jueves, 24 de noviembre de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 34 YA MWAKA-C


IJUMAA WIKI YA 34 YA MWAKA-C

Somo: Ufu 20:1-4, 11-21:2

Zab/kit: 84:3, 4, 5-6a, 8a

Injili: Lk 21:29-33

Nukuu:

 “Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu,” Ufu 20:4

 “Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena,” Ufu 21:1

Wakati iishapo kuchipuka, mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba majira ya mavuno yamekwisha kuwa karibu. Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea, tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu,” Lk 21:30-31 

Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe,” Lk 21:32-33

TAFAKARI: “Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.”

Wapendwa wana wa Mungu, katika Injili ya leo, Yesu Kristo anatupa wosia kwa yale yatakayojiri ikiwa ni hitimisho la nyakati. Yesu anatumia mifano ya kawaida kulingana na mazingira ya watu wake. Katika jambo hili la kusoma alama za nyakati, Yesu anatumia mfano wa mti aina ya Mtini. Naye anasema, Wakati iishapo kuchipuka (Mitini), mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba majira ya mavuno yamekwisha kuwa karibu. Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea, tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu,” Lk 21:30-31.

Ufalme huu wa Mungu ni ule aliofunuliwa katika maono Yohana. Ni ufalme ambao utaushinda uovu kwa wema kama tulivyosoma katika simulizi la ono la Yohana kuhusu lile joka-ibilisi wa zamani, na yule mnyama-wale wote wanaojiinua na kujitananisha na Mungu. Hawa ni miungu watu. Ni ufalme ulioshuka kutoka mbingu, yaani, neno kufanywa mwili, kumwilishwa na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Hivi ndivyo Yohana alivyofunuliwa katika maono: “Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu,” Ufu 20:4

Ufalme na utawala huu ushasimikwa kuanzia pale ilipoaanza safari nzima ya wokovu wa mwanadamu, neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Huu ni ukweli usiopitwa na wakati. Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe,” Lk 21:32-33. Ukweli huu wa neno kutokupitwa na wakati ulishafunuliwa pia kwa njia ya maono aliyofunuliwa Yohana.

Hapa Yohana anamzungumzia Kristo Yesu, ambaye ndiye hakimu wetu wa upendo, haki na kweli. Weupe wa kiti chake wasema yote kuhusu hukumu yake. “Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana,” Ufu 20:11. Wale wote wasioishi katika upendo wa kweli, haki, na kweli katika yote, hawatakuwa majasiri kuuona uso wa hakimu huyu.

Ndugu yangu unaye safiri  nami katika tafakari hii, utakuwa na ujasiri huo siku hiyo, kuutazama uso wa hakimu huyu aliye haki? Jibu ni rahisi sana; ‘jitazame unavyoishi leo na sasa.’

Wapendwa katika Kristo, kuwa katika  ufalme wa Kristo ni kufanana na Kristo katika kufikiri, kuona, kutenda, na kuishi. Yesu anatuambia sote kwamba, “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate,” Lk 9:23. Zeozi au mtihani huu wa maisha si wa  mara moja tu, bali kila siku ya maisha yako na yangu.

Na kuwa kweli mwanafunzi wa Yesu ni kuuchukua msalaba na kumfuata Yesu. Yesu analisema jambo hili wazi kabisa bila kuficha kitu. Naye anasema,Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu,” Lk 14:27. Je, waufahamu msalaba wako? Hapa napo jibu ni rahisi tu; ‘Tazama vilema vyako.’ ‘Tazama udhaifu wako!’ ‘Tazama changamoto zako katika maisha agano unayoyaishi leo na sasa!’

Ni katika kuvijua vilema vyake na kulenga katika ukamilifu ingawa udhaifu upo ndiyo pona na salama yake. Ni katika kuujua udhaifu wako na kuchukua hatua kuelekea ukamilifu ukilitazama tumaini la kweli katika Kristo mbele yako, ndiyo ongoka yako. Na, ni katika kuishi maisha agano kila mtu kadiri ya wito wake ndipo ulipo mlango wa mbinguni au kuzimu. Mlango wa mbinguni kwa kuishi utakatifu wa agano hilo kadiri ya wito wako, na mlango wa kuzimu kwa kuishi kinyume au kulisaliti agano hilo kadiri ya wito wako,  na hasa kile ulichoitiwa kuishi.

Yohana anatuambia jinsi itakavyokuwa mwisho wa safari hiyo niliyoisema hivi punde kwa kila mmoja wetu kuishi kile alichoitiwa katika utakatifu wake. Naye Yohana anasema,  “Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao,” Ufu 20:12. Hapa tunafunuliwa hukumu ile ya mwisho ya kila mmoja kadiri ya matendo yake.

Na hiki ndicho kitakachotokea kadiri ya maona aliyofunuliwa Yohana, ambacho kwa uhakika Kristo kesha tufunulia siri hiyo. Kwa lugha ya picha Yohana anasema, “Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake,” Ufu 20:13. Hukumu kadiri ya matendo inasema zaidi hukumu ile ya kila mmoja na inayolenga maisha yako leo na sasa. Na swali la nafsi la kujiuliza ni hili; Je, maisha yangu yanaakisi kile nilichoitiwa na kukiishi?

Na hukumu la jumla yenye kulenga ‘kufanyika vyote upya,’ ndiyo anayoiongelea Yohana pia kwa lugha hii ya picha, kwamba, “Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto,” Ufu 20:14.  Na walioenenda vyema katika matendo yao watauridhi uzima huo wa milele na kutawala pamoja na Mwana-Kondoo milele yote. Kinyume chake ni kwamba, “iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto,” Ufu 20:15.

Kutokuwepo au kuandikwa katika kitabu hiki cha uzima kwa maanisha kwamba ingawa maisha hapa duniani ni jukumu la muda mfupi, hukufanya lolote jema kwa kipindi hicho cha kujiandaa. Lolote jema ufanyalo leo na sasa licha ya udogo wake, na wakati mwingine kutoonekana na watu, Malaika zake Mungu hulirekondi katika kitabu hiki cha uzima. Je, Yesu anasema nini juu ya hukumu hii?

Yesu anatukumbusha tukio hili  na kusema, “Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai. Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake. Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu. Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu,” Yoh 5:25-29. Wafu watakaoisikia sauti ya Mwana wa Adamu na kuwa hai ni wale walioishi muda wote hofu ya Mungu.

Baada ya zoezi hili la haki, upendo, na kweli kufanyika na Hakimu wetu huyu asiye na upendeleo, Yohana anatuambia alichokiona. “Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena,” Ufu 21:1. Huu ndio ule ukamilifu wa vyote kufanywa upya. “Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe,” Ufu 21:2. Je, ushukapo mji huu mpya utakukuta katika hali gani?

Tumsifu Yesu Kristo!

“Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena,” Ufu 21:1

Tusali:-Ee Yesu, yatengeneze tena maisha yetu hasa pale tulipoikosea njia na kufuata yaliyo yetu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario