JUMANNE WIKI YA 34 YA MWAKA-C
Somo:
Ufu 14:14-19
Zab/kit: 96:10, 11-12, 13
Injili: Lk 21:5-11
Nukuu:
“Na
malaika mwingine akatoka katika hekalu, akimlilia kwa sauti kuu yeye aliyekuwa
ameketi juu ya lile wingu, Tia mundu wako, ukavune; kwa kuwa saa ya kuvuna imekuja;
kwa kuwa mavuno ya nchi yamekomaa,” Ufu 14:15
“Na malaika mwingine akatoka katika ile
madhabahu, yule mwenye mamlaka juu ya moto; naye akamlilia kwa sauti kuu yule
mwenye mundu ule mkali, akisema, Tia mundo wako mkali, ukachume vichala vya
mzabibu wa nchi, maana zabibu zake zimeiva sana,” Ufu 14:18
“Haya mnayoyatazama,
siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa,” Lk
21:6
“Akasema,
Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu,
wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao,” Lk 21:8
“Nanyi
mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi
kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi,” Lk 21:9
TAFAKARI:
“Nina siku, muda, na dakika hii tu ya kuishi.”
Wapendwa wana wa Mungu,
wakati wa Yesu wapo walio vutwa sana na
ulimwengu huu na fahari yake kama ilivyo leo. Wapo waliolitazama Hekalu ya
Yerusalemu na kupambwa kwake wakaishia hapo tu wasione zaidi ya Hekalu hilo.
Yesu anatutaka tutazame zaidi ya kile tunachokiona. Naye Yesu aliwaambia, “Haya
mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo
halitabomoshwa,” Lk 21:6. Tunachotakiwa kukitazama ni uwepo wa ufalme wa kweli
wa Mungu na siyo fahari na mamlaka za kibinadamu tu.
Kutokana
na ukweli huu kuna hatari ya watu kuja na tafsiri zao kuhusu mwisho wa nyakati
kwa lengo hasa la kuwaogopesha watu kwa manufaa yao binafsi. Yesu Kristo anatoa
angalizo na kusema, “Angalieni, msije mkadanganyika, kwa
sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira
yamekaribia. Basi msiwafuate hao,” Lk 21:8. Hawa ndio wale wajulikanao kama
manabii wa uongo kadiri ya Maandiko Matakatifu. “Kwa maana watatokea makristo
wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate
kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule,” Mt 24:24. Je, leo si jambo la
kawaida mtu kujiita nabii, askofu, mtume, n.k?
Mambo haya, mfano
uaskofu, ukasisi, nk, hakuna anayejitwalia, bali hutwaliwa na Mungu peke yake,
ikiwa ni hitaji la Kanisa mahalia kama Mwili wa Kristo inapoonekana inafaa na
mhusika anastahili kadiri ya mamlaka iliyopewa Kanisa na Kristo mwenyewe. “Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika
wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe
matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi,” Ebr 5:1.
Hata Kristo
hakujitwalia mwenyewe kuwa kuhani Mkuu. “ Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza
nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi
leo nimekuzaa,” Ebr 5:5. Tujihadhari sana na manabii hawa wa uongo.
Mwisho wa nyakati hauji
upesi kama tusemavyo au kufikirivyo licha ya mwamba kabla ya mwisho huo
kutatokea matokeo ya kutisha. Yesu leo anatuambia ukweli wa jambo hili, “Nanyi
mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi
kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi,” Lk 21:9. Tunapoona mtu anapanga
hadi tarehe ya matukio haya ya mwisho wa nyakati yeye kaupata wapi ukweli huo
zaidi ya hiki anachotuambia Kristo?
Ndugu yangu tunaye
safiri sote katika tafakari hii usisahau maneno haya ya wahenga wetu: “Wajinga
ndio waliwao.” Yohana katika somo letu la kwanza anaendelea kutufunulia siri ya
nyakati hizo za mwisho. Nyakati za mwisho zina tafasiri mbili; Moja, kuna
mwisho wa nyakati wa wewe kama wewe, yaani, siku ya kiama yako. Na pili, kuna
mwisho wa nyakati katika ujumla wote, yaani, kila kitu kitaumbwa upya.
Somo letu la leo,
yaani, somo la kwanza, linasimulia kiama ya mwisho ya wewe na mimi kama
tulivyo. Ndugu yangu, kuzaliwa siyo lazima, ila kufa ni lazima kwa vile
tushazaliwa. Na mavuno haya ya mwisho ya kila mmoja wetu hufanywa na malaika
husika kadiri ya mpango wa Mungu. Katika maono yale ya mwisho, Yohana aliona
hivi, “Na malaika mwingine akatoka katika hekalu, akimlilia kwa sauti kuu yeye
aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu, Tia mundu wako, ukavune; kwa kuwa saa ya
kuvuna imekuja; kwa kuwa mavuno ya nchi yamekomaa,” Ufu 14:15. Ukweli ni kwamba
kila mmoja wetu ana siku yake, na siri hii hakuna anayeijua isipokuwa Mungu
mwenyewe. Malaika upewa agizo tu na Mungu kufanya mapenzi yake Mungu.
Hivyo, kwa kujua kwa
uhakika ipo siku nitakufa na kuuacha ulimwengu huu, sina budi kujiandaa kwa
siku hiyo ingawa sijui ni lini. Maandalizi ni lazima kwa sababu kufa ni kweli
isiyopingika. Katika kuvuna kwake Mungu anavyo vigezo vyake kwa maana, “mawazo
yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana,” Isa 55:8.
Jambo la msingi kupita yote ni kujiandaa. Na tazama, “malaika mwingine akatoka
katika ile madhabahu, yule mwenye mamlaka juu ya moto; naye akamlilia kwa sauti
kuu yule mwenye mundu ule mkali, akisema, Tia mundo wako mkali, ukachume
vichala vya mzabibu wa nchi, maana zabibu zake zimeiva sana,” Ufu 14:18. Kumbe
kwa kweli hii, yanipasa kuishi kama vile nina siku, muda, na dakika hii tu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Nanyi
mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi
kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi,” Lk 21:9
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, nakushukuru kwa zawadi ya uhai, na yote nayakabidi katika mikono
yako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario