Sikukuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume
30 Novemba
Somo: Rum 10:9-18
Zab: 19: 8-11
Injili: Mt 4:18-22
“Kwa
sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni
mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka,” Rum 10:9
“Kwa
maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata
wokovu,” Rum 10:10
“Akawaambia,
Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu,” Mt 4:19
“Mara
wakaziacha nyavu zao, wakamfuata,” Mt 4:20
TAFAKARI:
“Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.”
Wapendwa
wana wa Mungu, mtihani mkubwa kwa mtu yeyote yule siyo hii tuifanyayo mashuleni
na hata vyuoni, bali ni mtihani huu wa “kuamua,” uwe nini katika maisha yako.
Si rahisi kufanya maamuzi hayo na kuchukua njia nyingine mpya kabisa usiyojua
kifuatacho huko mbeleni. Mtu huwa na uhakika kwa kile alichokiishi jana na
anachokiishi leo na sasa. Huu ni mzunguko wa kawaida katika maisha ya kila
mmoja wetu. Kuwekeza maisha yako yote kwa kile usichokijua humjengea mtu hofu.
Leo
Kanisa linapofanya sikukuu za watakatifu na kwa maana ya pekee leo sikukuu ya
Mt. Andrea Mtume, ni kusadifu yale waliyoyaamua na kuyaishi na ndiyo ukuaji wa
Kanisa na uhai wake. Walifanya uamuzi wa kuacha yale waliyoyazoea na yaliyokuwa
yanawapa usalama na kufuata kile wasichokijua wakijisalimisha kabisa katika
hicho. “Mara
wakaziacha nyavu zao, wakamfuata,” Mt 4:20.
Mtume Andrea akiwa na
ndugu yake Simoni Petro walikuwa wavuvi. Kazi hii iliwapa usalama na mahitaji
yao ya kila siku. Yesu anawaita wamfuate nao wanaacha pale pale waliyokuwa
wanafanya na kumfuata. Uamuzi huu ni mzito sana. “Naye
alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni
aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa
wavuvi,” Mt 4:18. Kazi hii ndiyo iliyowapa mkate wao wa kila siku. Embu fikiri
leo kwa kazi unayofanya hasa wale wanaopata kipato kilichonona, aje mtu tu na
kukuambia nifuate. Nini kitakuwa kitu cha kwanza kufanya? Bila shaka utaanza
kumpiga maswali mazito na mwisho kumchukulia kama mwendawazimu hivi.
Mitume hawa wanayaacha
yote na kumfuata. Yesu “Akawaambia,
Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu,” Mt 4:19. Kuwa wavuvi wa watu
ni mabadiliko mazima ya mfumo na namna ya kutenda na kuishi. Hapa ndipo
tunaposema Mitume hawa walikuwa majitu ya sifa. Mioyo yao ilikuwa na ushupavu
wa hali ya juu. Ni vigumu sana mtu kuubadili mfumo wa maisha yake aliouzoea.
Yesu Kristo alikuwa kila kitu katika maisha yao. Walijua
pia hakuna wokovu pasipo Kristo. Iliwezekanaje hivyo haraka? Bila shaka kwa
Nguvu na Neema za Mungu iliwezekana pale walipoonyesha utayari wao wa kumsikia
Yesu na kumfuata. Mtume Paulo anatuambia, “kwa
sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni
mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka,” Rum 10:9. Jambo hili la
kujisalimisha kabisa mikono mwa Yesu halikuwa na mashaka ndani ya mioyo ya hawa
Mitume ingawa halikuwa jambo rahisi kufanya. “Kwa
maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata
wokovu,” Rum 10:10
Wapendwa wana wa Mungu,
sababu nyingine ya uwepo wetu hapa duniani licha ya kwamba ni kwa muda mfupi,
ni kuwaelezea watu wengine habari njema ya wokovu wetu. Wewe uliyebahatika
kuifahamu siri hii usibaki nayo mwenyewe. Ni furaha kubwa sana mbele ya Mungu kama
watakuwepo baadhi ya watu waliofika mbinguni kwa sababu ulitumia muda wako
kuwaelezea habari njema ya wokovu kwa maisha yao. Mitume waliona na kuupokea
wajibu huu mkubwa. “Maana sisi hatuwezi kuacha
kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia,” Mdo 4:20. Neno hili sasa si kwa
Wayahudi tu, ila lapaswa kusikika duniani kote.
Kwa
kupitia Kristo sote tumeunganishwa na kuwa familia moja yenye mastahili sawa
mbele ya Mungu, na warithi wa ufalme wake. “Kwa
maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote,
mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina
la Bwana ataokoka,” Rum 10:12-13. Mitume kwa namna ya pekee waliuona wajibu huu
mkubwa wa kulihubiri neno la Mungu pasipo woga.
Msingi wa haya yote ni
Imani ile waliyokuwa nayo Mitume, na kwa namna ya pekee leo Mama Kanisa
anapofanya sikukuu ya Mt Andrea Mtume. Hivyo
chanzo cha imani hiyo ni kusikia neno la Kristo. “Basi imani, chanzo chake ni
kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo,” Rum 10:17. Je, watu watasikiaje
bila kuambiwa? Kumbe leo pia tunakumbushwa mimi na wewe kwamba kwa Sakramenti
ya Ubatizo tunafanywa wamisionari. Ni wajibu wa kila Mbatizwa kulitangaza neno
la uzima na wokovu kwa watu wote. “Lakini
nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote,
Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu,” Rum 10:18.
Hivi ndivyo
walivyofanya Mitume, na leo Kanisa limesimama likiwa Kristo ndiye msingi wake
Imara, na Mitume. Mimi na wewe tunadaiwa kuyatoa maisha yetu kama walivyofanya
Mitume ili habari njema iwafikie wote ambao bado hawajasikia. Je, nifanye vipi?
Anza hapo hapo ulipo! Kuwa chumvi na mwanga ili uso wa Kristo uonekana katika
maisha yao na yako.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Maana,
ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena
ole wangu nisipoihubiri Injili!” 1Kor 9:16
Tusali:
Ee Yesu, wajalie neema na nguvu wale wote wanaofanya kazi ya kimisionari, na
hasa kwenye mazingira magumu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario