingine la wazazi ni manyanyaso kwa mwali wao. Manyanyaso yakimfumo yasiyokwisha. Mnamfanya mwali wenu kama remote/kiongozea mbali. Anakuwa kama dekio lenu. Mwajiona ndoa yenu ni bora kuliko ya mwali huyu. Mbona yenu hatuyasemi. Yawezekana wewe ulimpenda huyo mume wako kwa kipande tu cha muwa. Usicheke! Kinachowaunganisha wawili na kuwa familia ni fumbo kubwa sana. Hivyo, “Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa,” Kol 3:21. Waacheni waishi maisha yao. Ni kweli yawezekana kabla ya mtoto wenu kuoa au kuolewa vimiminika (tumafuta, tusukari, tunyama, tunguo twa mtimba, na hata tupesa) vilikuwa vingi nyumbani. Baada ya ndoa, hayo yamepungua au kutoweka kabisa. Je hamjui ya kwamba, "kwa sababu hayo ndiyo mlioitiwa ili mrithi baraka?" 1Pt 3:9c. Kuyakosa hayo isiwe kero na shiiida kwa ndoa yao.

Ndoa inakuwa na uhai haya yakizingatiwa kadiri ya mtazamo wa Mtume Petro. "Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka," 1Pt 3:8-9.

4. Changamoto za leo kwenye familia, na wajibu wake:

Ndugu yangu, maneno hayo ni mazito sana kwa wanandoa. Kwa upande wa kina mama, wapo wanaoishi kwenye ndoa bado hawana utambuzi au tofauti na usichana wao. Mama kwenye ndoa tambua kwamba kila siku yakupasa "kupungua" kwa ajili ya familia yako "iongezeke." Familia yaani Baba na watoto wenu waongezeke; upendo, furaha,  afya, akili na mambo mengine mengi tu. Je, utapunguaje? Mtume Petro anatuambia, "kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi; bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyo haribika; yaani roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu," 1Pt 3:3-4. Mtume Petro hapa hapingi mama usiende saloon au kutokuvaa vizuri; bali muelewe kwamba hayo siyo vipauwa mbele katika familia.

Wengi tumetumia muda mwigi nje badala ya ndani. Vikao kila siku visivyoisha. Sema za kiroho januari hadi decemba, mikutano ya injili hadi manane ya usiku, nk. Je, saa ngapi utaijenga nyumba yako? Huku ni kukosa busara kama tunavyoaswa, "Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe, kadhalika mwanamke mzuri asiye na akili," Mit 11:22. Kwa maana hiyo, "kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe," Mit 14:1. Wakati mwingine tunamtafuta mchawi wakati mchawi mwenyewe ndiwe wewe. “Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana. Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao,” Kol 3:18-19. Huu ni wajibu msingi katika maisha ya ndoa na ufahamu wake.

Wanawake wengi ni wawivu kupindukia. Jua likichomoza tu utakuta mkeka upo nje. Nikujigalagaza kwenye mkeka kama dagaa wa kigoma. Masikini wa Mungu labda mumewe alivutiwa na umbo lake la kushikika, baada ya nusu mwaka afadhali ya mkuyu wa handeni. Licha ndoa ni zaidi ya haya ya nje, ila nayo huleta matamanio ya kutazama kwingine kama tulipo kuna pazia na kiza. Elewa mumeo kama ameajiriwa au kujiajiri mwenyewe, awapo huko naye ameolewa na hiyo kazi yake. Awapo nyumbani anaitaji amani na utulivu. Wanawake wengi hawana muda wa kuyasoma mapigo ya mioyo ya waume zao. Mmewe akifika nyumbani tu anadakiwa mlangoni na risala ya mahitaji; utasikia, unajua hakuna sukari, chumvi, unga, nk. Mpe kwanza nafasi ya kupumzika. Muulize habari za huko alikotoka. Muulize angependa kupata nini kabla ya ulichoandaa. Wakati mwingine kuandaa meza anafanya mfanyakazi wa ndani. Au akifanya yeye utashangaa. Ugali kaupika saa sita mchana  wakati mumewe kafika nyumbani saa kumi jioni. Ugali unatoka jasho tu. Kwa nin usiandae mboga tu na wakati mumeo anapata chai ukawa unasonga ukali?

Angalia! Huko alikotoka kila mahali kuna ‘bar’ na nyama choma. Na nyumba nyingi pembezoni mwa barabara kuna kibao kimeandikwa "vyumba bado vipo." Ni kwa namna hii sebule ujeuka kuwa kwenye Bar. Pale anahudumiwa vizuri na kwa ujuzi. Huuliwa, "uncle tukusaidie nini? Anajibu, "bia, kilimanjaro." "Ya baridi "au ya moto? Mhudumu anasisitiza. Kwa vile nyumbani weshagombana na mkewe, anajibu, "ya baridi." Tazama binti huyu hakai mbali na mteja wake. Wewe ulipomwandalia chakula ulirudi kwenye mkeka wako. Binti huyu hukaa nyuzi 45 hivi. Baba huyu akimeza fundo moja la bia ananyanyua macho anakutana na tabasam. Kama Baba huyu alikuwa na mpango wa kunywa bia moja huongeza zadi 5. Hapa kwishakuwa sebuleni pake. Nani wa kulaumiwa?

Wanawake wengi huwasema vibaya sana waume zao. Wengine ufikia hata kuwaita waume zao "vyuma chakavu," kama nilivyokwisha kusema hapo mwanzo. Onyaneni kindugu tena mkiwa chumbani.

Baadhi ya wanaume nao ni balaa! Kumtukana hata kumpiga mkewe mbele za watu au marafiki zake na watoto ni fursa. Ona matusi hayo anavyoyafyatua kama bomu la skadi. "Mwanamke gani wewe nimekuokota bar? Bado sijaoa!" Unayasema maneno haya mbele ya watoto wako. Hata kama ni kweli hubakia maumivu makubwa kwa watoto.  Mtume Petro anasema, "ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu, na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe." 1Pt 3:7. Mke wako haitaji ununulie ndege ili awe na furaha. Ni wewe tu kusadifu kila kitu kidogo anachokifanya nyumbani. Mmefikia hatua ya kuwaita wake zenu "magoli kipa." Mkimaanisha wao ni kudaka tu! Jambo hili halipendezi mbele ya Mungu. Nyote wawili yawapasa kusomana tabia na kupongezana kwa kila kitu mfanyacho kizuri. Mmeo akikununulia kitu kabla ya kukikosoa mpongeze na kumwambia siku nyingine ukitaka ninunulia kitu itapendeza tukienda sote wawili. Kiukweli Wanaume hatuna uhalisi wa kuchambua uzuri kama uzuri, tupo zaidi katika idadi ya kitu au vitu.

Wapendwa wana wa Mungu, wazazi wetu wana nafasi yao muhimu sana katika maisha yetu kama viumbe shirikishi katika uumbaji na Mungu, mahusiano yetu kimaagano yana nafasi yake katika umilele wetu, na hivyo isiwe sababu ya kudharau au kukengeuka na kuwakana wazazi wetu. Mwisho yatupasa kujua wajibu wetu kwa wazazi, maisha yetu ya kimaagano kila mmoja kadiri ya wito wake, na kusudi la kuumbwa wetu na uwepo wetu hapa duniani. Yote haya ni maandalizi ya maisha ya umilele, kama ilivyo amri ya nne wa Mungu, Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako,” Kut 20:12

Kijana Felix aliyemaliza masomo yake ya udaktari alibahatika kumwoa mwanamke mwenye elimu kama yake. Mwanamke huyu alijipenda sana kupita kiasi kutokana na mazingira ya makuzi yake. Ni kweli alitoka familia yenye pesa na tajiri sana.

Felix alitoka familia masikini sana, na soma yake ilikuwa ya shida sana. Felix alifika hapa alipo kwa kutegemea biashara ndogo ndogo za mama yake mzazi. Baba yake Felix alifariki muda mrefu, Felix angali darasa la pili.

Akiwa ameajiriwa na kuwa na mji wake, mama yake mzazi alipenda kumtembelea mtoto wake. Kwa bahati mbaya au nzuri Mama yake Felix alifika na kumkuta mke wa mtoto wake. Kwa namna alivyokuwa mama yake Felix, mke wa Felix alikuwa na mashaka naye kwani alionekana kama ombaomba fulani hivi. Hata kwa kujitambulisha kote kule mke wa felix hakuweza kumpokea vizuri na kulazimika kumwifadhi moja ya vyumba vya stoo.

Alipofika Felix kutoka kazini mkewe alimwambia ujio wa mwanamke mmoja mchafu na waajabu kutokea, na kusema, “eti mama huyo hapa stoo anasema kuwa wewe ni mwanaye.” Felix kwa aibu naye hakumpokea vizuri mama yake, na ndipo ugomvi ulipoanzia. “Kama unasema kuwa wewe ni mama yangu piga mahesabu ya gharama zote ulizonitunza na kunilea nami nitakulipa,” Felix alimwambia mama yake kwa hasiri.

“Naombeni munionyeshe uhani nami nikirudi nitakupa hesabu yangu,” mama yake Felix mjibu Felix. Baada ya muda kidogo mama yake Felix alirudi akiwa amejipaka kinyesi chake mwili mzima na kumwambia Felix, “haya naomba uniogeshe na hii ndiyo gharama yangu kwa siku moja tu katika utoto wako. Kutokana na harufu ile, Felix hakuweza hata kumsogelea Mama yake. Je, Yesu angemlipa nini Mama yake kwa mahangaiko aliyoyapata hadi chini ya msalaba alipokata roho? Yesu anamkabidhi mama yake Kanisa na kusema, “Mama tazama mwanao.” Je, watambua nafasi yako katika familia?

Tumsifu Yesu Kristo!

“Mwanangu, wakati wa kufanikiwa uendelee katika unyenyekevu; hivyo utapewa kuliko mwenye ukarimu,” YbS 3:17

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie amani ya kweli, upendo na tulizo kwenye familia zetu ambazo leo hazipo tayari kutaabikiana. Amina

Familia Takatifu ya Yesu, Maria, na Yosefu, Mtuombee.