lunes, 7 de noviembre de 2016

TAFAKARI: KUTABARUKIWA BASILIKA LA LATERANI


Kutabarukiwa Basilika la Laterani

Somo I: Eze 47:1-2, 8-9, 12

Zab: 46:2-3, 5-6, 8-9

Somo II: 1Kor 3:9-11, 16-17

Injili: Yoh 2:13-22

Nukuu:

Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi po pote utakapofikilia mto huo,” Eze 47:9 

Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa,” Eze 47:12 

Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu,” 1Kor 3:9

Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo,” 1Kor 3:11

Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi,” 1Kor 3:17

akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara,” Yoh 2:16 

Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila,” Yoh 2:17 

Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha,” Yoh 2:19

Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake,” Yoh 2:21 

TAFAKARI: “Nasi ni shamba la Mungu Jengo la Mungu, Msingi wake ni Yesu Kristo.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anasheherekea siku ya Kutabarukiwa Basilika la Laterano. Historia fupi kuhusu Basilika hii ya Laterano:

Laterano (kwa Kilatini Lateranus) ni mtaa wa Roma maarufu hasa kwa sababu kulikuwa na Ikulu mojawapo la Kaisari Konstantino Mkuu. Lakini pamoja na ukweli huo, inaonyesha kwamba Plautius Lateranus ilikuwa familia moja tajiri katika Falme ya Roma. Plautius alituhumiwa na Mfalme Nero kwa kula njama dhidi ya Mfalme. Matokeo ya tuhuma hii ilikuwa kunyang’anywa na kugawanywa kwa mali za familia hii. Hivyo, Mfalme Constantino baada ya yeye kuruhusu Ukristo  katika Dola la Roma (Hati ya Milano 313) ikulu iligeuzwa kuwa Kanisa  ambalo liliwekwa wakfu na Papa Melkiades  (314), na mpaka leo linaheshimiwa na Kanisa Katoliki  kama Kanisa kuu la Jimbo  la Roma na la ulimwengu mzima.

Tofauti na wanavyodhani wengi, Ukulu wa Papa ni katika Kanisa hilo, si katika Basilika la Mt. Petro huko Vatikano. Jina rasmi ni Kanisa la Kristo Mkombozi, lakini watu wanaliita kwa kawaida kanisa la Mt. Yohane (Mbatizaji) kwa kuwa nyuma yake ipo batizio kuu tena juu ya ukuta wake wa mbele kandokando ya sanamu  ya marumaru ya Yesu, zipo zile za Yohane Mbatizaji na Mtume Yohane.

Ndani, juu ya altare kuu yanatunzwa mafuvu ya vichwa vya Mtume Petro na Mtume Paulo. Ndani ya Kanisa hilo mara tano ulifanyika mtaguso ambao kila mmoja unahesabiwa na Kanisa Katoliki kuwa Mtaguso Mkuu. Mpaka uhamisho wa Avignon (karne ya 14) Mapapa waliishi karibu na Kanisa hilo, na mpaka leo seminari kuu ya jimbo (pamoja na chuo kikuu  cha Kipapa cha Laterano) iko nyuma yake. Eneo lote ni nje ya mamlaka ya nchi ya Italia na linahesabiwa kuwa sehemu ya nchi huru ya Vatikano.

Wapendwa pamoja na maelezo hayo mazuri kuhusu historia ya Kutabarukiwa kwa Basilika hii, masomo yetu leo yote matatu yanatutaka kutafakari na kuona kuwa “Nasi ni shamba la Mungu Jengo la Mungu, Msingi wake ni Yesu Kristo,” kwa Sakramenti ya Ubatizo. Msingi wa Kanisa hili ni Kristo wenyewe aliyelisimamisha kwa mateso, kifo na ufufuko wake. “Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo,” 1Kor 3:11. Kwa mateso, kifo, na  ufufuko wake Kristo miili yetu imehuishwa na kuwa hekalu la Roho Mtakatifu.

Kwa kuwa tumehuishwa na kuupokea huo Utakatifu hatupaswi kulibomoa hekalu hili kwa hatia yoyote ile, na hasa dhambi. Yeyote yule atakayeliharibu hekalu hili, Mungu naye atamharibu. Leo hekalu hili la Roho Mtakatifu linafanyiwa vituko vya aibu na vya kusikitisha. Embu fikiri mtu anapomkata vipande vipande mwenzake kwa sababu ya pesa na utajiri. Embu fikiri ni mimba ngapi zinaharibiwa na kutolewa kwa kila sekunde. Embu tazama ni wazee wangapi na walemavu wa ngozi wanavyouwawa. Hakika, “Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi,” 1Kor 3:17. Tuone thamani na wajibu kuulinda uhai na kuutetea. Uhai ni mali ya Mungu na zawadi ya Mungu kwetu.

Hekalu hili, yaani kila Mbatizwa ni Takatifu. Na tunapoongelea Kanisa kwa maana ya kwanza kabisa siyo Jengo bali ni kila aliyebatizwa. Na tunapoongelea Kanisa hai maana yake ni kila aliyebatizwa na anayeishi ahadi zake za ubatizo vyema katika kujali na kuwajibika ipasavyo. Kujali na kuwajibika huku kunachukua pande zote mbili, yaani, Kanisa kama Wabatizwa, na Kanisa Kama Jengo. Sura na mtazamo huu wa Kanisa la Mungu ni kama ilivyo shilingi. Mfuasi wa Kristo hawezi kujitenga na kuchagua kuwa sehemu moja tu na kuacha nyingine. Akifanya hivyo atakuwa bado hajakamilika.

Injili ya leo inatupa ufafanuzi mzuri kuhusu mtazamo huu wa Kanisa niliouelezea hapo juu. Yesu alipoingia hekaluni alikutana na mambo ya ajabu sana. Hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng'ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha. Kwa hali aliyoikuta na kuiona ilimbidi kuchukua hatua za haraka mara moja. Yesu “akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara,” Yoh 2:16. Hili ni Kanisa Takatifu, na  kama Jengo yapaswa kufanyika yaliyo matakatifu. Yesu hakuona haya kuvitawanya vyote vilivyokuwa ndani ya hekalu lile.

Wayahudi walipotaka kupewa Ishara ili wajue ni kwa mamlaka gani anayafanya hayo, “Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha,” Yoh 2:19. Hapa tunaona maana halisi ya Kanisa na Msingi wake, yaani, Kanisa kama Wabatizwa wote, na Msingi wake ni Kristo mwenyewe.  Kwa maneno hayo ya Yesu, kwamba, walivunje hekalu naye katika siku tatu atalisimamisha, “yeye alinena habari za hekalu la mwili wake,” Yoh 2:21.

Habari njema ya Kanisa hili ni yale aliyokwisha yatabiri Nabii Ezekieli kama tulivyosoma na kusikiliza somo la kwanza. Kwanza kabisa katika habari njema hiyo, Kanisa ni sakramenti ya wokovu wetu. Kwa kupitia Masakramenti yake tunapata neema na kujazwa uhai. Nabii Ezekieli anatumia lugha ya picha, “mito yenye maji yaponyayo,” yaani, kwa tafsiri tungesema ‘Masakramenti.’ Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi po pote utakapofikilia mto huo,” Eze 47:9.

Mto huu yaani,  Kanisa kwa sasa upo duniani kote, na Wabatizwa wote wenye kuishi ahadi zao za ubatizo wanazidi kuponywa na kupata neema za Mungu. “Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa,” Eze 47:12. Kwa vile Msingi wa Kanisa hili katika mfano huu wa mto na maji yake yenye kuponya ni Kristo, kupata neema na baraka hizi yakupasa kuwa ndani na katika Kristo Yesu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa,” Efe 5:29

Tusali:-Ee Yesu, tufanya viungo hai vya mwili wako, yaani, Kanisa kila mmoja wetu kadiri ya wito na nafasi yake. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario