lunes, 21 de noviembre de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 34 YA MWAKA-C


JUMATANO WIKI YA 34 YA MWAKA-C

Somo: Ufu 15:1-4

Zab/kit: 98:1, 2-3ab, 7-8, 9

Injili: Lk 21:12-19

Nukuu:

“Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema, Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa,” Ufu 15:3

“Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu; kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako; kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa,” Ufu 15:4b

Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu,” Lk 21:16-17 

Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu,” Lk 21:18

TAFAKARI:Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu,” Lk 21:17 

Wapendwa wana wa Mungu, katika Injili ya leo Yesu anawaambia wafuasi wake nasi pia maneno haya mazito, ‘Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu.’ Tutachukiwa kwa ajili ya jina la Yesu kwa sababu ukiwa ndani na katika Kristo Yesu watangaza vita dhidi ya uovu. Ndani na katika Kristo Yesu kuna kweli, haki, upendo, huruma, msamaha, na amani. Na zaidi ya yote, ndani na katika Kristo Yesu kuna njia ya kweli, ukweli kamili, na uzima wa milele, Yoh 14:6.

Lakini kustahimili hayo yote kutakugharibu subira na uvumilivu. Naye Yesu anatuambia, “Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu,” Lk 21:19. Mwenye subira ufikiri vyema tena kwa undani na upana wake. Mwenye subira huyatazama yote katika jana yake, leo yake, kesho yake, na umilele wake.

Kuwa mfuasi hai wa Kristo kuna mapaswa yake. Yesu anatuambia leo mapaswa ya kuwa mfuasi wake hai. Mapaswa yake ni kusalitiwa. Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu,” Lk 21:16-17. Badala yake, katika hali hii Yesu anatuambia tuwe na furaha. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12.

Yatupasa kufurahi kwa sababu katika mateso na ugumu huu wa kusimama katika kweli na haki, hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu,” Lk 21:18. Ndugu yangu tunaye safiri pamoja katika tafakari hii, elewa kwa hakika kabisa kama kweli huu mfuasi hai wa Kristo, ipo siku ufuasi wako utapimwa.

Na hilo kama litatokea jiachie kwake Kristo Yesu. “Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza mtakavyojibu; kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga,” Lk 21:14-15. Kama isivyowezekana kula keki na wakati huo huo kutokuila kwa kuishikilia, ndiyo lilivyo achilio la kweli katika mikoni ya Kristo Yesu.

Ukweli ni kwamba yote yaliyo ya kibinadamu yana ukomo wake. Ila penye uhai hata kama uhai huo una ukomo, nyuma yake kuna uhai mwingine, na wenye kuyashikilia hayo yote, yenye ukomo na ya umilele. Hakikisho hilo kesha tupa Kristo mwenyewe kwamba, tusiwe na shaka juu yake, na tusifikiri-fikiri na kupoteza tumaini la kweli.

Nguvu na uwezo wa Mungu kwa namna yoyote ile mwanadamu hawezi kupima wala kujua kina chake. Yohana anaonyeshwa baadhi tu katika maono. “Kisha nikaona ishara nyingine katika mbingu, iliyo kubwa, na ya ajabu; malaika saba wenye mapigo saba ya mwisho; maana katika hayo ghadhabu ya Mungu imetimia,” Ufu 15:1. Mungu asingekuwa huruma na stahimilivu, hakuna hata mmoja kati yetu ambaye angesalia bila kuipata ghadamu yake.

Ndiyo maana Malaika mbinguni hawachoki kumwimbia Mungu na kumsujudia muda wote. “Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema, Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa,” Ufu 15:3. Je, kwa hali na mazingira yako hapo ulipo huna sababu ya kumtukuza Bwana Mungu wako?

Malaika wa Mungu wanatupa sababu ya kumwimbia Mungu na kumsujudu. Nao wanayatenda hayo  “Kwa kuwa wewe (Mungu) peke yako u Mtakatifu; kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako; kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa,” Ufu 15:4b. Na fungu lililo bora zaidi ni kuyaachia yote mikoni mwa Mungu, yawe yale tuyawezayo kwa ufahamu wetu mdogo, na hata yale yaliyo jificha nje ya uwezo wetu.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Kwa kuwa wewe peke yako u Mtakatifu; kwa maana mataifa yote watakuja na kusujudu mbele zako; kwa kuwa matendo yako ya haki yamekwisha kufunuliwa,” Ufu 15:4b

Tusali:-Ee Yesu, tujalie subira. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario