ALHAMISI WIKI YA 31 YA MWAKA-C
Somo:
Flp 3:3-8a
Zab/kit: 105:2-3, 4-5, 6-7
Injili: Lk 15:1-10
Nukuu:
“Maana sisi tu tohara,
tumwabuduo Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala
hatuutumainii mwili,” Flp 3:3
“Nalitahiriwa siku ya
nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa
Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo,” Flp 3:5
“Lakini mambo yale
yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo,” Flp 3:7
“Naam, zaidi ya hayo,
nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua
Kristo Yesu, Bwana wangu,” Flp 3:8
“Nawaambia,
Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja
atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya
kutubu,” Lk 15:7
“Nawaambia,
Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi
mmoja atubuye,” Lk 15:10
TAFAKARI:
“Nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua
Kristo Yesu, Bwana wangu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
imani yetu na mwelekeo wake msingi wake ni Kristo Yesu. Kristo ndiyo msingi kwa
sababu kwake twaiona njia, kweli, na uzima kwa kule tunapokutamani yaani, uzima
wa milele, Yoh 14:6. Hivyo kile tulicho, na yote tuliyo nayo na tunayojivunia
katika ukamilifu wake bila Kristo bado yana upungufu mkubwa. “Maana sisi tu
tohara, tumwabuduo Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala
hatuutumainii mwili,” Flp 3:3.
Wapo kati yetu
waaminifu sana na wakweli katika kutimiza yale yaliyokuwa yakifanyika katika
mila na desturi zetu bila hata kuhoji ukweli wake. Mara zote tumepelekwa katika
mambo hayo kwa hofu kubwa, na wakati mwingine ni vigumu kuelewa faidha ya elimu
yako katika hatua ya kukukomboa kutoka katika giza. Na hili ndilo
alilolishikilia Mtume Paulo kabla ya ufahamu wake juu ya kweli katika Kristo
Yesu. Naye anatuambia, “Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli,
wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati,
ni Farisayo,” Flp 3:5. Kuzishika sheria na kudumisha mila na desturi za kabila
lake na utaifa wake aliupa nafasi ya kwanza bila kuhoji kweli iliyopo ndani
yake.
Hapa si semi kwamba
hatupaswi kuzishika na kuziheshimu mila na desturi zetu, bali nachokazia hapa
ni kwamba tuziheshimu mila hizo na kuzishika endapo zina kuweka huru katika
kweli na haki. Ni baada ya Paulo kugundua
hakukwa huru katika mila na desturi hizo za kiyahudi anatoa ushuhuda na
kusema, “Lakini mambo yale yaliyokuwa
faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo,” Flp 3:7. Huyu sasa
ni Paulo anayeufahamu ukweli kama ulivyo, na siyo maswala ya ushabiki usio na
maana kama tunavyoona kwa wapenzi wa soka hata siasa.
Hakuna jambo zuri na
furaha ya kweli unapotambua kweli kwa kile ukiaminicho na kukifuata. Faida
kubwa katika jambo hili ni kuishi bila hofu hata kama katika uhalisia wa jambo
hili umegubikwa na mazingira hatarishi. Ni katika kiwango na hali hii, Mtume
Paulo anasema, “Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili
ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu,” Flp 3:8. Huyu ni
Paulo asiyekuwa na hofu yoyote ile kwa kweli aliyoigundua ndani na katika
Kristo Yesu. Na hapa ndipo tunapopata furaha ya kweli, na kushiriki fuhara ya
Mungu katika upendo na huruma yake. Na furaha hii tunaipata pale tu
tunapojisalimisha kwake pasipo shaka licha ya udhaifu wetu unaotokana na hali
yetu katika ubinadamu wetu. Mtume Paulo ambaye alilitesa Kanisa la mwanzo na
sasa hupo huru ndani na katika Kristo Yesu, ni mfano wa kuigwa.
Wapendwa wana Mungu, Injili
ya leo, Yesu anatoa mifano miwili yenye kuonyesha furaha ya Mungu tunapomrudia
baada ya kutambua njia ya uzima aliyotuandalia.
Mfano wa kwanza, ni mtu mwenye kondoo mia na kumpoteza mmoja. Naye Yesu
anatuambia, “Vivyo hivyo kutakuwa na furaha
mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye
haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu,” Lk 15:7. Mfano wa pili ni huu wa mwanamke yule
mwenye shilingi kumi akapoteza moja. Naye Yesu anatuambia, “Vivyo hivyo kuna
furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye,” Lk
15:10.
Shauku hii ya kutafuta
kimoja kilichopotea itusukume kujiweka karibu zaidi na Mungu. “Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache
mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye
atamsamehe kabisa,” Isa 55:7. Mungu wetu anamaanisha kweli hili
alisemalo, yaani kutusamehe kabisa tunapofanya toba ya kweli na majuto.
Mzaburi anatuambia
ukweli huu kwa kusema, “Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe
utanijulisha hekima kwa siri, Unisafishe
kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji,”
Zab 51:6-7. Huyu ndiye Mungu anayependa kuanza upya nawe katika yote licha ya historia yako mbaya ya huko nyuma.
Je, upo tayari kuanza upya na Mungu?
Wapendwa katika Kristo,
usipoteze muda wako mwingi kwa kuziangalia dhambi na uovu wa wenzako ilhali
nawe upo kwenye mtego huo huo. Yesu kuwa karibu na wadhambi kwa mfano daraja na
mpatanishi wetu na Mungu, anaonekana naye mdhambi kadiri ya mitazamo ya
Mafarisayo ambao walipenda kujionyesha wasafi nje ila ndani ni ubatili mtupu. “Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa
wakimkaribia wamsikilize. Mafarisayo
na waandishi wakanung'unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi,
tena hula nao,” Lk 15:1-2. Mimi na wewe hatuna tofauti na watoza ushuru na
wenye dhambi. Tunahitaji huruma ya Mungu na msamaha wake.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Nawaambia,
Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi
mmoja atubuye,” Lk 15:10
Tusali:-Ee
Yesu, yatengeneze maisha yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario