JUMATATU WIKI YA 32 YA MWAKA-C
Somo:
Tit 1:1-9
Zab/kit: 24:1-2, 3-4ab, 5-6
Injili: Lk 17:1-6
Nukuu:
“ikiwa mtu
hakushitakiwa neno, naye ni mume wa mke mmoja, ana watoto waaminio,
wasioshitakiwa kuwa ni wafisadi wala wasiotii,” Tit 1:6
“Maana imempasa askofu
awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni
wakili wa MUNGU; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira,
asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu,” Tit 1:7
“Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye;
akitubu msamehe,” Lk 17:3
“Na
kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema,
Nimetubu, msamehe,” Lk 17:4
“Mitume
wakamwambia Bwana, Tuongezee imani,” Lk 17:5
“Bwana
akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu
huu, Ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii,” Lk 17:6
TAFAKARI:
“Tuongezee Imani Bwana.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Habari Njema yetu ya leo,
yaani, Injili, tunaona utendaji wa hekima iliyo safi. Mtu anayeongozwa na
yaliyomema kamwe hawezi kumwingiza mwingine kwa yaliyo mabaya. Kwa kufanya
hivyo ni kuisaliti dhamiri njema ambayo Mungu ametupatia ili tuwe wawakilishi
kwa yaliyo mema kama yeye alivyo mwema. Licha ya kwamba maisha hayakosi makwazo
ya hapa na pale, Yesu anatupa angalizo kwa wale ambayo ndani yao Mungu kwa nia
njema amewapa uwezo wa kuwa na dhamiri njema ila kwa ubinafsi wao wanakuwa
vikwazo kwa wengine. Yesu anasema adhabu ya mtu huyo, “Ingemfaa
zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko
kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa,” Lk 17:2. Je, ni mara ngapi unakuwa
kikwazo kwa mwenzako ilhali tunajua?
Basi
ndugu zangu katika ukweli huu, yaani, kuwa watu wanaongozwa na dhamiri safi si
wakati wa kufanya ‘jino kwa jino.’ Je, upo tayari kutoa msamaha pale ambapo
yule aliyekukosea yupo tayari kuomba msamaha? Je, wasimama tu katika kweli iliyo ndani yako bila kuona ukunyufu wa
anayekuomba msamaha? Tuelewe kwamba, wokovu wa mtu si kwa ajili yake peke yake,
bali kwa ajili ya wengine pia. Kuna furaha kubwa sana mbingini na kwa Mungu
wetu, pale baadhi ya watu uliowajua
wamepata kuiona mbingu kupitia kwako kwa tendo tu la kutoa msamaha. Hivyo Yesu
anasema, “Jilindeni; kama ndugu yako
akikosa, mwonye; akitubu msamehe,” Lk 17:3.
Tuonyane kindugu mara zote.
Ndugu yangu, lengo
lako katika upatanishi liwe kumpata ndugu yako na wala siyo kumpoteza. “Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi
kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe,” Lk 17:4. Tusiwe tayari kuhesabu kushindwa kwake kwa kutimiza
yale aliyoyahaidi, bali tutazame utayari wake kwa kuliona kosa na kuwa tayari
kutubu. Mazoea yaliyokwisha kuwa tabia ya mtu ni vigumu kuachana nayo kwa mara moja.
Tuwe tayari kutoa
muda wa kutosha kwa mtu kujirudi na kujirekebisa. Hapa na katika hali hii,
tumwombe Mungu atupe Imani dhamini ya kuamini kazi yake kwa wengine wanaovutwa
kwake licha kwa polepole. Ni katika ukweli huu Mitume wa Yesu wanamwomba Yesu
awaongezee imani ya kuyabeba hayo pale yatakapotokea, Lk 17:5. Naye Yesu
akawajibu, “Kama mngekuwa na
imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe
baharini, nao ungewatii,” Lk 17:6. Kumbe
ili mambo yaende vizuri hatunabudi ya kuwa na imani thabiti.
Uthabiti huu wa Imani
pamoja na kuwa ndicho kigezo cha kukomaa kiroho, unabeba uzito zaidi kwa wale
walio hesabiwa haki hiyo na Mama Kanisa kwa nafasi mbali mbali. Leo katika somo
letu la kwanza tunaona sifa ya kuwa Askofu kadiri ya hitaji lile la Kanisa la
mwanzo kama ifuatavyo; “Maana imempasa askofu awe mtu
asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili
wa MUNGU; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe
mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu,” Tit 1:7. Kiongozi licha ya
kubeba dhamana kadiri ya ofisi yake, Kiongozi ni kioo cha jamii.
Na zaidi ya hayo,
Askofu ilimbidi “awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki,
mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake,” Tit 1:8. Uwepo wa Askofu ni utimilifu,
ukamilifu, na uwakilishi wa Kristo pale alipo. Askofu ni, mtetezi wa Imani,
ikiwa ni pamoja na kufundisha imani ya kweli. Hivyo ni wajibu wetu kushirikiana
vyema na Askofu wetu wa jimbo katika kukuza, kuimarisha, na kuikoleza imani ya
kweli.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kama ndugu yako
akikosa, mwonye; akitubu msamehe,” Lk 17:3
Tusali:- Ee Yesu, tujalie
neema ya kuishi imani ya kweli. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario