jueves, 24 de noviembre de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 34 YA MWAKA-C


JUMAMOSI WIKI YA 34 YA MWAKA-C

Somo: Ufu 22:1-7

Zab/kit: 95:1-2, 3-5, 6-7

Injili: Lk 21:34-36

Nukuu:

“Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung'aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo, katikati ya njia kuu yake, Ufu 22:1-2a

 “Kisha akaniambia, Maneno haya ni amini na kweli. Naye Bwana, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumwa wake mambo ambayo hayana budi kuwako upesi. Na tazama, naja upesi; heri yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki,” Ufu 22:7

Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo,” Lk 21:34 

Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu,” Lk 21:36

TAFAKARI: Mambo haya hayana budi kuwako upesi.”

Wapendwa wana wa Mungu, katika Injili ya leo Yesu anatupa angalizo kuhusa maisha yetu hapa duniani. Naye anasema, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo,” Lk 21:34. Kwa vile hatuijui siku ya kiama yetu, yatupasa kuwa macho huku taa zetu zikiwa zinawaka kama wale wanawali watano wenye busara, Mt 25:4.

Katika kile kituo cha tisa, njia ya msalaba, kipindi cha Kwaresma, tunaambiwa kwamba Yesu anaanguka mara ya tatu. Moja ya mateso tunayomzidishia Yesu ni dhambi hii kama sala isemavyo, “mara nyingi mno ninajibovusha kwa kupenda mno starehe, anasa na tafriji.” Maisha yetu hapa duniani ni mafupi sana ukilinganisha na maisha ya umilele. Kila mmoja wetu anapaswa kuyapa maisha haya kipaumbele akilenga maandalizi ya maisha ya umilele.

Katika jambo hili Yesu anatuambia, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu,” Lk 21:36. Kukesha huku ni kufanana na Kristo kila siku kwa kutenda mema na kuishi utakatifu ule aliouishi ukijipokea kama ulivyo binadamu. Kuishi kama Kristo ni kuishi katika maisha ya utakaso. Ni kurejesha ile sura na mfano wa Mungu ndani yako ilipotezwa na kuchakazwa na dhambi. Huu ndio ufalme aliokuja kuusimika Yesu Kristo duniani, yaani, kurudisha taswira ile ya Mungu ndani ya mioyo ya wanadamu.

Kwa vile hii ndiyo siri aliyotufunulia angali hapa duniani, basi mwisho huo wa nyakati Yesu Kristo, Mwana-Kondoo, atasimama kama hakimu katika pendo, kweli na haki. Na hivi ndivyo Yohana alivyofunuliwa katika maono yake; “Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung'aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo, katikati ya njia kuu yake, Ufu 22:1-2a. Na kwa vile njia kuu ni moja, yaani, mauti, na Kristo kesha yashinda mauti kwa mateso, kifo, na ufufuko wake, kila nafsi lazima itaonya mauti hayo, na kukutana na hakimu huyu wa aliye upendo, haki, na amani.

Katika hukumu hiyo, Mungu atarejesha kusudio lake la mwanzo, yaani, kutokuwa na hali ya kufa kama walivyoishi wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Hawa, kwenye ile bustani ya Edeni kabla ya kudondoka kwao, Mwa 2:8-25. Na rejesho lenye mfanano huo ndicho alichofunuliwa Yohana katika maono, yaani, “Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa,” Ufu 22:2b.

Hali, mazingira, na utawala wa mji huo mpya utakuwa kama ifuatavyo; “Wala hapatakuwa na laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia; nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao,” Ufu 22:3. Hali, mazingira, na utawala huu utakuwa katika milele yote.

Taswira au muonekano wa mji huo ni ishara tosha ya ushindi dhidi ya utawala wa giza kwa kuuleta mwanga halisi, na uovu kwa kutamalaki kwa wema. “Wala hapatakuwa na usiku tena; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu huwatia nuru, nao watatawala hata milele na milele,” Ufu 22:5. Je, wasadiki haya? Basi kama huyasadiki haya, tazama kitendawili kuhusu kifo, yaani, “tuliwajua, tumeishi nao, wanatoweka kwa mpango tusioujua, na hao walioondoka hakuna aliyerudi na kutuambia chochote….” Kesho ni zamu ya nani…, hakuna anayejua! Ila kati yako na yangu mmoja wetu au wote tu watarajiwa wa kesho hiyo tusiyoijua.

Ndugu yangu, katika maono yale, Yohana aliambiwa hivi; “Maneno haya ni amini na kweli. Naye Bwana, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumwa wake mambo ambayo hayana budi kuwako upesi. Na tazama, naja upesi; heri yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki,” Ufu!!! 22:6-7. Hatuna ujanja! Tujiandae!

Tumsifu Yesu Kristo!

Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu,” Lk 21:36

Tusali:-Ee Yesu, tujalie kifo chema. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario